Ingawa nimetumia masaa mengi katika shughuli hiyo, kwangu si kitu, nikifananisha na kazi niliyofanya kwa miaka yapata ishirini na tatu katika kukiandaa kitabu hiki, tangu kuzitafuta na kuzirekodi hadithi, kuziandika kwa kuzitafsiri kwa ki-Swahili, kuzitafsiri kwa ki-Ingereza, kuzichambua, kusoma nadharia mbali mbali ili kutajirisha uchambuzi, na kurekebisha tafsiri na uchambuzi tena na tena.
Bahati ni kwamba miaka ya sabini na kitu, nilianza pia kufundisha somo la fasihi simulizi ("Oral Literature") na nadharia ya fasihi (Theory of Literature") katika idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika kufundisha nilijionea mwenyewe kuwa hapakuwa na kitabu nilichoona kinafaa kwa somo la fasihi simulizi kwa wanafunzi wa kiwango cha chuo kikuu. Kuna usemi kuwa kama kitabu unachosoma huridhiki nacho, andika hicho kitabu unachokitaka.
Hali hiyo ya kukosekana kitabu kilichofaa katika ufundishaji wangu ilinihamasisha kutafakari masuala niliyokuwa nakumbaba nayo katika kuandika kitabu changu. Nilipania kuwa kiwe kinafaa kwa kufundishia. Miaka ilipita, nami nikawa natafiti, natafakari, na kuandika kiasi nilivyoweza. Wakati huo huo, nilikuwa nahangaika kuziboresha tafsiri za hadithi katika muswada. Shughuli hii ilinifundisha mengi kuhusu tafsiri, kama nilivyogusia katika makala iliyochapishwa katika jarida la Metamorphoses.
Historia ya kitabu hiki ni ndefu, na labda nitaweza kuiandika kiasi fulani siku za usoni. Ninakumbuka, kwa mfano, kwamba nilipokuwa nasomea masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin, 1980-86, nilichukua somo la nadharia ya fasihi katika idara ya "Comparative Literature" lililofundishwa na Professor Keith Cohen. Kati ya nadharia tulizojifunza ni "Structuralism." Professor Cohen alitupa "homework" ya kuchambua hadithi yoyote kwa kutumia nadharia ya "Structuralism."
Nilitumia fursa hii kuichambua hadithi ya "The Tale of Two Women," ambayo imo katika Matengo Folktales. Mtu anayefahamu angalau kidogo nadharia ya "Structuralism" ataona athari zake, japo kidogo, katika uchambuzi wangu.
Baada ya harakati za aina aina kwa miaka mingi, nilichapisha kitabu hiki mwaka 1999. Ndoto yangu ya kuandika kitabu cha kutumiwa katika ufundishaji wangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam haikutimia nilivyotarajia. Niliondoka Tanzania mwaka 1991, nikaja kufundisha katika idara ya ki-Ingereza Chuoni St. Olaf, huku nikiwa bado naufanyia kazi mswada wangu. Kwa hivi kitabu kilichapishwa huku Marekani, na wanaokisoma ni wa-Marekani, kuanzia katika jamii hadi vyuoni, kama nilivyoelezea hapa na hapa.
Masimulizi ni mengi, na kama nilivyogusia, labda nitafute wasaa miaka ijayo niandike kumbukumbu zangu za historia ya kitabu hiki.


