Tuesday, July 14, 2015

Nawashangaa CCM

Ninawashangaa wanaCCM wanaolalamikia mchakato wa chama chao wa kumpata mgombea urais. Mwaka 2010 CHADEMA walilalamika sana kwamba wamefanyiwa rafu na CCM. Hakuna yeyote katika CCM aliyewasikiliza CHADEMA, wala kuwaonea huruma. CCM wote waliibeza CHADEMA, kwamba ingojee uchaguzi ujao.

Sasa leo wanalalamika kuwa wamefanyiwa rafu huko huko CCM. Sio kwamba hao wanachukia rafu. Wanalalamika kwa sababu rafu wamefanyiwa wao. Mimi kama raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa naona kuwa hawana sababu ya kulalamika, kwani wanavuna walichopanda. Labda watajifunza umuhimu wa kutetea haki wakati wote na kwa yeyote.

Sunday, July 12, 2015

Kesho Naanza Tena Kufundisha

Hiki ni kipindi cha kiangazi, ambacho kwa ki-Ingereza huitwa "summer." Katika chuo chetu cha St.Olaf, walimu hatuwajibiki kufundisha kipindi hiki, ambacho hudumu karibu miezi minne. Ila kama mwalimu anapenda, anaweza kufundisha. Kozi za kipindi hiki cha kiangazi hudumu wiki yapata tano, lakini kozi inafanana kwa uzito wake sawa na kozi za muhula wa kawaida.

Kwa miaka niliyofundisha hapa, mara kwa mara nimefundisha kozi wakati wa kiangazi. Uzuri wake mojawapo ni kuwa wanafunzi huwa wachache, na kwetu tunaofundisha fasihi, ni wakati mzuri wa kujaribisha vitabu vipya. Kozi ambayo nitafundisha kipindi hiki ni fasihi ya Afrika (African Literature).  Nitatumia vitabu kutoka sehemu mbali mbali za Afrika.

Kitabu kimojawapo ni Minaret, ambayo ni riwaya ya Leila Aboulela wa Sudan. Nilifundisha riwaya hii muhula uliopita, na iliwavutia wanafunzi na mimi pia. Ingawa ni hadithi ya kubuniwa inatupa picha nzuri ya maisha ya watu wa Khartoum, ambao ni wa-Islam wa tabaka la juu, si walalahoi. Wanafunzi wangu walishukuru kusoma riwaya hii kwa vile iliwapa fursa ya kuielewa angalau misingi ya u-Islam. Kutokana na jinsi tulivyopendezwa na riwaya hii, niliamua kuifundisha tena, na ninapangia kufundisha riwaya zingine za Leila Aboulela siku za usoni, panapo majaliwa.

Kitabu kingine ni The Thing Around Your Neck, ambacho ni mkusanyo wa hadithi za Chimamanda Ngozi Adichie wa Nigeria. Huyu ni mwandishi ambaye ametukuka miaka ya karibuni na anasifika sana. Nimefundisha kazi zake kadhaa: Purple Hibiscus, Half of a Yellow Sun, na Americanah. Ni mwandishi mwenye kipaji sana, ingawa ni mdogo kwa umri.

Nitafundisha pia tamthilia mbili za Ama Ata Aidoo wa Ghana: The Dilemma of a Ghost and Anowa. Aidoo ni mwandishi mkongwe, ambaye alianza kujipatia umaarufu kimataifa miaka ya sitini na kitu kwa tamthilia na hadithi fupi, na hatimaye riwaya. Nimefundisha baadhi ya kazi zake. Nimefundisha The Dilemma of a Ghost mara kadhaa.

Kitabu kingine nitakachofundisha ni The Tuner of Silences, ambayo ni riwaya ya Mia Couto wa Msumbiji. Sijawahi kusoma chochote alichoandika mwandishi huyu, lakini ninajua kuwa ni maarufu. Kwa hivyo, niliona nijiongezee ufahamu wangu sambamba na kufundisha kazi ya fasihi kutoka katika lugha ambayo si ya ki-Ingereza. Riwaya hii imetafsiriwa kutoka k-Reno. Ingawa katika idara yetu ya ki-ingereza hapa chuoni St. Olaf tunapendelea kufundisha kazi zilizoandikwa kwa ki-ingereza, tunaona si vibaya mara moja moja kufundisha kazi zilizotafsiriwa kwa Ki-Ingereza.

Nitafundisha pia tamthilia ya Athol Fugard iitwayo Valley Song. Huyu ni mwanatamthilia maarufu wa Afrika Kusini, ambaye tamthilia zake kadhaa nimewahi kufundisha. Mifano ni Master Harold and the Boys, A Lesson From Aloes, na Sorrows and Rejoicings. Nimefundisha Sorrows and Rejoicings mara kadhaa, na kila mara nazidi kuguswa upya.

Kitabu cha sita ni The Beautiful Things That Heaven Bears, ambayo ni riwaya ya Dinaw Mengestu, mwandishi chipukizi wa Ethiopia. Sijawahi kusoma kazi yoyote ya mwandishi huyu, ila najua kuwa tayari ameshajijengea sifa. Nimeanza kusoma hii riwaya yake na ninaiona ni yenye mvuto mkubwa kwa jinsi inavyoelezea maisha ya vijana wa ki-Afrika hapa Marekani. Hii ni dhamira moja muhimu katika riwaya ya Americanah ya Chimamanda Ngozi Adichie, ambaye nimemtaja hapo juu.



Tuesday, July 7, 2015

Ukiwa na Siri Iweke Kitabuni

Wengi wetu tumesikia kwamba ukiwa na siri iweke kitabuni; mw-Afrika hataiona. Kwetu wa-Tanzania, hali ni hiyo hiyo. Mwaka hadi mwaka, tumekuwa tukisikia jinsi utamaduni wa kusoma vitabu unavyokosekana Tanzania. Si jambo la kujivunia.

Nimekuwa nikiandika mara kwa mara hali ninayoiona hapa Marekani, katika matamasha ya vitabu, maduka ya vitabu, na maktaba. Wa-Marekani kama inavyoonekana katika picha nilizoweka hapa, wana tabia tofauti.

Picha ya katikati niliipiga katika tamasha la vitabu Minneapolis. Ya chini niliipiga katika tamasha la vitabu Mankato. Picha ya juu kabisa sikumbuki niliipata wapi. Zote zinaonyesha jinsi watu wanavyosaka vitabu na kuchungulia yaliyomo. Sijui kama kuna siri iliyofichwa kitabuni ambayo hawataigundua.

Ninaweza kuleta mfano moja mdogo kutokana na kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambamo nimeweka taarifa kuhusu wa-Marekani na wa-Afrika. Tangu kichapishwe, mwaka 2005, maelfu ya wa-Marekani wamekisoma. Wanazijua siri zilizomo.

Mama mmoja m-Tanzania aliyeanzisha na anaendesha taasisi fulani alikuja hapa Marekani kuonana na washirika wake. Kwenye jimbo la Colorado aliulizwa kama amesoma kitabu hiki. Alikiri kuwa hakuwa amekisoma. Baada ya kurudi Tanzania, aliwasiliana nami akanielezea tukio hili. Tulifanya mpango, nikampelekea nakala.

Hiyo si hali ya kujivunia. Wenzetu wa-Marekani wanazoeshwa kuvipenda vitabu tangu utotoni. Wanakulia katika utamaduni huo. Kutokana na kulelewa katika utamaduni huo, hata wazee wananunua na kusoma vitabu, kama vilivyowahi kuandika katika blogu hii.

Sunday, July 5, 2015

Majadiliano na Profesa Joseph Mbele

MAJADILIANO HAYA YAFENYIKA KATI YA MANDELA PALLANGYO. NA PROFESA JOSEPH MBELE WA CHUO KIKUU CHA OLAF CHA MAREKANI.
PROFESA JOSEPH MBELE

Safari yako ya uandishi ilianza muda mrefu. Je ni kipi kinakutia moyo na kuzidi kufanya kazi hii ngumu?
PROF: JOSEPH MBELE
Mimi ni mwalimu na ninauona uandishi kama sehemu ya ufundishaji au aina ya ufundishaji. Ndio maana uandishi wangu unaelekea zaidi katika mambo yanayoelimisha. Kazi pekee niliyoitamani hata kabla sijaanza shule ilikuwa ni ualimu. Kwa hivyo, ninapenda kuandika kama ninavyopenda kufundisha darasani.

Uliwahi kukutana na maneno mabaya kama kukatishwa tamaa au kukashifiwa wakati ulipokuwa unaanza fani?
PROF: JOSEPH MBELE
Sikuwahi kukutana na maneno ya aina hiyo tangu mwanzo. Uandishi wangu umekuwa zaidi wa kitaaluma, ambao unatokana na utafiti. Hakuna wakati ambapo uandishi wangu huo umeleta maneno mabaya au ya kukatisha tamaa. Lakini kwa kuwa ninaandika pia magazetini na mitandaoni kuhusu masuala ya kawaida ya maisha, wakati mwingine nakutana na maneno mabaya. Hapa ninamaanisha maneno yasiyozingatia hoja, bali yananilenga mimi. Ninawaona wanaofanya hivyo kuwa ni wajinga, wasiojiamini, kwani hata hawajitambulishi. Ninawaheshimu watu wanaopinga hoja kwa hoja. Wanatajirisha mijadala na wanatupanua mawazo.

Umeandika vitabu vingi. Licha ya kuwa ni Profesa mwenye kazi nyingi. Je unawezaje kutenga muda wa kuandika na kutekeleza majukumu mengine kwa ufasaha? Na je vitabu vyako vinapatikanaje?
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema, uandishi wangu kwa ujumla ni mwendelezo tu wa ufundishaji. Uandishi unanisaidia kufafanua mambo akilini mwangu. Ninapoandika kuhusu masuala ya kawaida ya jamii, najiona ninaburudisha akili yangu. Mara kwa mara naandika kwa mizaha, na hiyo inaburudisha. Baada ya burudani hiyo, akili inakuwa tayari kufanya kazi ngumu. Uandishi wa masuala ya kawaida, pamoja na usomaji wa vitabu, ni burudani ya kutosha.
Vitabu vyangu vinapatikana mtandaoni, http://www.lulu.com/spotlight/mbele na Amazon.com. Vinapatikana kama vitabu halisi, lakini vingine pia kama vitabu pepe. Ninapenda vipatikane Tanzania pia. Kwa sasa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kinapatikana kwenye kituo cha utalii cha Burunge, mkoani Manyara: imborutours@gmail.com
kitabu 1

Fani hii ya uandishi, unadhani vijana tumeivamia? Au basi unaridhishwa na kiwango cha uandishi wa vijana hasa tunaochipukia?
PROF: JOSEPH MBELE
Ninadhani yeyote mwenye hamu ya kuandika awe huru kufanya hivyo. Kinachotakiwa ni uvumilivu, kwani haiwezekani kuwa mwandishi bora haraka bila uzoefu. Pia, ni lazima vijana na waandishi kwa ujumla wawe wasomaji makini. Kutegemea na aina ya uandishi ambayo kijana anataka kuandika, awasome waandishi wa mataifa mbali mbali waliotukuka katika aina ile ya uandishi.

Watu wengi wanadhani kazi ya uandishi inalipa na kutajirisha haraka-haraka. Wakati mwaandishi uambulia mrahaba wa asilimia kumi (10%) katika mauzo ya kazi yake ama asilipwe kabisa.
PROF: JOSEPH MBELE
Mwandishi aandike pale anapoona ana jambo la kusema. Msukumo utoke ndani mwake, na akisha andika ajisikie ametua mzigo. Asihamakie mambo ya nje, kama vile pesa. Mategemeo ya pesa hayaleti uandishi bora. Fundisho hili tumepewa na waandishi maarufu, kama vile Ernest Hemingway wa Marekani na Mario Vargas Llosa wa Peru. Jambo la msingi ni mwandishi kuiridhisha nafsi yake, na kuikubali kazi yake, kwamba imewasilisha kwa uaminifu na ukweli yale aliyokuwa nayo moyoni. Akiridhika kabisa, hiyo ni tunu bora kuliko pesa. Fedha ni matokeo. Vile vile, ni waandishi wachache sana duniani wanaopata fedha ya kuwawezesha kumudu maisha kutokana na uandishi. Waandishi chipukizi watambue hilo, na wale ambao hawana nia ya dhati ya kuwa waandishi wakumbuke hilo, wasije wakajisumbua na ndoto za bure.
Ninavyofahamu, mrahaba wa 10% au zaidi kidogo ni wa kawaida duniani kote, isipokuwa kwa waandishi maarufu.

Je wewe unadhani ni sahihi mtu kuandika kitabu mwaka ama zaidi na kulipwa ujira wa kipuuzi namna hii?
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema, msukumo wa mwandishi uwe kusema yaliyomo moyoni mwake, kwa uaminifu na ukweli kadiri inavyowezekana. Kutokana na hilo, waandishi makini hutumia muda mwingi kurekebisha maandishi yao. Ukisoma habari za waandishi maarufu, kama Hemingway, utashangaa jinsi walivyokuwa wanarekebisha maandishi yao mara nyingi sana, na pengine kuishia kutoridhika na kuyaweka kando. Haraka haraka haina baraka. Kitabu kinaweza kuhitaji miaka mingi kukifikisha katika hali ya kumridhisha mwandishi makini. Mimi mwenyewe nilitumia miaka yapata 23 kukiandaa kitabu cha Matengo Folktales.
kitabu 2

Wachapishaji wengi duniani walikuwa kama miungu watu. Na hata basi hao watunzi waliokuwa na vipaji vikubwa kama akina Shaaban Robert, bado awakuwa na sauti mbele yao. Walikiwa ni watu wa kunyenyekewa sana na hata watu kujipendekeza. Ili tu kazi zao zichapishwe.
Lakini sasa naona kiburi hiki kinaanza kufyekwa-fyekwa na utandawazi. Mimi ninaomba utufafanulie ni namna gani waandishi wanaoteseka miaka na miaka wanaweza kufanya kusudi kuchapisha kazi zao kwa kutumia mtandao
PROF: JOSEPH MBELE
Ni kweli, wachapishaji wamekuwa kama miungu watu. Hata Shaaban Robert alilalamika kuhusu wachapishaji. Ni kweli kuwa siku hizi kuna tekinolojia za uchapishaji mtandaoni ambazo zinamwezesha mwandishi yeyote kuchapisha kitabu chake. Kinachotakiwa ni kwa mwandishi kujibidisha kusoma kuhusu tekinolojia hizi na akiamua, azitumie. Kuna aina tofauti za uchapishaji wa mtandaoni, na ni juu ya mwandishi kuamua anaipenda zaidi ipi.

Je kuna madhara gani yanaweza kujitokeza katika mfumo wa kujichapishia katika hiyo mitandao?
PROF: JOSEPH MBELE
Sidhani kama kuna madhara. Badala yake, naona uchapishaji wa mtandaoni umeleta demokrasia zaidi katika uwanja wa uchapishaji, tofauti na jadi tuliyozoea ya wachapishaji kuhodhi mamlaka.
Kuna watu ambao wanalalamika kuwa uhuru huu umesababisha machapisho ya viwango duni kuchapishwa kiholela. Hilo ni suala tata. Tukiangalia kwa upande wa wasomaji ambao tunaweza kuwaita wateja, nafikiri tunapaswa kutambua kuwa wao ndio waamuzi. Ninaamini kuwa wataweza kupambanua kati ya kilicho bora na kilicho duni.

Mtu anapochapisha katika mtandao labda. Labda mwingine anataka tu achapishe haraka-haraka ili aonekane na kupata pesa, bila hata kazi yake kuhaririwa uoni ni tatizo pia?
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema hapa juu, ninawategemea wateja. Kama mwandishi atachapisha kitabu duni, anaweza kuwadanganya wanunuaji wa mwanzo, lakini wateja huambiana kuhusu kitu walichonunua. Kama ni kibovu, kitakosa wanunuaji. Isipokuwa, labda niongezee kuwa mtazamo wangu huu umejengeka katika imani kwamba wateja ni watu wenye akili, kwani kama akili yao ni duni, hoja yangu itadhoofika.

Kuingia kwa teknolojia kwa kasi. Je unahisi ipo siku haya makampuni ya kuchapisha yatageuka na kuwa maghala?
PROF: JOSEPH MBELE
Suala hili linajadiliwa sana katika ulimwengu wa leo. Jambo moja linalojitokeza ni kwamba makampuni kama yale ya Marekani yameshaanza kujihami kwa kuingia katika matumizi ya hizi tekinolojia mpya za uchapishaji, sambamba na uchapishaji wa jadi. Hakuna anayejua kama uchapishaji wa jadi utakufa kabisa. Nikitoa mfano wa kuwepo kwa vitabu pepe, jambo moja ambalo ni wazi ni kuwa watu wengi wanataka kushika kitabu mkononi kama zamani, pamoja na kwamba siku hizi kuna vitabu pepe.

Licha ya mfumo wa kujichapishia mtandaoni kwa mrahisi kidogo. Uoni kama ni ishara ya kukubali na kukaribisha ukoloni mpya kwa mikono miwili? Au kusema shikamoo ukoloni?
PROF: JOSEPH MBELE
Tekinolojia ya kujichapishia mtandaoni, kama nilivyosema, imeboresha demokrasia katika uchapishaji. Kwa msingi huo, hata waandishi ambao hawakuwa na fursa ya kujieleza kwa walimwengu sasa wanayo fursa. Ukoloni wa fikra ambao ulisambazwa sana na vitabu, vitabu vilivyochapishwa kwa mtindo wa kibabe kama tulivyosema hapa juu, unaweza kupigwa vita na wanyonge kwa kutumia tekinolojia hii ya uchapishaji mtandaoni.

Kuna watu wanaondika. Na wapo wengi wanaojifunza kuandika na wanapenda! Lakini wanakatishwa tamaa kutokana na mifumo iliyopo kama kupuuzwa na kuachwa.
Naomba uwape neno na kuwatia nguvu.
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema hapa juu, mtu mwenye nia ya dhati ya kuandika hawezi kuyumbishwa. Anafuata msukumo wa moyoni mwake hadi mwisho. Anayekatishwa tamaa ni yule ambaye hakuwa thabiti katika nia na msukumo wa ndani. Mimi mwenyewe, naandika vitabu kwa sababu siridhiki na vile ninavyovisoma. Ninaandika vitabu ambavyo ningependa viwepo bali havipo, vitabu ambavyo ningependa kuvisoma, bali sivioni. Kwa hivi, kwa kiasi kikubwa ninajiandikia mwenyewe. Siyumbishwi na yeyote.
Ustahimilivu ni muhimu katika uandishi. Waandishi maarufu wa kimataifa wanaongelea jambo hilo. Wanakumbana na vipingamizi, lakini hawakati tamaa. Kipingamizi kimoja ni kuwa kuna nyakati ambapo mwandishi anashindwa kuandika. Akili haifanyi kazi. Mwandishi wa kweli hakati tamaa. Anajua kuna wakati utakuja ambapo ataweza kuendelea kuandika.
Vile vile wako waandishi ambao kazi zao zilikataliwa mara nyingi na wachapishaji. Hawakukata tamaa. Baada ya kuchapishwa, kazi hizo hizo zilizokataliwa zilikuja kuwa maarufu. Mwandishi mwenye msukumo wa
kutoka ndani, ana kiu ya kuandika. Akisha andika anakuwa na faraja au furaha. Hawezi kuacha kuandika, wala hawezi kukatishwa tamaa.

Picha zote kwa hisani ya http://www.josephmbele.blogspot.com
CHANZO: Mandelapallangyo.com

Friday, July 3, 2015

Mungu (Allah) Hana Ubaguzi

Blogu yangu hii ni uwanja huru kwa fikra na mijadala, ikiwemo mijadala kuhusu dini. Leo, kwa kifupi na lugha rahisi, napenda kuibua suala la dini na ubaguzi.

Laiti sisi tunaosema tuna dini tungetambua kuwa Mungu hana ubaguzi. Mungu, ambaye kulingana na tofauti za lugha, huitwa kwa majina mbali mbali, anathibitisha jinsi anavyowapenda wanadamu, wa dini zote, na wasio na dini.

Mungu anateremsha baraka zake bila ubaguzi. Anawapa uzazi watu wenye dini, sawa na wasio na dini. Wa-Islam wanazaa, wa-Kristu wanazaa, wa-Hindu wanazaa, na wa dini zingine kadhalika. Wasio na dini wanazaa.

Mungu anateremsha mvua kuotesha mbegu katika mashamba ya wa-Islamu, ya wa-Hindu, ya wa-Kristu, na ya wengine, hata wasio na dini. Kuku wa mu-Islam anataga mayai na kuangua vifaranga, sawa na kuku wa m-Kristu, sawa na kuku wa asiye na dini. Mungu hana ubaguzi katika kuteremsha neema zake.

Sasa basi, kwa nini wanadamu wengi wanaosema wana dini ni wabaguzi? Kwa nini wanatumia kigezo cha dini kujifanya wao ni bora kuliko wengine? Wanapobaguana namna hii, wanafuata njia ya Mungu au ya shetani?

Thursday, July 2, 2015

Leo ni Kumbukumbu ya Kifo cha Hemingway

Leo ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwandishi Ernest Hemingway. Alikufa tarehe 2 Julai, mwaka 1961, nyumbani mwake Ketchum, Idaho. Alikufa katika nyumba nayoonekana pichani ambayo ilipigwa na Jimmy Gildea wakati wa safari zake za kuandaa filamu ya Papa's Shadow.

Maelezo ya namna Hemingway alivyokufa yanapingana kidogo. Kila mtu anakiri kuwa alikufa kwa risasi ya bunduki. Karibu kila mtu anasema kuwa Hemingway alijiua kwa kujipiga risasi, akiwa peke yake ghorofa ya juu.

Lakini mke wake, Mary Welsh Hemingway, ambaye wakati wa tukio alikuwa katika nyumba hiyo kwa chini, alitoa tamko kuwa ilikuwa ni ajali:

Mr. Hemingway accidentally killed himself while cleaning a gun this morning at 7:30 A.M. No time has been set for the funeral services, which will be private.

Kila ninapowazia kifo cha Hemingway, nakumbuka jinsi alivyokuwa na mikosi ya ajali katika maisha yake. Ninavyowazia kuwa alijiua, nakumbuka misiba kadhaa ya watu kujiua katika ukoo wa Hemingway. Ninawazia pia kuwa mimi nimeishi miaka mingi kumzidi Hemingway, ambaye alizaliwa mwaka 1899 akafa mwaka 1962.

Ninajiuliza nimefanya nini katika miaka yangu yote hii, nikijifananisha na Hemingway, ambaye alikuwa mwandishi maarufu aliyeongoza njia kwa aina yake ya uandishi, akapata tuzo ya Nobel mwaka 1954.

Hemingway aliongelea kifo, tena na tena, katika maandishi yake. Kauli yake moja inayojulikana zaidi ni hii:

Every man's life ends the same way. It is only the details of how he lived and how he died that distinguish one man from another.


Wednesday, July 1, 2015

Vitabu Nilivyojipatia Wiki Hii

Kama ilivyo kawaida yangu, napenda kuongelea vitabu nimeongeza katika maktaba yangu. Wiki hii, ambayo bado haijaisha, nimejipatia vitabu vinne. Cha kwanza ni Jake Riley: Irreparably Damaged, kilichotungwa na Rebecca Fjelland Davis. Nilikinunua tarehe 28 mwezi huu, katika tamasha la vitabu, Deep Valley Book Festival, mjini Mankato kutoka kwa mwandishi, ambaye tumefahamiana miaka kadhaa. Kufuatana na maelezo, hii ni hadithi ya kubuniwa.

Katika tamasha hilo, nilinunua pia kitabu kiitwacho No Behind, kilichotungwa na Louise Parker Kelly. Tuliongea kidogo, na mwandishi, akaniambia kuwa ni mwalimu na kuwa kitabu chake ni hadithi ya kubuniwa, kuhusu maisha na harakati za mtoto wa shule eneo la Washington D.C.

Kitabu kingine ambacho nilikipata jana ni Noontide Toll. Ni mkusanyo wa hadithi fupi za Romesh Gunesekera, mwandishi mahiri sana wa Sri Lanka. Sikumbuki kama nilikinunua kitabu hiki. Huenda wachapishaji wameniletea kwa kuwa nimewahi kuagiza vitabu vingine vya Gunesekera kwa kufundishia. Gunesekera ni mmoja wa waandishi wanaonivutia sana kwa uwezo wao wa kutumia ki-Ingereza.

Kitabu kingine, Lucy: the Beginnings of Humankind, nilikinunua jana katika duka la vitabu la chuoni St. Olaf. Waandishi wake ni Donald Johanson na Maitland Edey. Nilivutiwa na jina la Lucy kwenye uso wa kitabu, nikahisi kuwa kitabu kinamhusu binadamu wa kwanza, ambaye masalia yake yalivumbuliwa Ethiopia. Nilipokisogelea, niliona kuwa ni hivyo.

Kutokana na maelezo kwenye jalada la mbele, kitabu hiki kinasimulia namna uvumbuzi huu ulivyotokea na maelezo kuhusu binadamu huyu wa kwanza. Kwa mujibu wa uchambuzi katika gazeti la The New York Times Book Review, dhamira ya kitabu hiki ni "One of the most compelling scientific investigations ever undertaken." Ni wazi kuwa kitabu hiki ni hazina isiyo kifani. 

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...