Friday, July 20, 2012

Bado Niko Songea

Bado niko Songea. Jana asubuhi sikumsikia muadhin. Nadhani nilizidiwa na usingizi. Lakini baadaye kidogo nilisikia mlio wa kengele za Kanisa Katoliki. Nadhani zilikuwa za kanisa kuu la Jimbo, ambalo liko hapa mjini Songea.

Kama nilivyosema katika ujumbe wangu wa juzi, naona ni jambo jema kukumbushana kwamba kuna Muumba. Haijalishi kwangu kama nakumbushwa na muadhin msikitini au kengele kanisani.Mimi sio mtu wa dini sana, ni muumini wa kawaida sana, isipokuwa naona umuhimu wa kuikumbuka dini na kujitahidi kufuata maadili yake.

Jana mchana nilienda Ruhuwiko, kumtembelea dada yangu. Tulipata fursa ya kuongea masuala ya familia na mengine mengi. Nilitegemea pia kwenda kutembelea chuo kikuu kipya kilichofunguliwa hivi karibuni na Kanisa Katoliki hapa mjini. Ratiba ya jana haikuniwezesha kufanya hivyo. Nategemea nitapata fursa hiyo leo.

Mimi nilisomeshwa na Kanisa Katoliki. Sitasahau msisitizo katika taaluma, nidhamu na maadili ya kazi nilivyofundishwa katika shule zao, ambayo yamenifikisha hapa nilipo. Nitashukuru daima.

Leo, Insh'Allah, nitaendelea na ziara zangu hapa Songea, na pia kukutana na wadau mbali mbali.


Thursday, July 19, 2012

Nimefika Songea Tena, Alhamdullilah

Jana jioni nimefika Songea tena. Alhamdullilah. Nimeshinda hapa leo. Nimekutana na ndugu na jamaa, na pia Mheshimiwa Sikapundwa, mmiliki wa blogu ya Tujifunze Kusini. Soma taarifa yake hapa.

Asubuhi sana, kabla hatujaamka, nilisikia jogoo akiwika, na wakati huo huo nilimsikia muadhin akitukumbusha wajibu wetu kwa Muumba. Nilimsikia akisema Allah u akbar. Ni jambo jema sana kwetu waumini, iwe ni wa-Kristo au wa-Islam, kukumbuka au kukumbushwa dhana hiyo ya Allah u akbar, kwamba Mungu ndiye mwenye mamlaka juu ya kila kitu, ndiye mwenye uwezo kuliko mwingine yeyote.

Sunday, July 15, 2012

Nimetoka Arusha Salama

Jana nimetoka Arusha, nikasafiri salama hadi Dar es Salaam. Nilikuwa na wasi wasi kiasi kikubwa nilipokuwa kwenye baadhi ya mitaa ya Arusha, kutokana na namna watu wanavyoendesha magari, piki piki, baiskeli, na kadhalika. Kwenye mitaa hiyo, uendeshaji ni wa kutisha, nami nilikuwa nikitembea mitaani kwa woga, roho mkononi.

Nashukuru nimesalimika hadi kuja tena Dar es Salaam, ambapo napo katika sehemu mbali mbali, uendeshaji ni roho mkononi. Lakini naamini Arusha ni zaidi.

Thursday, July 12, 2012

Arusha ni ya CHADEMA

Juzi usiku hapa Arusha, nilipanda teksi kuelekea hotelini nilikofikia. Humo njiani nilimwuliza dreva wa teksi kuhusu hali ya kisiasa Arusha baada ya mbunge Godbless Lema wa CHADEMA kuachishwa ubunge.

Alinijibu bila kusita kuwa mbunge wa Arusha ni Godbless Lema, pamoja na kuwa halipwi mshahara. Akaongezea kuwa hata ukifanyika uchaguzi, halafu liwekwe jiwe kugombea, likiwa limeandikwa CHADEMA, jiwe hilo litapigiwa kura na kushinda.

Kwangu hizo ni kauli zenye uzito mkubwa. Kwenye masuala ya jamii, nauheshimu sana uchambuzi wa madereva wa teksi. Niliwahi kusema hivyo katika makala hii hapa.

Wednesday, July 4, 2012

Tanga, Mji wa Baiskeli Nyingi

Kitu kimoja kilichovuta hisia yangu, tangu nilipofika Tanga mara ya kwanza, miaka yapata kumi iliyopita, ni jinsi watu wengi wanavyotembelea baiskeli. Mji huu una baiskeli nyingi sana. Hali ni hiyo hadi sasa.

Jambo moja linalonishangaza ni jinsi baiskeli nyingi zinavyopita mitaani usiku bila taa. Sijui watu wa hapa wanawezaje kuimudu hali hiyo, bila wasi wasi. Wanaume kwa wanawake wanatembelea baiskeli mjini hapa.  Jana, tukiwa kwenye Barabara ya Nne, nilimwona mama mmoja amevaa ile aina ya hijab ambayo inafunika hadi uso, kasoro macho. Alikuwa akipita mtaani akiwa amepanda baiskeli.

Hali hiyo ya mji wa Tanga kuwa ni mji wa baiskeli inanipa mawazo kadhaa. Kwanza, kupanda baiskeli namna hiyo, badala ya magari, ni mazoezi bora kwa mwili na afya. Pili, kutumia baiskeli ni jambo jema kwa mazingira, tofauti na utitiri wa magari ambao huchafua hewa ya miji kama Dar es Salaam.

Huu utumiaji wa baiskeli kiasi hicho unanikumbusha mji wa Lamu, kule Kenya. Kule watu wengi hutumia usafiri wa punda. Sijawahi kuona mji wenye punda wengi kama Lamu, na ni usafiri ambao nadiriki kusema una mantiki nzuri kuliko utitiri wa magari kama ilivyo Dar es Salaam.

Ninatalii Tanga

Kwa siku kadhaa sasa nimekuwa mtalii katika mji wa Tanga. Kama wanavyojua ambao wamefika mjini hapa, Tanga ni mji uliotulia sana, ukifananisha na Dar es Salaam, ambao ni mji wa kero nyingi na wajuaji wengi pia.

Jana mchana nilikuwa nimekaa nje ya hoteli ambapo nimefikia. Hapo nje kuna viti vingi na meza, kwani ni sehemu ya wateja kujipatia vyakula na vinywaji. Alipita muuza gazeti nami nikatoa pochi yangu nikanunua magazeti mawili. Muuza gazeti akaenda zake.

Dakika chache baadaye, alipita mtu mmoja akanisogelea na kuniambia kuwa pochi yangu iko chini ya kiti nilichokalia. Nikaangalia, nikaiona. Huyu jamaa hakusimama, bali aliendelea na safari yake, ila najua alinisikia nilipomshukuru. Ingekuwa hajaniambia, sijui mambo yangekuwaje, maana nina hakika ningesimama na kuondoka, bila kujua pochi iko wapi. Pochi ilikuwa na kadi za hela (credit cards), vitambulisho, na kadhalika.

Nimeshapita mitaa kadhaa ya hapa mjini, ambayo nilikuwa siifahamu. Vile vile, nimeona ilipo shule ya Galanos, ambayo ina historia na umaarufu wa pekee sio Tanga tu bali nchini. Nilipokuwa nasoma Mkwawa High School, 1971-72, tulikuwa tunaisikia sana shule ya Galanos.

Insh'Allah leo au kesho nitaenda maktaba ya Tanga, ambayo nimeshaitembelea mara kadhaa. Nitapenda kuona hali yake ya sasa. Mara ya mwisho nilipopita hapo niliona kuwa inahitaji ukarabati mkubwa. Ilijengwa na wakoloni wa ki-Ingereza. Mwalimu Nyerere, ambaye wapika majungu wa Tanzania wanakazana kumbeza, alizienzi maktaba, sambamba na suala zima la elimu. Lakini leo, wa-Tanzania tumepania zaidi kuwekeza katika baa kuliko maktaba au shule. Huko maktabani wa-Tanzania hawaonekani, labda wawe wanafunzi wanaojiandaa kwa mitihani.

Watu wa Tanga walikuwa na bahati ya pekee ya kujengewa maktaba kubwa namna hii. Wangeitumia vizuri, pia kuiwekea vitabu na majarida, leo wangekuwa mbali sana kielimu, ukifananisha na sehemu nyingine za nchi.Lakini sijui ni wangapi katika mji huu wenye mazoea ya kusoma katika maktaba hii.

Ninajiona ni mtalii hapa Tanga. Mbali ya kuangalia sehemu mbali mbali za mji, ninalipia malazi, chakula, vinywaji, usafiri, na huduma zingine kadha wa kadhaa. Ni faraja kubwa kutambua kuwa pesa ninazotumia hapa zinachangia uchumi wa mji huu. Ni pesa ambazo ninaolipwa kule Marekani, ambako nafanya kazi wakati huu. Wazo hili la kuchangia uchumi wa hapa nchini linanifanya nijisikie vizuri.

Monday, July 2, 2012

Nimetua Tanga

Niko Tanga, ambapo niliwasili juzi tarehe 30, nikitokea Dar es Salaam. Tulisafiri na basi la Tashriff, ambalo nililifurahia sana. Kwanza, kwa kipindi kirefu katika safari, tulikuwa tunaangalia video za hotuba za Mwalimu Nyerere. Jambo hilo lilinifurahisha sana, nikizingatia umuhimu wa mchango wa Mwalimu Nyerere, umuhimu wa kuukumbuka na kuuenzi mchango huo, na pia nikizingatia jinsi umbumbumbu uliochanganyika na majungu unavyozidi kushamiri nchini Tanzania kuhusu Mwalimu Nyerere.

Baada ya hizo hotuba, tuliwekewa miziki. Lakini jambo la kuvutia pia ni jinsi dreva alivyokuwa anaendesha gari kwa ustaarabu na hekima, akiwa anaangalia mwendo vizuri. Kwa kweli, nawajibika kuipa hongera kampuni ya Tashriff kwa yale niliyoyashuhudia.

Nimeshafika Tanga mara kadhaa. Ni mji maarufu katika historia na utamaduni Tanzania. Katika safari zangu hizo, nimepiga picha kadhaa, na niliandika habari za maktaba ya Tanga. Safari hii, kama ningekuwa nimejiandaa vizuri, ningekwenda hadi Machui, kijiji alikozaliwa Shaaban Robert. Ningekwenda kuona kaburi lake.

Ninamwenzi mwandishi huyu. Nimeandika makala juu yake ambayo imechapishwa katika Encylopedia of African Literature, na makala nyingine ambayo nimeichapisha katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Pia nimeandika kuhusu kitabu chake kilichochapishwa miaka michache tu iliyopita, kiitwacho Barua za Shaaban Robert. Soma hapa. Mchango aliotoa Shaaban Robert, mwenyeji wa mji huu wa Tanga, katika uandishi Tanzania na duniani kwa ujumla ni mkubwa sana. Ingetakiwa tuwe na maadhimisho yake ya mara kwa mara, tuwe na maandishi na makongamano kuhusu mchango wake, tuwe na kozi mbali mbali mashuleni kutathmini maandishi yake; tuwe na makala magazetini kuhusu kazi zake, na mambo mengine ya aina hiyo. Kampuni za utalii zingekuwa mstari wa mbele katika kuzihifadhi na kuzitumia kumbukumbu hizi. Lakini hilo halitafanikiwa kwa hali tuliyo nayo nchini, ya kutokuwa na utamaduni wa kusoma vitabu.

Haya ndio baadhi ya mawazo niliyo nayo, wakati huu, nikiwa katika mji huu wa Tanga. Kama sitafika kijijini Machui safari hii, nitahakikisha ninafanya hivyo safari nyingine, Insh'Allah.


Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...