Wednesday, October 19, 2016

Nimepata Vitabu Vipya vya Uislam

Leo nimepata vitabu kadhaa vya u-Islam kutoka kwa profesa Nadia Mohamed wa Minneapolis Community and Technical College. Huyu profesa, mzaliwa wa Misri, tulifahamiana mwaka jana. Muhula uliopita nilimwalika kutoa mhadhara katika darasa langu, Muslim Women Writers. Nilimwalika tena, na amekuja leo.


Katika vitabu alivyonipa leo, kuna nakala za Quran, yaani tafsiri tofauti. Kabla, nilikuwa na tafsiri mbili: moja ya Abdallah Yusuf Ali, yenye maelezo ya kina, ambayo nimekuwa nayo kwa miaka mingi, na ya pili aliyonipa Profesa Nadia Mohamed alipotembelea darasa langu muhula uliopita, kama nilivyoripoti katika blogu hii.

Lakini leo, amenipa The Message of the Quran, iliyotafsiriwa na kufafanuliwa na Muhammad Asad. Humo kuna Quran kwa hati ya ki-Arabu, na hicho ki-Arabu kipo pia kwa hati ya ki-Rumi. Na kuna tafsiri ya ki-Ingereza, pamoja na maelezo ya kina. Nakala ya Abdallah Yusuf Ali ina sura mbili: hati ya ki-Arabu na tafsiri ya ki-Ingereza.

Profesa Nadia Mohammed amenipa nakala zingine mbili za Quran, tafsiri ya Abdallah Yusuf Ali, ila ni tofauti na ile niliyokuwa nayo tangu zamani, kwa kuwa hii ni tafsiri tu bila yale maelezo. Hizi nakala ni vitabu vidogo kwa ukubwa, na kwa hivi ni rahisi kubebwa popote. Zinaonekana pichani hapa kushoto, zikiwa na majalada tofauti.

Kuna uzuri wa kuwa na tafsiri mbali mbali za Quran. Tunaambiwa kwamba ki-Arabu cha Quran ni cha pekee, sio rahisi kukitafsiri kwa lugha yoyote. Maneno yake mengi yana utajiri wa maana na ladha ambao ni mtihani mkavu kwa yeyote anayejaribu kutafsiri. Kutokana na ukweli huo, ambao unahusika pia katika tafsiri ya lugha yoyote, ni bora kusoma tafsiri mbali mbali. Nilimwambia hivyo Profesa Nadia Mohamed, ambaye ni mtaalamu, akaafiki.

















Vitabu vingine alivyonipa ni viwili vidogo vidogo. Kimoja kinaitwa A Brief Illustrated Guide to Understanding Islam na mtunzi ni I.A. Ibrahim. Cha pili ni Wisdom for Life & The Afterlife: A Selection of Prophet Muhammad's Sayings, ambacho ni mkusanyiko wa mafundisho ya Mtume Muhammad, yaliyotafsiriwa na Samir Saikali kwa ki-Ingereza, kutoka ki-Arabu, na kuchapishwa na Islamic Literacy Project.




Friday, October 14, 2016

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.


Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe
. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi
! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.

(CHANZO: Blogu ya Hapakwetu)

Monday, October 10, 2016

Ki-Ingereza Kama Lugha ya Ulimwengu

Jana, katika blogu hii, nilikiongelea kitabu cha Charles Derber, People Before Profit, ambacho kinahusu utandawazi. Katika kukisoma kitabu hiki, nilivutiwa na maelezo yake, na nikapata hamasa ya kufuatilia mada ya utandawazi kwa namna nyingine.

Nilikumbuka kwamba nina kitabu cha David Crystal, English as a Global Language, ambacho nilikinunua miaks michache iliyopita, ila nilikuwa nimekipitia juu juu tu. Leo nimeamua kukisoma, na ninaona jinsi maelezo yake kuhusu lugha ya ki-Ingereza yanavyofungamana na suala la utandawazi. Kwa mfano, katika utangulizi wake, mwandishi anasema,

"We have as yet no adequate typology of the remarkable range of language contact situations which have emerged as a consequence of globalization, either physically (e.g. through population movement and economic development or virtually (e.g. through Internet communication and satellite broadcasting)." (xi)

Kitu kimoja kilichonifanya nikumbuke kitabu cha David Crystal ni kuwa huyu ni mtaalam maarufu ulimwenguni wa masuala ya lugha. Nilipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1973, nikisomea "Literature" na "English," ndipo niliposoma maandishi ya Crystal, sambamba na mabingwa wengine, kama vile Frank R. Palmer, John Lyons, Noam Chomsky, Sydney Greenbaum, na Randolph Quirk. Kumbukumbu hiyo ndiyo ilinifanya ninunue kitabu cha Crystal, English as a Global Language miaka michache iliyopita. Sasa, kwa kuwa ninafuatilia suala la utandawazi, ninaona nilifanya vizuri kununua kitabu hiki.

Pamoja na kuelezea jinsi ki-Ingereza kilivyofanikiwa kuenea duniani na kinavyoendelea kuiteka dunia kama lugha ya mawasiliano ulimwenguni iliyo muhimu kuliko zote, Crystal anabainisha pia kuwa hatuwezi kuwa na uhakika kama hali hii itaendelea hivi siku za usoni. Kama nilivyoeleza katika ujumbe wa jana, nikinukuu kitabu cha People Before Profit, utandawazi hausambai bila upinzani kutoka katika jamii na tamaduni mbali mbali zinazotaka kulinda jadi na misingi yao.

Ni hivi hivi katika kuenea kwa ki-Ingereza. Crystal anatuelekeza kwenye kitabu cha Tom McArthur, The English Language, na anatumabia kuwa McArthur

"adopted a more synchronic perspective, moving away from a monolithic concept of English. His primary focus was on the kinds of variation encountered in the language as a consequence of its global spread. He suggested that English was undergoing a process of radical change which would eventually lead to fragmentation into a 'family of languages.'" (x)

Hilo wazo la ki-Ingereza kugawanyika katika vilugha mbali mbali linasisimua akili. Lakini, hata kama ki-Ingereza kitaishia kuwa vilugha vingi, ninategemea kuwa bado kutakuwa na misingi itakayodumu katika vi-Ingereza hivyo na kuendelea kuwawezesha watumiaji kuwasiliana na kuelewana. Hata wakati huu, tayari ki-Ingereza kina lahaja nyingi, sawa na ki-Arabu, ki-China, ki-Swahili, na lugha zingine.

Jambo la muhimu la kuzingatia, kwa nchi kama Tanzania, ni hoja ya msingi ya English as a Global Language, kwamba hakuna namna ya kukizuia ki-Ingereza kutawala dunia kama lugha ya mawasiliano. Tupende tusipende, lazima tutafute namna ya kuhakikisha kuwa tunaijua lugha hiyo. Tusipumbazwe na siasa reja reja zilizovaa gwanda la utaifa, tukasahau kwamba ki-Ingereza ndiyo nyenzo na silaha itakiwayo katika mapambano ya ulimwengu wa utandawazi wa leo na kesho.

Saturday, October 8, 2016

People Before Profit: Kitabu Kuhusu Utandawazi

Leo nimejipatia kitabu kiitwacho People Before Profit kilichoandikwa na Charles Derber. Nimeanza kukisoma leo hii hii.

Kwanza, niseme kuwa kitabu hiki kina utangulizi ulioandikwa na Noam Chomsky. Hilo pekee ni ishara ya thamani ya kitabu hiki, kwani Chomsky ni mchambuzi maarufu wa masuala ya ulimwengu kwa mtazamo wa kimaendeleo. Ninamheshimu sana, kama ninavyowaheshimu wachambuzi kama Seymour Hersh na Amy Goodman.

People Before Profit ni hazina ya elimu. Kinafafanua dhana ya utandawazi. Kwanza kinaelezea ukale wa utandawazi, na kwamba utandawazi una historia ndefu. Haukuanza zama zetu hizi, bali umekuwepo kwa miaka maelfu na maelfu, ukibadilika katika kila zama.

Pili kitabu kinaelezea uhusiano wa utandawazi na tekinolojia, kama vile mapinduzi ya miundombinu na viwanda. Tatu, kitabu kinaelezea mahusiano ya utandawazi na utamaduni, na hasa katika mazingira ya leo, kuna suala la mahusiano ya utandawazi na itikadi, kama vile demokrasia.

Kuna dhana kadhaa juu ya utandawazi ambazo tunapaswa kuzihoji, kwa mfando dhana ya kwamba utandawazi unaondoa tofauti miongoni mwa nchi na jamii mbali mbali, na kuifanya dunia iwe na sura moja. Dhana hii imekuwa ikijadiliwa sana.

Inahojiwa, kwa mfano na watu wanaosema kwamba pamoja na juhudi za utandawazi kuufunika ulimwengu, kuna pia nguvu za jamii na tamaduni mbali mbali zinazopambana ili kujilinda, kujihami, na kuendelea kuwepo kwa misingi tofauti na ile ya utandawazi. Nami, katika warsha zangu, kama zile nilizowahi kuendesha Arusha na Dar es Salaam, nilijaribu kuibua masuala haya.

Kifupi ni kwamba kitabu hiki kinaibua masuala muhimu ya kuelimisha kuhusu hiki kinachoitwa utandawazi. Ninakipendekeza kwa yeyote anayethamini elimu.

Wednesday, October 5, 2016

Tafsiri ya "Ye Tradefull Merchants," Shairi la Edmund Spencer

Siku kadhaa zilizopita nilichapisha mashairi mawili ya Edmund Spencer katika blogu hii. Nilivutiwa na wazo la kuyatafsiri mashairi haya, ingawa magumu, ili kuchangamsha akili yangu na kujipima ufahamu wangu wa lugha.

Siku ile ile, nilijaribu kutafsiri "Ye Tradefull Merchant," tangu mwanzo hadi mwisho, halafu nikaamua kuiweka kando tafsiri yangu, kwa kuwa sikuridhika na namna nilivyotafsiri vipengele viwili vitatu. Leo, bila kutegemea wala kupangia, nimepata hamu ya kurekebisha vipengele hivyo.

Ninafahamu kwamba, kwa mujibu wa nadharia za tafsiri, tafsiri ni dhana tata. Kutafsiri ni sawa na kujaribu kukikamata kitu kinachoteleza sana. Kwa ujumla, tunajidanganya au tunadanganyana tunaposema tumetafsiri utungo wowote wa fasihi. Hata hivyo, kwa kuzingatia jadi yetu ya kujidanganya na kudanganyana, ninaleta tafsiri yangu ya "Ye Tradefull Merchants."

---------------------------------------------------------------------------------------------

YE TRADEFULL MERCHANTS (Edmund Spencer)

Ye tradefull merchants, that with weary toyle,
Do seeke most pretious things to make your gain,
And both the Indias of their treasures spoile,
What needeth you to seeke so farre in vaine?
For loe! my love doth in her selfe containe
All this worlds riches that may farre be found:
If saphyres, loe! her eies be saphyres plaine;
If rubies, loe! hir lips be rubies sound;
If pearles, hir teeth be pearls, both pure and round;
If yvorie, her forhead yvorie weene;
If gold, her locks are finest gold on ground;
If silver, her faire hands are silver sheene:
     But that which fairest is but few behold,
     Her mind, adornd with vertues manifold.

ENYI WAFANYA BIASHARA MAKINI

Enyi wafanya biashara makini, mnaomenyeka na kazi,
Mkitafuta vitu ghali kujipatia faida,
Na India zote mbili mwazipora utajiri wao,
Nini mnajisumbua kutafuta mbali kote huko?
Kwani, hakika, mpenzi wangu anao nafsini mwake,
Utajiri wote wa dunia upatikanao mbali huko:
Kama ni yakuti, lo! macho yake ni yakuti bayana;
Kama ni akiki, lo! midomo yake ni akiki murua;
Kama ni lulu, meno yake ni lulu, safi za mviringo;
Kama ni nakshi ya pembe ndovu, panda la uso wake linayo;
Kama ni dhahabu, nywele zake ni dhahabu bora ya ardhini;
Kama ni uzuri wa fedha, mikono yake ni mizuri hivyo:
     Lakini kilicho kizuri kabisa na wachache wanakiona,
     Ni akili yake, iliyojaa mema maridhawa.

Tuesday, October 4, 2016

Wadau wa Vitabu Vyangu Kwenye Mkutano wa Africa Network

Jana jioni nilirudi kutoka Ohio, katika Chuo cha Denison, ambako nilikwenda kushiriki mkutano wa Africa Network kama nilivyoripoti katika blogu hii. Nina mengi ya kusema kuhusu mkutano ule, na hapa napenda kusema neno juu ya maprofesa wanaoonekana nami pichani hapa kushoto, ambao wote walinigusa kwa namna walivyoongelea vitabu vyangu.

Huyu aliyeko kushoto ni Stephen Volz, profesa wa Chuo cha Kenyon. Tumefahamiana miaka kadhaa katika mikutano ya Africa Network. Aliwahi kuishi Botswana akijitolea chini ya mpango wa Peace Corps. Juzi, nilipowasili kwenye ukumbi wa mkutano, ulikuwa wakati wa chakula cha jioni. Nilienda kukaa kwenye meza ambayo ilikuwa na kiti cha ziada. Mmoja wa watu waliokuwa wameketi hapo ni Profesa Volz.

Baada ya kusalimiana, profesa Volz alianza hima kutuambia kuwa alikuwa anajiandaa kwenda Botswana na wanafunzi wa Associated Colleges of the Midwest (ACM), na kwamba atatumia kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika programu hiyo. Nilifurahi kusikia hivyo, ingawa sikushangaa, kwa sababu msukumo mojawapo wa mimi kuandika kitabu hiki ulianzia kwenye mikutano ya bodi ya ACM nilipoombwa kuandika chochote cha kusaidia ufahamu wa tamaduni. Niliwahi kuelezea msukumo huo katika blogu hii.

Kulia hapo pichani ni Profesa Kristofer Olsen wa Chuo Kikuu cha Montana. Huyu naye tumefahamiana kwa miaka kadhaa. Nilimfahamu wakati wa mkutano mojawapo wa Africa Network uliofanyika katika Chuo cha Denison, alipokuwa moja wa watumbuizaji katika kikundi cha ngoma za kiafrika. Baada ya hapo tulikuwa marafiki katika Facebook.

Siku moja aliniandikia ujumbe kuwa alikuwa anafundisha kozi ya "Mythologies," na kati ya vitabu walivyokuwa wanasoma ni kitabu changu cha Matengo Folktales. Aliniulizia kama ningekuwa tayari kuongea na wanafunzi wake kutumia Skype, nami nilikubali, tukapanga siku na tukafanikisha darasa hilo kama nilivyoandika hapa.


Katika mhadhara wake kwenye mkutano wa juzi, kama anavyoonekana hapa kushoto, Profesa Olsen aliongelea kozi yake, akasema kuwa mwanzoni, watu waliposikia anapangia kutunga na kufundisha kozi ya "Mythologies," walidhani alikuwa anamaanisha jadi za Wagriki na Warumi wa kale. Hawakutegemea kuwa alikuwa anataka kufundisha jadi za mataifa mbali mbali hata wa leo. Ndipo akaamua kutumia kitabu cha Matengo Folktales, ambacho alikifahamu tangu alipokuwa mwanafunzi katika Chuo cha St. Olaf.

Profesa Olsen alituelezea kwamba wanafunzi wake walivutiwa kuonana na kuongea nami tulipojumuika kwa Skype. Walivutiwa kuniona mimi mwandishi wa kitabu cha Matengo Folktales walichokuwa wanasoma na pia kunisikia nikiimba nyimbo zilizomo katika hadithi hizo.

Maelezo ya Profesa Olsen yaliwagusa wasikilizaji. Hatimaye, mkutano ulipoisha, wanabodi wenzangu wa Africa Network waliniomba niandae video kutokana na Matengo Folktales ili iwekwe kwenye tovuti ya Africa Network. Nilikubali wazo hilo.

Monday, October 3, 2016

Mkutano wa Africa Network


Wikiendi hii nilikuwa chuoni Denison, katika jimbo la Ohio, kuhudhuria mkutano wa Africa Network, mtandao wa vyuo vinavyoshughulikia masomo juu ya Afrika. Nimekuwa mwanabodi wa Africa Network tangu mwanzo, na nimeshuhudia historia yake hadi leo. Mtandao wa wanachama na washiriki wetu unaendelea kupanuka.

Picha zote zinazoonekana hapa nilipiga mimi, ambaye naonekana hapa kushoto.




Mikutano ya Africa Network ni fursa ya waalimu na watafiti kubadilishana mawazo na uzoefu katika taaluma na nyanja mbali mbali zinazohusu Afrika. Wikiendi hii, tulipata fursa ya kusikia na kujadili mada juu ya masuala kama uhifadhi na usambazaji wa kumbukumbu kidigitali, historia ya kale ya Afrika na umuhimu wake katika masomo juu ya Afrika, kuboresha viwango na ubora katika elimu ya juu, program za kupeleka wanafunzi Afrika.
Mkutano wetu huo ulijumlisha washiriki kutoka Marekani na nchi kadhaa za Afrika. Kwa ujumla wetu, tuna uzoefu wa utafiti katika nchi nyingi za Afrika, kama vile Ghana, Kenya, Msumbiji, Senegal, Tanzania, Uganda, Zambia, na Zimbabwe. Taaluma tunazowakilisha ni kama anthropolojia, uchumi, fasihi, historia, na lugha.




Nitaendelea kuandika kuhusu mkutano wa wikiendi hii, kwani ninazo kumbukumbu nyingi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...