Tarehe 9 mwezi huu, nilienda Chuo Kikuu cha Minnesota kutoa mhadhara. Mada niliyoombwa kuongelea ni "Embracing African and African American Culture." Hiyo ilikuwa ni fursa nyingine kwangu kuelezea mtazamo wangu juu ya mahusiano baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika. Nilikuwa na mambo manne ya kuelezea: umuhimu wa mada ya mahusiano baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika, umuhimu wa kutambua utata na matatizo ya uhusiano huo, umuhimu wa kuelewa tulifikaje hapa tulipo, na umuhimu wa kutafakari namna ya kusonga mbele.
Kuhusu umuhimu wa mada, nilisisitiza kwamba watu weusi ulimwenguni wanakabiliana na matatizo ya pekee, tofauti na watu wengine. Nilisema kwamba waasisi wa "Pan-Africanism" walitambua jambo hilo vizuri. Kuhusu kipengele cha pili, nilitoa mifano na kufafanua migogoro na kutoelewana baina ya wa-Marekani Weusi na Wa-Afrika. Kuhusu tulivyofika hapa tulipo, niliongelea historia ya Afrika, tangu mwanzo, ambako tulikuwa jumuia moja, hadi pale watu wa Ulaya, kwa msukumo wa ubepari, walipofika na kuwachukua wa-Afrika kwa mamilioni kuwapeleka utumwani mbali na Afrika na papo hapo, kwa msukumo huo huo wa ubepari, wakavamia bara la Afrika na kulifanya makoloni.
Hapo ndipo wa-Afrika waliopelekwa Marekani wakaanza kuwa na historia tofauti na ile ya wa-Afrika waliobaki Afrika, kwani Marekani kulikuwa na mfumo wa utumwa na ubaguzi wa rangi na ukandamizwaji wa aina ya pekee. Hapo ndipo tofauti kubwa lilijengeka katika pande hizo mbili katika tamaduni, mitazamo, hisia, na mambo mengi mengine. Chimbuko la misuguano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi ni hilo, kwani walipitia njia tofauti. Jukumu lililopo ni kujielimisha. Wa-Afrika wajielimishe kuhusu historia ya wa-Marekani Weusi. Wajielimishe kwa dhati. Wa-Marekani Weusi wajielimishe kuhusu historia ya wa-Afrika. Wajielimishe kwa dhati. Mimi kama mwanafasihi ninafahamu kuwa fasihi ina mchango mkubwa katika elimu hiyo.
Kwa kiasi kikubwa, mhadhara huo ulifuata mwelekeo wa mhadhara niliotoa mwezi Januari katika mkusanyiko wa Nu Skool. Imekuwa ni bahati kupata fursa mbili kuelezea mawazo yangu na kusikiliza na kujadili masuali na maoni mbali mbali.
Thursday, April 12, 2018
Sunday, April 8, 2018
Nimenunua Kitabu cha Grimm Brothers
Leo, nilikwenda Apple Valley kumpelekea mama mmoja Mmarekani Mweusi nakala ya kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kama zawadi, kwa kuwa alikuwa ameniambia anapenda kujifunza kuhusu utamaduni wa Afrika.Baada ya kukutana naye, nilikwenda katika duka la Half Price Books. Nilipita upesi sehemu yenye vitabu vya Hemingway, halafu nikaenda kwenye sehemu yenye vitabu vvya bei ya chini kabisa, yaani "clearance" kwa ki-Ingereza cha Marekani.
Hapo ingawa nilishawishika kununua kitabu hiki au kile, kikiwemo The Inheritance of Loss cha cha Kiran Desai,sikununua. Nilishawishika kuhusu hiki kitabu cha Desai kwa sababu muhula huu ninafundisha kitabu chake kingine, Hullabaloo in the Guava Orchard.
Badala ya vitabu hivyo, nilinunua The Complete Illustrated Stories of the Brothers Grimm. Kitabu hiki nimekifahamu kwa miaka mingi, kwani hao ndudu wawili, Wajerumani, Jacob na Wilhelm Grimm ndio wanaotambulika kama waasisi wa taaluma ya ukusanyaji na uchambuzi wa hadithi za jadi.
Walirekodi hadithi sehemu mbali mbali katika nchi yao wakaanza kuzichapisha mwaka 1812. Walifanya kazi hiyo kwa miaka mingi, wakaanza vile vile kutafakari mambo yanayojitokeza katika hadithi za jadi. Kwa namna hiyo waliasisi taaluma ambayo nami ninashughulika nayo.
Kuna mjadala wa tangu zamani kuhusu kama ndugu hao wawili walichapisha hadithi kama walivyosimuliwa au walizihariri ili kuondoka vipengele walivyoona havifai kimaadili na vinginevyo. Hili ni suala tata hadi leo, katika jamii kadhaa, kama vile Marekani.
Ninazo hadithi mbali mbali zilizorekodiwa na hao ndugu wawili, lakini kitabu hiki ni muhimu kwa sababu kina hadithi zote kwa pamoja.
Thursday, March 29, 2018
Kitabu Kinaendelea Kupigiwa Debe Nebraska
Ninaandika ujumbe huu kuelezea ujumbe juu ya kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kutoka Nebraska, jimbo mojawapo la Marekani. Waumini wa kanisa la ki-Luteri la Marekani, ELCA, wa sinodi ya Nebraska wana programu ya kuzuru Tanzania iitwayo vision trip, kujifunza masuala ya utamaduni na maisha ya wa-Tanzania na kubadilishana uzoefu, ili kujenga mahusiano na maelewano.
Mwaka hadi mwaka, waratibu wa programu wamekipendekeza kitabu changu hicho. Leo nimeona chapisho la mwongozo kwa ajili safari ya mwaka 2018. Humo, kama ilivyokuwa miaka iliyopita, kitabu changu kimeendelea kupendekezwa kwa wasafiri:
For those persons wanting to more deeply explore cultural differences between Africans and Americans, the book Africans and Americans by Joseph Mbele is recommended. This book is available at: www.africonexion.com
Tafsiri kwa ki-Swahili:
Kwa wale wanaotaka kufuatilia zaidi tofauti za tamaduni baina ya wa-Afrika na wa-Marekani, kitabu "Africans and Americans" cha Joseph Mbele kinapendekezwa. Kitabu hiki kinapatikana www.africonexion.com
Ninafurahi na kushukuru kwamba watu wanaona umuhimu wa kitabu hiki. Kingekuwa hakina manufaa, wangeacha kukipendekeza tangu zamani. Niliwahi kukutana na baadhi ya hao wasafiri wa Nebraska katika safari ya kwenda Tanzania wakiwa na kitabu changu, kama nilivyoandika katika blogu ya ki-Ingereza. Ninafurahi kuwa kitabu changu kinasaidia lengo la kujenga maelewano baina ya wa-Tanzania na wa-Marekani.
Monday, March 19, 2018
Nimenunua CD za "Hamlet"
Leo niliingia katika duka la vitabu la chuoni St. Olaf kununua vitabu ambavyo nilikuwa nimepangia tangu jana. Lakini wakati naangalia vitabu, niliona kifurushi cha CD za Hamlet, tamthilia ya Shakespeare.Hiyo niliiona kama bahati ya pekee, kwa sababu siku chache zilizopita niliandika katika blogu hii kuwa tunasoma Hamlet. Ilikuwa ni wazi kuwa CD hizi nimeziona wakati muafaka. Nilichukua hicho kifurushi cha CD, nikakijumlisha na vitabu nilivyopangia kununua nikalipia vyote.
Jioni hii nimefungua kifurushi nikaona ziko CD tatu. Zimeandaliwa na Folger Theatre, ambacho ni kitengo cha Folger Shakespeare Library, ambayo ndio makataba kubwa kuliko zote duniani za kazi za William Shakespeare na machapisho juu yake. Watafiti kutoka duniani kote wanafanya utafiti katika maktaba hii. Hamlet, kama ilivyo tamthilia zingine za Shakespeare, inapatikana katika matoleo mbali mbali. Folger Shakespeare Library ina toleo lake.
Kama nilivyosema, nimeanza kusikiliza jioni hii. Nimevutiwa sana na utambaji wa tamthilia. Wameonyesha uhodari mkubwa wa kuwasilisha sio tu maneno ya tamthilia bali pia vitu kama hisia na mazingira ya matukio. Kwa mfano, nimevutiwa sana na namna wanavyowasilisha tukio la kuonekana mzimu wa baba yake Hamlet. Mtu unasikiliza na unajhisi uko kwenye tukio unashuhudia.
Kusoma ni kutafsiri. Kusoma kwa sauti ni kutafsiri kwa namna ya pekee. Ni tabia ya tafsiri kwamba kila mtu anaibuka na yake. Ndio maana ninasema kuwa hizi CD zinagusa kwa namna ya pekee. Mimi mwenyewe, kwa kuzingatia ukweli huo, nilisoma kwa sauti shairi la W. B. Yeats, "The Second Coming," nikaweka katika blogu hii. Nilitaka niweke wazi kwa kutumia sauti uelewa wangu na hisia zangu juu shairi hili. Ni tafsiri yangu. Ukisikiliza usomaji wa wengine, ambazo zinapatikana mtandaoni, utajionea tafsiri tofauti za shairi hili hili.
Saturday, March 17, 2018
Tunasoma "Hamlet"
Muhula huu nina mwanafunzi mwingine aliyeamua kujitungia kozi yake mwenyewe na kuifanya chini ya usimamizi wangu. Utaratibu huu uko hapa chuoni St. Olaf, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii.Kwa kushauriana nami, mwanafunzi alijitungia kozi juu ya "The Living and the Dead: Folklore and Tragedy." Tulikubaliana kusoma Agamemnon (Aeschylus), Beowulf (translated by Seamus Heaney), Inferno (Dante Alighieri), Hamlet (William Shakespeare), Othello (William Shakespeare), Love in the Time of Cholera (Gabriel Marcia Marquez), na As I Lay Dying (William Faulkner). Tumeshasoma Beowulf, na sasa tuna soma Hamlet.Napenda kusema neno kuhusu Hamlet katika mkabala wa kozi yetu hii.
Kwanza napenda kusema kuwa niliwahi kuongelea Hamlet katika blogu hii. Nilifanya hivyo kwa kujikumbusha tamthilia hii maarufu. Lakini sasa tunaisoma tukiwa na lengo la kuihusisha na mada ya kozi "The Living and the Dead: Folklore and Tragedy."
Hamlet ni tamthilia ya tanzia ("tragedy.") Hilo halina utata. Hamlet ana masononeko akikabiliwa na maamuzi magumu kufuatia kifo cha baba take katika mazingira ya kutatanisha. Katika tamthilia hii tunakutana na watu walio hai na pia mzimu wa baba yake Hamlet. Ujumbe wa mzimu ni kuwa aliuawa na mdogo wake, ambaye ni mfalme aliyeko madarakani. Baada ya mauaji hayo, mdogo huyu alimwoa mama yake Hamlet. Kuwepo kwa mzimu kunatupa fursa ya kujionea mfu aliye hai. Katika mazungumzo, wahusika wanaongelea masuala ya kifo na uhusiano wake na uhai. Mama yake anajaribu kumtuliza:
Good Hamlet, cast thy nighted color off,
And let thine eye look like a friend on Denmark.
Do not for ever with thy vailed lids
Seek for thy noble father in the dust.
Thou know't 'tis common, all that lives must die,
Passing through nature to eternity.
Act 1. Sc II
Hamlet mwenyewe anaonekana akijiuliza iwapo ni bora kuendelea kuishi na kukabiliana na magnum ya maisha au kujiua ili kuyamaliza. Tunamsikia akitafakari suala hilo katika hotuba yake maarufu "To be or not to be" ambayo ni moja kati ya hotuba maarufu kabisa katika tamthilia za Shakespeare:
Ham. To be, or not to be, that is the question:
Whether 'tis nobler in the mind to suffer
The slings and arrows of outrageous fortune
Or to take arms against a sea of troubles,
And by opposing end them. To die--to sleep--
No more; and by a sleep to say we end
The heartache, and the thousand natural shocks
That flesh is heir to. 'Tis a consummation
Devoutly to be wished. To die--to sleep.
To sleep--perchance to dream: ay, there's the rub!
For in that sleep of death what dreams may come
When we have shuffled off this mortal coil,
Must give us pause....
Act. III. Sc. I
Ninapenda kusema kuwa mwanafunzi wangu na mimi tumeanza vizuri kuiitafakari mada ya "The Living and the Dead.: Folklore and Tragedy." Kila kitabu kina mchango wake katika kuilezea mada hii. Haya tutayadhihirisha kadiri kozi inavyoendelea.
Thursday, March 8, 2018
Nimenunua Vitabu Vipya vya Mashairi
Katika siku chache zilizopita, nimenunua vitabu vipya viwili vya mashairi. Kimoja ni Collected Poems: 1974-2004 cha Rita Dove, ambacho nilikinunua mjini Moscow, Idaho. Kingine ni Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibrahim Hussein ambacho nilikinunua mtandaoni Amazon.Nilipokuwa Moscow katika tamasha la Hemingway, niliingia katika duka la Book People of Moscow. Niliangalia, nikaona kitabu hiki Collected Poems, ambacho sikukifahamu kabla. Nilivutiwa kwa sababu nilifahamu habari za Rita Dove, kwamba ni mshairi maarufu sana, aliyepata tuzo kadhaa ikiwemo tuzo ya Pulitzer.
Zaidi ni kuwa niliwahi kusoma insha yake "Either I'm Nobody, or I'm a Nation," ambayo ni uchambuzi wa mashairi ya Derek Walcott. Nilikuwa ninafundisha tungo za Walcott, nikaitafuta makala hii na niliona ilivyojaa tafakari na ilivyoandikwa kwa ustadi. Makala hii ilinithibitishia kuwa Rita Dove ana akili sana. Hii ikawa sababu kubwa ya mimi kununua Collected Poems.
Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibrahim Hussein niliinunua baada ya kuiona imetajwa mtandaoni Amazon. Nilikuwa sifahamu kuwepo kwake, lakini kwa jinsi ninavyomwenzi Ebrahim Hussen ambaye nilimfahamu tulipokuwa wote katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, yeye akiwa mhadhiri wakati ninasoma, na hatimaye tukawa tunafundisha wote, niliona ninunue kitabu hiki. Mimi mwenyewe nimechapisha makala juu ya tungo za Ebrahim Hussein katika Encyclopedia of African Literature iliyohaririwa na profesa Simon Gikandi.
Nimeanza kuyasoma mashairi yaliyomo katika vitabu vyote viwili. Tayari nimeona kuwa Rita Dove anaandika kwa nidhamu ya hali ya juu, ya kutumia maneno yanayohitajika tu, na anatupeleka sehemu mbali mbali za dunia, tangu enzi za kale hadi leo, kama anavyofanya Derek Walcott katika tungo zake, iwe ni mashairi au tamthilia. Diwani ina washairi wengi chipukizi. Ni fursa yao kuonekana kwa wasomaji.
Tuesday, March 6, 2018
Mdau wa Kitabu Amekuja Tena
Hapa pichani ninaonekana na De'Vonna, mmoja wa waandaaji wa maonesho ya waandishi yaliyoitwa Minnesota Black Authors Expo, ambayo niliyaelezea katika blogu hii. Anaonekana ameshika kitabu changu, Africans and American:Embracing Cultural Differences. Picha tulipiga wakati wa maonesho. Amenilitea ujumbe kuwa anahitaji nakala nyingine ya hiki kitabu.Kwa kuzingatia jinsi mama huyu alivyo na ushawishi katika jimbo hili la Minnesota, hasa miongoni mwa wenzake wa-Marekani Weusi, nimeguswa na ujumbe wake kwa namna ya pekee. Tangu nilipoandika kitabu hiki, nilikuwa na dukuduku ya kujua wa-Marekani Weusi watakuwa na maoni gani kuhusu yale ninayosema juu ya mahusiano yao na sisi wa-Afrika. Nilielezea dukuduku hiyo katika blogu ya ki-Ingereza.
Kama inavyoeleweka, mahusiano hayo yanawatatiza baadhi ya watu. Kwa hivyo ninapopata mrejesho kutoka kwa hao wenzetu, ninauchukulia kwa uzito wa pekee. Nimefarijika na kufurahi kwamba De'Vonna anataka nakala nyingine ya kitabu changu. Sijui anakipeleka wapi, au atakitumia vipi, lakini hii si hoja.
Subscribe to:
Posts (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Ukizunguka mitaani Dar es Salaam, utakuta matangazo mengi ya waganga wa kienyeji. Waganga hao wanatoka sehemu mbali mbali, kama vile Sumbaw...
-
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...