Wednesday, September 29, 2010

Programu za Kupeleka Wanafunzi Tanzania

Leo hapa chuoni St. Olaf tulikuwa na shughuli ya kuzitangaza programu za masomo ambamo chuo kinapeleka wanafunzi wake.

Tunafanya hivyo mara moja kwa mwaka. Walimu washauri wa programu tunakuwepo na taarifa mbali mbali za programu tunazohusika nazo, na wanafunzi wanakuja kupata taarifa hizo, na pia kujiandikisha iwapo wana nia ya kujiunga na programu hizo.

Vyuo vingi hapa Marekani vina programu za aina hiyo, na vyuo kadhaa vinapeleka wanafunzi Tanzania. Hii inatokana na kufahamu faida wanayopata wanafunzi kwa kwenda kuishi na kujifunza katika nchi zingine. Inapanua akili na upeo. Kuishi miongoni mwa watu wa utamaduni tofauti kunampa kijana fursa ya kukomaa kwa namna mbali mbali na kuwa tayari kwa maisha ya zama zetu za utandawazi wa leo. Programu hizi zinachangia maelewano mema duniani.

Pamoja kazi yangu ya kufundisha katika idara ya ki-Ingereza hapa St. Olaf, ninashughulika katika program zinazopeleka wanafunzi nchi za ki-Afrika, ikiwemo Tanzania. Nimefanya shughuli hii kwa miaka yote niliyofundisha hapa ughaibuni, katika programu kama LCCT, ACM Tanzania, na ACM Botswana. Leo nilijipanga kwenye meza kama inavyoonekana katika picha, nikingojea wanafunzi, nimwage sera.

Hii ni fursa ya kuitangaza nchi. Kama nilivyowahi kusema kwenye blogu hii, picha ni vielelezo murua kabisa. Ni lazima niseme kuwa shughuli hii ya kuitangaza Tanzania ilikuwa inanipendeza sana miaka ya mwanzo, wakati Tanzania ilipokuwa kweli nchi ya kupigiwa mfano, ambayo nilikuwa najivunia. Tanzania ile, ya Mwalimu Nyerere, inatoweka. Nchi inazidi kuwa ya matabaka ya wenye mali wanaostarehe, na maskini wanaoteseka. Badala ya jamii yenye amani na utulivu, tunaendelea kuona kushamiri kwa ukatili kama ule unaofanywa dhidi ya albino na wale wanaoitwa vibaka. Program hizi za kuleta wanafunzi Tanzania zinaiingizia nchi hela nyingi, lakini naogopa kuwa hela hizi zinachotwa na mafisadi. Siku hizi, ninapowaambia wanafunzi hao kwenda Tanzania, ninasema nikiwa na wasi wasi. Lakini naendelea kufanya shughuli hii, kwani ni muhimu, sio tu kwa hao wanafunzi, bali kwa nchi yetu na yao, na dunia kwa ujumla, kama nilivyoandika hapa.

3 comments:

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Mwl. Mbele, pamoja na wasiwasi huo ulio nao bado unaweza kupeleka wanafunzi Tanzania.

Hongera!

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe. Ingawa katika maelezo yangu inaonekana kama ni kazi ya mteremko, ukweli ni kuwa ni kazi nzito. Jambo mmoja linaloleta wasi wasi muda wote ni usalama wa hao wanafunzi wanapokuwa kule kwetu.

Kwa mfano, wanakumbana na hali inayotokana na imani ya wa-Swahili kuwa kila mzungu ni tajiri. Kwa hivi, hata vibaka wanawapigia mahesabu hao wanafunzi.

Na ikitokea ajali, kwa mfano, na mwanafunzi akadhurika, sheria na taratibu za kushughulikia hali hiyo ni nyingi huku Marekani, na kama wewe ni kiongozi wa msafara, una majukumu mengi ya ajabu wakati huo, vinginevyo, wanasheria wa Marekani wanachangamkia sana tenda ya kufungua mashtaka.

Hofu ya mashtaka inavifanya hata vyuo vyenyewe viishi kwa wasi wasi wakati wanafunzi wako mbali namna hii. Kwa hivi wewe kiongozi wa msafara inabidi ulale jicho moja wazi, hata kama umetokea kwenye ulabu baa.

Anonymous said...

kwa kweli profesa hapo mimi nimekuelewa sana!
swala la usalama kwa wanafunzi wageni ni swala nyeti sana tofauti na tunavyofikiri tulio wengi wetu!!!
nakutakia mafanikio mema katika hiyo shughuli nzito ya kuitangaza nchi yetu!!
Huo ni zaidi ya uzalendo unaoufanya wewe!!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...