Jana tumeanza muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf, nami nimeanza kufundisha leo. Masomo yangu kwa muhula huu ni matatu: First Year Writing, African Literature, na Muslim Women Writers.
Tumeanza vizuri. Nimepata fursa ya kuwaeleza wanafunzi mambo ya msingi kuhusu falsafa yangu ya ufundishaji, na kuhusu masomo. Nimesisitiza wajibu wa kufikiri na kuchambua masuala, wajibu wa kujenga hoja. Nimesisitiza msimamo wangu wa kulinda na kutetea uhuru wa fikra na kujieleza. Nimewahahakishia wanafunzi kuwa wawe tayari kukabiliana na fikra na hoja mbali mbali.
Siku ya kwanza ya muhula ni kama kitendawili. Hatujui safari itakuwaje, siku hadi siku, lakini tunategemea matokeo mema. Ingawa uzoefu wangu wa kufundisha unaendelea kuongezeka muda wote, haiwezekani kupanga na kuwa na uhakika nini kitatokea. Jambo pekee lisilobadilika ni kwamba kila muhula ni tofauti na mwingine.
Friday, September 9, 2016
Thursday, September 8, 2016
Wasomaji Wangu Wa Nebraska Waendao Tanzania
Nina jadi ya kuwaongelea wasomaji wangu katika blogu hii, kama njia ya kuwaenzi. Ni jambo jema kwa mwandishi kufanya hivyo. Leo ninapenda kuwakumbuka wasomaji wangu wa sinodi ya Nebraska ya Kanisa la Kiluteri la Marekani, ambao tangu zamani wamekuwa na programu ya kupeleka watu Tanzania kuendeleza uhusiano baina yao na wa-Luteri wa Tanzania. Hao wasafiri, sawa na wenzao wa sinodi zingine za Marekani, wamekuwa wakitumia kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika kujiandaa kwa safari, ili kuzielewa tofauti za tamaduni za Marekani na Afrika. Ni elimu muhimu katika ulimwengu wa utandawazi wa leo, ambayo nje ya ufundishaji wa darasani, ninashughulika nayo.
Wakati huu ninapoandika, waumini wa Nebraska wanajiandaa kwa safari ya Tanzania, ambayo itafanyika mwezi Februari mwaka 2017. Wameitangaza safari hii mtandaoni, na mratibu mojawapo wa safari, Martin Malley, ameniandikia ujumbe leo akisema, "We still recommend your book." Katika ukurasa wa 16 wa chapisho la maelezo na maandalizi ya safari, kitabu hicho kimetajwa.
Ninapowakumbuka wasomaji wangu wa Nebraska, ninakumbuka nilivyokutana katika uwanja wa ndege wa Amsterdam na kikundi cha watu wa Nebraska waliokuwa wanakwenda Tanzania, tukasafiri pamoja. Mimi sikuwajua, ila wao walinitambua, kama nilivyoelezea katika blogu yangu ya ki-Ingereza.
Tuesday, September 6, 2016
Tamko la ACT-Wazalendo Kuhusu Hali ya Nchi
Tamko Rasmi la Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo kuhusu HALI YA NCHI
Dar Es Salaam, Jumanne, 06 Septemba 2016
Utangulizi
Jana Jumatatu, 5 Septemba 2016, Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo ilikutana katika kikao chake cha kawaida. Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilipokea, kujadili na kuidhinisha Taarifa kuhusu HALI YA NCHI. Taarifa hii sasa inatolewa rasmi kwa umma. Taarifa ipo katika maeneo makubwa manne: Hali ya kisiasa, hali ya kiuchumi, umoja wa kitaifa na hitimisho.
Hali ya Kisiasa
Kamati Kuu imezingatia kuwa Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeanisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Hata hivyo, katika awamu hii ya tano, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kuzuia shughuli za siasa kwa kutumia nguvu ya Jeshi la Polisi na hata Jeshi la Wananchi. Kwa mujibu wa serikali ya CCM, shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani inapaswa kukoma mapema baada ya uchaguzi. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi.
Kisiasa, tunatambua kwamba Viongozi wa CCM wamepoteza mvuto kwa wananchi na sasa wanamsukuma Mwenyekiti wao Rais Magufuli kutumia jeshi katika kuokoa taswira ya Chama cha Mapinduzi mbele ya umma.
Kwa kuzingatia hali ya kisiasa nchini kwa sasa, Kamati Kuu ya chama chetu:
i) Tunalaani na kupinga kwa nguvu zetu zote hatua za Serikali ya Chama cha Mapinduzi za kuvunja Katiba na kujaribu kuweka pembeni utawala wa sheria.
ii) Tunapinga vitendo vinavyozidi kushamiri katika serikali hii ya CCM ya kujaribu kuendesha nchi kwa ubabe na matamko ya viongozi badala ya utawala wa sharia.
iii) Tutasimama imara, na tutaungana na vyama vingine vya siasa pamoja na taasisi zingine za kiraia katika kulinda mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa maoni, na utawala wa sheria katika nchi yetu
Hali ya Kiuchumi
Katika miaka 10-15 iliyopita, nchi yetu imejenga uchumi ambao umekuwa ukikua kwa kiwango cha asilimia 6-7 kwa mwaka katika kipindi chote hiki. Ukuaji huu wa uchumi ulitokana na juhudi za nchi katika kuvutia wawekezaji na kuchochea shughuli za uzalishaji mali kwa wananchi wenye kipata cha chini. Awamu ya tano ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi imerithi changamoto ya uchumi unaokua bila kuwafaidisha wananchi wa kawaida. Hili ndilo tulitegemea Serikali mpya ishughulike nalo.
Kamati Kuu imeshtushwa na hali ya kuanza kudorora kwa shughuli za uchumi katika kipindi cha miezi kumi ya utawala wa awamu ya tano. Kwa mfano:
a) Taarifa za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake (Quarterly Economic Review na Monthly Economic Review) kwa robo ya mwisho ya mwaka 2015 (Oktoba – Desemba 2015 ) zinaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilikuwa 9%. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 (Januari – Machi 2016) kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilishuka hadi kufikia 5.5%. Kiuchumi, hii inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Magufuli umepungua kwa 4%.
b) Shughuli za uchumi zinazohusu wananchi masikini zimeshuka kutoka kasi ya ukuaji ya 10.20% robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 2.7% katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita. Hii ina maanisha kwamba Wananchi wetu wanazidi kudumbukia kwenye ufukara kwa kasi tangu awamu ya tano ya Serikali ya Chama Mapinduzi iingie madarakani
c) Ukuaji wa sekta ya ujenzi katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 ilikuwa 13.8% lakini ukuaji wa sekta hii katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ilikuwa ni 4.30%, ikiwa ni tofauti ya takribani -10%. Hii ni kwa sababu uwekezaji katika sekta hii umeanza kushuka.
d) Kasi ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji imeporomoka kutoka kukua kwa 14.50% robo ya mwisho ya 2015 mpaka kukua kwa 7.9% robo ya kwanza ya 2016, ikiwa ni kuporoka kwa 7% katika kipindi cha miezi 6 tu ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli. Kuporomoka kwa sekta ya usafirishaji itaathiri watu wengi, wakiwemo madereva, matingo, pamoja na mama Ntilie wanaowauzia chakula. .
Kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya uchumi katika nchi, Kamati Kuu:
a) Tunaitaka serikali izingatie sayansi ya uchumi katika kuendesha uchumi wa nchi. Uamuzi wa CCM wa kuitelekeza serikali yake kwa mwanasiasa mmoja anayedhani ndiye anayejua kila kitu na yeye kugeuka kuwa mshauri wa washauri wa uchumi itasambaratisha uwekezaji nchini na kuua kabisa juhudi za miaka 20 za kuvutia wawekezaji na kujenga uchumi shirikishi.
b) Inahimiza wananchi kuzingatia kuwa msingi wa uchumi wetu ni uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Msingi wa kuvutia wawekezaji ni utawala wa sheria. Juhudi za serikali ya CCM za kuua utawala wa sheria zitaua uwekezaji na kuangamiza uchumi wa nchi. Tusirihusu CCM iue uchumi wa nchi kwa maslahi yake ya kisiasa na viongozi wake.
Umoja wa Kitaifa
Nchi yetu imefanya juhudi kubwa katika miaka 50 iliyopita katika kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuhakikisha kuwa makabila, dini na baadaye vyama vya siasa tunaishi bila kukamiana. Juhudi za dhati za kupambana na ubaguzi ndiyo umekuwa msingi imara wa kujenga Umoja wa Kitaifa na amani tunayojivunia.
Hata hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa utawala mpya wa Serikali ya CCM, kupitia Mwenyekiti wake mpya na Rais wa Jamhuri wa Muungo, umeanza kwa juhudi na kasi kubwa kuchokonoa na kumomonyoa misingi ya utaifa na umoja wetu. Sasa tunaye Rais asiyechagua maneno na asiyejua aongee nini na wapi. Vijana waliosoma kwa bidii katika mazingira ya shule zilizotelekezwa na serikali ya CCM anawaita VILAZA.
Katikati ya uhasama mkubwa wa kisiasa na kijamii huko Zanzibar Rais wetu amefunga safari, sio kujaribu kutibu majeraha yaliyosababishwa na kuchezewa kwa sanduku la kura, bali kuchochea uhasama chini ya ulinzi wa vyombo vyetu vya dola vyenye jukumu la kulinda na kudumisha amani. Sasa Rais wetu, kupitia kauli zake, ameanza kuubomoa muungano wetu uliojengwa kwa unyenyekevu na katika mazingira magumu.
Kila asimamapo kuhutubia, jambo moja la kutarajiwa kutoka katika kinywa cha Rais wetu ni matamshi yanayodhoofisha nguzo fulani ya umoja, mshikamano na undugu wetu kama taifa. Yote haya yakitokea chama chake cha CCM ama kimekaa kimya au kinachekelea. Inasikitikitisha kwamba Chama kilichoasisiwa na Mwalimu Nyerere kinamruhusu kiongozi wake kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na kuchochea chuki katika jamii ya watanzania.
Kwa kuzingatia mtikisiko mkubwa katika umoja na mshikamano wa kitaifa unaoendelea nchini, Kamati Kuu:
a) Tunalaani juhudi zinazofanywa na Serikali ya CCM kupitia Mwenyekiti wao za kuchochea chuki katika jamii ya watanzania na kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na amani ya nchi
b) Tunatoa wito kwa watanzania wote waipendayo nchi yao kusimama kidete katika kulinda misingi ya nchi yetu na kukataa chuki inayoanza kujengwa na utawala wa CCM
c) Tunatoa wito wa kipekee kwa viongozi wetu wa dini na wakuu wa nchi waliopita, hususani Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na Mzee Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na wazee wengine wanaoheshimika katika nchi yetu wavae ujasiri wa kumuonya Mwenyekiti wa CCM kuwa juhudi zake za kuchochea chuki katika jamii yetu ya watanzania zitasambaratisha Taifa letu.
Hitimisho
i) Sisi kama chama cha siasa, tunaendelea kusisitiza kuwa tutaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kupambana na ufisadi na kujenga uwajibikaji nchini.
ii) Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa kuheshimu na kulinda demokrasia na kuzingatia utawala wa sheria nidyo msingi wa mapambano dhidi ya ufisadi. Tunasisitiza kuwa mtu yeyote, wa kawaida au kiongozi, anayesema kwamba anaweza akapambana na ufisadi kwa kukanyaga misingi ya demokrasia na utawala wa sheria mtu huyo ni mwomgo na kwa kweli ni fisadi na anataka kujenga himaya mpya ya ufisadi. Mtu huyo, pamoja na mambo yake yote, yafaa akataliwe na kudharauliwa haraka!
iii) Tunasisitiza kuwa msingi wa uchumi wetu ni kuvutia uwekezaji wa ndani nan je ya nchi. Kuzingatia utawala wa sheria ndiyo msingi wa kuvutia uwekezaji. Juhuzi za hivi karibuni za serikali ya CCM za kujaribu kuua utawala wa sharia ni juhudi ovu za kuua uchumi wa nchi yetu. TUZIKATAE juhudi za kuua utawala wa sheria kwa kuwa zitaangamiza taifa letu kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kiongozi wa Chama
Dar es Salaam, Jumanne 6 Septemba 2016.
Sunday, September 4, 2016
Naomba Kitabu Changu Kipigwe Marufuku
Imenibidi nitoe ombi hili la kupigwa marufuku kitabu changu kwa sababu za msingi. Kwanza kama mtu mwingine yeyote mtiifu kwa serikali, ninatambua wajibu wangu wa kuripoti jambo lolote linalokwenda kinyume na maelekezo au matakwa ya serikali. Pili, mimi sina mamlaka kisheria ya kukipiga marufuku kitabu chochote. Kwa hivi, ninaiangukia serikali.
Mawazo yaliyomo katika kitabu hiki yasipodhibitiwa, yakiachwa yaenee, yatajenga ukaidi miongoni mwa raia na tabia ya kutowaheshimu viongozi. Ninaelewa kuwa ni juu ya serikali kufikiri na kufanya maamuzi. Wajibu wa raia ni kutii. Raia wakiachwa huru kufikiri na kujiamulia mambo, kuna hatari kwamba misingi imara ya amani na utulivu nchini itaharibika na itakuwa vigumu kwa nchi kutawalika.
Saturday, September 3, 2016
Shakespeare Ametawala Mawazo Yangu Leo
Kwa miezi kadhaa, nimekuwa nikiwazia kuandika makala juu ya utangulizi wa The Dilemma of a Ghost, tamthilia ya Ama Ata Aidoo wa Ghana. Utangulizi huu umeitwa "Prelude" katika tamthilia hiyo, ambayo Ama Ata Aidoo aliitunga alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu Ghana, Legon, ambapo alihitimu mwaka 1963. Tamthilia yake iliigizwa kwa mara ya kwanza mwaka 1964 na kuchapishwa mwaka 1965.
Nimefundisha tamthilia hii mara kadhaa, na kwa miezi kadhaa nimepata hamu ya kuchambua utangulizi wake, yaani "Prelude." Nimeona kwamba hakuna mhakiki yeyote ambaye ameichambua sehemu hii ya tamthilia hii kwa kiwango kinachoniridhisha. Hii "Prelude" si rahisi kuifafanua. Ninahisi hii ndio sababu ya wachambuzi kuiacha kando.
Ni katika kuwazia jadi hii ndio nikajikuta ninamkumbuka Shakespeare. Katika "Prelude" yake, Ama Ata Aidoo ametumia dondoo za lugha ambazo zinatupeleka kwa Shakespeare. Sishangai, nikizingatia kuwa Ama Ata Aidoo alisomea ki-Ingereza na fasihi katika mfumo wa elimu wa ukoloni wa ki-Ingereza. Kwa maana hiyo, Ama Ata Aidoo alilelewa katika mfumo ambao walilelewa waandishi wa enzi zake, na waliofuatia, kama vile Efua Sutherland, Wole Soyinka, na James Ngugi, ambaye baadaye alibadili jina na kujiita Ngugi wa Thion'go.
Baada ya kujiridhisha kwamba kuna athari za Shakespeare katika "Prelude" ya The Dilemma of a Ghost, ndipo nikawa nawazia kutafuta ushahidi katika tamthilia za Shakespeare. Kwa miezi yote hii, nilikuwa na uhakika kwamba baadhi ya athari zimetoka katika tamthilia kadhaa na pia mashairi ya Shakespeare, na baadhi ya athari nilihisi zilitokana na au tamthilia ya The Merchant of Venice au Hamlet.
Kwa miezi kadhaa, kabla ya kuanza kufukuafukua maandishi ya Shakespeare leo, nimekuwa nikitafakari vipengele vya "Folklore" ambavyo ninavyoviona katika "Prelude." Pia nimekuwa nikitafiti zaidi vipengele hivyo, kwa kufuatilia maandishi ya wataalam kama William Bascom. Sina shaka kwamba tafakari hiyo na utafiti vitaniwezesha kuifafanua "Prelude" na matumizi ya "Folklore" katika tamthilia nzima ya The Dilemma of a Ghost.
Monday, August 29, 2016
Suluhu ya Maandamano
Ni muhimu kila mtu awe huru kutoa mawazo yake, kuliko kunyamazishwa. Wanataaluma katika saikolojia wanatufundisha kuwa ukandamizaji au unyamazishaji, kwa maana ya "repression," una madhara makubwa. Sigmund Freud, Carl Jung, na wafuasi wao ni kati ya wanataaluma hao.
Watu wakiwa huru kujieleza, wanapata ahueni kisaikolojia, na hii ni muhimu kwa afya ya mtu binafsi na kwa afya ya jamii. Kuhusu madhara ya "repression," hata wahenga walitahadharisha, waliposema "kimya kingi kina mshindo mkuu."
Wakati huu, wa-Tanzania wanapita katika kipindi kigumu sana, kutokana na mvutano uliozuka baina ya wapinzani wanaotaka kufanya maandamano nchi nzima kupinga kile wanachoita udikteta, na papo hapo, polisi, serikali, na baadhi ya raia hawataki maandamano haya yafanyike. Wengine wamesema watafanya maandamano yao ili kuyapinga yale mengine.
Ninaona hili si suala gumu. Wote wanaotaka kuandamana wapewe fursa ya kufanya hivyo, ili mradi wahakikishe kuwa maandamano yao ni ya amani, kama inavyotaka sheria. Sioni tatizo iwapo maandamano ya wapinzani yatafanyika sambamba na maandamano ya hao wengine.
Kitu rahisi ni waandaaji wa maandamano ya aina zote kukaa na polisi na kukubaliana utaratibu wa maandamano hayo. Kwenye mji kama Dar es Salaam, kwa mfano, wapinzani wanaweza kufanya maandamano yao Kinondoni, na hao wengine wakafanya maandamano yao Ilala. Sio lazima maandamano ya aina mbali mbali yafanyike katika mtaa huo huo na wakati huo huo. Jambo la msingi ni kutafuta namna ya kuwawezesha watu kuandamana kwa amani, kama katiba na sheria zinavyotamka.
Waandaaji wanaweza kujipanga kuhakikisha kuwa maandamano yao ni ya amani. Kwa mfano, waandaaji wa maandamano wanaweza kuwateua viongozi wengi wa maandamano. Kila kiongozi atakuwa na watu wake, kama vile kumi au hata ishirini, ambao ana wajibu juu yao, Hao wanakuwa pamoja wakati wa maandamano. Na kiongozi mwingine anakuwa na watu wake. Hata wakiwa waandamanaji elfu tano, hii inawezekana. Ninachopendekeza hapa ni utaratibu kama ule wa nyumba kumi kumi alioanzisha Mwalimu Nyerere, ambapo kila nyumba kumi zina kiongozi wake.
Sababu ya kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa maandamano hayaingiliwi na watu wasiohusika, kama vile vibaka. Wakati huo huo, polisi wawepo kusaidia kutoa ulinzi, kama inavyotaka katiba na sheria.
Maandamano ni haki ya wananchi wote. Ni muhimu kwamba tutafute kila njia ili kuhakikisha haki zisihujumiwe. Badala ya kuzuia maandamano na kuwatisha watu, jambo ambalo linajenga uhasama katika jamii, naona ni bora kukaa na kutafuta njia ya kuwezesha watu kutekeleza uhuru na haki zao na papo hapo kuhakikisha kuwa amani inadumishwa. Ninaamini kuwa hayo yote yanawezekana. Kwa ki-Ingereza tungesema kuwa hayo malengo mawili sio "mutually exclusive."
Sunday, August 28, 2016
Kimya (Muyaka bin Haji)
"Kimya kina mshindo mkuu," || ndivyo wambavyo wavyele.
Kimya chataka k'umbuu, || viunoni mtatile:
Kimya chataka k'umbuu, || viunoni mtatile:
Kimya msikidharau, || nami sikidharawile.
Kimya
kina mambo mbele
Tahadharini na kimya.
Kimya ni kinga kizushi || kuzukia wale wale.
Kimya kitazua moshi || mato msiyafumbule.
Kimya kina mshawishi || kwa daima na milele.
Kimya kina
mambo mbele:
Tahadharini
na kimya.
Kimya vuani maozi || vuani mato muole!
Kimya kitangusha mwanzi || mwendako msijikule.
Kimya chatunda p'um'zi || kiumbizi kiumbile!
Kimya kina
mambo mbele:
Tahadharini
na kimya.
(Muyaka bin Haji, 1776-1840)
Subscribe to:
Posts (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Ukizunguka mitaani Dar es Salaam, utakuta matangazo mengi ya waganga wa kienyeji. Waganga hao wanatoka sehemu mbali mbali, kama vile Sumbaw...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Jina la Shaaban Robert ni maarufu miongoni mwa wa-Tanzania na wengine wa nchi zingine wanaokijua ki-Swahili. Lakini, tujiulize ni wa-Tanza...