Ingawa nilirejea hapa Marekani kutoka Tanzania wiki moja tu iliyopita, nilikuta ujumbe kutoka kwa mwenyekiti wa kamati, Milo Larson, akinikumbusha kuhusu maonesho hayo. Alinikumbusha kuwa nahitajika kupeleka vitabu vyangu kwenye maonesho. Katika picha hapo juu, Mzee Larson anaonekana akiandaa meza yangu.
Kwa hapa Marekani, nimezoea hali hii ya kuitwa sehemu mbali mbali nikazungumze na pia kupeleka vitabu. Ni tofauti na hali ninayoiona Tanzania.
Leo, kwa mfano, nimekutana na huyu mama, ambaye aliniambia kuwa alisoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Hii ilikuwa ni ajabu, kwani nami nilisoma katika Chuo hicho hicho, miaka ya kabla yake. Halafu, aliniambia kuwa alishachukua kozi moja ya Profesa Harold Scheub iliyohusu fasihi hadithi za Afrika. Profesa huyu ndiye aliyesimamia tasnifu yangu ya shahada ya udaktari. Kweli milima haikutani, binadamu hukutana.
Tabia hii si ngeni kwa wa-Marekani. Huwa wanapenda kumbukumbu za aina hii. Wengi wanapenda mwandishi atie sahihi kwenye kitabu wanachonunua. Nami leo nimefanya hivyo kwa wateja wangu.
Katika mji wa Faribault kuna wa-Somali wengi, ambao wamefika miaka ya karibuni. Leo hapo kwenye maonesho nilikutana na hao wa-Somali wawili. Huyu aliyeko kushoto anaishi kwenye mji mwingine. Lakini huyu wa kulia ni rafiki yangu, ambaye anafuatilia maandishi na shughuli zangu kuhusu masuala ya tamaduni. Ni kijana makini, na tunapangia kushirikiana katika shughuli hizo.