Saturday, January 12, 2019

Mwongozo wa "Song of Lawino"

Nimechapisha kijitabu ambacho ni mwongozo wa Song of Lawino. Wanafunzi na wasomaji wa fasihi ya Afrika, angalau wa enzi za ujana wangu, wanafahamu kwamba Song of Lawino ni utungo maarufu wa Okot p'Bitek wa Uganda. Mwongozo wangu unaitwa Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino.

Huu ni mwongozo wangu wa pili kuuchapishwa, baada ya Notes on Acebe's Things Fall Apart, mwongozo ambao umekuwa ukitumiwa na wanafunzi na waalimu wa fasihi sehemu mbali mbali duniani kama nilivyowahi kugusia katika blogu hii.

Kila mwongozo unaongelea kazi tajwa lakini pia unagusia kazi zingine za fasihi ili kupanua uwanja wa ufahamu juu ya fasihi. Kila mwongozo unaingiza pia vipengele vya nadharia ya fasihi vinavyohusika katika kazi inayojadiliwa.  Kwa hiyo, kwa kusoma mwongozo moja, mtu anajifunza au anapata fursa ya kutafakri mambo mengi.

Nina nia ya kuandika miongozo mingine ya kazi muhimu za fasihi ya Afrika. Unaweza kujipatia mwongozo huu mpya na vitabu vyangu vingine katika duka la mtandaoni

Friday, January 11, 2019

Wanachuo wa Gustavus Adolphus Wameenda Tanzania

Tarehe 7, nilikwenda kukutana na wanachuo wa Gustavus Adolphus College ambao walikuwa wanaondoka kwenda Tanzania katika programu ya masomo. Hii ni programu ambayo imekuwepo miaka mingi. Wanafunzi wengi zaidi wanasomea uuguzi, na wanakwenda Tanzania ili kuelewa suala la uuguzi linakuwaje katika utamaduni tofauti na wa Marekani.

Nimekuwa nikialikwa kila mara kuongea nao kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni kutokana na kwamba wanasoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na tunapokutana wananiuliza maswali yatokanayo na niliyoandika au mengine. Maswali yalikuwa ya aina mbali mbali, yakiwemo kuhusu mtazamo wa waTanzania juu ya waMarekani na pia kuhusu hali ya kisiasa Tanzania.

Hapa kushoto ninaonekana na viongozi wa msafara, Profesa Barbara Zust na Mchungaji Todd Mattson. Profesa Zust ndiye mwaandaji wa kozi na kila mwaka anaweka kitabu changu kama muhimu kwa wanafunzi. Maelezo mafupi ya programu ya mwaka huu ni haya hapa.

Tuesday, December 4, 2018

Nashukuru Niliandika Kitabu Hiki

Nashukuru niliandika kitabu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nasema hivi kutokana na jinsi kinavyothaminiwa na watu wanaokitumia. Taarifa hizi ninazipata kutoka kwao.

Wiki hii kwa mfano, nimepata mawasiliano kutoka kwa waalimu wawili. Profesa Artika Tyner, kiongozi mojawapo wa Chuo Kikuu cha St. Thomas ameniandikia kuwa anahitaji nakala za kitabu hii, nami nimempelekea. Niliwahi kumwongelea katika blogu hii, baada ya kukutana naye kwa mara ya kwanza. Tangu tukutane, amekuwa mpiga debe wangu wa dhati. Namshukuru.

Nimepata pia ujumbe kutoka kwa Profesa Barbara Zust wa Chuo cha Gustavus Adolphus kunialika kwenda kuongea na wanafunzi anaowapeleka Tanzania katika programu ambayo imedumu miaka mingi. Kama ilivyo kawaida yake, ananiomba nikaongee na wanafunzi kuhusu masuala yaliyomo katika Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kama kawaida, watakuwa wameskisoma na wanasubiri fursa ya kuniuliza masuali. Miaka yote nimefurahi kukutana na wanafunzi hao.

Ninafarijika na kushukuru kwamba nilijiingiza katika shughuli hii ya kuwasaidia watu kutafakari na kuelewa tofauti za tamaduni na athari za tofauti hizo, ili kujizatiti kabla na wakati wa kukutana na watu w utamaduni wa kigeni. Nashukuru niliandika kitabu hiki, ambacho  kimenirahishia kazi hiyo, na papo hapo ni chachu ya tafakari na mazungumzo ya kuelimisha. Nashukuru kuona kuwa wadau kama hao niliowataja, wenye wadhifa mkubwa katika jamii, wanaona umuhimu wa mchango wangu, nami sitawaangusha.

Saturday, November 24, 2018

Kumbukumbu ya Matengo Folktales Kutajwa Katika "Jeopardy."

Kipindi kama hiki, mwaka jana, kitabu cha Matengo Folktales kilitajwa katika kipindi maarufu cha televisheni kiitwacho Jeopardy." Ilikuwa tarehe 23 Novemba, nami niliandika taarifa katika blogu hii.

Tukio hili la kushtukiza lilinifungua macho nikatambua kuwa "Jeopardy" ni maarufu sana hapa Marekani. Bado sijui taarifa za kitabu changu zilifikaje kule, ila ninafurahia kuwaambia waMarekani taarifa hizo kila ninaposhiriki matamasha ya vitabu.

Thursday, November 22, 2018

Vitabu Kama Zawadi ya Sikukuu

Kwa watu wengi, huu ni wakati wa maandalizi ya sikukuu ya Krismasi. Pamoja na mengine, ni kununua zawadi kwa ajili ya ndugu, marafiki na kadhalika. Hapa Marekani, vitabu ni zawadi mojawapo inayothaminiwa.

Hapa kushoto ni picha niliyopiga tarehe 16 Novemba katika duka la vitabu la Barnes and Nobel mjini Burnsville. Inaonyesha kabati la vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka. Nilipiga picha hiyo kwa sababu kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kipo hapo. Kimekuwepo kwa wiki nyingi. Bila shaka kuna wateja wanaoingi na kuchungulia kwenye kabati hilo ili kupata wazo juu ya kitabu cha kununua, kwani tayari kimependekezwa na watu wazoefu wa vitabu.

Utamaduni wa kuvihesabu vitabu kama zawadi muafaka kwa sikukuu au mazingira yeyote mengine unanivutia, kama nilivyowahi kueleza katika blogu hii. Ninatamani utamaduni huu uote mizizi katika nchi yangu. Nawazia furaha watakayokuwa nayo watoto kwa kupewa vitabu kama zawadi, kwa sababu ninajua kuwa watoto wanapenda vitabu, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.  Nawazia namna ambavyo mitazamo na fikra za watu zingeboreka kwa kuwa na utamaduni wa kuthamini na kusoma vitabu vya aina mbali mbali.

Saturday, November 10, 2018

Nimeongea na Lumen Christi Book Club

Miezi kadhaa iliyopita, nilipata mwaliko wa kwenda Lumen Christi Catholic Community kuongelea kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Aliyenialika ni Jackie ambaye alikuwa amekisoma kitabu hicho. Alisema kwamba jumuia ya waumini hao wana klabu yao ya usomaji vitabu, na kwa sasa wamejikita katika vitabu vinavyohusu Afrika.

Nilipoingia ukumbini, niliona meza imepangwa vizuri karibu na mlandoni, yenye vitabu vyangu na vya waandishi wawili ambao tunafahamiana: Maria Nhambu ambaye alizaliwa Tanzania, na Afeworki Ghorghis, jaji mstaafu wa mahakama kuu ya Eritrea.

Baada ya Jackie kunitambulisha, nilielezea kifupi nilivyokulia Tanzania, katika utamaduni wa wa-Matengo, na hatimaye nilivyokutana na utamaduni wa Marekani, nilipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, na kufikia kuwa mshauri kwa vyuo vinavyopeleka wanafunzi Afrika, kama nilivyoandika katika utangulizi wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Katika kuelezea uandishi wangu juu ya masuala ya utamaduni, nilianza na kitabu cha Matengo Folktales.

Baada ya hapo, Jackie alitaja vipengele vilivyomo kitabuni ili nielezee, na wengine waliniuliza masuali yao. Kati ya masuala tuliyoongelea ni "gifts" (sio kwa maana ya zawadi), uzee, na "African time." Nilielezea nilivyoandika kitabuni kuhusu masuala hayo. Klabu hii ya vitabu ni ya aina yake, kwa maana kwamba watu wanahudhuria hata bila kusoma kitabu kinachojadiliwa.

Mkutano ulikuwa mzuri na wenye manufaa. Binafsi, nilitoa shukrani kwa fursa ya kufahamiana na watu wapya, kwani inatajirisha maisha yangu. Nilifurahi kuweza kuwaelezea shughuli zangu kama mtoa ushauri chini ya mwavuli wa Africonexion.  Baada ya mimi kurejea nyumbani, Jackie aliniletea ujumbe kwamba atanitambulisha kwa mkurugenzi wa East Side Freedom Liabrary ambaye wakati huu anaandaa programu kuhusu Afrika. Sikuwa ninajua kuhusu maktaba hiyo. Ninasubiri.

Thursday, October 25, 2018

Nimepeleka Vitabu kwa wa-Matengo

Mwezi Julai mwaka huu nilikwenda Tanzania, nikiwa nimechukua vitabu vingi. Baadhi ni vile nilivyoandika mwenyewe, ambavyo niliviwasilisha katika maduka ya Kimahama, na A Novel Idea. Nilichukua pia nakala 16 za Matengo Folktales kwa ajili ya kuzipeleka kwa wa-Matengo, wilayani Mbinga, katika mkoa wa Ruvuma.

Ninasema hivyo, na kutaja kabila langu, nikijua kwamba kwetu wa-Tanzania, hii ni kauli tata, isiyopendeza, kwani inaashiria upendeleo au ubaguzi kwa msingi wa kabila. Utamaduni wa Tanzania, uliojengwa na chama cha TANU, hauafiki ubaguzi wa makabila au wa aina nyingine. Sasa kwa nini nimetoa kauli hiyo? Kwa nini niliamua kupeleka nakala hizi za Matengo Folktales kwa wa-Matengo? Napenda kuthibitisha kwamba nilifanya jambo muafaka.

Matengo Folktales ni mkusanyo wa hadithi za jadi ambazo nilizirekodi nyumbani u-Matengo miaka ya sabini na kitu. Nilizirekodi katika kaseti, kisha nikachagua hadithi kumi na kuzitafsiri kwa ki-Ingereza. Niliandika uchambuzi wa kila hadithi na nikaongezea insha ya kitaaluma kuhusu hadithi. Huu ukawa ni mswada ambao ulichapishwa kama Matengo Folktales.

Mimi ni mwanataaluma katika taaluma hii inayojulikana kama "Folklore." Kama ilivyo katika taaluma zingine, tuna taratibu na maadili ya utafiti, uandishi na uchapisahji. Kati ya hayo ni utaratibu wa kuwarudushia fadhila watu wanaowezesha utafiti wetu. Watafiti tusiwe tunachukua yale tunayopewa bila kuwarejeshea kwa namna moja au nyingine wale wanaotupa hayo tunayotafuta. Dhana hiyo huitwa "reciprocity" kwa ki-Ingereza.

Kuna nämna mbali mbali za kurudisha fadhila, kufuatana na mila na desturi za mahali husika na kufuatana na ridhaa ya mtu binafsi anayetuwezesha. Kuna namna mbali mbali za kutoa shukrani. Kwa upande wangu, na kwa watafiti wengi, namna bora kabisa ya kurudisha fadhila ni kuwapa nakala ya yale ninayorekodi na kuondoka nayo, kama vile kaseti au picha ninazopiga.

Kwa msingi huo, baada ya kuchapisha Matengo Folktales, nilijua kwamba nina wajibu wa kupeleka nakala kwa wa-Matengo. Kwa kuwa nimechapisha kitabu kwa ki-Ingereza, ilibidi nisubiri hadi ipatikane sehemu muafaka ya kupeleka.

Fursa imepatikana kwa kuwepo kwa shule za sekondari. Hizi nakala 16 nilimkabidhi mwalimu Frank Kinunda mjini Mbinga, baada ya mawasiliano naye, naye amezisambaza kwenye hizo shule. Zitawaelimisha vijana na walimu kuhusu utamaduni wa wahenga, na pia kuhusu taaluma ya "Folklore." Vile vile, kwa kuwa  nimeandika kwa uangalifu mkubwa kama mwalimu wa lugha ya ki-Ingereza, Matengo Folktales ni kitabu cha kujiongezea ujuzi wa ki-Ingereza. Kitabu hiki kinatumika kufundishia katika vyuo hapa Marekani, na ninafurahi kimeanza kuwa mikononi mwa wanafunzi na walimu Tanzania

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...