Monday, April 6, 2015

Bemidji Yamwenzi Mary, Mke wa Hemingway

Jioni ya tarehe 4 Aprili, baada ya kurejea kutoka Leech Lake Tribal College karibu na mji wa Bemidji, niliingia mtandaoni nikiwa na lengo la kuona kama kuna taarifa zozote kuhusu mkutano wetu. Katika ukurasa wa Facebook wa Chuo, niliona taarifa na picha za mkutano ule:

Hilo lilinivutia. Lakini niliona pia taarifa nyingine, kuhusu namna mji wa Bemidji unavyomwenzi Mary Welsh, aliyekuwa mke wa nne na wa mwisho wa Ernest Hemingway. Mary Welsh alizaliwa karibu na Bemidji akakulia na kusoma mjini hapo.

Kisha alienda kusoma katika Chuo Kikuu cha Northwestern karibu na Chicago. Alikuja kuwa mwandishi katika magazeti hapo Chicago na hatimaye London, akajipambanua kama mwandishi wa habari za vita. Huko ndiko alikokutana na Ernest Hemingway na baadaye wakafunga ndoa.

Nilifahamu hayo yote na mengine mengi, kutokana na utafiti wangu wa miaka kadhaa. Nilifahamu tangu zamani kuwa Mary Welsh alizaliwa eneo la Bemidji, na nilikuwa nawazia kwenda kule kufanya utafiti juu yake. Mary Welsh Hemingway alitanguzana na Ernest Hemingway katika safari ya Afrika Mashariki mwaka 1953-54. Walizunguka Kenya, Tanganyika, hadi Uganda, ambako walipata ajali mbili za ndege, mfululizo.

Mary Hemingway alisafiri hadi Mbeya, na ameelezea hayo na mengi mengine katika kitabu chake kiitwacho How it Was. Nasikitika kuwa wa-Tanzania, kwa kukosa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu, hawafahamu hayo. Wangekuwa wana utamaduni huo, wangeweza kutumia habari na maandishi kama haya ya Mary Welsh Hemingway na Hemingway mwenyewe kwa manufaa makubwa, hasa katika utalii. Hali ni mbaya kwamba wa-Tanzania hawashtuki wakielezwa habari za vitabu namna hii. Nimethibitisha hayo, kama nilivyoandika katika blogu hii.

Wenzetu katika nchi kama Cuba, Hispania na Marekani wanafaidika sana na maandishi ya Hemingway. Cuba wanaitunza sana nyumba ya Hemingway, Finca Vigia, na hata baa alimokuwa anakunywa, mjini Havana, ni kivutio kikubwa cha watalii. Kule Hispania kuna mji wa Pamplona ambao ulipata umaarufu duniani na umaarufu huu unaendelea, baada ya Hemingway kuutembelea na kuangalia mchezo wa "bull fighting," akaandika juu yake katika riwaya iitwayo The Sun Also Rises. Maelfu ya watalii wanafurika Pamplona. Hapa Marekani, nyumba alimoishi Hemingway, kama vile kule Oak Park (Illinois)na Key West (Florida), ni vivutio vikubwa kwa watalii.

Hayo ndio yaliyonijia akilini wakati nasoma taarifa ya mji wa Bemidji kumwenzi Mary Welsh Hemingway. Jambo moja kubwa lililoelezwa katika taarifa ile ni utunzi wa tamthilia juu ya Mary Welsh Hemingway, unaofanywa na Catie Belleveau baada ya utafiti wa muda mrefu.

Hoja sio kwamba ni lazima nasi tujitose na kujishughulisha na Hemingway na mke wake, ingawa kufanya hivyo kungetuletea manufaa kama wanayopata wenzetu wa Cuba, Pamplona, Oak Park na Key West. Ninachotaka kusisitiza ni umuhimu wa kujifunza kutoka kwa hao wenzetu.

Sisi tunao waandishi maarufu kama Mgeni bin Faqihi wa Bagamoyo, aliyetunga Utenzi wa Ras il Ghuli. Je, tunajua habari zake? Tunaye Shaaban Robert. Je, ni wa-Tanzania wangapi wanajua angalau mahali alipozaliwa, sehemu alimoishi, na mahali alipozikwa? Je? wahusika katika wizara za utalii na utamaduni wanafahamu habari hizo? Na je, wanafahamu kuwa taarifa hizo ni hazina ambayo tungeweza kuitumi? Binafsi ninatekeleza wajibu wangu kwa kuandika kuhusu mambo haya, kama nilivyofanya katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, ambacho nitashangaa kikipata wasomaji Tanzania.

Saturday, April 4, 2015

Nimerejea Salama Kutoka Leech Lake Tribal College

Nilirejea jana jioni kutoka Leech Lake Tribal College, kwenye mkutano kuhusu "Narratives of Identity." Nilikuwa mmoja wa wanajopo wanne waliotoa mada, na mada yangu ilikuwa "Being African in America."

Niliongelea uzoefu wangu katika miaka mingi ya kuishi na kufundisha hapa Marekani, nikielezea kazi kubwa isiyoisha ya kujitambulisha kama mu-Afrika, ambaye ni tofauti na mu-Amerika Mweusi. Nilielezea jinsi suala hilo linavyosabisha mikanganyiko na kutoelewana baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika tuishio Marekani.

Nilisema wazi kuwa namna wanavyojiita na kujitambulisha wa-Marekani Weusi ni tofauti na namna tunavyojiita na kujitambulisha sisi wa-Afrika. Nilimnukuu Chimamanda Ngozi Adichie wa Nigeria ambaye katika mahojiano na katika riwaya yake maarufu ya Americanah, ameelezea vizuri suala hilo.

Nilimnukuu pia mwandishi Jamaica Kincaid wa Antigua, pande za Caribbean, ambaye pamoja na kuwa ni mweusi pia, hakuwahi kujiita kama wanavyojiita  wa-Marekani Weusi. Hayo mawazo yake niliyasoma katika mahojiano yaliyochapishwa mwaka 1991 katika jarida la Mississippi Review.

Nilisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki ya kila jamii kujiita au kujitambulisha kwa majina wanayoyataka au yanayowaridhisha wenyewe. Watu wengine sherti wafuate njia hiyo badala ya kuwapachika watu majina ya utambulisho kama walivyofanya wakoloni.

Nilienda mbali zaidi na kuelezea suala la haki ya kila jamii kujieleza wenyewe, sio kuzimishwa kama walivyotuzimisha wakoloni, na wao wakawa wanaandika juu yetu.

Siwezi kuelezea hapa yote niliyosema. Nawazia kuendelea kutafakari suala hilo na kujisomea zaidi, na kuwasoma upya watu kama Frantz Fanon, Aime Cesaire, na Ngugi wa Thiong'o, ili hatimaye niandike makala kamili.

Hiyo jana, wakati nilipokuwa najitambulisha mkutanoni, nilisema kuwa nimeleta vitabu vyangu viwili kama zawadi kwa maktaba ya chuo cha Leech Lake Tribal College. Vitabu hivyo ni Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales. Vitabu hivi vilipokelewa kwa furaha na shukrani tele.

Nina hakika kuwa mkutano ule umesisimua watu. Jana hiyo hiyo, katika ukurasa wa Facebook wa Leech Lake Tribal College iliandikwa taarifa hii:

We had some great speakers on campus today for the Narratives of Identity presentations. One of the many memorable remarks from today's visit was by Joseph Mbele, St Olaf College- “I am not a person of color. I am Tanzanian which is a concept of colonization. Only when I came to America was I referred to as black. Naming yourself, knowing yourself, is a right…Construction of identities are not fixed and it’s our right to identify ourselves.”

(Picha ya juu kabisa na ya katikati ni kutoka Leech Lake Tribal College)

Thursday, April 2, 2015

Mijadala Kuhusu Vitabu Katika Maktaba ya Bemidji, Minnesota

Ni usiku saa saba kasoro, nami nimo chumbani mwangu katika Hampton Inn hapa mjini Bemidji. Ninasoma gazeti la hapa liitwalo "The Bemidji Pioneer" la jana, yaani tarehe 2.

Nimevutiwa sana na habari kuhusu utaratibu walio nao katika mji huu wa kukusanyika katika maktaba yao na kufanya mijadala kuhusu vitabu. Nanukuu habari nzima, ambayo iko ukurasa wa 2:

Public Library book discussion set

BEMIDJI--The Bemidji Public Library offers a monthly book discussion program--the next session will take place at noon April  13. The program will run for approximately an hour.

The book for discussion will be "The Devil in the White City: Murder, Magic and Madness at the Fair that Changed America" by Eric Larson.

Nimejikuta nawazia mengi. Je, utaratibu wa aina unawezekana katika miji ya Tanzania? Kuna maktaba katika miji kama Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Mwanza, Iringa, Songea, Lushoto, Mbinga, Karatu, na Mbulu. Hizo nimeziona mwenyewe, sio za kusikia.

Je utaratibu wa kuchagua na kujadili kitabu fulani kila mwezi unawezekana? Tusianze kutoa visingizio. Makampuni ya vitabu kama Mkuki na Nyota, Tanzania Publishing House, Dar es Salaam University Press, Ndanda Mission Press, na E&D Publishers yamechapisha na yanaendelea kuchapisha vitabu vingi sana.

Kampuni ya Mkuki na Nyota, kwa mfano imekuwa ikichapisha  vitabu vya Shaaban Robert kwa wingi, na kwa jamii yetu inayodai kuwa inakienzi ki-Swahili, mtu ungetegemea kuwa vitabu hivyo vinawindwa kama tunavyowinda kitimoto au bia za baridi.

Kuhusu gharama, wa-Tanzania kwa ujumla hawawezi kushindwa kuvinunua. Angalia jinsi wanavyochangia sherehe, jinsi wanavyofurika kwenye mechi za kabumbu, jinsi wanavyofurika kwenye burudani mbali mbali. Hela sio tatizo; ziko tele.

Nini kinazuia kuwepo katika jamii yetu kwa utamaduni kama huu wa jamii ya Bemidji wa kujadili vitabu?


Nimewasili Bemidji, Minnesota

Alasiri hii, nimewasili mjini Bemidji, nikiwa njiani na wenzangu watatu, ambao tumesafiri pamoja kutoka Minneapolis. Tutalala hapa, na kesho asubuhi tunakwenda Leech Lake Tribal College kwenye mkutano  kuhusu "Narratives of Identity." Mimi ni mmoja wa watoa mada wanne. Mada yangu itakuwa "Being African in America."

Tulipokuwa tunakuja, tulisimama kidogo katika mji uitwao Akeley, ili kuona sanamu ya Paul Bunyan, mhusika maarufu katika masimulizi ya jadi ya sehemu hii ya Minnesota, ambaye anajulikana sana pia Marekani na ulimwenguni. Sanamu hii inamwonyesha akiwa ameshika shoka lake. Ili kujionea jinsi sanamu hii ilivyo kubwa, ifananishe na sisi watatu ambao tumesimama hapo Mbele yake.


Tulipoingia Bemidji, tulikwenda moja kwa moja kwenye sanamu nyingine ya Paul Bunyan, ambayo inamwonyesha akiwa na fahali wake wa buluu ambaye ni sehemu muhimu ya masimulizi kuhusu mhusika huyu. Sanamu hiyo, sawa na ile ya Akeley, ni kubwa sana.

Kwa mujibu ya masimulizi, Paul Bunyan alikuwa jitu kubwa la ajabu, nadhani kumzidi hata Liongo Fumo, shujaa katika masimulizi ya jadi ya wa-Swahili, wa-Pokomo, na wengine katika mwambao wa Kenya.

Bemidji ni mahali ambapo niliwahi kufika miaka mitatu hivi iliyopita, lakini tangu muda mrefu kabla ya hapo nimetamani kuja kwa shughuli za utafiti wangu juu ya mwandishi Ernest Hemingway.

Mary Welsh, mke wa nne na wa mwisho wa Ernest Hemingway alizaliwa na kukulia eneo hili la Bemidji, kabla hajaenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Northwestern, karibu na Chicago. Katika safari zake Kenya, Tanganyika, na Uganda, mwaka 1953-54, Hemingway alitanguzana na mke wake huyu.

Panapo majaliwa, nitakuja Bemidji kufanya utafiti huo. Kwa leo nimefurahi kuziona hizi sanamu, na kujionea jinsi Paul Bunyan alivyo maarufu eneo hili. Jina lake liko kila mahali. Nimeona mtaa wenye jina hilo, biashara mbali mbali, hata kampuni ya mawasiliano ya intanenti.

Hata katika hoteli tunamolala usiku huu, Hampton Inn, nimeona picha kubwa ya Paul Bunyan katika ukuta wa mgahawa. Kwangu mimi kama mtafiti wa masimulizi na mambo mingine ya jadi ("folklore"), nimeguswa sana na kupata hamasa ya kufanya utafiti juu ya Paul Bunyan.


Wednesday, April 1, 2015

Tunahitaji Demokrasia, Lakini Tunahitaji Vyama vya Siasa?

Bila shaka tutakubaliana kuwa tunahitaji demokrasia, yaani mfumo wa utawala ambao ni wa umma, unaendeshwa na umma, kwa maslahi ya umma. Kwa ki-Ingereza wanasema "rule of the people, by the people and for the people."

Hii ndio maana na tafsiri ya demokrasia. Lakini je, tunahitaji chama cha siasa? Tunahitaji vyama vya siasa? Ni lini wa-Tanzania walikaa na kulitafakari suali hili? Kwa kweli hawajawahi kufanya tafakari hii. Badala yake wamekurupuka na wazo la chama au vyama, kikasuku tu.

Hata wale tunaowaita wasomi wetu nao wameshindwa kuhoji hali hii. Wameshindwa kujinasua kutokana na mtazamo huu, badala ya kufanya kile kinachoitwa kwa ki-Ingereza "thinking outside the box."

Nimeelezea zaidi huu ukurupukaji, mkanganyiko, na ukasuku wa wa-Tanzania katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Sunday, March 29, 2015

Chama cha Kijamaa na Uzalendo Tanzania (C.K.U.T.)

Nimeona leo katika mtandao wa Facebook kuwa kuna chama kipya cha siasa ambacho kinawania usajili. Kinaitwa Chama cha Kijamaa na Uzalendo Tanzania (C.K.U.T.).

Kama ni chama cha Kijamaa, kitanifurahisha, tofauti na CCM, chama ambacho kinahujumu ujamaa na mapinduzi kwa ujumla, kama yalivyoelezwa katika "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na maandishi mengine.

Kuanzisha chama au kujumuika na wengine katika chama kwa misingi ya amani ni moja ya haki za binadamu. Na mimi nina haki ya kuwa nilivyo, raia ambaye si mwanachama wa chama cho chote cha siasa, haki ambayo inahujumiwa na katiba ya Tanzania iliyopo kwa kuwa inaniwekea vikwazo nikitaka kugombea uongozi katika siasa.

Pamoja na yote, ninapenda tu kusisitiza kuwa vyama vya siasa vijitegemee. Tutengue sheria ya kuvipa ruzuku, kama nilivyoandika katika blogu hii.

Saturday, March 28, 2015

Vyama vya Siasa Vijitegemee

Ninaandika ujumbe huu kwa wa-Tanzania wenzangu. Ninatoa hoja kuwa vyama vya siasa vijitegemee. Tuachane na utaratibu wa sasa wa serikali kuvipa ruzuku vyama vya siasa. Nimeweka picha yangu hapa kuthibitisha kuwa ninayeandika ujumbe huu ni mimi, si "anonymous."

Fedha inayotolewa na serikali kama ruzuku kwa vyama vya siasa ni kodi ya walipa kodi wote, na wengi wao si wanachama wa chama cho chote cha siasa. Ruzuku hii ni hujuma dhidi ya hao walipa kodi ambao si wanachama wa chama cho chote cha siasa. Ni hujuma, ingawa imehalalishwa kisheria. Sheria na haki si kitu kile kile. Ukaburu ulikuwa halali kisheria, lakini ulikuwa ni hujuma dhidi ya haki.

Fedha inayotolewa kwa vyama hivi ni nyingi sana, mamilioni mengi ya shilingi kila mwezi. Ni fedha ambazo zingeweza kununulia madawati na vitabu mashuleni, kulipia mishahara ya walimu au madaktari, kukarabati barabara, kuwanunulia baiskeli walemavu wanaotambaa chini, kujenga maghala ya kuhifadhia mahindi ambayo yanaoza katika mikoa kama vile Ruvuma, na kadhalika.

Kutoa ruzuku kwa chama kimoja tu, kama kingekuwepo kimoja tu, tayari ni hasara na hujuma. Sasa tunavyo vingi, na hasara ni kubwa mno. Utitiri wa vyama unavyoongezeka, hali itazidi kuwa mbaya. Huduma za jamii zitaendelea kuzorota, na hata kutoweka, kwa fedha kutumika kama ruzuku kwa vyama vya siasa.

Kama kweli vyama hivi vina maana kwa wanachama wao, wanaweza kuvichangia vikastawi bila tatizo. Vyama kama Simba, Yanga, Maji Maji, na Tukuyu Stars havitegemei ruzuku. Wanachama, kwa mapenzi waliyo nayo kwa vyama vyao, wanaviwezesha kuwepo na kustawi, na hawako tayari vitetereke. Wako tayari kuvichangia wakati wowote ikihitajika. Nini kitawazuia wanachama wa vyama vya siasa kufanya vile vile, kama kweli vyama hivi vina maana kwao?

Sisi raia ambao si wanachama wa vyama vya siasa tuna wajibu wa kuanza kampeni ya kushinikiza itungwe sheria ya kufuta ruzuku kwa vyama vya siasa, ili kuokoa fedha, ziweze kutumika kwa huduma muhimu kwa jamii yetu.

Kama umevutiwa na makala hii na ungependa kufuatilia zaidi mawazo yangu ya kichokozi na kichochezi, utayapata kwa wingi katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...