Tofauti moja ya wazi ni kuwa matamasha ya vitabu ni mengi zaidi, maradufu, Marekani kuliko Tanzania. Marekani kuna matamasha makubwa ya kitaifa na matamasha makubwa kiasi ya kiwango cha majimbo, na pia matamasha ya kiwango cha miji. Mtu ukitaka, unaweza kuzunguka nchini Marekani ukahudhuria matamasha ya vitabu kila wiki, kila mwezi, mwaka mzima. Angalia, kwa mfano, orodha hii hapa. na hii hapa.
Kwa upande wa Tanzania, hali ni tofauti. Matamasha ya vitabu hayafanyiki mara nyingi. Tunaweza kuwa na tamasha la vitabu la kitaifa mara moja kwa mwaka. Lakini hatuna utamaduni wa kuwa na matamasha ya sehemu mbali mbali za nchi, kwa mfano tamasha la vitabu mikoa ya Kusini, tamasha la vitabu mikoa ya Magharibi, mikoa ya Mashariki, na kadhalika.
Tofauti hizi zinatokana na tofauti za utamaduni wa kusoma vitabu. Utamaduni wa kusoma vitabu umejengeka miongoni mwa watu wa Marekani, tangu utotoni. Watoto, hata wanapokuwa wadogo sana, husomewa vitabu; vijana, watu wazima, na wazee husoma vitabu. Utawakuta katika matamasha ya vitabu, kama ninavyoeleza mara kwa mara katika blogu hii.
Katika matamasha ya vitabu ya Marekani, ni kawaida waandishi kuwepo. Wengine huja kuonesha na kuuza vitabu vyao. Wengine huwa wamealikwa kama wageni rasmi. Waandishi huongelea vitabu vyao. Nilivyoona Tanzania ni kwamba wachapishaji ndio huleta vitabu kwenye matamasha. Mtu ukihudhuria matamasha hayo, ukawa na hamu ya kujua kuhusu vitabu vya mwandishi fulani, utaongea na mchapishaji. Mwandishi humwoni.
Ninaona kuwa hii ni dosari. Ni jambo ambalo tunaloweza kujifunza kutoka kwa wa-Marekani. Kuwepo kwa waandishi ni kivutio kimojawapo katika matamasha ya vitabu. Hapa Marekani, ni kawaida kuona matangazo katika vyombo vya habari, au mabango kwenye meza za waandishi yameandikwa "MEET THE AUTHOR." Ni kivutio. Watu hupenda kuonana na waandishi, kuongea nao, kununua vitabu na kusainiwa, na pia kupiga nao picha.
Utaratibu huu ungeweza kufanyika Tanzania, ungesaidia. Ninafahamu, kwa mfano, kwamba wengi wanalijua jina la Ngoswe. Wamesikia, na wanatumia usemi "Ya Ngoswe mwachie mwenyewe Ngoswe." Lakini hawajui asili ya jina Ngoswe. Kumbe, hili ni jina la tamthilia ya Ngoswe: Penzi Kitovu cha Uzembe iliyotungwa na Edwin Semzaba.
Kutokana na umaarufu wa jina la Ngoswe, kama waandaaji wa tamasha la vitabu wangeweka tangazo kuwa mtunzi wa Ngoswe atakuwepo katika tamasha, naamini itakuwa ni kivutio kwa watu kuhudhuria tamasha. Ninaweza kutoa mifano mingine. Jina kama Kinjeketile ni maarufu. Ebrahim Hussein, mwandishi wa tamthilia ya Kinjeketile akijitokeza katika tamasha la vitabu, atakuwa kivutio. Kadhalika Euphrase Kezilahabi, mwandishi wa riwaya maarufu kama Rosa Mistika na Dunia Uwanja wa Fujo.
Waandishi, wachapishaji, na wadau wengine wa vitabu tunakubaliana kwamba kuna haja kubwa ya kujenga utamaduni wa kusoma vitabu katika nchi yetu ya Tanzania. Hilo wazo langu la kuboresha matamasha ya vitabu huenda likachangia mafanikio ya ndoto yetu.