Nimeona taarifa leo kuwa msikiti umechomwa moto huko Saudi Arabia. Ni msikiti wa dhehebu la Shia. Kwa wale wasiofahamu, wa-Islam, kama walivyo wa-Kristu, wana madhehebu mengi, kama vile Sunni, Shia, Ismailia, Ahmadiya na Tijanniya.
Habari ya msikiti kuchomwa moto imenikera, kama ninavyokerwa na habari za kuchomwa moto kanisa au nyumba nyingine ya ibada ya dini yoyote. Nimesema tena na tena kuwa
ninaziheshimu dini zote, ninaiheshimu
misahafu ya dini zote, na ninazihehimu
nyumba za ibada za dini zote. Ninaamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya busara ambayo tunapaswa kuifuata.
Sawa na waumini wa dini zingine, nami nililelewa katika imani kwamba dini yangu ndiyo pekee dini ya kweli. Nilifundishwa kwamba nje ya dini yangu, nje ya u-Katoliki, hakuna wokovu. Ninajua kuwa wa-Islamu nao wanafundishwa hivyo hivyo, kuwa nje ya u-Islamu hakuna wokovu. Niliwahi kuwa mwanachama katika mtandao wa Radio Imaan, wa wa-Islam. Waliniambia kuwa mimi ni kafiri na kwamba nisiposilimu sitaingia ahera.
Hii ndio hali halisi. Binafsi nimeamua kujitungia mwelekeo nilioutaja hapa juu, ingawa ninajihesabu kama m-Katoliki. Katika hilo, simtumikii wala kumfuata binadamu. Natumia akili yangu na kufuata dhamiri yangu.
Kwa nini mtu uchome moto msikiti wowote, kanisa lolote, au nyumba ya ibada ya dini yoyote? Kwa nini usikemee kuchomwa moto kwa msikiti wa Shia kwa vile tu wewe ni Sunni, au ni m-Kristu, au ni m-Hindu? Kwa nini usikemee kuchomwa moto kanisa, kwa vile tu wewe si m-Kristu?
Kama hukemei, unaufumbia macho uozo ambao siku moja utakuja kusababisha nyumba ya ibada yako ichomwe moto. Usishangae ikitokea hivyo, wala usikasirike, kwani roho yako haina tofauti na ya yule atakayefanya uhalifu huo. Kilichopo ni kujitambua.
Tumelelewa na tunalelewa katika njia ya giza. Tuamke. Tuanze kujijengea mtazamo mpya wa kuheshimiana wanadamu wote, kila watu na imani yao, wenye dini na wasio na dini, na tuwalee watoto wetu katika njia hiyo.
Hayo ndio mawazo yaliyonijia niliposoma taarifa ya kuchomwa msikiti wa Shia kule Saudia. Ni mawazo yanayoendelea kunisonga na kuisumbua akili yangu. Kama unaona nimepotoka au ninapotosha, nawe ni muumini wa dini, kumbuka kuwa una wajibu wa kujitokeza, kukosoa, na kurekebisha. Ukiacha kufanya hivyo, kumbuka kuna jehenam au motoni, kama tunavyoita wa-Kristu. Na ukichangia, ukajiita "anonymous," unajisumbua na unajidanganya, kwani ingawa mimi sitakutambua, Mungu (Allah) anakuona na atakufichua siku ya kiyama. Kazi kwako.