Tuesday, November 27, 2012

Tanzania: Nchi ya Mavuvuzela

Kama ilivyo kawaida yake, Kipanya hakosi neno. Kwenye katuni hapa kushoto katoboa ukweli: Tanzania ni nchi ya mavuvuzela. Tukubaliane kwa hilo.

Monday, November 26, 2012

Wanafunzi Wangu wa ki-Ingereza Muhula Huu

Leo nimepiga picha na baadhi ya wanafunzi wangu ambao nimekuwa nikiwafundisha muhula huu somo la uandishi wa lugha ya ki-Ingereza.

Wanafunzi wote wanaosoma hapa chuoni St. Olaf wanatakiwa kusoma somo hilo kama msingi wa masomo ya chuo. Kwa vile wanafunzi ni wengi, tunawagawa katika madarasa madogo, yasiyozidi wanafunzi 18 kila darasa. Uchache huu unamwezesha mwalimu kumsaidia kila mwanafunzi ipasavyo, kwa kuhakiki uandishi wake na kumpa mawaidha.






Ninapenda kufundisha masomo yote ninayofundisha. Ninawapenda wanafunzi. Lakini kwa vile mimi ni mwandishi, ninapenda kwa namna ya pekee kufundisha uandishi wa lugha ya ki-Ingereza.

Kutumia ki-Ingereza vizuri kabisa ni mtihani mkubwa, kama mwandishi maarufu Ernest Hemingway alivyokiri na kutukumbusha. Hata huku ughaibuni kwa wenye lugha hii, wengi hujiandikia tu na kuamini kuwa wameandika ki-Ingereza vizuri. Kukaa nao na kuwaonyesha njia nzuri ni bahati na baraka ambayo ninaifurahia.

Sunday, November 25, 2012

Rais Obama Anunua Vitabu

Jana Rais Obama aliripotiwa akinunua vitabu kwenye duka dogo, kwa lengo la kuchangia mapato ya wafanya biashara wadogo. Alitanguzana na binti zake, akanunua vitabu 15 vya watoto, kwa ajili ya kuwagawia ndugu. Picha ionekanayo hapa ni ya J. Scott Applewhite, Associated Press.

Niliposoma taarifa hii, nilijiuliza je, ni lini tumewahi kuwaona vigogo wa Bongo wakinunua vitabu? Ni lini umewahi kumwona kigogo wa Bongo akiwa na wanawe katika duka la vitabu? Pia nilikumbuka kuwa niliwahi kuuliza katika blogu hii kama unaweza kumpa m-Tanzania kitabu kama zawadi ya Krismasi au Idd el Fitri. Soma hapa.

 Kama vigogo wa Bongo wangekuwa na utamaduni wa kuvithamini vitabu, wangeweza kuleta mabadiliko makubwa nchini. Wangeweza kuanzisha maktaba vijijini. Wangeweza kuanzisha klabu za usomaji wa vitabu.

Vigogo hao husafiri sana nje ya nchi. Kwenye viwanja vya ndege, iwe ni O'Hare, Schippol, Heathrow, Johannesburg, au Istanbul, kuna maduka ya vitabu. Vigogo hao wangeweza kununua vitabu kila wanaposafiri na kuvipeleka kwenye maktaba za mkoa, shule na vyuo. Hebu fikiria, ukimpelekea hata tu kamusi ya ki-Ingereza mwalimu wa shule kule Lindi au Kalenga, unakuwa umeleta mapinduzi fulani katika ufundishaji kwenye shule hiyo.

Sisemi tu kwa kujifurahisha au kuwalaumu wengine. Mimi mwenyewe nanunua sana vitabu, na hadi sasa ninavyo zaidi ya elfu tatu. Niliposoma Marekani, 1980-86 nilinunua vitabu vingi sana, nikarejea navyo Tanzania. Ingawa watu walinishangaa kwa kuleta vitabu badala ya gari, vitabu hivyo vimewafaidia wanafunzi na wasomi wengi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Baada ya kuja kufundisha Marekani, 1991, nimenunua vitabu vingi zaidi. Nikifanikiwa kuvisafirisha nitakaporudi Tanzania, itakuwa ni hazina kubwa kwa wapenda elimu. Ila sina hakika kama nitaweza kuvisafirisha, kwani ni vingi mno. Itabidi wa-Tanzania wafanye mchango waniletee hela za kusafirishia vitabu hivyo. Uwezo wanao sana, kama inavyothibitika katika michango ya sherehe mbali mbali. Vinginevyo huenda nikaamua kuviuza hapa hapa Marekani nipate hela za kununulia angalau bajaji. Itanisaidia baada ya kustaafu Tanzania.

Thursday, November 22, 2012

Kanisa Katoliki Mjini New Prague, Minnesota

Jana nilifika mjini New Prague hapa Minnesota, kwa shughuli binafsi. Nilishawahi kupita kwenye mji huu mara kadhaa, na kitu kimoja kilichonivutia tangu mwanzo ni kanisa Katoliki ambalo liko katikati ya mji, pembeni mwa barabara.

Watu waliniambia tangu zamani kuwa kanisa hili lilijengwa na wahamiaji kutoka Czechoslovakia, na kwamba madirisha yake ya vioo (stained glass) yanavutia sana. Nilikuwa na hamu ya siku moja kwenda kusali hapo na pia kuangalia hayo madirisha. Mimi hupenda nyumba za ibada za dini mbali mbali kama nilivyoeleza hapa na hapa.












Jana, kwa vile nilikuwa mjini hapo, nilihakikisha nimepiga picha ya kanisa hilo, ingawaje ni kwa nje tu. Nilipata fursa ya kuona kuwa pembeni mwa kanisa kuna shule. Huu ni utamaduni wa kanisa Katoliki, kwamba panapojengwa kanisa, na huduma zingine ziwepo, hasa shule na hospitali. Nilivyoliangalia hilo kanisa na hiyo shule, nilikumbuka kijijini kwangu, kwani kule nako hali ni hiyo hiyo.

Monday, November 19, 2012

Kwa wa-Luteri wa Tungamalenga, Iringa

Makanisa mengi ya ki-Luteri Marekani, ELCA, yana ushirikiano na makanisa ya ki-Luteri ya Tanzania na nchi zingine. Kanisa la Shepherd of the Valley, ambalo liko hapa Minnesota, lina uhusiano na kanisa la Tungamalenga, mkoani Iringa. Kwa taarifa zaidi, soma hapa.

Nimewahi kutembelea Shepherd of the Valley kuongea na wanafunzi wa Chuo cha Gustavus Adolphus ambao walikuwa hapo kufanya maandalizi ya safari ya Tanzania, kama nilivyoelezea hapa.

Kwa miaka mingi kiasi nilifahamu kuhusu uhusiano baina ya Shepherd of the Valley na Tungamalenga.  Kila ninapoliwazia kanisa la Shepherd of the Valley, au ninapoliona, naiwazia Tungamalenga, ingawa mimi si m-Luteri. Kwa vile liko pembeni mwa barabara, ninaliona kanisa hilo kila ninapoenda kutoa mihadhara katika Chuo cha Mazingira.

Sikuwahi kufika Tungamalenga, hadi mwaka jana, niliposafiri na wanafunzi wa ki-Marekani kutoka Iringa kwenda hifadhi ya Ruaha. Ghafla tulipita sehemu iitwayo Tungamalenga. Nilishtuka, kwa sababu sikuwa hata najua kama Tungamalenga iko katika njia hiyo, karibu kabisa na hifadhi ya Ruaha.

Picha inayoonekana hapa juu nilipiga tarehe 13 Novemba, nilipokuwa narudi kutoka kwenye Chuo cha Mazingira. Kwa miaka miwili au zaidi nilitaka niweke picha ya Shepherd of the Valley hapa katika blogu yangu, nikiwawazia wa-Luteri wa Tungamalenga.

Saturday, November 17, 2012

Mdau Wangu Mpya, Mhadhiri wa Mankato

Nimempata mdau mpya, mhadhiri katika chuo cha North Central, mjini Mankato, Minnesota. Natumia neno mdau au wadau kwa maana ya wasomaji wa vitabu vyangu ambao wanajitokeza na kujitambulisha kwangu. Nina kawaida ya kuwataja wadau hao katika hii blogu yangu, kama unavyoweza kusoma hapa na hapa.

Leo napenda nimwongelee huyu mdau mpya, Mhadhiri Davis. Wiki kadhaa zilizopita, nilipigiwa simu na Profesa Scott Fee wa Chuo Kikuu cha Minnesota, Mankato, akisema kuwa wakati anapiga simu, yuko katika mazungumzo na Mhadhiri Becky Davis, wakiongelea kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Alinipa fursa nikasalimiana na Mhadhiri Davis, ambaye anaonekana pichani hapa kushoto.

Waalimu hao walikuwa katika maandalizi ya kupeleka wanafunzi Afrika Kusini. Pamoja na kuongelea upatikanaji rahisi wa nakala za kitabu hiki, walikuwa wananialika Mankato kuongea na wanafunzi. Bila kusita, niliupokea mwaliko wao. Falsafa yangu ni kuwa Mungu kanipa fursa ya kuelimika sio ili nimwage mbwembwe bali niwafaidie wanadamu.

 Profesa Scott Fee tulifahamiana miaka kadhaa iliyopita, wakati anaandaa msafara wa wanafunzi wa kwenda Afrika Kusini. Katika maandalizi hayo, aliamua kutumia kitabu changu hicho. Kama sehemu ya maandalizi ya safari, alinialika chuoni kwake kuongea na wanafunzi kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni, kama nilivyoelezea kitabuni. Nilienda, nikaongea na wanafunzi, ambao walikuwa wengi, kama ninavyokumbuka.

Baada ya kutajiwa jina la Mhadhiri Davis, niliingia mtandaoni kutafuta taarifa zake. Yeye ni mwandishi makini, kama ilivyoelezwa hapa. Nafurahi kuunganishwa na mwandishi mwenzagu, kwani kutakuwa na fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu.

Nashukuru kwamba kazi yangu ya kutafakari na kuandika kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni inawagusa na kuwafaidia wengine. Insh'Allah, siku itakapowadia, nitaenda Mankato na kutoa mchango wa kiwango cha juu kwa kadiri ya uwezo wangu.

Tuesday, November 13, 2012

Kitabu cha Mazungumzo ya Nelson Mandela

Leo nimenunua kitabu cha Nelson Mandela, Conversations with Myself. Ingawa sijui nitakisoma lini, kutokana na utitiri wa vitabu vyangu, nimekinunua kutokana na umaarufu wa Mandela na kutokana na ukweli kwamba kumbukumbu zake na mawaidha yake ni hazina kubwa.

Idadi ya vitabu vinavyosimulia na kuchambua mchango wa Mandela vinaendelea kuchapishwa. Yeye mwenyewe pia amejitahidi kuandika. Kwa mfano, tulipokuwa vijana, tulikifahamu kitabu chake kiitwacho  Long Walk to Freedom. Haikuwa rahisi mtu usikijue kitabu hiki, kwani kilichapishwa katika mfululizo maarufu wa vitabu vya shirika la Heinemann, ambalo tulilifahamu sana kutokana na vitabu vyake ambavyo tulikuwa tunavisoma.

Miaka ya karibuni, Mandela amejikakamua akaandaa kitabu cha hadithi, Nelson Mandela's Favorite African Folktales. Ni mkusanyiko wa hadithi za asili za ki-Afrika.

Kwa kuangalia juu juu, nimeona kuwa hiki kitabu cha Conversations with Myself ni mkusanyiko wa barua mbali mbali za Mandela na maandishi mengine ambayo yanatufunulia picha ya Mandela sio tu kama mwanasiasa na mpigania ukombozi maarufu bali kama binadamu. Ni kitabu kikubwa, kurasa 454. Nitakuwa nakisoma kidogo kidogo. Isipokuwa ni kimoja kati ya vitabu vya pekee kabisa katika maktaba yangu.


Nimeenda Tena Chuo Cha Mazingira, Minnesota

Leo nilitembelea tena Chuo cha Mazingira, mjini Apple Valley. Kama alivyofanya mwaka hadi mwaka, Mwalimu Todd Carlson alinialika kwenda kuongea na wanafunzi wake kuhusu uwiano baina ya masimulizi ya jadi na mazingira. Mwalimu Todd Carlson, anaonekana pichani kushoto kabisa










Mwalimu Carlson huwaeleza wanafunzi kuhusu masimulizi ya jamii mbali mbali za asili, kama vile wa-Marekani Wekundu, wenyeji wa asili wa Australia, na pia wa-Khoisan wa pande za kusini mwa Afrika.

Anatumia pia kitabu changu cha Matengo Folktales. Kila ninapoenda kuongea na wanafunzi hao, nawakuta wamesoma angalau sehemu fulani muhimu za kitabu hicho.



 


Kutokana na maandalizi hayo anayofanya Mwalimu Carlson, mazungumzo yangu na wanafunzi pamoja na masuali yao huwa ya kiwango cha juu.


Kama ilivyokuwa safari zilizopita, sote tumefurahia ziara yangu ya leo.

Friday, November 9, 2012

U-Islam Watekwa Nyara

Leo nimejipatia kitabu kiitwacho The Great Theft: Wrestling Islam From the Extremists. Mwandishi ni Khaled Abou El Fadl, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles, ambaye kwenye jalada nyuma ya kitabu, ametajwa kuwa "one of the world's preeminent Islamic scholars and an accomplished Islamic jurist."

Nikitafsiri kwa ki-Swahili, ni kwamba mwandishi huyu ni mmoja wa wataalam wa u-Islam ambao wanaongoza hapa duniani na pia ni mwanasheria mahiri wa sheria za ki-Islam. Nimeanza kukisoma kitabu hiki leo hii. Tayari ninaona kuwa hiki kitabu ni moto wa kuotea mbali, kwa jinsi kinavyouelezea na kuutafsiri u-Islam kwa mujibu wa misahafu yake, na kwa jinsi kinavyowabomoa hao wanaoitwa wa-Islam wenye siasa kali. Mwandishi anawabainisha kuwa ni wapotoshaji, kwenye masuala kama nafasi ya wanawake katika u-Islam, jihad, haki za binadamu, ugaidi, na vita.

Kitabu hiki kinanikumbusha kitabu changu kingine, kiitwacho Muhammad: A Biography of the Prophet, ambacho nilikifurahia sana, nikakitaja katika blogu hii. Yeyote anayetaka kujielimisha kuhusu Mtume Muhammad ni vema akasoma kitabu hiki, ambacho gazeti la Muslim News lilikisifu kwamba kinaondoa umbumbumbu uliopo, na ni kitabu muhimu kwa wasio wa-Islam na wa-Islam pia.

Basi nimeona kuwa kitabu cha The Great Theft ni kimoja kati ya hivi vitabu vinavyofafanua kwa umahiri mkubwa ukweli kuhusu u-Islam, tofauti na yale yanayosemwa na hao wanaoitwa wa-Islam wenye siasa kali, ambao wameuteka nyara na wanaupotosha u-Islam. Ushauri wangu ni kuwa tuvisome vitabu hivi. Lakini je, kwa wa-Tanzania, ambao kwwa ujumla ni wavivu wa kujifunza lugha mbali mbali na ni wavivu wa kusoma vitabu, elimu hii itawafikia?

Thursday, November 1, 2012

Lord of the Flies: Riwaya ya William Golding

Kila siku naviangalia vitabu vyangu nilivyo navyo hapa ughaibuni. Ni vingi sana. Jana nilikichomoa kitabu kimojawapo, Lord of the Flies, kilichotungwa na William Golding, ili nikiongelee hapa katika blogu yangu. Lord of the Flies ni moja ya vitabu vilivyonigusa sana nilipokisoma nikiwa sekondari. Kilikuwa ni kitabu kimojawapo cha lazima katika somo la "Literature." Kilituvutia sana vijana wa wakati ule.

Ni kitabu cha hadithi ya kubuniwa, yenye ujumbe mzito kuhusu tabia ya binadamu. Tunawaona vijana wadogo kutoka U-Ingereza wakiwa wamepata ajali ya meli na kuachwa katika kisiwa peke yao. Hakuna mtu mzima. Wanawajibika kujipanga ili waweze kuendelea kuishi, kwa kutegemea uwindaji humo kisiwani, na wanawajibika kujitungia utaratibu wa kuendesha jamii yao.

Hao ni watoto waliolelewa katika maadili mazuri huko kwao u-Ingereza, lakini katika mazingira ya kupotelea humo kisiwani, tunawaona wakididimia kimaadili, na hatimaye tunashuhudia wanavyoanza kuwa wabaya kabisa, na hii jamii yao inagubikwa na ukatili.

Hatimaye, kwa bahati kabisa, meli inaonekana kwenye upeo wa macho baharini. Insogea hadi kufika hapa kisiwani. Vijana wanaikaribia na nahodha anapowaona anashangaa kuona walivyoathirika katika kuishi wenyewe bila watu wazima. Anaposikiliza masimulizi yao, anashindwa kuamini jinsi walivyopoteza ustaarabu waliolelewa nao.

Hayo ndiyo ninayokumbuka kuhusu dhamira ya riwaya hii. Tangu wakati ule tulipoisoma riwaya hii nilifahamu kuwa ni riwaya ambayo imewapa changamoto kubwa wanasaikolojia na wanafalsafa wa tabia ya binadamu, kwa maana kwamba inazua masuala mazito. Je, watoto ni malaika kama tunavyodhani au wana silika ya ubaya wa kupindukia kama wabaya wengine wowote? Je, hayo tunayoyaita maadili yana mshiko kiasi gani, au yanategemea tu mazingira, na kwamba mazingira yasipokuwepo, maadili yanaweza kutoweka kabisa?

Lakini kuna pia suala la sanaa ya mwandishi Golding, ambayo imetukuka sana. Ana ubunifu wa hali ya juu, wa kumgusa sana msomaji, jinsi anavyoelezea maisha na mahusiano ya hao watoto humo kisiwani. Matumizi yake ya lugha yalikuwa ni kivutio kimoja kikubwa sana kwangu. Niliguswa na jinsi anavyoelezea mazingira, kwa mfano.

Nilipokuwa mwanafunzi Mkwawa High School, niliendeleza juhudi zangu za uandishi ambazo nilianza miaka iliyotangulia. Niliandika hadithi iitwayo "A Girl in the Bus," ambayo ilichapishwa katika jarida la BUSARA, lilokuwa maarufu katika vyuo vikuu vya Afrika Mashariki. Hii ilikuwa ni hadithi yangu ya kwanza kuchapishwa katika jarida la kimataifa. Nakumbuka jinsi nilivyofurahi kuisoma hadithi yangu katika jarida maarufu namna hii, ambamo walikuwa wanaandika waandishi maarufu wa Afrika Mashariki, na mimi nikiwa ni kijana wa "High School" tu. Nilikuwa na furaha isiyoelezeka, wakati napitapita mjini Iringa. Katika hadithi hii niliiga kwa kiasi fulani mtindo wa William Golding katika kuelezea mazingira.

Mwaka huu, nikiwa katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nililitafuta jarida BUSARA nikaisoma hadithi yangu, kwa furaha na mshangao kuwa niliweza kuandika vizuri namna ile wakati wa ujana wangu. Lakini, William Golding alichangia.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...