Saturday, May 11, 2013

TAMKO LA CCM MKOA WA MOROGORO KUHUSU VURUGU ZILIZOTOKEA RUAHA JANA JIONI


Ndugu wananchi Tarehe 24/4/2013 ulifanyika uchaguzi wa mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Ruaha. Vyama vilivyoweka wagombea vilikuwa CCM na CHADEMA. Hata hivyo mgombea wa Chadema alienguliwa baada ya CCM kumuewekea pingamizi kwa sababu alikuwa na mapungufu yaliyomwondolea sifa ya kuwa mgombea kwa mujibu wa sheria. Hivyo basi CCM ilitangazwa mshindi na siku hiyo hiyo Chadema wakashinda kitongoji.

Wana CCM waliyapokea matokea bila vurugu na wakakubali kuwa Mwenyekiti wa Kitongoji ni wa CHADEMA. Tarehe 09.05.2013 ili kuwa siku ya kukabidhiwa rasmi ofisi kwa Mwenyekiti mpya wa Kijiji cha Ruaha, lakini wenzetu CHADEMA wakataa kumkubali huyo Mwenyekiti na wakaamua kuanzisha vurugu kubwa sana katika kijiji cha Ruaha na maeneo ya karibu yaliosababisha uharibifu mkubwa wa mali.Wamechoma nyumba, wamefunga barabara na kusababisha uvunjifu mkubwa wa amnai eneo hilo. 
Tunalaani sana vurugu hizo zilizosababishwa na kundi la watu wenye nia mbaya na nchi hii wanaotaka kuivunja amnai tulionayo, wananchi wa morogoro na Watanzania kwa ujumla Tunavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua mara moja kurudisha amani ili wananchi waendelee na shuguli zao za kila siku za kujiletea maendeleo. Kwa wale wote waliochochea vurugu hizo wachukuliwe hatua mara moja na sheria ichukue mkondo wake.


Imetolewa CCM Morogoro

10.05.2012

Wednesday, May 8, 2013

Nimekutana na Mjukuu wa Mahatma Gandhi

Jioni hii tumepata bahati ya kuwa na Ela Gandhi, mjukuu wa Mahatma Gandhi. Alikuja kutoa mhadhara chuoni Carleton hapa mjini petu. Mada ya mhadhara wake ilikuwa, "The Challenges Facing Post-Apartheid South Africa."

Mama Ela Gandhi, ambaye alizaliwa Durban, ni mwanaharakati wa masuala ya amani na maendeleo. Aliongelea historia ya Mahatma Gandhi na mafundisho yake kuhusu namna ya kukabiliana na matatizo ya hujuma dhidi ya haki. Alisisitiza kuwa njia aliyofundisha Gandhi ya kutotumia mabavu na vita inatujengea mtandao wa urafiki na kuheshimiana, tofauti na vita, ambayo matunda yake ni kujenga mtandao wa maadui.

Alielezea umuhimu wa mafundisho ya watu kama Mahatma Gandhi, Albert Lutuli, Martin Luther King, na Nelson Mandela. Kisha alielezea changamoto zinazoikabili Afrika Kusini leo, kwani mategemeo ya wengi wakati wa kupambana na mfumo wa ukaburu hayajapatiwa ufumbuzi.

Nilikwenda kwenye mhadhara huu na baadhi ya wanafunzi wangu, ambao muhula huu tunasoma fasihi ya Afrika Kusini. Tumefurahi kumsikia Mama Ela Gandhi akiongelea masuala ambayo tumekuwa tukiyajadili darasani. Kwa mfano, katika kipindi cha leo, wakati tunasoma hadithi ya Nadine Gordimer iitwayo "A Chip of Glass Ruby" katika kuelezea dhamira mbali mbali zilizomo, nilikuwa nimewaelezea dhana ya  "Group Areas" inayotajwa katika hadithi hiyo. Kwa bahati nzuri, Mama Ela Gandhi katika mhadhara wake alifafanua dhana hiyo ya "Group Areas" vizuri kabisa.

Baada ya mhadhara wake, watu tulipata fursa ya kupiga naye picha. Nilipomwambia kuwa mimi ni m-Tanzania, alifurahi akakumbushia historia njema ya mahusiano baina ya nchi yake na Tanzania, akataja kazi nzuri iliyofanywa na Julius Nyerere. Nami niliongelea jinsi tulivyopata bahati Tanzania ya kujumuika na wakimbizi kutoka Afrika Kusini, baadhi wakiwa wahadhiri wetu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na wengine wakiwa viongozi wa vyama vya ukombozi ambao walifika kutoa hotuba. Kwa mfano, niliwataja Albie Sachs na Gora Ebrahim.

Nukta Tano za Mwigulu Nchemba

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, Ndugu Mohamedi Mtoi ameandika ujumbe ufuatao kuhusu mambo ya Mwigulu Nchemba, mbunge wa Iramba Magharibi kwa tiketi ya CCM:
---------------------------------------------------------------

NUKTA TANO (5) ZA MWIGULU KUKOSA HOFU YA MUNGU NA KUJAWA MAWAZO YA USHETANI NDANI YAKE.

Baada kufutwa kwa mashtaka ya ugaidi dhidi ya Rwekatare nimejiridhisha kuwa. Mwigulu hana utu, binadamu unapo kosa utu juu ya binadamu mwenzako unadondokea kwenye sifa za mnyama, lakini ukikubali kuwa wapo wanyama lakini pamoja na unyama wao wana tunu ya kumsaidia binadamu kwenye mambo mbalimbali kama vile kulima, kuwinda na hata kama kitoweo wakati wa maakuli. Basi mtu akikosa sifa za unyama (Mnyama) moja kwa moja anajivisha sifa za ushetani.

Kama hivyo ndivyo, leo Mwigulu Nchemba amedondokea kwenye sifa za ushetani! Sija muweka kwenye kundi hilo kwa bahati mbaya bali kwa matendo yenye hoja na tafakuri jadidi.

Kwa nini.

1. Kwa mipango yake ya
kishetani ya ugaidi kwa ajili unafuu na ujiko wa kisiasa, amesababisha Rwekatare
kuteseka mbaroni kwa takribani mwezi mmoja sasa. Mtu anaye
weza kutesa nafsi ya mtu mwingine hana tofauti na shetani anaye tesa roho na nyama za mwili wa binadamu.

2. Kwa mipango yake ya
kishetani, Mwigulu alishindwa kufikiria maradhi ya Rwekatare (Kisukari) maradhi
yanayo hitaji namna ya uangalizi maalumu kwenye vyakula na
hata mazoezi. Ni shetani pekee ndio mwenye
sifa ya kutomjali binadamu anaye teseka kwa maradhi. Hii ni zaidi ya sifa ya unyama maana mbwa au paka wako nyumbani anaweza kukuonea huruma.

3. Familia ya Rwekatare na hasa watoto wameteseka na
kuathirika kisaikolojia kwa kipindi chote ambacho baba yao alitegewa
mtego wa kishetani. Huenda huko mashuleni wameitwa "Watoto wa gaidi" Nani mwenye uwezo wa kupangusa maumivu ya kisaikolojia waliyo yapata watoto hao kwa kipindii chote baba yao alipo kuwa anaitwa gaidi?! Ni binadamu mwenye roho ya aina gani anaweza kuwa na furaha huku akijua kuwa watoto
wako wanaumia na kuteseka?

4. Ni binadamu wa aina gani anayeweza kuandaa shutma za uongo na
kuwaaminisha watanzania kuwa
niza kweli huku akimtaja Mungu kuwa anaweza kumpelekea ushahidi wake?! Na tangu lini Mungu akawa na shufaa ya kupokea ushahidi kutoka kwa
wanadamu twenye mapungufu na maadhaifu lukuki mbali na mitume walio kuwa wanapewa maagizo na Mungu kwa njia ya kuoteshwa?!

5. Imeandikwa, "mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi
yako" ikaandikwa tena "Usimshuhudie
mwenzako uongo", Mwigulu anasali kanisa gani ambalo hakuwahi kupata mafundisho haya?!, na ni binadamu wa aina
gani anaye yafanya haya huku akiwa amekusudia tena na kuapa ndani ya
nyumba inayopewa sifa ya utukufu?! Mtu huyu ana hofu ya Mungu ndani
yake?!

HITIMISHO.

Mimi namuona Mwigulu kama shetani kwa kuwa amekuwa na
mipango ya kishetani ambayo sasa
imekwama pamoja na ushetani wake. Na sasa ni wakati wa kumuombea aende ushetanini akapeleke ushahidi wake maana umeshindikana hapa duniani penye macho ya binadamu wenzake ambao ni wengi na kimsingi kuna kale kamsemo "Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu".

• Kumradhi kwa niliye mkwaza! Ni mtazamo na maono yangu.

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:  

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii: Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.
-----------------------------------
Makala yangu hii hapa juu nimeshaichapisha mara kadhaa katika blogu hii. Ila nimeona niilete tena. Ikumbukwe tu kwamba wakati Mwalimu alipoandika, upinzani haukuwa makini na wenye nguvu kama ilivyo leo. Nyerere angekuwa hai leo, nina hakika angeungana na CHADEMA katika kupambana na ufisadi. Yeyote ambaye amefuatilia mawazo ya Mwalimu katika hotuba na vitabu vyake mbali mbali, atakubaliana nami kwa hilo.

Friday, May 3, 2013

Chakula cha Jioni na Mzee Patrick Hemingway

Kwa siku mbili tatu hivi, nimeandika kuhusu ziara yangu Montana kuonana na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliye bado hai wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Kwa mfano, soma hapa.

Nilienda na wanafunzi wawili, ambao walikuwa miongoni mwa wanafunzi niliowapeleka Tanzania mwezi Januari mwaka huu, kwa kozi niliyoiita "Hemingway in East Africa." Katika  msafara wetu, alikuwepo pia baba mzazi wa mwanafunzi mmojawapo, ambaye alitupa usafiri wa ndege yake, na rubani wake.

Katika picha hapa kushoto, tunaonekana wote, na mwenyeji wetu, Mzee Patrick Hemingway na mkewe Carol, wakati wa chakula cha jioni. Kutoka kulia kwenda kushoto hapo mezani ni mwanafunzi Jimmy, Mzee Patrick Hemingway, Bwana Cooper (mwenye ndege), rubani, mwanafunzi Clay, Mama Carol, na mimi.

Tulienda kupata chakula cha jioni siku tuliyowasili Montana, yaani tarehe 27. Ilikuwa ni baada ya masaa kadhaa ya kuongea na Mzee Patrick Hemingway, akajibu masuali yangu kuhusu baba yake Ernest Hemingway na maandishi yake yahusuyo Afrika. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya mimi kuandaa safari hii ya kwenda kumwona.

Mazungumzo yetu yalikuwa marefu, na ilifikia wakati niliona nihitimishe, ili kutomchosha sana Mzee wetu. Lakini Mzee Hemingway ni mwongeaji sana. Pamoja na uzee wake, ana kumbukumbu nzuri sana ya mambo na anapenda kusimulia michapo ya miaka ile ya zamani, ikiwemo ile inayomhususu Ernest Hemingway.

Ziara yetu ilikuwa ya mafanikio makubwa sana. Sote tunakubaliana hivyo, akiwemo Mzee Patrick Hemingway mwenyewe, kama alivyonieleza leo kwenye simu. Leo nimepata barua kutoka kwa mzee mwenye ndege, na kati ya mambo aliyoandika ni "It was a truly remarkable, memorable, and thought provoking weekend."

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...