Saturday, December 25, 2021

Krismasi Katika Fasihi

Pamoja na mambo mengine, fasihi inaweza kubeba tafakari au taswira ya yale tunayokutana nayo maishani.Leo, siku ya Krismasi, napenda kuanzisha tafakari juu ya fasihi na Krismasi. Kwa upande wangu, kazi za fasihi ninazozikumbuka wakati huu wa Krismasi ni hizi:

1) "A Christmas Carol" (hadithi ya Charles Dickens)
2) "Journey of the Magi" (shairi la T.S. Eliot)
3) "Christ Climbed Down" (shairi la Lawrence Ferlinghetti)

Kazi hizi zote zina mambo mengi yanayohusu Krismasi na pia yanayogusa hisia kwa umahiri wa sanaa. KiIngereza kilivyotumika katika "Journey of the Magi," kwa mfano, kinagusa sana, na ubunifu wa simulizi yake ni wa kusisimua. Ninajiona mwenye bahati kuifahamu lugha hiyo vizuri sana, kwa undani kabisa, na ninafaidi uhondo.

Kwa upande mwingine, shairi la Ferlinghetti linasisimua kwa jinsi linavyokejeli kugeuzwa kwa Krismas kuwa si tukio la kidini bali la kibiashara. Kwa maana hiyo, Ferlinghetti anatukumbusha yale waliyoandika akina Marx na Engels katika "Communist Manifesto" kuhusu namna ubepari unavyohujumu na kunajisi mambo mbali mbali.

Huu ni wakati wa muafaka kwa wapenzi wa fasihi kutafuta tungo hizi, na zingine, kuzisoma au kurudia kuzisoma, na kuzitafakari.

Thursday, November 11, 2021

Msomaji na Mpiga Debe Wangu Aikwaa Tuzo

Jana niliandika taarifa za msomaji na mpiga debe wangu Joy Zenz, mKenya aishiye uJerumani.

Napenda niseme kuwa juhudi zake za kuwaunganisha akina mama waAfrika waliko Ulaya na kwingineko na kuwahamasisha katika masuala ya maendeleo kwao na kwa bara la Afrika yamemfanya atambuliwe na kutuzwa kwa namna mbali mbali.

Leo nimeona taarifa kuwa ameikwaa tuzo muhimu ya Global Africa Awards. Nimefurahi na ninampongeza kwa dhati msomaji wangu huyu na mpiga debe.

Tuesday, November 9, 2021

WaKenya Wazidi Kukinadi Kitabu


Nimewahi kuandika mtandaoni tena na tena nikiwasifu na kuwashukuru waKenya kwa jinsi walivyokuwa bega kwa bega nami katika utafiti na uandishi wangu.

Huku Marekani, waKenya wamekuwa wasomaji na wapiga debe wangu wakuu kama nilivyotamka, kwa mfano, hapa na hapa.

Sasa amejitokeza mKenya mwingine, Joy Awe, aishiye uJerumani. Yeye ni mwanzilishi na mratibu wa jumuia iitwayo African Women in Europe.

Ameweka picha zake mtandani akiwa na kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, pamoja na ujumbe huu:

Highly recommended book to read especially diaspora or anyone wanting to do business in Africa. Available on Amazon.

Naendelea kuwashukuru waKenya kwa mshikamano nami.

Sunday, November 7, 2021

Simulizi za Wanawake waAfrika Waishio Ulaya


Ninaandika ujumbe huu nikiwa ninavisubiri vitabu viwili vya wanawake waAfrika waishio Ulaya. Napenda nielezee jinsi nilivyopata taarifa za vitabu hivi.

Tarehe 31 Mei hadi 4 Juni mwaka huu nilishiriki mkutano mkubwa mtandaoni, "Trade With Africa Business Summit." Mwandaaji, Toyin Umesiri, alikuwa ameniomba nikazungumzie kitebu changu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilifanya hivyo, nikijikita katika kuongelea vipengele vya tamaduni vinavyohitaji kuzingatiwa katika biashara baina ya waAfrika na waMarekani.


Kwenye mkutano ule, nilipata kufahamiana na mtoa mada Joy Wanjiru Zenz, mama mKenya aishiye uJerumani na ni mwanzilishi na mwendeshaji wa jumuia ya wanawake waAfrika waishio Ulaya. Alishuhudia jinsi kitabu changu kilivyokuwa kinatajwa na baadhi ya washiriki wa mkutano.

Siku kadhaa baada ya mkutano, Joy nami tuliwasiliana,  akanieleza kuwa wanajumuia wake wamechapisha vitabu kuhusu maisha yao Ulaya. Nilivutiwa na taarifa hii. Ninayafahamu maisha ya waAfrika Marekani, lakini si Ulaya. Ilibidi nimwambie Joy kuwa ninahitaji vitabu hivi. Ninavisubiri kwa hamu.

Saturday, November 6, 2021

Msomaji Wangu Mpya, mTanzania wa Czech

Wiki hii ya kwanza ya Novemba, 2021, nimemmpata msomaji mpya, Corona Cermak, mTanzania aishiye Jamhuri ya Czech. Nilisikia jina lake kwa mara ya kwanza kutoka kwa dada Joy Wanjiru Zenz, mKenya aishiye uJerumani, ambaye aliniambia kuwa kuna huyu mTanzania mwandishi aishiye Czech.

Katika kufuatilia Facebook, YouTube, na Instagram, nimeona shughuli za Corona, za ufundishaji wa kiSwahili na uandishi wa vitabu vya watoto. Vitabu alivyochapisha ni The Rooster's VoiceSauti ya Jogoo, na Grandma Pipi and the Roses.

Juzi nilimwandikia kuwa nimeagiza vitabu vyake Amazon, naye hima akaniletea picha akiwa ameshika kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. alichoagiza hivi karibuni mtandaoni.

Mara tu baada ya kukipata kitabu changu, amekisoma na kukiongelea mitandaoni Instagram na Facebook akiwahimiza watu waendao Marekani, Ulaya, na Tanzania wakisome. Amesema pia kuwa ameagiza kitabu changu cha Matengo Folktales. Ni bahati njema kufahamiana na mwalimu na mwandishi mwenzangu, mTanzania aishiye ughaibuni. Tunategemea kubadilishana mawazo na uzoefu.

Friday, October 15, 2021

Mdau Kajipatia Kitabu

Huyu dada, Tanya, alihudhuria mazungumzo yangu na wana Rotary Club of Brooklyn Park tarehe 6 Oktoba. Mada yangu ilikuwa "Cultural Differences in the Global Village."

Nilipomaliza hotuba yangu, wakati wa masuali na majibu, dada huyu alijitokeza akasema kuwa yeye ni mfanyakazi katika sekta ya elimu na kwamba kwamba alivutiwa na mhadhara wangu akaongeza kuwa mawazo na maudhui yangu yanahitajika mashuleni.

Tulikubaliana kushirikiana kushughulikia changamotto zilizopo mashuleni. Baadaye nilimpelekea hiki kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kama hatua ya kwanza katika safari yetu hiyo.

Tuesday, October 12, 2021

KITABU MUHIMU KWA MAJADILIANO

Tarehe 5 Oktoba, Profesa Artika Tyner anayefundisha sheria katika Chuo Kikuu cha St. Thomas, alikweka picha hii hapa kushoto, akaambatiisha ujumbe huu: "New book alert: This book is an essential guide for intercultural dialogue. Thank you Dr. [Mbele] for sharing knowledge and wisdom." 

Nitafsiri kwa kiSwahili: "Tangazo la kitabu: Kitabu hiki ni mwongozi muhimu kwa majadiliano baina ya tamaduni. Asante Daktari Mbele kwa kutushirikisha ujuzi na hekima."

Profesa Tyner ni mmoja wa maprofesa wanaokitumia kitabu changu cha awali, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, katika masomo. Yeye alianza kukitumia katika programu ya kuwapeleka waMarekani Ghana kujifunza. Ni mmoja wa waMarekani weusi wenye mshikamano na Afrika. Pia ni mwandishi maarufu katika taaluma ya sheria na uongozi, na pia huandika vitabu kwa watoto. 

Kauli yake juu ya kitabu changu ina uzito wa pekee.

Friday, October 8, 2021

Maongezi yangu na Rotary Club ya Brooklyn Park, Minnesota

Tarehe 6 Oktoba, nilikwenda Brooklyn Park, Minnesota, kufuatia mwaliko wa Rotary Club. Tulikuwa tumekubaliana kuwa nikahudhurie mkutano wao na kuongelea mada ya  "Cultural Differences in the Global Village."

Siku iliyofuata, Rotary Club waliandika ujumbe katika ukurasa wao wa Facebook:

“We had the honor to hear from Professor Joseph Mbele at our Wednesday meeting. His incredible wisdom, insight, knowledge, passion, and heart to connect people across all cultures was so inspiring. We can create united and connected communities if we change our approach and adopt the strategies and mindset that Professor Mbele shared. Thank you Professor for joining us!”

Wednesday, October 6, 2021

NIMEHUTUBIA MKUTANO WA AMERIKA YA KUSINI

Jana, tarehe 5 Oktoba, jioni, nilihutubia mkutano ulioandaliwa na vyuo vikuu viwili vya Colombia, Amerika ya Kusini. Mada yangu ilikuwa "Culture and Business: a Broad Perspective From Africa to. Latin America." 

Kwa zaidi ya mwaka, mada ya utamaduni na biashara imenivutia. Nilipoanza kuipenda, niliandika "Culture and Business Between Africans and Americans." Halafu, nilihutubia Trade With Africa Business Summit nikiwa nimealikwa kuongelea kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Hatimaye sasa, nilipopata mwaliko kutoka Colombia, nilijikuta niko tayari kutosha. Kasoro pekee ilikuwa kwamba sikuufahamu utamaduni wa Amerika ya Kusini kama ninavyoufahamu ule wa Afrika na Marekani. Kwa hiyo, nilijielimisha kiasi kabla ya siku ya mkutano.

Nilijifunza mengi ya msingi, ambayo yalinifanya nitamke na kusisitiza mkutanoni kwamba utamaduni wa Amerika ya Kusini unafanana kiasi kikubwa na ule wa Afrika. Kwa hiyo, biashara baina ya pande hizi mbili itakuwa rahisi. Nilitoa angalizo kuwa itabidi kuzingatia tofauti za lughha zilizopo katika hizi pande mbili za dunia, ili kuleta uangalifu katika mawasiliano, utangazaji wa biashara, na kadhalika.
 

Saturday, October 2, 2021

Uandishi si Lelemama

Mimi kama mwandishi, ninakumbuka juhudi ninayofanya na taabu ninayopata katika kuandika vitabu. Kitabu cha Matengo Folktales, kwa mfano, kilichukua miaka yapata 23 kukiandaa, yaani tangu kurekodi hadithi, kazi yenye usumbufu mwingi, kuzitafsiri, kurekebisha tafsiri tena na tena, tena na tena, halafu kuziandikia uchambuzi, na kurekebisha tena na tena, huku nikifanya utafiti maktabani juu ya mada ya hadithi za jadi, ili niweze kuchambua hadithi zilizomo kitabuni kwa upeo unaofaa katika kufundishia vyuoni, na kadhalika. Nilijikuta nikitafakari mambo mengi ya aina hiyo, wakati mwingine nakwama kabisa, halafu baada ya muda najikongoja tena, hivi hivi, na baada ya miaka yapata 23 ndio nikachapisha "Matengo Folktales." Kitabu cha Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences, ingawa ni kidogo sana, kurasa 43 tu, nacho kilinichukua yapata miaka 15 kukiandaa. Nilipigika na kuchakarika. Lakini baada ya kuchapisha, najiona mwenye faraja kubwa na ushindi.

Sunday, September 19, 2021

Msomaji Amejipatia "Chickens in the Bus"

 

Jana, tarehe 18 Septemba, nilimpelekea msomaji anayeonekana nami pichani nakala ya kitabu changu kipya, Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Huyu mama, kutoka Togo, amekuwa msomaji wangu wa tangu zamani. Anavyo vitabu vyangu vya awali: Matengo Folktales na Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Mara aliposikia nimechapisha kitabu kingine, aliagiza nakala. 

Nina bahati ya kuwa na wasomaji makini namna hii. Huyu mama ni msomi na mzoefu katika idara ya ustawi wa jamii. Ninategemea kupata mrejesho adimu kutoka kwake atakapomaliza kusoma kitabu hiki.  

Saturday, September 11, 2021

Nimehudhuria Selby Ave JazzFest

Leo nimehudhuria tamasha liitwalo Selby Ave JazzFest mjini St. Paul, Minnesota. Sikuwahi kuhudhuria tamasha hili linalofanyika kila mwaka. Nilishindwa kufuatilia. 

Kuhudhuria kwangu leo kumetokana na mkurugezi wa In Black In kunifahamisha kuhusu kuwepo kwa tamasha hili, kisha kunialika na kuniambia kuwa nitakaribishwa kwenye banda la In Black Ink. Ndivyo ilibyofanyika leo.

Nimefurahi kukutana na watu wa kila aina, wengine ambao nimewafahamu tangu wakati uliopita hadi wapya machoni pangu. Pichani ninaonekana nikiwa na watu wawili ambao walisema wanatoka California. Wanafurahi baada ya maonezi na baada ya kujipatia vitabu walivyoshika.
 

Sunday, September 5, 2021

Msomaji wa Kwanza wa Kitabu Changu Kipya

Jana, tarehe 4 Septemba, 2021, nilipata nakala za kitabu changu kipya Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Hima nilimpa nakala jirani yangu, Mama Merri, mwalimu mstaafu anayependa sana kusoma maandishi yangu na ni mfuatiliaji wa shughuli zangu za kuelimisha waMarekani kuhusu utamaduni wa Afrika na tofauti zake na ule wa Marekani. 

Ni bahati njema kwa mwandishi kuwa na wasomaji na wafuatiliaji wa aina ya huyu mama. Lakini kwa hapa Marekani, bahati hiyo ninayo sana. Nina wasomaji na wafuatiliaji wengi.

Mama Merri alifundisha kwa miaka mingi katika shule za waHindi Wekundu. Alivyosoma kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences aliandika maelezo kuhusu namna utamaduni wao unavyofanana na ule wa waAfrika nilioelezea kitabu. Ninashukuru kwa elimu anayonipa.


 

Wednesday, September 1, 2021

Kitabu Changu Kipya: "Chickens in the Bus."

Jana, tarehe 31 Agosti, nilichapisha kitabu, Chickens in the Bus, kama kitabu halisi, baada ya kuwa nimekichapisha kama kitabu pepe siku kadhaa kabla. Nilipotangaza kuchapishwa hiki kitabu pepe, niliahidi kuwa kitabu halisi kiko njiani.

Kitabu hiki ni mwendelezo wa kitabu changu cha awali kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ambacho kimejipatia umaarufu na kusomwa na maelfu ya watu tangu nilipokichapisha, mwezi Februari, mwaka 2005.

Wasomaji kadhaa wa hiki kitabu cha awali walikuwa wananiuliza iwapo nilikuwa nawazia kuandika kingine cha kuendeleza mawazo yaliyomo, nami nikawa na nawazia kufanya hivyo kwa miaka na miaka.

Sasa nimetekeleza kwa kuchapisha Chickens in the Bus. Mwenye kutaka kujua angalau kijujuu nini ninaongelea katika kitabu hiki, anawaza kunisikiliza katika video hii.
 

Thursday, August 5, 2021

Msomaji Wangu Amefariki


Leo, tarehe 5 Agosti, niliamua kuanglia ujumbe niliochapisha kwenye blogu yangu mojawapo uitwao "Book Reviewed in 'The Zumbro Current.'" Ujumbe uliambatana na tahakiki ya kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Niliamua kufuatilia taarifa za mhakiki, Duane Charles Hoven, nikagundua kuwa alifariki miezi iliyopita, na hapa ni taarifa ya kufariki kwake.

Nimesikitika, hasa kwa kuwa sikuwahi kumwona, ingawa maskani yake ni maili thelathini tu kutoka hapa nilipo. Uhusiano wetu ni zaidi ya huu wa mwandishi na msomaji wake. Mchungaji Duane alisomea katika chuo cha St. Olaf ambapo ninafundisha, na alikuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa chuo. Apumzike kwa amani.

Uhakiki wake wa kitabu changu ni huu hapa:

Book Review: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences

The Abner Haugen Library at Zumbro Lutheran Church has a copy of this extremely helpful book on cultural differences between Americans and Africans. It is written by Joseph L. Mbele, a Tanzanian scholar who currently is a professor of English at St. Olaf College. Anyone traveling to another country or continent would find this short book well worth reading. A few of the topics covered are: eye contact, personal space, gender issues, gifts, how “time flies, but not in Africa.” Both my wife Ann and I recommend this 98-page book.

-Duane Charles Hoven. "The Zumbro Current," October 2014, p. 7.

Friday, July 30, 2021

Nimechapisha Kitabu Kipya, "Chickens in the Bus."

Leo ni siku ya furaha kwangu kwani nimechapisha kitabu kipya Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Wasomaji wa kitabu changu cha mwanzo Africans and Americans: Embracing Cultual Differences, walikuwa wakiniuliza iwapo ninapangia kuandika kitabu cha pili katika mada ya hicho. Nami nilikuwa nikiwazia, na kwa miaka yapata kumi na tano, nilikuwa nikiandika insha fupi fupi kwa lengo la hatimaye kuzikusanya na kuzichapisha kama kitabu.

Mtu anaweza kushangaa iweje nikatumia miaka kumi na tano kuandika kijitabu cha kurasa 40. Ni kwa sababu ninatambua kuwa uandishi bora unahitaji umakini wa hali ya juu. Ninaandika kiIngereza. Papo hapo somo mojawapo ninalofundisha hapa chuoni St. Olafni uandishi bora wa kiIngereza. Ninajua kuwa uandishi wa aina hiyo vigezo vyake ni "simplicity" na "clarity" ya hali ya juu kabisa. Kila sentensi ikidhi vigezo hivyo, na insha nzima ikidhi vigezo hivyo. Ninajikuta nikirebisha andiko langu mara nyingi sana, na ninajikuta ninakwama mara nyingi sana. Lakini baada ya miaka, matunda yanaonekana. Ndivyo ilivyokuwa kwa Chickens in the Bus.

Sunday, July 18, 2021

Utamaduni wa waCheki

Tarehe 10 Julai, katika tamasha liitwalo International Festival Faribault, nilipata fursa ya kutembelea banda la jumuia iitwayo Czech Heritage Club, yaani klabu ya urithi wa waCheki, yaani watu wenye asili ya Czechoslovakia. Tuliongea, wakaniambia kuwa kuna maonesho ("exhibition") ya utamaduni wa waCheki mjini Montgomery. Wakanipa jina la makumbusho ambako maonesho yamewekwa, na kwamba yatakuwepo hadi Septemba mwanzoni. Niliwaambia kuwa mimi ni mtafiti katika "folklore" na utamaduni kwa ujumla, na kwamba lazima nitaenda kuangalia maonesho.
Jana, tarehe 17, nilienda Montgomery, nikapata fursa ya kuangalia hifadhi. Ina mambo mengi sana ya historia na utamaduni. Nilipiga nyingi. Hapa naleta baadhi.












Tuesday, July 13, 2021

Tamasha la Kimataifa Faribault, Minnesota

Tarehe 10 Julai, 2021, nilishitiki International Festival Faribault, tamasha linaloandaliwa na Faribault Diversity Coalition mara moja kwa mwaka. Safari hii, nilimwalika Bukola Oriola, mwenye asili ya Nigeria, na mwanae Samuel Jacobs kuwa nami kwenye meza yangu na vitabu vyao.

Niliwahi kuwa mwanabodi wa Faribault Diversity Coalition na nimeshiriki tamasha mara nyingi. Wanakuwepo watu kutoka mataifa mbali mbali. Bendera za nchi zao zinapepea hapa uwanjani siku nzima. Katika ratiba ya tamasha, kunakuwepo muda wa watu kuandamana wakiwa na bendera zao kuelekea jukwaa kuu, na hapo kila mmoja hupata fursa ya kuelezea kifupi  bendera na nchi husika.
 

Monday, July 5, 2021

Jirani Yangu, Msomaji Wangu

Pichani katikati ni mama Merrilyn McElderry, na kushoto ni mjukuu wake. Nilijipiga picha hii nao juzi, tarehe 3 Juni, mjini Edina, jimbo la Minnesota. Merrilyn ni mwalimu mstaafu, msomaji makini wa maandishi yangu. Anayapenda na anafuatilia kwa karibu shughuli zangu kuhusiana na hadithi na mihadhara. Aliposoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, aliandika dondoo za kusisimua akifananisha utamaduni wa waAfrika na ule wa Wahindi Wekundu. Aliweza kufanya hivyo kirahisi kwa kuwa alishafanya kazi miaka 15 katika eneo wanamoishi waChippewa. Baraka iliyoje kwangu kuwa na wadau wa aina yake.

 

Sunday, June 27, 2021

Kitendea Kazi


Hii picha ya kitabu changu imetoka kwa Abraham Thomas aishiye Mto wa Mbu, Tanzania. Ni kitabu ambacho yeye na wenzake wamekuwa wakikitumia katika shughuli za kuongoza watalii na katika mazingira mengine.

Ukiona jembe limechakaa, ujue linatumika. Kitabu hiki ni sawa na jembe. Mashuhuda ni waMarekani wenye shughuli yoyote na waAfrika, pia waAfrika kama Abraham Thomas wenye shughhuli yoyote na waMarekani. Kinaepusha migogoro na kuchangia ufanisi.

Wednesday, June 23, 2021

KITABU KINAPATIKANA ARUSHA

Mjasiriamali wa Arusha anauza kitabu hiki ambacho kimekuwa gumzo huku nje ya Tanzania hadi hivi karibuni katika Trade With Africa Business Summit, mkutano uliohudhuriwa na watu maarufu kutoka nchi mbali kuanzia Umoja wa Afrika, hadi Israel, Ujerumani, Nigeria, Ghana, Afrika Kusini, na Marekani. Piga simu namba 0787 597 202

Sunday, June 13, 2021

Hitimisho la Trade with Africa Business Summit 2021

Video hii ni ya hitimisho la mkutano uliofanyika tangu Mei 31 hadi Juni 4, uitwao "Trade With Africa Business Summit." Nimeshautajataja mkutano huu hapa. Kila mtu alishukuru kwa kuhudhiria kutokana na elimu kubwa na pana iliyopatikana katika mihadhara na mijadala.

Mwaandaaji wa mkutano, Toyin Umesiri, alikuwa amenialika nikaongelee kitabu changu, "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences." Kitabu kilitajwatajwa kwenye mkutano, hata katika video hii ya dakika za mwisho za mkutano. Mtoa mada Vera Moore, mmiliki wa kampuni ya Vera More Cosmetics, anaonekana mwishoni kabisa akiwa ameshika kitabu. Tulishangaa amekipataje upesi namna ile.

Namshukuru Toyin kwa mwaliko wake. Ameniarifu kuwa ataendelea kunibebesha majukumu, nami niko tayari. Video zote za mkutano zinapatikana mtandaoni. Nikizingatia thamani ya elimu iliyomo, kulipia gharama iliyotajwa ni sawa na uwekezaji makini. Zinapatikana hapa: https://www.nazaru.trade/courses/5248326/content

Thursday, June 10, 2021

Nina Wasomaji Butiama kwa Mwalimu Nyerere

Sijawahi kufika Mwitongo, Butiama, lakini kitabu changu, ambacho ni kama nafsi yangu, kimefika. Pichani anaonekana mjukuu wa Mwalimu Nyerere akiwa anasoma kitabu hiki. Picha hii aliiweka mitandaoni akiwa ameambatisha ujumbe. Ninanukuu baadhi ya aliyosema.

"My Dad gave me this book to read this morning, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences by Joseph Mbele. I just finished it. One lesson I learned is to respect, understand, and see the value in both cultures. I would highly recommend this book." .................. "My Dad gave me this book, he felt that it could be helpful for me, I’ve lived in the US since I was 7, I’ve made the decision to move back this year. There are many things which I still question. It will be a long learning process, this book has given me hope." .................. "Thank you for writing this book Professor Mbele. I’ve learned quite a lot from reading it but I’ve also grasped a better understanding of many things which haven’t been clear to me before."

Naleta tafsiri yangu kwa kiSwahili:

"Baba alinipa kitabu hiki asubuhi hii nisome, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, cha Joseph Mbele. Nimemaliza sasa hivi. Jambo moja ambalo nimejifunza ni kuheshimu, kuelewa, na kuona thamani ya tamaduni zote mbili. Ninanipendekeza sana kitabu hiki."....

" Baba alinipa kitabu hiki, kwa kuona kwamba kingeweza kunisaidia. Nimeishi Marekani tangu nikiwa na miaka saba, na nimeamua kurejea nyumani mwaka huu. Kuna mambo mengi ambayo bado nayahoji. Itanichukua muda mrefu kujifunza; kitabu hiki kimenipa matumaini."....

"Asante kwa kuandika kitabu hiki Profesa Mbele. Nimmejifunza mengi kwa kukisoma na nimepata uelewa mzuri wa mambo mengi ambayo hayakuwa wazi kwangu."

Saturday, June 5, 2021

Ms. Vera Moore - Mdau Mpya wa Kitabu Changu

Wiki hii nzima, nimekuwa nikihudhuria mkutano mkuu uitwao Trade With Africa Business Summit. Mkutano umejumlisha wafanya biashara, wanadiplomasia, na wajasiriamali, na wengine kutoka nchi mbali mbali. Mwandaaji wa mkutano, Toyin Umesiri kutoka Nigeria, mjasiriamali na mhamasishaji wa biashara baina ya Afrika na Marekani, alikuwa amenialika kuongelea kitabu changu, "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences." Alikipigia debe mkutanoni, na kilitajwa mara kwa mara. Mjumbe mmoja, Vera Moore, mfanyabiashara maarufu wa vipodozi, alitusisimua alipokuwa akiongea, kwa kutuonyesha nakala ya kitabu akisema ameshanunua. Nilishangaa alivyokinunua haraka namna ile. Nafurahi kuwa na mdau maarufu huyu. Wengine wanakuja.

Friday, May 28, 2021

Nimealikwa Kuongelea Kitabu Changu

Nimealikwa kuongelea kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, katika mkutano mkubwa ujulikanao kama Trade With Africa Summit utakaofanyika kutumia mtandao tarehe 31 Mei hadi 4 Juni mwaka huu. Mkutano huu hufanyika mara moja kwa mwaaka.

Aliniaalika ni mwanaadji waa mkutano Toyin Umesiri, mjasiriamali na mhamasishaji maarufu wa biashara baina ya Afrika na nchi zingine, hasa Marekani. Aliamua kunialika baada ya kusoma kitabu changu kisha akanialika kwenye kipindi chake cha Nazaru TV na kufanya mahojiano nami.

Kwa miezi ya karibuni, mimi mwenyewe nimeanza kujibidisha kutafiti namna tofauti za tamaduni zinavyoathiri biashara. Mawazo yangu tayari yanaonekana katika kitabu changu, lakini ninayaendeleza na kuyafafanua. Mfano ya juhudi zangu ni makala katika Medium na maongezi katika YouTube.

Saturday, April 3, 2021

Kitabu Kimetua Abuja, Nigeria

Mwezi Machi 2021 umeisha vizuri kwangu. Kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kimetua Nigeria. Nilikuwa nimempelekea Jennifer Chinyelu Ikeaba-Obiasor, aonekanaye pichani, ambaye anaishi Abuja. Huenda hii ni nakala ya kwanza kuingia Nigeria.

Jennifer alisoma kitabu akaandika maoni kwa nyakati mbali mbali:

Ni kitabu murua chenyee upeo utakaowasidia waAfrika na waMarekani.

Uzoefu wangu unaendana na karibu kila kipengele kitabuni humu. Na kitawafungua macho watu wa tamaduni zote mbili.

Ninakipendekeza kitabu hiki kwa kila mmoja, akisome kwa sababu kitamgusa.

Jennifer nami tulikutana mtandaoni wiki chache zilizopita tukiwa wafuasi wa Toyin Umesiri, mhamasishaji maarufu wa biashara baina ya Afrika na Marekani, ambaye aliwahi kufanya mahojiano nami kuhusu kitabu changu na kuhusu athari za tamaduni katika biashara baina ya waAfrika na waMarekani. Jennifer ni mjasiriamali, mwanzishi na mkurugenzi mkuu wa Chiblenders Green. Katika juhudi za kueneza shughuli zake kimataifa, anafahamu umuhimu wa kuzielewa tamaduni za wengine. Katika muda mfupi wa kufahamiana naye, amenifundisha mengi na ninamshukuru.

Friday, January 29, 2021

Africonexion Yashiriki KAN Festival

Kuanzia tarehe 28 hadi 30 Januari hii, kwenye kituo cha MS TCDC, Arusha, kunafanyika tamasha liitwalo KAN Festival. Kwa kuwa sikuweza kwenda kuhudhuria, niliwasiliana na ndugu Thomas Ratsim wa Arusha akaniwakilishe. Mwaka jana aliniwakilisha pia, na ninatumia jina la Africonexion: Cultural Consultants, ambayo ni kampuni ndogo niliyosajili mwaka 2002 hapa katika jimbo la Minnesota, Marekani. 

Shughuli za Africonexion: Cultural Consultants ni kutafiti, kuandika, na kuelimisha kuhusu za tofauti za tamaduni katika dunia ya utandawazi wa leo. Wateja ni wa aina nyingi, kama vile waMarekani wanaokwenda Afrika na waAfrika wanaofika Marekani, taasisi, makampuni, jumuia na vyuo. Lengo ni kuwawezesha watu kuelewa changamoto za tofauti za tamaduni ili kuboresha mahusiano na ufanisi katika shughuli.

Matamasha ni fursa ya kutangaza shughuli za Africonexion: Cultural Consultants, ikiwemo kwa njia ya vitabu na maongezi na watu wanaokuja kwenye meza yetu, na pia ni fursa za kujifunza kutoka kwa watu wanaohudhuria matamasha. Ni fursa za kubadilishana mawazo na uzoefu.
 

Wednesday, January 27, 2021

Kitabu Kimefika Somalia

 Juzi tarehe 25, mama mmoja mSomali aishiye mjini Faribault hapa katika jimbo la Minnesota alinipigia simu. Nilikutana naye mara ya kwanza mwaka jana tamasha la kimataifa Faribault, nikampa nakala ya kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Alivyonipigia jana alisema kuwa alikuwa amerejea kutoka safarini Somalia. Baada ya maongezi na fupi ya simu, aliniandikia ujumbe huu: Joseph, I forgot to tell you that I took your book to Somalia. The people loved reading your book. Yaani, Joseph, nilisahau kukuambia kuwa nilienda na kitabu chako Somalia. Watu walifurahia kusoma kitabu chako.

Nafurahi kuona jinsi kitabu hiki kinavyokubalika na waAfrika wa kila taifa, jinsia, dini, na kadhalika. Kuna vipengele fulani katika kitabu hiki ambavyo ninaposoma, ninapata wasi wasi kuwa huenda niliandika bila kuwaza kuwa kuna waIslamu Afrika. Ajabu ni kuwa waIslamu wenyewe hawajawahi kukwazika. Mmoja kati ya wasomaji wa kitabu hiki wa mwanzo kabisa alikuwa mama muIslamu msomi kutoka Ivory Coast. Alikipenda sana kitabu hiki. WaIslamu wengi wa Afrika, wakiwemo maprofesa wamevutiwa na kitabu hiki. Siku chache zilizopita, nilileta taarifa ya mSomali mwingine. Namshukuru Mungu kwa yote.



Friday, January 1, 2021

Msomaji Wangu Kutoka Somalia

 

Huyu ni Salah Habib-Jama Mohamed kutoka Somalia, akiwa na kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Alihitimu shahada ya kwanza hapa katika Chuo cha St. Olaf.

Salah aliniambia katikaa maongezi ya simu kuwa aliwahi kuwa na kitabu hiki akakisoma.  Alikipenda sana, ila mtu alikiazima na sasa haijulikani kiko wapi. Nilicheka niliposikia hivyo, kwani nimewasikia waMarekani nao wakilaalamika kuwa nakala zao ziliazimwa na sasa hazijulikani ziliko, kwani waazimaji huwaazimisha wengine, na hivi kitabu kutoweka.

Katika ukurasa wake wa Facebook, Salah aliandika kuhusu kitabu hiki kwamba, "It is a great book and a must read allowing us to understand each other better with humor," yaani ni kitabu bora sana na muhimu kusomwa kwa namna kinavyotuwezesha kuelewana huku kikituchekesha.

Nafurahi kuwa kitabu kinapendwa na wote ambao wamekisoma. Nafarijika kuwa kinapendwa na waAfrika kutoka bara lote, wanawake kwa wanaume, wa makabila na dini mbali mbali. Nafarijika kuwa waMarekank nao wanakipenda, kwani mimi nimeelezea utamaduni wao ingawa si mMarekani. Nashukuru kuwa matokeo yamekuwa hayo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...