Friday, September 30, 2016

M-Kenya Kaniandikia Kuhusu Kitabu Changu

Nimefurahi sana, tangu usiku wa kuamkia leo, kupata maoni ya msomaji wa kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Msomaji huyu ni mama m-Kenya ambaye anaishi hapa Minnesota, Marekani. Aliniandikia katika Facebook ujumbe huu:

I did not tell you how precious your book is. My friend and I were reading it to our kids during a sleep over and it is amazing how your culture is similar to ours. You did well and it was very easy to understand and flow with. You are gifted Mwalimu. God bless you more. Thank you again for the great gift.

Huyu mama tulikutana tarehe 30 Aprili, mwaka huu, kwenye tamasha mjini Rochester. Alikuja kwenye meza yangu, tukasalimiana na kuongea. Alivutiwa na kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, akaulizia namna ya kukipata siku nyingine, kwa kuwa hakuja na hela. Hapo hapo nilimpa nakala ya bure. Alishangaa, akashukuru sana.

Nimefurahi kuwa ameniandikia maoni yake kuhusu kitabu hicho. Ninamfananisha na wa-Tanzania kadhaa ambao, baada ya kuniomba, nimewapa nakala za bure za kitabu hiki. Nilitegemea na ningefurahi iwapo wangeniletea neno kuhusu kitabu, lakini sikuwasikia tena. Nawajibika kusema kuwa sioni kama huu ni uungwana.

Ninapowazia jambo hilo, ninapata hisia kuwa huenda hao watu hawakusoma kitabu hicho. Wazo hilo linanifikia kwa kuzingatia ukweli kwamba utamaduni wa kusoma vitabu hauonekani katika jamii ya wa-Tanzania. Hili ni jambo ambalo limelalamikiwa na linaendelea kulalamikiwa na wadau wa vitabu kama vile waandishi na wachapishaji.

Kwa upande wa wa-Kenya, nimejionea kuwa wanao utamaduni wa kupenda vitabu, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii. Hali hiyo ninaishuhudia sio tu huku nje ya Afrika, bali pia  nchini mwao. Ushahidi moja wa wazi ni kuwa makala kuhusu vitabu si jambo geni katika magazeti ya Kenya. Kwa upade wa Tanznia, sijui ni lini niliwahi kuona gazeti la aina hiyo.

Hainifurahishi kusema mambo hayo kuhusu wa-Tanzania, lakini ninachosema ni ukweli nilivyouona. Ukweli unapaswa kusemwa, hata kama unauma. Hainishangazi kwamba hata katika soko la ajira, iwe ni Afrika Mashariki au kwingineko, wanajiamini kuliko wa-Tanzania.

Thursday, September 29, 2016

Darasa ni Popote

Tangu nilipokuwa mdogo, nilikuwa nataka kuwa mwalimu. Mungu si Athmani, ndoto yangu ilitimia. Ninafurahia kazi yangu na ninaifanya kwa dhati na kwa uadilifu. Ninaona raha kuwa na wanafunzi katika kutafakari masuala.

Zaidi ya kufundisha darasani katika jengo, ninapenda kushiriki matamasha. Matamasha hayo ni kama shule, fursa ya kuongea na watu juu ya shughuli zangu, kama vile utafiti na uandishi.

Uandishi ninauchukulia kama aina ya ufundishaji. Ni ufundishaji usio na mipaka, kwani maandishi yanakwenda popote, iwe ni vitabu halisi au vitabu pepe, iwe ni makala katika majarida au mtandaoni,  zote hizo ni njia za kuniwezesha kufundisha bila mipaka.

Ninafurahi kuwa nimejiingiza katika uwanja wa blogu. Blogu ni kumbi zinazonipa fursa ya kueneza mawazo yangu, ingawa kwa ufupi. Mara kwa mara ninaongelea vitabu na kutoa dondoo za kiuchambuzi zinazoweza kumpa mtu fununu ya mambo muhimu yaliyomo katika vitabu hivyo. Blogu zangu zinatoa fursa kwa watu kuchangia mawazo na mitazamo. Ninaendesha blogu kwa mtindo huo kwa kuwa ninaheshimu uhuru wa fikra ambao ndiyo injini inayoendesha elimu.

Ni wazi kwamba tafsiri yangu ya shule au darasa ni tofauti na ilivyozoeleka. Tekinolojia za mawasiliano zimeleta mazingira na fursa mpya. Fikra zetu kuhusu darasa au shule sherti zibadilike. Katika mazingira ya leo, darasa au shule ni dhana isiyofungwa au kufungamana na kigezo cha jengo, madawati, au mwalimu na wanafunzi kuonana ana kwa ana.

Leo kwa kutumia tekinolojia za mawasiliano, mwalimu anaweza kuendesha darasa kwa njia ya Skype, kama nilivyowahi kufanya kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Montana, au anaweza kuendesha darasa mtandaoni na wanafunzi wakiwa wametapakaa sehemu mbali mbali za dunia. Ninategemea kuwa wa-Tanzania, wakiwemo wanaotaka nirudi Tanzania nikafundishe, watasoma na kutafakari hayo niliyoandika hapa.

Thursday, September 22, 2016

David Robinson Ahutubia Chuo Kikuu cha Minnesota

Leo mchana nilikwenda Chuo Kikuu cha Minnesota, Minneapolis, kumsikiliza David Robinson, m-Marekani Mweusi anayeishi Mbeya, Tanzania, ambako ni mkulima wa kahawa. Huyu ni mtoto wa mwisho wa mwanariadha maarufu sana wa Marekani, Jackie Robinson, ambaye alikuwa pia mpinzani shujaa wa ubaguzi na mtetezi wa haki za wa-Marekani Weusi.

David Robinson aliamua kwenda kuishi Tanzania, kwenye kijiji cha Bara wilaya ya Mbozi. Alijitambulisha kwa wanakijiji akajieleza kuwa ni mtoto wa Afrika aliyepotezewa ughaibuni kwa karne kadhaa, katika utumwa, na sasa ameamua kurudi nyumbani. Wanakijiji walimpa shamba akaanza kulima kahawa. Aliungana na wanakijiji wengine, wakaanzisha chama cha ushirika kiitwacho Sweet Unity Farms

Aliongelea shughuli za chama chao cha ushirika, wanavyoshughulikia matatizo na changamoto na kujifunza. Alielezea mahusiano yao na wateja wa nchi mbali mbali, ikiwemo Marekani. Ingawa wao wako kijijini, wanashiriki katika uchumi wa ulimwengu, na ndio hali halisi ya utandawazi. Daima wanatafuta namna ya kujiweka kibiashara, pamoja na uwezo wao mdogo, katika ulimwengu ambao umetawaliwa na makampuni makubwa ya kimataifa.

Pichani hapa kushoto anaonekana David Robinson, Limi Simbakalia, mwanafunzi m-Tanzania wa Chuo cha St. Olaf ambapo ninafundisha, na mimi.

Kuna taarifa nyingi mtandaoni juu ya David Robinson na Sweet Unity Farms, yakiwemo mahojiano naye. Taarifa moja nzuri kabisa ni hii hapa. Aidha, kuna taarifa nyingi juu ya baba yake, mwanariadha Jackie Robinson. Mfano mmoja ni filamu hii hapa chini, inayoonyesha magumu aliyopitia na alivyopambana kishujaa katika mazingira ambayo yalikuwa mabaya sana kwa wa-Marekani Weusi.

Tuesday, September 20, 2016

"The Dilemma of a Ghost:" Tamthilia ya Ama Ata Aidoo

The Dilemma of a Ghost ni tamthilia ya kwanza ya Ama Ata Aidoo wa Ghana. Aliitunga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Ghana, Legon, ikaonyeshwa mara ya kwanza mwaka 1964, na kuchapishwa mwaka 1965. Ama Ata Aidoo aliendelea kuandika na bado anaandika, na kazi zake ni pamoja na tamthilia nyingine iitwayo Anowa, ambayo ilichapishwa mwaka 1970, hadithi fupi, na riwaya kadhaa.

The Dilemma of a Ghost inaongelea juu ya kijana wa Ghana aitwaye Ato aliyekwenda masomoni Marekani na huko akakutana na Eulalie, binti Mwamerika Mweusi. Huyu ni kati ya wale wa-Marekani Weusi wanaoiwazia Afrika kwa hamu kama mtu aliyeko ugenini anavyowazia nyumbani kwake.

Ato na Eulalie wanaoana na kurejea Ghana, ambako wanakumbana na mambo magumu. Kwanza ndugu zake Ato wanashtuka kusikia kuwa Ato ameoa bila kuwashirikisha. Halafu binti mwenyewe hana kabila wanalolitambua, na hata jina lake wanashindwa kulitamka, na kibaya zaidi, kwa mtazamo wao, ni kuwa binti huyo ni kizalia cha watumwa. Wanaukoo wanaona Ato amewasaliti.

Halafu, Eulalie naye anashindwa kuelewa na kufuata mila na desturi za hao ndugu. Wao wanamwona kama kizuka, kwa tabia zake, ikiwemo kukataa kunywesha dawa za kienyeji za kumwezesha kupata mimba. Mama mkwe wake, Esi Kom, anapofanya ukarimu wa kumletea konokono, ambao ni chakula cha heshima, Eulalie anashtuka, na haamini macho yake, na hatimaye anawatupilia mbali hao konokono. Jambo jingine linalowashangaza ndugu hao ni jinsi Eulalie anavyovuta sigara. Basi, inakuwa shida juu ya shida, na hatimaye binti anajikuta katika upweke na msongo wa mawazo.

Lakini, hatimaye, mama yake Ato anaridhia kumpokea huyu mkwe wake na anachukua hatua za kuwashawishi ndugu wote wampokee, kwa hoja kwamba mgeni hastahili kulaumiwa, bali mwenye lawama ni mwenyeji, yaani Ato. Ato anajikuta akiwa mpweke, aliyesongwa na mawazo, karibu kuchanganyikiwa. Ndivyo tamthilia inavyokwisha.

The Dilemma of a Ghost imejengeka katika mfumo wa hadithi za jadi ambazo huitwa "dilemma tales" ambao ni muundo unaowaacha wasikilizaji wakiwa na masuali yasiyojibika kirahisi. Katika tamthilia hii, suali moja muhimu ni nani wa kulaumiwa kwa matatizo yanayoibuka. Tamthilia hii inatumia pia aina nyingine za fasihi simulizi, kama vile nyimbo na methali. Vile vile kuna imani za jadi, kama vile juu ya mizimu na matambiko.

Ama Ata Aidoo ni mmoja wa waandishi wa ki-Afrika ambao ni hodari wa kutumia miundo na dhamira za masimulizi ya jadi. Hilo suala la kijana kujifanyia mwenyewe uamuzi wa kuoa au kuolewa bila kuwahusisha wazazi ni dhamira maarufu katika fasihi simulizi za Afrika, na matokeo ya kiburi hiki huwa si mema. Katika tamthilia ya Anowa, Ama Ata Aidoo ameiweka pia dhamira hiyo. Msichana Anowa anaamua kuolewa na kijana aliyemkuta bila wazazi kuhusika.

Tangu mwanzo, nilivutiwa na mtindo huu katika uandishi wa Ama Ata Aidoo, ambaye miaka ile alikuwa anajulikana kwa jina la Christina Ama Ata Aidoo. Ninakumbuka vizuri, kwa mfano, hadithi yake moja ya mwanzo kabisa iitwayo "In the Cutting of a Drink" ambayo niliisoma kwa mara ya kwanza miaka ya sitini na kitu, nilipokuwa mwanafunzi katika shule ya sekondari.

Nilivutiwa sana na hadithi hiyo kwa mtiririko wake sawa na wa mtambaji hadithi. Miaka ya baadaye, nilipojifunza somo la fasihi simulizi, nilianza kuelewa vizuri jinsi waandishi kama Ama Ata Aidoo wanavyotumia jadi hiyo.

Jambo muhimu sana jingine kuhusu Ama Ata Aidoo ni kuwa ni mwandishi mwenye kuchambua masuala ya jamii. Alivyokuwa anatunga The Dilemma of a Ghost, masuala kama ya mshikamano na mahusiano ya watu weusi ulimwenguni yaani "Pan-Africanism," yalikuwa yakivuma na kuwashughulisha viongozi maarufu kama George Padmore, W.B. Dubois, Kwame Nkrumah, Ahmed Sekou Toure, Jomo Kenyatta, na Julius Nyerere. Miaka iliyofuatia, Ama Ata Aidoo amekuwa akienda na wakati kama mwanaharakati katika masuala ya ukoloni mambo leo, haki za wanawake, na hata ujamaa. Sawa na ilivyokuwa kwa Mwalimu Julius Nyerere, Ama Ata Aidoo ni muumini wa fikra za kijamaa.

Saturday, September 17, 2016

Jionee Ukakamavu wa UVCCM

CCM ina kila sababu ya kujivunia vijana wake, yaani UVCCM. Sio tu ni vijana wanaozingatia wajibu wao wa kutetea na kutekeleza ajenda za serikali ya CCM, kama wanavyotamka katika tovuti yao, bali ni wakakamavu, ambao wako tayari kwa lolote.

Hapa naleta picha kadhaa kuthibitisha jambo hilo, nikizingatia usemi wa ki-Ingereza kwamba "a picture is worth a thousand words," yaani picha ina thamani sawa na maneno elfu. Jionee mwenyewe uwajibikaji na utendaji wa hao vijana.


Kwenye masuala ya itikadi, vijana hao wako mstari wa mbele pia. Angalia hilo bango walilobeba katika maandamano yao huko Visiwani.


















Kama hizi picha hazitoshi kukushawishi, basi angalia video hii hapa chini. Kwa kweli, CCM ina kila sababu ya kujivunia vijana wake.

Thursday, September 15, 2016

Ujumbe kwa Ndugu na Marafiki

Napenda kuwajulisha ndugu na marafiki kuwa leo tumemaliza wiki ya kwanza ya muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Nimeanza vizuri, kama nilivyogusia katika blogu hii, kwa ari kubwa. Wanafunzi wanaonekana wenye ari ya kujifunza. Sitawaangusha.

Tarehe 17 mwezi uliopita ilikuwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu. Nilitimiza miaka 65 ya maisha yangu. Ninavyoingia mwaka wa 66, ninamshukuru Mungu kwa kuniweka hai na mwenye uwezo wa kutekeleza majukumu yangu kama nilivyozoea.

Uhai na afya ni baraka kutoka kwa Mungu. Nitaendelea kutumia fursa hii, ambayo ni dhamana, kwa kufanya kazi zangu za kufundisha kwa juhudi yote na uadilifu, kusoma kwa bidii, na kuandika ili kuuneemesha ulimwengu kwa elimu.

Nawaombeni ndugu na marafiki mniombee ili nizingatie mwelekeo huo, nami nawaombea baraka na mafanikio.

Tuesday, September 13, 2016

Utangazaji wa Vitabu

Mara kwa mara, katika blogu hii, ninaandika kuhusu vitabu. Ninaongelea masuala kama uandishi wa vitabu, uchapishaji, na uuzaji. Mara kwa mara ninaviongelea vitabu kwa namna ya kuvitambulisha kwa wasomaji wa blogu hii, na pia kujiwekea kumbukumbu. Ninafurahi ninapopata taarifa kutoka kwa wasomaji wa blogu hii kuwa wamefuatilia taarifa zangu na kuvisoma vitabu nilivyoviongelea.

Ujumbe wa leo ninauelekeza kwa waandishi wa vitabu. Kama ilivyo desturi yangu, maelezo yangu yanatokana na uzoefu wangu kama mwandishi. Ujumbe wa leo ni mwendelezo wa yale ambayo nimewahi kuandika katika blogu hii.

Katika kutafiti suala hili la utangazaji wa vitabu, nimejifunza kuwa, kwa mwandishi, kuandika na kuchapisha kitabu si mwisho wa safari. Nimejifunza kutoka kwa waandishi na wachapishaji kwamba kwa namna moja au nyingine, mwandishi analo jukumu la kukitangaza kitabu chake.

Inaweza kutokea kwamba mchapishaji ana uwezo mkubwa wa kutangaza kitabu. Ana bajeti kubwa au mfumo wa kusambazia matangazo. Lakini, wachapishaji wengi hawana uwezo huo, au uwezo wao ni hafifu, na hivyo kumlazimu mwandishi abebe jukumu la kutangaza kitabu chake.

Hata kama mchapishaji ana uwezo mkubwa, mwandishi anayo pia nafasi ya kuchangia katika kukitangaza kitabu. Kwa hapa Marekani, jadi iliyojengeka ni kwa mwandishi kwenda sehemu mbali mbali kukitambulisha kitabu chake. Sehemu hizo zinaweza kuwa vyuo, maktaba, au maduka ya vitabu.

Ziara hizo, ambazo kwa ki-Ingereza huitwa "book tours," ni muhimu sana. Ratiba ya ziara hutangazwa kwenye vyombo vya habari mapema. Sehemu ambapo mwandishi ametegemewa kuja kuzungumzia kitabu, kama vile maktaba au duka la vitabu, panakuwa na matangazo pia. Wateja wanaofika hapo wanayaona matangazo hayo.

Kwa kuwa usomaji wa vitabu umejengeka katika utamaduni wa Marekani, ziara ya mwandishi huwavutia watu. Wakati mwandishi anapokuja, zinakuwepo nakala za kutosha za kitabu chake, ili watu wanaohudhuria waweze kununua nakala na kusainiwa na mwandishi.

Watu hapa Marekani wanapenda kusainiwa vitabu, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii. Mimi mwenyewe nimealikwa sehemu mbali mbali hapa Marekani kwenda kuongelea vitabu vyangu, hasa Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Njia nyingine muhimu kwa mwandishi kutangaza vitabu vyake ni kushiriki maonesho ya vitabu. Hapa Marekani kuna maonesho ya vitabu mara kwa mara, kwenye maeneo mbali mbali ya nchi. Mengine huwa ni ya sehemu fulani ya nchi, na mengine huwa ni ya kitaifa. Nimeshiriki maonesho haya mara kwa mara, na nimekuwa nikiandika taarifa katika blogu hii na pia blogu ya ki-Ingereza.

Mwandishi anaweza kulipia matangazo katika vyombo vya habari. Lakini kutokana na uzoefu wangu, ninasita kupendekeza utangazaji wa aina hii. Ni bora mwandishi atumie njia zisizo na gharama. Kwa mfano, mwandishi anaweza kupeleka nakala za kitabu chake kwa wahakiki, ili wasome na kuandika uchambuzi katika magazeti.

Vile vile, tuzingatie kuwa tunaishi katika dunia ya mitandao, ambayo imeleta fursa nyingi. Kwa mwandishi mwenye blogu au tovuti, ni rahisi kutangaza kitabu chake. Mimi mwenyewe ninafanya hivyo katika blogu zangu na katika tovuti ya Africonexion. Vile vile tekinolojia za uchapishaji zinatuwezesha kuchapisha moja kwa moja mtandaoni, na vitabu vikapatikana huko, kama ilivyo kwa vitabu vyangu.

Hata hivyo kuna aina ya utangazaji ambayo huenda ni muhimu kuliko zote. Hii ni aina ya utangazaji unaofanywa na wasomaji. Kama ilivyo katika biashara yoyote, wateja ni watangazaji wakuu. Mteja akiridhika au kufurahi, anakuwa mpiga debe mkuu wa bidhaa au huduma.

Sisi wote tunafanya utangazaji wa bidhaa na huduma. Tukiona filamu nzuri, tunawaambia wenzetu. Tukinunua simu bora, tunawaambia wenzetu. Tukiwa katika mji mgeni, tukataka kujua nyumba bora ya kufikia wageni, au hoteli nzuri, wenyeji au madreva wa teksi watatuelekeza. Tunafanya kibarua cha kutangaza bidhaa za watu bila malipo.

Na vitabu ni hivi hivi. Msomaji akishasoma kitabu akakipenda, hakosi kuwaambia wengine. Hivi ndivyo kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kilivyoenea kwa kasi hapa Marekani. Baadhi ya wasomaji wangu ambao wamekuwa wapiga debe wangu nimekuwa nikiandika habari zao katika blogu hii.

Utangazaji huu unaofanywa na wateja walioridhika au kufurahi unaaminika sana. Sisi sote tukiambiwa na marafiki au ndugu zetu kuhusu ubora wa bidhaa fulani au huduma fulani tunaamini bila kusita. Tunaweza kuwa na wasi wasi na matangazo yanayowekwa na watu tusiowajua katika vyombo vya habari. Huenda tunahisi kwamba wafanya biashara hawaangalii maslahi yetu bali yao wenyewe, na wako tayari hata kutuuzia bidhaa mbovu. Lakini tunajua kuwa marafiki au ndugu zetu wanazingatia maslahi yetu. Hii ndio sababu utangazaji unaofanywa na wateja una umuhimu sana.

Pamoja na yote niliyosema hapa juu, uamuzi wa kukitangaza kitabu unaweza kuwa na utata. Kwa upande moja, kitabu kikishachapishwa, kuna umuhimu wa kukijulisha kwa jamii. Kwa upande mwingine, kuna busara ya wahenga kuwa chema chajiuza; kibaya chajitembeza. Je, mwandishi afanyeje? Kwa mtazamo wangu, ni juu ya kila mwandishi kutafakari suala hili na kufanya uamuzi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...