Saturday, October 28, 2017

Papa's Shadow: Filamu Kuhusu Ernest Hemingway

Kampuni ya Ramble Pictures, ambayo inatengeneza filamu, imemaliza kutengeneza filamu inayohusu safari za mwandishi Ernest Hemingway Afrika Mashariki miaka ya 1933-34 na 1953-54. Nilishaandika taarifa za awali kuhusu filamu hiyo katika blogu hii.

Sehemu kubwa ya filamu hii ni mazungumzo baina ya Mzee Patrick Hemingway na mimi kuhusu safari hizo za Ernest Hemingway, falsafa yake juu ya maisha na sanaa. Patrick Hemingway ni moto pekee wa Ernest Hemingway aliye bado hai. Filamu inaelezea mambo juu ya mwandishi Ernest Hemingway ambayo yalikuwa hayafahamiki vizuri, hasa juu ya namna mwandishi huyu alivyoipenda Afrika.

Filamu hii inaitangaza Tanzania, kwa kuwa inaonyesha maeneo kadhaa ya nchi na watu wake, pamoja na safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro. Chimbuko muhimu la filamu hii ni kozi niliyotunga na kufundisha iitwayo Hemingway in East Africa. Nilisafiri na wanafunzi 29 wa chuo cha St. Olaf, ninapofundisha, tukawa tunapita katika maeneo kadhaa ya Tanzania ambamo Ernest Hemingway alipita, huku tukisoma na kujadili maandishi yake kuhusu sehemu hizo.

Wakati filamu hiyo ilipokuwa inatengenezwa, niliweka taarifa mtandaoni, na nilipeleka taarifa sehemu kadhaa katika mfumo wa serikali ya Tanzania, kuelezea jinsi filamu hii itakavyoitangaza Tanzania. Nilifarijika kupata ujumbe kutoka Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ukiafiki kuwa hii ni "fursa maridhawa ya kuitangaza Tanzania ulimwenguni" kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Filamu inapatikana katika tovuti ya Ramble Pictures.

2 comments:

Pascal Mambya said...

Kwa Sasa Mzee wangu ni Kama unarusha Jiwe tu hewani lakini haligongi kitu ila jua juhudi zako zitakumbukwa sana. Unafanya sehemu yako Mzee katika kujenga Nchi yako na hili ni jambo la faraja kubwa sana kwetu kwa vijana kama sisi tunaochipukia na tunajifunza mengi sana kutoka kwako

Sir Manyuka said...

Hongera sana prof,kwa kufanya sehemu yako katika ujenzi wataifa letu _ mama Tanzania

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...