Thursday, October 1, 2015

Kwa Wanadiaspora: Fursa ya Kuitangaza Tanzania

Naandika ujumbe huu kwako mwanadiaspora mwenzangu, kuelezea mradi ambao nimehusika nao, wa kitaaluma na wenye fursa ya kuitangaza Tanzania. Mradi huo ni filamu juu ya mwandishi maarufu Ernest Hemingway, ambaye aliwahi kutembelea nchi yetu na Afrika Mashariki kwa ujumla mwaka 1933-34 na 1953-54.

Kutokana na safari hizo, Hemingway aliandika vitabu, hadithi, insha, na barua. Maandishi hayo ni hazina, kwa jinsi yanavyoitangaza nchi yetu, iwapo tutaamua kuwa makini katika kuyatumia. Mfano ni hadithi ambayo wengi wamesikia angalau jina lake, "The Snows of Kilimanjaro."

Nilifanya utafiti wa miaka kadhaa juu ya mwandishi huyu, hatimaye nikatunga kozi, Hemingway in East Africa. Nilisafiri na wanafunzi wa ki-Marekani kwenda Tanzania, tukatembea katika baadhi ya maeneo alimopita Hemingway, huku tukisoma maandishi yake.

Kozi hii imemhamasisha Jimmy Gildea, mmoja wa wanafunzi hao, kutengeneza filamu, Papa's Shadow. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliye hai. Tunaongelea umuhimu wa Afrika katika maisha, safari, uandishi, na fikra za Ernest Hemingway. Filamu inaonyesha sehemu mbali mbali alimopita Hemingway, kama vile Longido, Arusha, Mto wa Mbu, Karatu, na Babati, na hifadhi kama Serengeti na Ngorongoro. Inaonyesha pia wanafamilia wa mtengeneza filamu wakipanda Mlima Kilimanjaro.

Filamu imekamilika, na mimi nimeiangalia, nikaipenda sana. Lakini, kwa mujibu wa taratibu na sheria, inatakiwa kulipia gharama kadhaa kabla haijaonyeshwa au kusambazwa. Kuna kampeni ya kuchangisha fedha, na mimi ni mchangiaji mojawapo. Zinahitajika dola 10,000, kama inavyoelezwa hapa.

Tofauti na miaka iliyopita, wanadiaspora tunatajwa na serikali ya Tanzania siku hizi kwa sababu tunapeleka fedha ("remittances"). Ni mchango muhimu kwa uchumi wa nchi yetu. Lakini huu mradi ninaoelezea hapa ni njia nyingine ya kuifaidia Tanzania. Filamu hii, mbali ya kuelimisha juu ya Hemingway, ni kivutio kwa watalii. Nasema hivi kwa kuwa najua namna jina la Hemingway na maandishi yake yanavyotumiwa na wenzetu sehemu zingine za dunia ambako Hemingway alipita au kuishi. Mifano ni miji kama vile Paris (Ufaransa) na Pamplona (Hispania), na nchi ya Cuba. Wanapata watalii wengi sana.

Hiyo ninayoelezea hapa ni fursa kwetu wanadiaspora wa Tanzania. Tukishikamana na kuchangia filamu hii hata hela kidogo tu kila mmoja wetu, tutasaidia kumalizia kiasi kinachobaki. Imebaki wiki moja tu na kidogo. Ukitaka, tafadhali tembelea na toa mchango wako hapa katika tovuti ya Kickstarter.

Monday, September 28, 2015

Kampeni za CCM Mwaka Huu

Najaribu kutafakari picha hii iliyopigwa katika moja ya mikutano ya kampeni za uchaguzi zinazoendelea Tanzania. Ina maana kwamba mwenye uwezo wa kupiga "push-up" nyingi ndio anafaa kuwa kiongozi? Je, ili uukwae ubunge, unatakiwa upige angalau "push-up" ngapi? Udiwani je? Na ili uwe waziri, unahitaji "push-up" ngapi? Na kwa uwaziri, ni sahihi tuwe na "push-up" tu au na kuruka viunzi pia? Na kwa kuzingatia uzito wa cheo cha uwaziri, kwa nini tusiongezee pia uwezo wa kunyanyua matofali angalau manne ya zege? Kwa kweli, tukifanya hivyo, tutapata serikali imara kabisa.

Sunday, September 27, 2015

Tumechangia Kanisa la Venezuela

Leo kanisani kwetu hapa mjini Northfield, kanisa Katoliki, tulikuwa na padri ambaye anatumikia kanisa fulani nchini Venezuela. Huyu padri ni m-Marekani, na kwa miaka yapata arobaini, mapadri wa-Marekani wamekuwa wamisionari katika kanisa hilo la Venezuela. Hata paroko wetu aliwahi kutumikia kanisa hilo kwa miaka mitano. Ananivutia kwa jinsi anavyoijua lugha ya ki-Hispania, na anawahudumia waumini hapa Northfield wanaotumia lugha hiyo.

Huyu padri mgeni alitoa mafundisho mazuri, na katika kuelezea utume wake Venezuela alituhimiza kwa maneno matatu: "Pray, say, pay." Alifafanua kwamba tusali kuwaombea waumini wa kanisa lile la Venezuela, tuwaeleze wengine kuhusu hali halisi na mahitaji ya kanisa lile, na tutoe mchango kulisaidia kanisa lile.

Niliguswa na maelezo yake, nikangojea muda wa kutoa mchango. Kilipopitishwa kijikapu cha mchango, nilikuwa tayari nimekwangua vijihela vilivyokuwemo katika pochi yangu nikavitumbukiza humo. Nilijisikia faraja na furaha kwamba vijihela hivyo vitakuwa na manufaa kwa kanisa lile la Venezuela, hasa kwa kuzingatia kuwa dola, hata zikawa chache, zinakuwa ni hela nyingi kwenye nchi kama Venezuela au Tanzania.

Mimi kama muumini wa dini, naiheshimu dini yangu, na dini zote. Ninafahamu kwamba zote ni njia wanazotumia wanadamu kuelekea kwa Mungu. Ni safari, kama safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro. Kuna njia kadhaa za kufikia kileleni Kilimanjaro. Na itakuwa ni wendawazimu kwa watu wanaochukua njia tofauti kuanza kugombana na kupigana hadi kuuana kwa msingi wa tofauti za njia wanazochukua. Kwa mtazamo wangu, ni wendawazimu kwa watu wa dini mbali mbali kubezana au kugombana.

Ninaziheshimu nyumba za ibada za kila dini. Niliwahi kuelezea katika blogu hii nilivyozuru nyumba za ibada za wa-Hindu, nchini India. Leo nimechangia kanisa lililoko Venezuela. Lakini sibagui. Kuna wakati niliona taarifa kuwa wa-Islam wa sehemu fulani Tanzania walikuwa wanachangisha fedha za kukarabatia msikiti wao. Nilipeleka mchango wangu, kwa moyo mkunjufu, ingawa mimi si mu-Islam bali m-Katoliki. Nitaendelea kufanya hivyo.

Ninachojali ni kuwa wanadamu wote wameumbwa na Mungu, na Mungu hana ubaguzi, kama nilivyoandika katika blogu hii. Ninafurahi kumiliki blogu, kitu ambacho kinaniwezesha kueneza mawazo yangu na kupambana na mawazo ambayo nayaona ni sumu, hata kama yanaenezwa kwa jina la dini.

Saturday, September 26, 2015

Nimehojiwa Kuhusu Hemingway na "Papa's Shadow"

Leo nimekuwa na mahojiano na mwandishi wa gazeti la Manitou Messenger linalochapishwa hapa chuoni St. Olaf. Ni gazeti la wanafunzi, ambalo limekuwa likichapishwa kila wiki kwa miaka 125. Mahojiano yetu yalikuwa juu ya filamu ya Papa's Shadow. Katika ujumbe wa kuomba mahojiano, mwandishi aliandika:

...we are doing a feature article this week on the documentary, Papa's Shadow and Ramble Pictures. We learned that you were instrumental in the inspiration for and production of this film, and we were hoping you could answer a few quick questions.

Katika mahojiano, tumeongelea nilivyoanza kuvutiwa sana na mwandishi Ernest Hemingway, nilipoombwa na Thomson Safaris kuongoza msafara mkubwa wa wanafunzi, wazazi na walimu, katika safari ya Tanzania mwaka 2002. Hatimaye, baada ya miaka mitano ya kusoma maandishi na habari za Hemingway, nilitunga kozi Hemingway in East Africa, kwa ajili ya Chuo cha Colorado.

Baadaye, niliona niunde kozi hiyo kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo cha St. Olaf. Nilifanya hivyo mwaka 2012. Wakati wa kuandikisha wanafunzi, alinifuata kijana aitwaye Jimmy Gildea, akaniomba nimruhusu kujiunga na kozi, kwa kuwa alimpenda Hemingway na alitaka kurekodi filamu ya kozi. Nilimsajili katika darasa.

Kozi ilikwenda vizuri, kama nilivyoandika hapa. Baada ya kurejea tena Marekani, baadhi yetu tulifunga safari ya jimbo la Montana kuonana na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway. Tuliongea naye sana.

Jimmy alikuwa amenirekodi ofisini mwangu nikizungumza juu ya Hemingway, akachanganya mazungumzo haya na yale tuliyofanya na Mzee Patrick Hemingway,na akaongezea mambo mengine aliyorekodi Tanzania. Kwa bahati nzuri, tulipomaliza kozi, familia ya Jimmy walikuja kumchukua wakaenda kupanda Mlima Kilimanjao. Papa's Shadow inaonyesha safari yao ya kupanda mlima. Ni rekodi nzuri sana. Ninaamini itawavutia watalii.

Kuna mambo mengine niliyomwambia huyu mwandishi wa Manitou Messenger. Hasa, nilisisitiza azma yangu ya kuendelea kufanya kila juhudi kuuelimisha ulimwengu juu ya namna Hemingway alivyoipenda Afrika na namna maisha yake na fikra zake zlivyofungamana na Afrika. Nilimwambia pia kuwa Jimmy ni mfano murua wa kuigwa na wahitimu wengine wa vyuo. Alifuata na anaendelea kufuata anachokipenda moyoni mwake, yaani kutengeneza filamu za kuelimisha. Yeye na vijana wenzake katika Ramble Pictures wanajituma kwa roho moja katika shughuli zao na hawatetereshwi na magumu au vipingamizi vyovyote.

Thursday, September 24, 2015

"Papa's Shadow" Yapongezwa na Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa

Tarehe 20 mwezi huu nilipeleka ujumbe Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa kuhusu filamu ya Papa's Shadow. Sikuandika ujumbe mrefu, bali niliwatumia kiunganishi hiki.

Bila kuchelewa, tarehe 22 nilipata ujumbe kutoka kwao, ukiwa umeandikwa na Ndugu Noel Kabanda. Uwakilishi unaafiki kuwa Papa's Shadow ni "fursa maridhawa ya kuitangaza Tanzania ulimwenguni" na unasisitiza kuwa "Serikali inatambua mchango wa sanaa katika kuitangaza Tanzania katika sekta mbali mbali ikiwemo utalii na utamaduni."

Kwanza, kwa kuzingatia uwingi wa majukumu yanayowakabili wawakilishi wetu katika balozi zetu, nimeona ni muhimu kusema nilivyoguswa na jinsi Uwakilishi ulivyoushughulikia ujumbe wangu.

Pili, ujumbe wa Uwakilishi unawatia moyo wahusika wa Ramble Pictures, ambao ndio watengeneaji wa Papa's Shadow. Timu nzima ya Ramble Pictures ni vijana wa ki-Marekani, na baadhi yao walikuja Tanzania mwaka 2013 kwenye kozi yangu ya Hemingway Katika Afrika Mashariki. Ni furaha kwangu, na jambo la kujivunia, kuwaeleza vijana hao kuwa Uwakilishi wa Kudumu waTanzania Umoja wa Mataifa umeipokea Papa's Shadow kwa namna hii.

Papa's Shadow si filamu ya maigizo. Ni filamu ya kuelimisha kuhusu mwandishi Ernest Hemingway. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ni maongezi baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliyebaki wa mwandishi Hemingway. Tunaongelea maisha ya Hemingway, safari zake, uandishi wake, na fikra zake kuhusu masuala mbali mbali. Tunawafungua macho walimwengu kuhusu namna Hemingway alivyoipenda Afrika na alivyokuwa mtetezi wa Afrika.

Hemingway alisafiri na kuishi Afrika Mashariki mara mbili, mwaka 1933-34 na 1953-54. Aliandika hadithi, insha, barua na maandishi mengine ambayo ni hazina kubwa. Wenzetu katika nchi zingine ambako Hemingway alipita au kuishi na akaandika habari za huko, wametumia fursa hiyo kujitangaza, na wanawavutia watalii wengi sana. Mifano ni miji kama Paris (Ufaransa), Havana (Cuba), Oak Park (Illinois, Marekani), Key West (Florida, Marekani), na Pamplona (Hispania). Hemingway anapendwa ulimwenguni kote ambako watu wana utamaduni wa kusoma vitabu. Sina shaka kuwa Papa's Shadow italeta msisimko wa aina hiyo kwa kuwaelekeza mashabiki wa Hemingway nchini kwetu.

Hamu ya kuona Tanzania inafunguka macho kuhusu fursa hii ilinihamasisha kufanya utafiti juu ya safari za Hemingway katika nchi yetu na maandishi aliyoandika. Kozi niliyotunga ilikuwa na lengo hili. Nilitaka pia kuwasaidia walimwengu kuelewa umuhimu wa Afrika katika maisha na uandishi wa Hemingway. Kwa msingi huo huo, nilishiriki kikamilifu katika kufanikisha filamu ya Papa's Shadow.

Nimeeleza hayo yote ili kuweka wazi umuhimu wa ujumbe wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa. Ni mfano wa mshikamano unaotakiwa baina yetu wanadiaspora, serikali, na wananchi wenzetu.

Tuesday, September 22, 2015

Nimenunua Kitabu cha Golding, "Lord of the Flies"

Zimepita siku nyingi kidogo tangu niandike ujumbe kuhusu vitabu nilivyonunua, au nilivyojipatia kwa namna nyingine. Viko vitabu kadhaa, hasa riwaya, ambavyo sikuvielezea.

Leo, baada ya kufundisha vipindi vyangu viwili, nilipita kwenye duka la vitabu la hapa chuoni. Niliangalia sehemu vinapouzwa vitabu kwa bei nafuu, nje ya duka, nikaona, kati ya vitabu vingi, kitabu cha William Golding, Lord of the Flies. Hapo hapo nilikumbuka miaka ya ujana wangu. Tulisoma kitabu hiki tulipokuwa kidatu tano Mkwawa High School, mjini Iringa. Huku nikikumbuka hayo yote, nilikinunua hima, ingawa nina hakika ninayo nakala nyingine niliyonunua zamani, ila itakuwa vigumu kuigundua ilipo katika utitiri wa vitabu vyangu.

Lord of the Flies ni riwaya niliyoipenda sana na ambayo ninaikumbuka sana. Ilinigusa kwa namna ya pekee kwa jinsi ilivyowachora wahusika, ambao ni watoto wa shule waliojikuta kwenye kisiwa peke yao baada ya ndege waliyokuwa wanasafiria kuanguka kisiwani humo na wao wakawa abiria pekee waliosalimika. Riwaya inaonyesha jinsi watoto hao, waliokulia katika jamii ya maadili na ustaarabu, walivyoanza kubadilika, wakawa wabaya na katili kupindukia.

Miaka ile, nilikuwa najikongoja katika uandishi wa hadithi fupi. Lord of the Flies ilinigusa kwa namna ya pekee, kwa ustadi wake wa kuelezea mazingira, ikachangia katika uandishi wa hadithi yangu, "A Girl in the Bus," ambayo ilichapishwa katika jarida la Busara. Hili lilikuwa ni jarida maarufu Afrika Mashariki, lililokuwa linachapishwa Nairobi.

Kuchapishwa kwa hadithi hii kulinipa furaha isiyoelezeka. Nilikuwa na mazoea ya kwenda katika maktaba ya mkoa Iringa, na daima nilikuwa napendezwa kuona jarida hili lenye hadithi yangu. Hata nilipoingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusoma, mwaka 1973, nilikuwa najisikia raha kuliona jarida hili  katika maktaba.

Lord-Flies of the Flies ni riwaya iliyowagusa watu ulimwenguni. Wanadamu kwa ujumla tunaamini kuwa watoto wana silika ya wema na usafi wa moyo. Wanafalsafa kama Jean-Jacques Rousseau walichangia kujenga imani hiyo. Lakini William Golding, katika riwaya yake hii ameelezea jinsi watoto wanavyobadilika na kuwa wabaya. Ni hadithi iliyowashtua walimwengu kwa namna ilivyoihoji dhana ya kwamba watoto ni kama malaika.

Nikizingatia kuwa Lord of the Flies ni moja kati ya riwaya maarufu kabisa katika lugha ya ki-Ingereza, nitaisoma kwa furaha, nikikumbuka ilivyonigusa enzi za ujana wangu. Miaka ilivyopita, nimesoma hadithi na tamthilia mbali mbali ambazo zimeelezea dhamira hii ya watu waliopotelea kwenye kisiwa mbali na walimwengu. Mifano ni The Odyssey ya Homer, Robinson Crusoe ya Daniel Defoe, na mashairi kadhaa ya Derek Walcott, kama vile "The Castaway." Hata baadhi ya wanafalsafa wa mkondo wa "existentialism" wameongelea uwepo wetu hapa duniani kwa kuufananisha na upweke wa watu waliotupwa na kusahauliwa. Ni dhamira ambayo imekuwa na mashiko ya pekee katika fikra na hisia za wanadamu.

Monday, September 21, 2015

Tafsiri ya Sala ya Papa Francis

Katika ujumbe wangu wa jana,niliweka sala ya Baba Mtakatifu Francis ya kuiombea dunia. Sala hii inagusia na kujumlisha mambo mengi, kama vile upendo kwa wanadamu wote na viumbe vyote bila mipaka, kuwajali wasiojiweza, kuyatunza na kuyaboresha mazingira.

Sala hii inatuelekeza kumwomba Mungu atupe ufahamu wa thamani ya kila kiumbe, ufahamu na namna maisha yetu yalivyofungamana na maisha ya viumbe vyote. Aidha, sala inathimiza kumtegemea Mungu katika juhudi zetu za kutafuta haki, upendo, na amani.

Katika sala hii kuna mafundisho muhimu ya dini mbali mbali, matarajio ya wanaharakati wa masuala mbali mbali ya jamii, na matarajio ya wanamazingira. Ni sala inayofundisha busara za zamani za jamii mbali mbali, kama vile wenyeji wa asili wa Amerika ("Native Americans"). Wazo lililomo katika sala hii la kuviangalia viumbe vyote kwa uchaji linanikumbusha falsafa ya mwandishi Shaaban Robert. Kati ya sentensi zinazonigusa kwa namna ya pekee katika sala hii ni,

All-powerful God, you are present in the whole universe
and in the smallest of your creatures.

Kuhitimisha maelezo yangu, napenda kusema kwamba sala hii ilivyo katika ki-Ingereza ikiwa imesheheni uchaji, busara, na maudhui, imeundwa kwa lugha iliyotukuka. Ninajiuliza iwapo tunaweza kuitafsiri kwa ki-Swahili, tukahifadhi utukufu wake kwa msingi wa uhalisia wa ki-Swahili. Ninajiuliza hivyo pamoja na kufahamu jinsi suala la tafsiri lilivyo gumu na tata. Ninatarajia kujaribu kuitafsiri sala hii siku zijazo.

A prayer for our earth

All-powerful God, you are present in the whole universe
and in the smallest of your creatures.
You embrace with your tenderness all that exists.
Pour out upon us the power of your love,
that we may protect life and beauty.
Fill us with peace, that we may live
as brothers and sisters, harming no one.
O God of the poor,
help us to rescue the abandoned and forgotten of this earth,
so precious in your eyes.
Bring healing to our lives,
that we may protect the world and not prey on it,
that we may sow beauty, not pollution and destruction.
Touch the hearts
of those who look only for gain
at the expense of the poor and the earth.
Teach us to discover the worth of each thing,
to be filled with awe and contemplation,
to recognize that we are profoundly united
with every creature
as we journey towards your infinite light.
We thank you for being with us each day.
Encourage us, we pray, in our struggle
for justice, love and peace.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...