Sunday, September 11, 2016

Umuhimu wa Kusoma Vitabu

Kusoma vitabu kuna manufaa mengi kwa mtu binafsi na kwa jamii. Tunaweza kuitafakari kauli hii kwa namna nyingi. Binafsi, daima ninakumbuka usemi wa Ernest Hemingway, "There is no friend more loyal than a book," yaani hakuna rafiki wa kweli kuzidi kitabu. Ni kauli fupi na rahisi kukumbukwa, lakini ninaiona kuwa yenye ukweli kabisa.

Kitabu ni rafiki ambaye yuko kwa ajili yako muda wowote unapomhitaji. Kitabu kinaweza kuwa mshauri wako, kiongozi wako, nguzo ya kuitegemea.

Akili ya binadamu inahitaji matunzo, sawa na bustani. Bustani inahitaji kurutubishwa na kupaliliwa. Ikiachwa ivamiwe na magugu, inageuka kichaka. Kusoma vitabu ni kurutubisha akili na kuipalilia. Kama mtu anaweza, ni muhimu kusoma vitabu vya aina mbali mbali: vya siasa, saikolojia, fasihi, sayansi, maisha ya watu maarufu, falsafa, historia, uchumi, na kadhalika.

Ni makosa kudhani kuwa kusoma vitabu kunawahusu wanafunzi na waalimu pekee. Kila mtu anapaswa kusoma vitabu. Tutafakari manufaa yake kwa afya ya akili ya binadamu kama yalivyoelezwa kwa ufupi katika makala hii. 

Saturday, September 10, 2016

Mashairi Mawili ya Edmund Spencer

Edmund Spencer ni mmoja kati ya washairi maarufu kabisa katika ki-Ingereza. Alizaliwa London mwaka 1552, akafariki 1599. Ni sahihi kusema kwamba shairi maarufu kabisa la Edmund Spencer ni utenzi uitwao "The Faerie Queene." Lakini Edmund Spencer ni maarufu pia kwa utunzi wa mashairi ya muundo wa "sonnet." Mwanatamthilia Shakespeare, ambaye alizaliwa mwaka 1564 na kufariki mwaka 1616, naye alikuwa mtunzi maarufu wa "sonnet."

Hapa naleta "sonnet" mbili za Edmund Spencer ambazo zinabainisha sanaa ya mshairi huyu. Ki-Ingereza cha mashairi haya ni cha zama zile, lakini ukikisoma kwa utulivu na umakini, utakielewa.

Katika "Ye Tradefull Merchants," mshairi anawasuta wafanya biashara wanaosafiri mbali kutafuta utajiri. Anawaambia kuwa mpenzi wake ana utajiri wa uzuri kuliko hata vito wanavyovihangaikia hao wafanya biashara. Utajiri wa mpenzi huyo si tu wa kimaumbile, bali pia akili.

Katika "Trust Not the Treason," mshairi anatahadharisha kuhusu ghilba na udanganyifu wa mwanamke, tusije tukanaswa katika mitego ya  mwenye ghilba na udanganyifu, kwani mitego hiyo huwa kama ndoana ya dhahabu ambayo imebeba chambo cha kuwanasia samaki wajinga, na mwisho wake ni balaa. Sherti niseme kuwa, kwa mtazamo wa leo, wengi tunakerwa na dhana hii ya kwamba mwanamke ni chanzo cha matatizo.

Sio jambo jema kuuwasilisha utungo wa fasihi kwa muhtasari. Ni kosa lililojadiliwa kinaganaga katika insha maarufu ya Cleanth Brooks, "The Heresy of Paraphrase," ambayo imo katika kitabu chake kiitwacho The Well Wrought Urn. Utungo wa fasihi unajieleza wenyewe kikamilifu. Ni lazima kuusoma wote kikamilifu na kwa umakini. Muhtasari ni hujuma dhidi ya utungo.

Nimalizie kwa kusema kuwa ninavutiwa na wazo la kuyatafsiri mashairi haya kwa ki-Swahili, kama chemsha bongo. Si kazi rahisi, lakini inavutia.
--------------------------------------------------------------------------------------------------

(1) YE TRADEFULL MERCHANTS

Ye tradefull merchants, that with weary toyle,
Do seeke most pretious things to make your gain,
And both the Indias of their treasures spoile,
What needeth you to seeke so farre in vaine?
For loe! my love doth in her selfe containe
All this worlds riches that may farre be found:
If saphyres, loe! her eies be saphyres plaine;
If rubies, loe! hir lips be rubies sound;
If pearles, hir teeth be pearls, both pure and round;
If yvorie, her forhead yvorie weene;
If gold, her locks are finest gold on ground;
If silver, her faire hands are silver sheene:
     But that which fairest is but few behold,
     Her mind, adornd with vertues manifold.


(2) TRUST NOT THE TREASON

Trust not the treason of those smyling lookes,
Until ye have theyr guylefull traynes well tryde:
For they are lyke but unto golden hookes
That from the foolish fish theyr bayts do hyde:
So she with flattring smyles weake harts doth guyde
Unto her love, and tempte to theyr decay;
Whome, being caught, she kills with cruell pryde,
And feeds at pleasure on the wretched pray.
Yet even whylst her bloody hands them slay,
Her eyes looke lovely, and upon them smyle,
That they take pleasure in her cruell play,
And, dying, doe themselves of payne beguyle.
     O mighty charm! which makes men love theyr bane,
     And thinck they dy with pleasure, live with payne.

Friday, September 9, 2016

Nimeanza Kufundisha Leo

Jana tumeanza muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf, nami nimeanza kufundisha leo. Masomo yangu kwa muhula huu ni matatu: First Year Writing, African Literature, na Muslim Women Writers.

Tumeanza vizuri. Nimepata fursa ya kuwaeleza wanafunzi mambo ya msingi kuhusu falsafa yangu ya ufundishaji, na kuhusu masomo. Nimesisitiza wajibu wa kufikiri na kuchambua masuala, wajibu wa kujenga hoja. Nimesisitiza msimamo wangu wa kulinda na kutetea uhuru wa fikra na kujieleza. Nimewahahakishia wanafunzi kuwa wawe tayari kukabiliana na fikra na hoja mbali mbali.

Siku ya kwanza ya muhula ni kama kitendawili. Hatujui safari itakuwaje, siku hadi siku, lakini tunategemea matokeo mema. Ingawa uzoefu wangu wa kufundisha unaendelea kuongezeka muda wote, haiwezekani kupanga na kuwa na uhakika nini kitatokea. Jambo pekee lisilobadilika ni kwamba kila muhula ni tofauti na mwingine.

Thursday, September 8, 2016

Wasomaji Wangu Wa Nebraska Waendao Tanzania

Nina jadi ya kuwaongelea wasomaji wangu katika blogu hii, kama njia ya kuwaenzi. Ni jambo jema kwa mwandishi kufanya hivyo. Leo ninapenda kuwakumbuka wasomaji wangu wa sinodi ya Nebraska ya Kanisa la Kiluteri la Marekani, ambao tangu zamani wamekuwa na programu ya kupeleka watu Tanzania kuendeleza uhusiano baina yao na wa-Luteri wa Tanzania.

Hao wasafiri, sawa na wenzao wa sinodi zingine za Marekani, wamekuwa wakitumia kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika kujiandaa kwa safari, ili kuzielewa tofauti za tamaduni za Marekani na Afrika. Ni elimu muhimu katika ulimwengu wa utandawazi wa leo, ambayo nje ya ufundishaji wa darasani, ninashughulika nayo.


Wakati huu ninapoandika, waumini wa Nebraska wanajiandaa kwa safari ya Tanzania, ambayo itafanyika mwezi Februari mwaka 2017. Wameitangaza safari hii mtandaoni, na mratibu mojawapo wa safari, Martin Malley, ameniandikia ujumbe leo akisema, "We still recommend your book." Katika ukurasa wa 16 wa chapisho la maelezo na maandalizi ya safari, kitabu hicho kimetajwa.

Ninapowakumbuka wasomaji wangu wa Nebraska, ninakumbuka nilivyokutana katika uwanja wa ndege wa Amsterdam na kikundi cha watu wa Nebraska waliokuwa wanakwenda Tanzania, tukasafiri pamoja. Mimi sikuwajua, ila wao walinitambua, kama nilivyoelezea katika blogu yangu ya ki-Ingereza.


Tuesday, September 6, 2016

Tamko la ACT-Wazalendo Kuhusu Hali ya Nchi

Tamko Rasmi la Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo kuhusu HALI YA NCHI
Dar Es Salaam, Jumanne, 06 Septemba 2016
Utangulizi
Jana Jumatatu, 5 Septemba 2016, Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo ilikutana katika kikao chake cha kawaida. Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilipokea, kujadili na kuidhinisha Taarifa kuhusu HALI YA NCHI. Taarifa hii sasa inatolewa rasmi kwa umma. Taarifa ipo katika maeneo makubwa manne: Hali ya kisiasa, hali ya kiuchumi, umoja wa kitaifa na hitimisho.
Hali ya Kisiasa
Kamati Kuu imezingatia kuwa Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeanisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Hata hivyo, katika awamu hii ya tano, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kuzuia shughuli za siasa kwa kutumia nguvu ya Jeshi la Polisi na hata Jeshi la Wananchi. Kwa mujibu wa serikali ya CCM, shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani inapaswa kukoma mapema baada ya uchaguzi. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi.
Kisiasa, tunatambua kwamba Viongozi wa CCM wamepoteza mvuto kwa wananchi na sasa wanamsukuma Mwenyekiti wao Rais Magufuli kutumia jeshi katika kuokoa taswira ya Chama cha Mapinduzi mbele ya umma.
Kwa kuzingatia hali ya kisiasa nchini kwa sasa, Kamati Kuu ya chama chetu:
i) Tunalaani na kupinga kwa nguvu zetu zote hatua za Serikali ya Chama cha Mapinduzi za kuvunja Katiba na kujaribu kuweka pembeni utawala wa sheria.
ii) Tunapinga vitendo vinavyozidi kushamiri katika serikali hii ya CCM ya kujaribu kuendesha nchi kwa ubabe na matamko ya viongozi badala ya utawala wa sharia.
iii) Tutasimama imara, na tutaungana na vyama vingine vya siasa pamoja na taasisi zingine za kiraia katika kulinda mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa maoni, na utawala wa sheria katika nchi yetu
Hali ya Kiuchumi
Katika miaka 10-15 iliyopita, nchi yetu imejenga uchumi ambao umekuwa ukikua kwa kiwango cha asilimia 6-7 kwa mwaka katika kipindi chote hiki. Ukuaji huu wa uchumi ulitokana na juhudi za nchi katika kuvutia wawekezaji na kuchochea shughuli za uzalishaji mali kwa wananchi wenye kipata cha chini. Awamu ya tano ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi imerithi changamoto ya uchumi unaokua bila kuwafaidisha wananchi wa kawaida. Hili ndilo tulitegemea Serikali mpya ishughulike nalo.
Kamati Kuu imeshtushwa na hali ya kuanza kudorora kwa shughuli za uchumi katika kipindi cha miezi kumi ya utawala wa awamu ya tano. Kwa mfano:
a) Taarifa za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake (Quarterly Economic Review na Monthly Economic Review) kwa robo ya mwisho ya mwaka 2015 (Oktoba – Desemba 2015 ) zinaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilikuwa 9%. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 (Januari – Machi 2016) kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilishuka hadi kufikia 5.5%. Kiuchumi, hii inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Magufuli umepungua kwa 4%.
b) Shughuli za uchumi zinazohusu wananchi masikini zimeshuka kutoka kasi ya ukuaji ya 10.20% robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 2.7% katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita. Hii ina maanisha kwamba Wananchi wetu wanazidi kudumbukia kwenye ufukara kwa kasi tangu awamu ya tano ya Serikali ya Chama Mapinduzi iingie madarakani
c) Ukuaji wa sekta ya ujenzi katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 ilikuwa 13.8% lakini ukuaji wa sekta hii katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ilikuwa ni 4.30%, ikiwa ni tofauti ya takribani -10%. Hii ni kwa sababu uwekezaji katika sekta hii umeanza kushuka.
d) Kasi ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji imeporomoka kutoka kukua kwa 14.50% robo ya mwisho ya 2015 mpaka kukua kwa 7.9% robo ya kwanza ya 2016, ikiwa ni kuporoka kwa 7% katika kipindi cha miezi 6 tu ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli. Kuporomoka kwa sekta ya usafirishaji itaathiri watu wengi, wakiwemo madereva, matingo, pamoja na mama Ntilie wanaowauzia chakula. .
Kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya uchumi katika nchi, Kamati Kuu:
a) Tunaitaka serikali izingatie sayansi ya uchumi katika kuendesha uchumi wa nchi. Uamuzi wa CCM wa kuitelekeza serikali yake kwa mwanasiasa mmoja anayedhani ndiye anayejua kila kitu na yeye kugeuka kuwa mshauri wa washauri wa uchumi itasambaratisha uwekezaji nchini na kuua kabisa juhudi za miaka 20 za kuvutia wawekezaji na kujenga uchumi shirikishi.
b) Inahimiza wananchi kuzingatia kuwa msingi wa uchumi wetu ni uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Msingi wa kuvutia wawekezaji ni utawala wa sheria. Juhudi za serikali ya CCM za kuua utawala wa sheria zitaua uwekezaji na kuangamiza uchumi wa nchi. Tusirihusu CCM iue uchumi wa nchi kwa maslahi yake ya kisiasa na viongozi wake.
Umoja wa Kitaifa
Nchi yetu imefanya juhudi kubwa katika miaka 50 iliyopita katika kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuhakikisha kuwa makabila, dini na baadaye vyama vya siasa tunaishi bila kukamiana. Juhudi za dhati za kupambana na ubaguzi ndiyo umekuwa msingi imara wa kujenga Umoja wa Kitaifa na amani tunayojivunia.
Hata hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa utawala mpya wa Serikali ya CCM, kupitia Mwenyekiti wake mpya na Rais wa Jamhuri wa Muungo, umeanza kwa juhudi na kasi kubwa kuchokonoa na kumomonyoa misingi ya utaifa na umoja wetu. Sasa tunaye Rais asiyechagua maneno na asiyejua aongee nini na wapi. Vijana waliosoma kwa bidii katika mazingira ya shule zilizotelekezwa na serikali ya CCM anawaita VILAZA.
Katikati ya uhasama mkubwa wa kisiasa na kijamii huko Zanzibar Rais wetu amefunga safari, sio kujaribu kutibu majeraha yaliyosababishwa na kuchezewa kwa sanduku la kura, bali kuchochea uhasama chini ya ulinzi wa vyombo vyetu vya dola vyenye jukumu la kulinda na kudumisha amani. Sasa Rais wetu, kupitia kauli zake, ameanza kuubomoa muungano wetu uliojengwa kwa unyenyekevu na katika mazingira magumu.
Kila asimamapo kuhutubia, jambo moja la kutarajiwa kutoka katika kinywa cha Rais wetu ni matamshi yanayodhoofisha nguzo fulani ya umoja, mshikamano na undugu wetu kama taifa. Yote haya yakitokea chama chake cha CCM ama kimekaa kimya au kinachekelea. Inasikitikitisha kwamba Chama kilichoasisiwa na Mwalimu Nyerere kinamruhusu kiongozi wake kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na kuchochea chuki katika jamii ya watanzania.
Kwa kuzingatia mtikisiko mkubwa katika umoja na mshikamano wa kitaifa unaoendelea nchini, Kamati Kuu:
a) Tunalaani juhudi zinazofanywa na Serikali ya CCM kupitia Mwenyekiti wao za kuchochea chuki katika jamii ya watanzania na kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na amani ya nchi
b) Tunatoa wito kwa watanzania wote waipendayo nchi yao kusimama kidete katika kulinda misingi ya nchi yetu na kukataa chuki inayoanza kujengwa na utawala wa CCM
c) Tunatoa wito wa kipekee kwa viongozi wetu wa dini na wakuu wa nchi waliopita, hususani Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na Mzee Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na wazee wengine wanaoheshimika katika nchi yetu wavae ujasiri wa kumuonya Mwenyekiti wa CCM kuwa juhudi zake za kuchochea chuki katika jamii yetu ya watanzania zitasambaratisha Taifa letu.
Hitimisho
i) Sisi kama chama cha siasa, tunaendelea kusisitiza kuwa tutaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kupambana na ufisadi na kujenga uwajibikaji nchini.
ii) Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa kuheshimu na kulinda demokrasia na kuzingatia utawala wa sheria nidyo msingi wa mapambano dhidi ya ufisadi. Tunasisitiza kuwa mtu yeyote, wa kawaida au kiongozi, anayesema kwamba anaweza akapambana na ufisadi kwa kukanyaga misingi ya demokrasia na utawala wa sheria mtu huyo ni mwomgo na kwa kweli ni fisadi na anataka kujenga himaya mpya ya ufisadi. Mtu huyo, pamoja na mambo yake yote, yafaa akataliwe na kudharauliwa haraka!
iii) Tunasisitiza kuwa msingi wa uchumi wetu ni kuvutia uwekezaji wa ndani nan je ya nchi. Kuzingatia utawala wa sheria ndiyo msingi wa kuvutia uwekezaji. Juhuzi za hivi karibuni za serikali ya CCM za kujaribu kuua utawala wa sharia ni juhudi ovu za kuua uchumi wa nchi yetu. TUZIKATAE juhudi za kuua utawala wa sheria kwa kuwa zitaangamiza taifa letu kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kiongozi wa Chama
Dar es Salaam, Jumanne 6 Septemba 2016.

Sunday, September 4, 2016

Naomba Kitabu Changu Kipigwe Marufuku

Naiomba serikali ikipige marufuku kitabu changu, CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Kitabu hiki kina mawazo ambayo ni kinyume na yale yanayotakiwa na serikali. Kama vile hii haitoshi, kitabu hiki ni cha uchochezi. Tusikubali kurudia makosa kama yale ya kale ambapo Socrates alikuwa anawachochea watu, hasa vijana, wahoji mambo yanayokubalika katika jamii.

Imenibidi nitoe ombi hili la kupigwa marufuku kitabu changu kwa sababu za msingi. Kwanza kama mtu mwingine yeyote mtiifu kwa serikali, ninatambua wajibu wangu wa kuripoti jambo lolote linalokwenda kinyume na maelekezo au matakwa ya serikali. Pili, mimi sina mamlaka kisheria ya kukipiga marufuku kitabu chochote. Kwa hivi, ninaiangukia serikali.

Mawazo yaliyomo katika kitabu hiki yasipodhibitiwa, yakiachwa yaenee, yatajenga ukaidi miongoni mwa raia na tabia ya kutowaheshimu viongozi. Ninaelewa kuwa ni juu ya serikali kufikiri na kufanya maamuzi. Wajibu wa raia ni kutii. Raia wakiachwa huru kufikiri na kujiamulia mambo, kuna hatari kwamba misingi imara ya amani na utulivu nchini itaharibika na itakuwa vigumu kwa nchi kutawalika.

Saturday, September 3, 2016

Shakespeare Ametawala Mawazo Yangu Leo

Leo Shakespeare ametawala mawazo yangu, nami ninapenda kuelezea ilivyotokea. Ni maelezo yanayoweza kubainisha namna akili yangu inavyofanya kazi ninapohangaika kuandika makala ya kitaaluma.

Kwa miezi kadhaa, nimekuwa nikiwazia kuandika makala juu ya utangulizi wa The Dilemma of a Ghost, tamthilia ya Ama Ata Aidoo wa Ghana. Utangulizi huu umeitwa "Prelude" katika tamthilia hiyo, ambayo Ama Ata Aidoo aliitunga alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu Ghana, Legon, ambapo alihitimu mwaka 1963. Tamthilia yake iliigizwa kwa mara ya kwanza mwaka 1964 na kuchapishwa mwaka 1965.

Nimefundisha tamthilia hii mara kadhaa, na kwa miezi kadhaa nimepata hamu ya kuchambua utangulizi wake, yaani "Prelude." Nimeona kwamba hakuna mhakiki yeyote ambaye ameichambua sehemu hii ya tamthilia hii kwa kiwango kinachoniridhisha. Hii "Prelude" si rahisi kuifafanua. Ninahisi hii ndio sababu ya wachambuzi kuiacha kando.

Katika kuitafakari hii "Prelude," nimeona kuwa ujuzi wangu wa taaluma ya "Folklore" utakuwa nyenzo muhimu. Vile vile, nimeona kuwa italazimu kugusia jadi ya tamthilia ya nchi za Magharibi kuanzia Ugriki ya zamani.

Ni katika kuwazia jadi hii ndio nikajikuta ninamkumbuka Shakespeare. Katika "Prelude" yake, Ama Ata Aidoo ametumia dondoo za lugha ambazo zinatupeleka kwa Shakespeare. Sishangai, nikizingatia kuwa Ama Ata Aidoo alisomea ki-Ingereza na fasihi katika mfumo wa elimu wa ukoloni wa ki-Ingereza. Kwa maana hiyo, Ama Ata Aidoo alilelewa katika mfumo ambao walilelewa waandishi wa enzi zake, na waliofuatia, kama vile Efua Sutherland, Wole Soyinka, na James Ngugi, ambaye baadaye alibadili jina na kujiita Ngugi wa Thion'go.

Baada ya kujiridhisha kwamba kuna athari za Shakespeare katika "Prelude" ya The Dilemma of a Ghost, ndipo nikawa nawazia kutafuta ushahidi katika tamthilia za Shakespeare. Kwa miezi yote hii, nilikuwa na uhakika kwamba baadhi ya athari zimetoka katika tamthilia kadhaa na pia mashairi ya Shakespeare, na baadhi ya athari nilihisi zilitokana na au tamthilia ya The Merchant of Venice au Hamlet.

Kwa hivi, leo nimeteremsha kabatini buku langu kubwa liitwalo The Yale Shakespeare, ambalo lina tamthilia zote za Shakespeare na mashairi yake yote. Kila tamthilia imetanguliwa na insha iliyoandikwa na mchambuzi mahiri na imeambatana na maelezo ya dhana, misemo na maneno ambayo watumiaji wa leo wa ki-Ingereza inaweza kuwawia vigumu kuelewa.

Kwa miezi kadhaa, kabla ya kuanza kufukuafukua maandishi ya Shakespeare leo, nimekuwa nikitafakari vipengele vya "Folklore" ambavyo ninavyoviona katika "Prelude." Pia nimekuwa nikitafiti zaidi vipengele hivyo, kwa kufuatilia maandishi ya wataalam kama William Bascom. Sina shaka kwamba tafakari hiyo na utafiti vitaniwezesha kuifafanua "Prelude" na matumizi ya "Folklore" katika tamthilia nzima ya The Dilemma of a Ghost.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...