Monday, August 17, 2015

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kusherehekea siku hii. Kati ya hao marafiki, napenda kuwataja wawili wanaoonekana pichani hapa kushoto. Kulia anaonekana Larry Fowler, na kushoto anaonekana Bob Mitchell. Mwaka jana nilipokuwa nimelazwa hospitalini mjini Minneapolis, walifunga safari kuja kuniona. Zikipita wiki mbili tatu hatujaonana, hawakosi kunitafuta. Wanafurahi kupiga gumzo na michapo nami.

Waliniletea ujumbe siku zilizopita, wakisema kuwa siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu wangependa kunipeleka mahali tukale chakula cha mchana. Siku zilivyopita, walikuwa wananikumbusha. Leo, nilipomaliza kufundisha, Larry alinifuata chuoni St. Olaf tukaenda kwenye hoteli ambapo tulipata chakula na kupiga michapo.

Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuishuhudia siku hii. Ni neema ambayo sistahili. Napaswa kutambua kwamba kila siku katika maisha yangu ni dhamana, niitumie kwa mambo mema. Nizingatie wajibu wa kuvitumia kikamilifu vipaji alivyonipa Mungu kwa manufaa ya wanadamu.

Wengi hawakupata bahati ya kufikia umri niliofikia, lakini wamefanya makubwa, yasiyo kifani. Kama ilivyo kawaida yangu, nawakumbuka hasa waandishi maarufu, kama William Shakespeare, Alexander Pushkin, Ernest Hemingway, na Shaaban Robert. Hawakuishi miaka mingi kama yangu. Kuwafikiria watu kama hao kunanifundisha unyenyekevu. Siwezi kujivunia chochote nilichoweza kufanya, bali ni kumshukuru Mungu na kuendelea kumtegemea.

Inavyoonekana, kila ninaposherehekea kumbumbuku ya siku ya kuzaliwa kwangu, fikra zangu za msingi kuhusu maisha yangu zinajirudia. Ninajikuta nikifananisha mchango wangu ulimwenguni na ule wa watu maarufu, na kukiri kuwa, ingawa ninajitahidi, mchango wangu bado ni hafifu. Nimekuwa nikiandika hivyo katika blogu hii. Hii ni changamoto kwangu, daima na siku zijazo.

Sunday, August 16, 2015

CCM na Suala la Makapi na "Oil Chafu"

CCM inatuambia kuwa hao wanaotoka CCM na kuhamia UKAWA ni makapi au "oil chafu." Kila kukicha tunashuhudia hao wanaoitwa makapi na "oil chafu" wanavyoendelea kumwagikia UKAWA.

Kama hayo wanayosema CCM ni ukweli, basi ni kwamba CCM ni dampo kubwa la takataka. Ndio maana, pamoja na hayo makapi na hiyo "oil chafu" wanavyoendelea kumwagikia nje, CCM inasema iko imara. Kama kweli CCM iko imara, ni wazi CCM ni dampo kubwa la takataka. Unaweza ukachota mkokoteni mzima wa takataka na dampo likabaki salama.

Sasa suali linakuja. Kwa nini miaka yote hii CCM ilikuwa inajinadi kama chama makini, chama safi? Kwa nini CCM ilikuwa inatuambia kuwa ndio chama pekee kinachofaa kuiongoza Tanzania?

Hayo wanayosema CCM sasa yananikumbusha na yanathibitisha aliyoandika Mwalimu Nyerere miaka ya mwisho ya uhai wake, kwamba kuna uozo katika uongozi wa CCM, kwamba kuna kansa katika CCM. Anayetaka kufuatilia suala hilo asome kitabu cha Mwalimu Nyerere kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, kilichochapishwa Harare mwaka 1993.

Mimi kama raia ambaye si mwanachama wa chama chochote ninachongojea ni Oktoba mwaka huu, CCM ing'olewe madarakani. Tujue moja.

Monday, August 10, 2015

Bendera ya Tanzania Itapepea Faribault, Minnesota, 22 Agosti

Tarehe 22 Agosti, nitashiriki tamasha la kimataifa mjini Faribault, Minnesota. Nimeshalipia gharama. Nitakuwa na meza ambapo nitaweka vitabu vyangu na machapisho mengine.

Hapo nitaongea na watu siku nzima kuhusu shughuli zangu za ufundishaji, utafiti, uandishi, na utoaji ushauri kuhusu athari za tofauti za tamadauni, ushauri ambao ninautoa kwa wanafunzi na waalimu wa vyuo vya Marekani na watu wengine waendao Afrika, taasisi na jumuia zenye mahusiano na wa-Afrika, na kadhalika.

Nitaweka pia mabango ya filamu ya "Papa's Shadow." Filamu hiyo, ambayo ni ya maelezo ("documentary"), kwa kiasi kikubwa ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliyebaki. Tunajadili maisha na maandishi ya Ernest Hemingway, hasa yale yanayohusu Afrika. Filamu hii itaanza kuonyeshwa hivi karibuni katika majumba ya sinema na itakuwa inapatikana katika DVD na kadhalika. Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti ya Ramble Pictures.

Jambo jingine la pekee ni kuwa, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa tamasha la kimataifa mjini Faribault, bendera ya Tanzania itapepea, sambamba na bendera za mataifa mengine. Siku chache zilizopita, nilipeperusha bendera hii katika tamasha la Afrifest, mjini Brooklyn Park, kama nilivyoripoti katika blogu hii.

Ninapokuwa Tanzania, ninaweza kuiangalia bendera ya Tanzania nikawa ninaguswa kwa namna fulani, lakini hisia hizo huwa za pekee zaidi huku ughaibuni. Ingekuwa natoka Dar es Salaam kwenda kushiriki tamasha Mtwara, Chake Chake au Mbeya nisingeona sababu ya kubeba bendera ya Tanzania, labda kama tamasha ni la kimataifa. Na hata ningebeba, watu hawangekuwa na duku duku nayo au mshangao. Ni kitu walichozoea.

Lakini mambo ni tofauti huku ughaibuni. Sina namna ya kuelezea vizuri ninachomaanisha. Labda kwa kuwa niko mbali, nina hisia za pekee kuhusu kijiji changu cha Lituru, kata yangu ya Litembo, wilaya yangu ya Mbinga, mkoa wangu wa Ruvuma, na nchi yangu ya Tanzania.

Isipokuwa, jambo moja ni wazi, na linaelezeka: watu watakaohudhuria tamasha mjini Faribault wataiona bendera ya Tanzania. Bendera hii itatokea katika picha mbali mbali watakazopiga siku hiyo na kuzihifadhi, kuwapelekea marafiki au kuziweka mitandaoni.

Sunday, August 9, 2015

Shaaban Robert na Mbaraka Mwinshehe Waliongelea Umuhimu wa Shule

Nikiachilia mbali jinsi wazazi wangu walivyohimiza elimu, nikiachilia mbali jinsi Mwalimu Nyerere alivyohimiza elimu, naukumbuka kwa namna ya pekee mchango wa mwandishi Shaaban Robert na mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe katika kuhimiza elimu.

Ninakumbuka jinsi baba yangu, nilipokuwa shule ya msingi, alivyokuwa ananitia msukosuko iwapo nilishindwa kupata 100% katika zoezi lolote au mtihani wowote. Ninakumbuka pia jinsi Mwalimu Nyerere alivyokuwa anahimiza elimu, kwa watu wote, kuanzia watoto hadi wazee, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.

Shaaban Robert ni mtu anayenifanya nimkumbuke baba yangu. Nilijionea hayo niliposoma kitabu kiitwacho Barua za Shaaban Robert, ambacho habari zake niliziandika katika blogu hii. Humo tunaona jinsi Shaaban Robert alivyokuwa anamhamasisha mdogo wake Yusuf Ulenge afanye bidii katika elimu, akimtimizia mahitaji yote ya shule. Kwa wazazi na walezi, Shaaban Robert ni mfano wa kuigwa.

Mbaraka Mwinshehe, mwanamuziki ambaye wakati wa ujana wangu alitingisha Afrika Mashariki, ya Kati, na Kusini kwa nyimbo na muziki wake, aliimba wimbo maarufu wa kuwaasa vijana wazingatie elimu. Wimbo huo, "Enyi Vijana Sikilizeni," unaweza kuusikiliza hapa:

https://archive.org/details/EnyiVijanaSikilizeni

Saturday, August 8, 2015

Maajabu Katika Siasa Tanzania, 2015

Kuna maajabu mengi katika siasa Tanzania. Mimi si bingwa wa uchambuzi wa mambo hayo, na wala siamini kama kuna bingwa. Ila kila mtu ana uhuru wa kuchambua aonavyo. Oktoba tutaona tuko wapi, na kama uchaguzi utakwenda kiustaarabu, tutawajibika kuyapokea matokeo.

Hebu nirudi kwenye mada yangu ya maajabu ya siasa Tanzania. Edward Lowassa amejitoa CCM na kuibukia CHADEMA (UKAWA). Tayari amezua zogo. Watu wanarusha makombora kwake, kwa CHADEMA, na kwa UKAWA. Wanasema kwa nini CHADEMA impokee mtu ambaye wamekuwa wakimtukana kama fisadi mkubwa.

Ajabu ni kwamba hakuna mahakama yoyote ambayo imemwona Lowassa kuwa fisadi. Amehukumiwa na hisia za watu pamoja na majungu ya magazetini, katika blogu, na vijiweni. Amekosewa haki ya msingi, kwa mujibu wa tangazo la kimataifa la haki za binadamu, haki ya kwamba mtu anayetuhumiwa au kushtakiwa kwa kosa, lazima ahesabiwe kuwa hana kosa hadi mahakama ithibitishe vinginevyo.

Kwa hivi, wote wanaomwita Lowassa fisadi, au waliomwita fisadi (wakiwemo CHADEMA) wajirekebishe. Wamtendee haki Lowassa. Hadi mahakama ithibitishe, Lowassa ana haki ya kuonekana hana kosa, na kuingia kwake CHADEMA hakuna dosari.

Kwa CHADEMA na UKAWA kumkaribisha Lowassa ni sahihi kabisa. Ni jambo la busara CHADEMA wamwombe radhi kwa kumtukana kwa miaka mingi, yaishe. Na yeye ameonyesha roho nzuri kwa kuja kwenye chama chao, bila kinyongo. Ameonyesha moyo unaoendana na mafundisho ya dini yetu ya u-Kristu ya kuwasamehe wanaotutendea mabaya.

Kwa upande wa CCM ni kwamba Lowassa muda wote wamekuwa naye bega kwa bega. Alikuwa mkuu wa idara yao ya mambo ya nje. Hata baada ya kukatwa kwenye uchaguzi wa mgombea urais, hawakumtukana. Lakini ghafla, baada ya yeye kuhamia CHADEMA (UKAWA) wameanza kumtukana, kwamba ni kapi. Vigogo wa CCM wanaohamia upinzani wanatukanwa kwamba ni makapi.

Kwa maana hiyo, hao akina Asha Rose Migiro, Bernard Membe, Mizengo Pinda, January Makamba, Hamisi Kigwangwala, Emmanuel Nchimbi, na wengine, wakae chonjo. Wakae mkao wa kula. Wakitimkia upinzani, hapo hapo watajikuta wanaitwa makapi.

Haya ni kati ya maajabu ya siasa Tanzania

Tuesday, August 4, 2015

Mwandishi Seenaa Aongelea Kitabu Chake Mjini Minneapolis

Juzi Jumapili, nilipata ujumbe wa Facebook kutoka kwa rafiki yangu Peter Magai Bul wa Sudan aishiye Chicago kwamba kuna rafiki yake mwandishi, Seenaa Godana-Dulla Jimjimo, anakuja Minneapolis kuongelea kitabu chake, The In-Between: The Story of African-Oromo Women and the American Experience. Jana, baada ya kumaliza kufundisha na kupumzika kidogo nilikwenda Minneapolis kumsikiliza mwandishi huyu.

Ukumbi ulijaa watu, na karibu wote ni wa-Oromo wanaoishi hapa Minnesota. Nilifurahi kuonana na wanawake wawili na mwanamme mmoja ambao niliwahi kuwafundisha hapa chuoni St. Olaf. Tulifurahi kukutana.

Walikuwepo wazungumzaji watatu ambao waliongelea masuala yanayowahusu wa-Oromo kama vile ukandamizwaji wanaofanyiwa na jeshi la Ethiopia, harakati zao za ukombozi dhidi ya Ethiopia, unyanyaswaji na ukandamizwaji wa wanawake katika jamii ya wa-Oromo. Mzungumzaji mmojawao aliongelea juu ya mwandishi Seenaa na kitabu chake.

Baada ya hapo, mwandishi Seenaa alikaribishwa kuongea. Alielezea mambo muhimu yalyoathiri maisha yake, msukumo alioupata kwa mama yake katika elimu, kujitambua na kujiamini. Aligusiia umuhimu wa wa-Oromo kujituma katika kupigania haki zao na haki na usawa kwa wanawake, akawasihi viongozi wa dini wawe mstari wawemo katika kuihamasisha jumuia katika harakati hizo.  Kufuatia maongezi hayo, mwandishi alijibu masuali ya wasikilizaji.

Hatimaye mwandishi alikaribishwa kusaini vitabu vyake. Watu wengi tulijitokeza tukapanga foleni ya kununua vitabu ili kusainiwa. Nilipokaribia mezani, wanafunzi wangu walinizuia kulipia kitabu, wakalipia wao. Wakati wa kusaini, mwandishi alifurahi sana kuniona, kwani alishaelezwa habari zangu na Peter Magai Bul. Tulifurahi, tukapiga picha kabla na baada ya kusaini.

Nimeanza kukisoma kitabu. Nina hamu ya kujua mawazo na mtazamo wa dada huyu kuhusu masuala yanayowahusu wa-Oromo kuanzia kwao Oromia hadi huku ughaibuni. Inavyoonekana, kwa mujibu wa utangulizi wa kitabu, mwandishi anakwenda mbali ya kuwaongelea wa-Oromo tu. Kwa mfano, kuhusu suala la haki za wanawake, anawaongelea wanawake kwa ujumla, si wa-Oromo tu.

Niliguswa kuona jinsi shughuli ya kukutana na mwandishi na kuongelea kitabu ilivyowavutia watu wengi namna hii. Nilivutiwa na usikivu wao kwa wazungumzaji na masuali waliyouliza. Imenifanya nitambue kuwa hao wenzetu wameelimika na wanathamini elimu. Nimebaki ninajiuliza iwapo wanadiaspora wa ki-Tanzania tuna mwamko huo huo.

Sunday, August 2, 2015

Bendera ya Tanzania Katika Tamasha la Afrifest 2015

Jana, tarehe 1 Agosti, tamasha la Afrifest lilifanyika mjini Brooklyn Park, Minnesota. Hili ni tamasha ambalo huandaliwa mara moja kwa mwaka na bodi ya Afrifest Foundation ambayo mimi ni mwenyekiti wake. ili kuwakutanisha wa-Afrika, watu wenye asili ya Afrika waishio Marekani ya Kaskazini, Kati, na Kusini, pamoja na Caribbean, na pia watu wa mataifa mengine. Lengo kubwa ni kufahamiana, kuelimisha, na kuuenzi mchango wa watu weusi duniani kote, katika nyanja mbali mbali.

Hiyo jana ilikuwa ni mara ya kwanza kwa bendera ya Tanzania kupepea kwenye tamasha la Afrifest. Baada ya kushiriki matamasha na kujionea wenzetu wanavyotumia fursa kuzitangaza nchi zao, nilijiuliza kwa nini nisitafute bendera ya Tanzania, kama nilivyoeleza katika blogu hii.

Hatimaye, nilifanya uamuzi wa kununua bendera, niwe ninaipeperusha kwenye matamasha ninayoshiriki, maadam fursa zipo. Hapo kushoto naonekana na binti zangu Assumpta na Zawadi kwenye meza yetu, hiyo jana.
Sawa na kuweka vitabu mezani katika tamasha, ambavyo huwavutia watu waje kuulizia habari zake, sawa na kutundika bendera ya kampuni yangu ya Africonexion: Cultural Consultants, ambayo nayo huwavutia watu waje kuulizia maana ya Africonexion, bendera hiyo nayo ni kivutio na kianzio cha mazungumzo kuhusu Tanzania.

Miaka yote, nimekuwa nikishiriki matamasha chini ya kivuli cha kampuni yangu ya Africonexion: Cultural Consultants. Hata hivi katika kuelezea shughuli zangu, sikujiwekea mipaka, kwani utafiti wangu, ufundishaji, uandishi na utoaji ushauri katika masuala ya athari za tofauti za tamaduni, nagusia dunia yote, ikiwemo Tanzania. Lakini kuitundika bendera ya Tanzania kama nilivyofanya jana kunaongeza mwonekano wa nchi katika nchi za dunia.

Kwa kuwa bendera hiyo ilipepea hapo uwanjani siku nzima, kila mtu katika umati wa waliohudhuria tamasha aliiona. Wengi wa waliohudhuria walipiga picha hapo uwanjani, na haikwepeki bendera kuonekana katika baadhi ya picha.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...