Thursday, September 23, 2010

Nimeipata Nakala ya "Tendehogo."

Nilipokuwa Tanzania mwaka huu, nilikutana na rafiki yangu, mwandishi Edwin Semzaba, kama nilivyoandika hapa. Jambo moja tuliloongelea ni kutafsiri tamthilia yake ya Tendehogo. Basi, niliporejea hapa chuoni St. Olaf ninapofundisha, nilienda maktaba na kuagiza nakala ya tamthilia hii. Kwa vile nakala haiko hapa, waliniagizia kutoka Maktaba ya Congress iliyoko Washington DC.

Nimeshapata nakala hiyo, na sasa inabidi nianze mikakati ya kuitafsiri. Kazi ya kutafsiri kazi ya fasihi ni ngumu, yenye changamoto nyingi, hata kama mtu unazijua lugha husika vizuri sana. Hata kama lugha husika ni zako za kuzaliwa nazo au za tangu utotoni, kama kilivyo ki-Matengo na ki-Swahili kwa upande wangu.

Ninasema hivyo kutokana na uzoefu. Nimejishughulisha na kutafsiri tungo za ki-Swahili na hadithi za ki-Matengo kwenda ki-Kiingereza. Niliwahi hata kuandika makala kuhusu kutafsiri hadithi ya ki-Matengo. Soma hapa.

Miaka michache iliyopita nilianza kutafsiri Tendehogo, lakini nakumbuka nilitafsiri kurasa labda mbili au tatu. Sasa, pamoja na wasi wasi nilio nao kuhusu uwezo wangu, itabidi nijipige moyo konde na kuanza kuogelea.

4 comments:

Simon Kitururu said...

Yani hapa wakati nakusoma kuna rafiki yangu kaniuliza unaongelea nini. Nikamueleza kuhusu nia yako ya kutafsiri hiki kitabu . Akauliza umeshamaliza kukitafsiri kwa maana anahisi kitakuwa ni kitabu kizuri kama kuna mtu anaona umuhimu wake wa kutafsiriwa.Nimejitahidi kujieleza.

Kwa kifupi ungekuwa umeshakitafsiri mteja wa kwanza alishapatikana.

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe. Ni tamthilia inayohusu biashara ya utumwa iliyofanyika upande wetu wa dunia, yaani Afrika Mashariki. Katika tamthilia hii tunauona msafara wa watumwa kutoka bara, chini ya mmiliki wao Harun, ambaye ni mu-Arabu.

Ni tamthilia inayozua masuala kadhaa miongoni mwa hao wahusika, wanapoongea kuhusu asili yao, itikadi, jinsia, na kadhalika. Tunaona migongano ya misimamo na fikra baina ya wahusika. Ingawa suala la utumwa ni zito na la kuhuzunisha, "Tendehogo" ni tamthilia yenye burudani pia na vichekesho.

Tamthilia hii ni changamoto ya kuitafakari dhana ya utumwa, maana si suala lililokuwepo zamani tu, lipo hadi leo, kwa namna mbali mbali. Ndio umuhimu wa utamaduni wa kujisomea, na ndio maana tunailalamikia jamii ya Tanzania kwa kutokuwa na utamaduni huo.

John Mwaipopo said...

kazi ya kutafsiri sio ndogo kama baadhi ya watu wanavyoweza kudhani. awali nilidhani ni kazi nyepesi kabla sijaibukulia darasani. hakika ni mara chache sana kwa kazi iliyotafsiriwa (katika 'target language') kupeleka ujumbe ule ule kwa asilimia 100 kama ilivyolengwa na mwandishi wa lugha ya awali (tunaita 'source language'). hakika kinachofanyika ni attempts tu. hizi attempts ndizo zinafanikiwa kwa asilimia fulani kutegemea weledi na umahiri wa mtafsiri mwenyewe. kutokamilika kwa 100% kufikisha ujumbe kunaathiriwa na vitu mbali mbali vikiwemo umahiri, weledi, nyakati (kama kutafsiri leo maandiko ya mwaka 1920), hadhira, mazingira, kutokuwepo maneno yafaayo katika kugha lengwa na kadhalika.

kwa mfano, unaweza kujikuta katika wakati mgumu kutafsiri hekaya, sema za mnyama ng'ombe, kama unalenga hadhira ya wahindi kutokana namna jamii ya wahindu wanavyomchukulia ng'ombe tofauri labda na wamasai. shida hiyo pia inajitokeza kwa mnyama nguruwe katika jamii tofauti hapa duniani.

nakutakia kila la heri katika kutafsiri 'tendehogo'

Simon Kitururu said...

@John: Ndio maana kuna wakati na wasiwasi na BIBLIA.:-(

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...