Monday, June 27, 2016

Masuali Kuhusu Uislam Kutoka Katika Blogu ya Kimbilia

Nimeshaandika mara kwa mara kuwa blogu yangu hii ni uwanja huru wa fikra, mawazo, na mitazamo. Ninakaribisha mijadala, na hoja za kuchangamsha bongo, wala sijali kama zinawatatiza watu. Ninasimamia uhuru wa watu kutoa mawazo.

Dini ni mada mojawapo ninayopenda kuona inajadiliwa. Wakati wengi wanaamini kuwa tujiepushe na mijadala ya dini, mimi ninasema kuwa mijadala ya dini ni muhimu. Kwa msingi huo, leo ninaleta mada ya dini kwa staili ya pekee.

Siku chache zilizopita, niliona makala juu ya u-Islam katika blogu ya Kimbilia. Ni makala inayoibua masuali mengi juu ya u-Islam. Inastahili kusomwa na kujadiliwa. Kati ya masuala yanayotokana na makala hii ni suala la haki na uhuru wa mtu kuwa na dini, kutokuwa na dini, au kubadili dini. Binafsi, ninatetea uhuru na haki hiyo, kama nilivyotamka katika blogu hii.  Tangazo la kimataifa la haki za binadamu linatambua haki hiyo.

Ningependa kujua kwa nini watu waliojitoa katika u-Islam, kama vile Wafa Sultan, mzaliwa wa Syria, na Ayaan Hirsi Ali, mzaliwa wa Somalia, wanasumbuliwa na kutishiwa maisha yao. Je, huu ni msimamo wa u-Islam, au ni upotoshaji? Ni haki kumwingilia mtu uhuru wake wa kuamini dini aitakayo, au uhuru wake wa kubadili dini au kuishi bila dini? Masuala hayo na mengine yanajitokeza katika blogu ya Kimbilia. Bora tuyatafakari na kuyajadili.

Sunday, June 26, 2016

Nilivyokutana na Askofu Yakobo Komba (Yafunani)

Kati ya mambo ninayoyakumbuka sana ya ujana wangu ni jinsi nilivyokutana na Askofu Yakobo Komba, ambaye sasa ni marehemu. Alikuwa anajulikana zaidi kwa jina la Yafunani, ambalo ni jina la baba yake. Nilikutana na kuongea naye mwaka 1970, nilipokuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika seminari ya Likonde, mkoani Ruvuma, Tanzania.

Baada ya kusoma shule ya msingi Litembo, 1959-62, nilijiunga na seminari ya Hanga, mkoani Ruvuma, 1963-66, na baadaye seminari ya Likonde, 1967-70. Seminari hizi ni za Kanisa Katoliki. Zilikuwa zinachagua wanafunzi waliojipambanua kimasomo na kitabia katika shule zao. Pamoja na masomo ya kawaida ya shule zingine nchini, tulikuwa tunaandaliwa kuwa mapadri.

Kwa miaka yetu ile, ili kuwa padri ilikuwa lazima mtu afaulu masomo ya angalau kidatu cha nne, na baada ya hapo alikwenda kusomea falsafa na teolojia katika seminari kuu, kwa miaka kadhaa. Kanisa Katoliki lilihakikisha kuwa mapadri wana elimu ya shuleni kuizidi jamii waliyokuwa wanaihudumia. Miaka ile, elimu ya kidato cha nne ilikuwa ni elimu ya juu.

Nilipokuwa Hanga na Likonde, nilikuwa ninapenda sana kusoma. Kila siku, wakati wa mapumziko, nilikuwa napenda kwenda maktabani kusoma. Ninavyokumbuka, Hanga na Likonde zilikuwa na maktaba kubwa kuliko shule nyingine mkoani Ruvuma.

Kutokana na tabia yangu ya kusoma sana, nilifahamu mambo mengi, na nilikuwa na tabia ya kuwaelezea wanafunzi wengine mambo niliyokuwa ninayapata katika majarida, vitabu, na magazeti. Nilikuwa ninafahamu mambo kuhusu Kanisa Katoliki katika nyanja za historia na siasa ambayo hayakuniridhisha. Hayo sikuwa nawaambia wengine.

Yaliyonikera zaidi ni mawili. Kwanza ni matamko ya Papa ya karne kadhaa zilizopita kuruhusu uvamizi na uporaji wa nchi za mbali uliokuwa ukifanywa na mataifa ya Ulaya. Pili ni msimamo wa kanisa nchini Msumbiji juu ya harakati za ukombozi zilizokuwa zinaendelea nchini humo. Kanisa nchini Msumbiji lilikuwa likiwaasa waumini kutojihusisha na harakati za ukombozi.

Nilianza kuwa na mashaka kama kweli nitaweza kuwa padri. Nilifadhaika sana. Niliogopa kumwambia mkuu wa shule kuwa ninasita kuendelea na njia ya upadri. Niliogopa wazazi wangu, ambao walikuwa wa-Katoliki wa dhati, watajisikiaje. Nilisongwa sana na mawazo. Kilikuwa ni  kipindi kigumu sana kimawazo katika maisha yangu. Sikuwa na raha.

Siku zilivyokwenda, tukiwa kidato cha nne, nilijua kuwa itafika siku lazima ukweli ujulikane. Nilijipiga moyo konde, nikaenda kwa mkuu wa shule na kumweleza kwa kifupi kuwa ninajisikia kuwa sina wito wa upadre. Kama ninakumbuka vizuri, alinijibu vizuri akanishauri niendelee kutafakari.

Siku moja, ndipo akaja Askofu Yakobo Komba shuleni Likonde. Wote tulikuwa tunamwogopa sana. Niliingiwa na hofu kubwa mkuu wa shule aliponiambia kuwa  Askofu amekuja kuongea nami. Nilikuwa sijawahi kuongea na Yafunani ana kwa ana.

Nilikwenda ofisini. Nilishangaa alivyonipokea kwa utulivu. Ninakumbuka maneno aliyoniambia. Daima yamekuwa akilini mwangu. Alisema: Waalimu wako wamekuwa wakiniambia kuwa wewe ndiye mwanafunzi unayeongoza darasani, nami nilikuwa natarajia kuwa ukishakuwa padri, uwe sekretari wangu. Lakini walimu wameniarifu kuwa umebadili mawazo kuhusu upadri. Ingawa nilikuwa na mategemeo, Mungu ndiye anayejua na kuongoza. Tafadhali, kokote utakakoenda, zingatia kuishi na kufanya kazi kwa uaminifu kufuatana na mapenzi ya Mungu.

Kusema kweli, sikuamini kama huyu aliyekuwa anaongea nami kwa utulivu na upendo ni huyu huyu Yafunani tuliyekuwa tunamwogopa. Maneno yake na nasaha zake zilinituliza kabisa moyo wangu. Tangu hapo, niliishi nikiwa na utulivu wa moyo na mawazo. Niliendelea na kazi zangu za kusoma, kujiandaa kwa mtihani wa taifa wa kumaliza kidato cha nne. Tulifanya mtihani ule mwaka 1970, na matokeo yalipofika nilishika nafasi ya kwanza katika kufaulu katika seminari ya Likonde.

Ninavyokumbuka hayo, ninatambua wazi kuwa mambo ya kanisa yaliyonikera miaka ile hayako leo. Kanisa lilichukua mwelekeo wa kukiri makosa ya zamani, na kubadilika. Misimamo ya Kanisa Katoliki leo haina utata kwangu, bali ni ya kujivunia. Mfano halisi ni Laudato Si, waraka wa kichungaji wa Papa Francis.

Saturday, June 25, 2016

Ninasoma "A Moveable Feast"

Nina tabia ya kusoma vitu vingi bila mpangilio, na niliwahi kutamka hivyo katika blogu hii. Kwa siku, naweza kusoma kurasa kadhaa za kitabu fulani, kurasa kadhaa za kitabu kingine, makala hii au ile, na kadhalika. Sina nidhamu, na sijui kama kuna umuhimu wa kuwa na nidhamu katika usomaji.

Siku kadhaa zilizopita, niliandika katika blogu hii kuhusu vitabu nilivyochukua katika safari yangu ya Boston. Nilisema kuwa kitabu kimojawapo kilikuwa A Moveable Feast cha Ernest Hemingway. Ni kweli, nilikuwa ninakisoma, sambamba na vitabu vingine, makala na kadhalika. Matokeo yake ni kuwa inachukua muda kumaliza kitabu.

A Moveable Feast ni kitabu kimojawapo maarufu sana cha Hemingway. Wako wahahiki wanaokiona kuwa kitabu bora kuliko vingine vya Hemingway, ingawa wengine wanataja vitabu tofauti, kama vile A Farewell to Arms, For Whom the Bell Tolls, na The Old Man and the Sea. Hemingway alikuwa mwandishi bora kiasi kwamba kila msomaji anaona chaguo lake.

Ninavyosoma A Moveable Feast, ninaguswa na umahiri wa Hemingway wa kuelezea mambo, kuanzia tabia za binadamu hadi mandhari za mahali mbali mbali. Picha ninayopata ya mji wa Paris na maisha ya watu katika mji huo miaka ya elfu moja mia tisa na ishirini na kitu haiwezi kusahaulika. Ni tofauti na picha ya Paris tuliyo nayo leo.

Hemingway haongelei maisha ya starehe na ulimbwende. Watu wanaishi maisha ya kawaida, na wengine, kama yeye mwenyewe na mke wake Hadley, wanaishi maisha ya shida. Mara kwa mara Hemingway anaongelea alivyokuwa na shida ya hela, ikambidi hata mara moja moja kuacha kula ili kuokoa hela.

Inasikitisha kusikia habari kama hizi, lakini pamoja na shida zake, Hemingway anasisitiza kwamba Paris ulikuwa mji bora kwa mwandishi kuishi. Anasema kuwa gharama za maisha hazikuwa kubwa. Alikuwa na fursa ya kuwa na waandishi maarufu waliomsaidia kukua katika uandishi, kama vile Gertrude Stein, Ezra Pound, na Scott Fitzgerald.

A Moveable Feast, kama vile Green Hills of Africa, ni kitabu chenye kuongelea sana uandishi na waandishi. Hemingway anatueleza alivyokuwa anasoma, akitegemea fursa zilizokuwepo, kama vile duka la vitabu la Shakespeare and Company lililomilikiwa na Sylvia Beach. Anatuambia alivyowasoma waandishi kama Turgenev, Tolstoy, D.H. Lawrence, na Anton Chekhov. Anatueleza alivyokuwa anajadiliana na wengine kuhusu waandishi hao.

Hayo, kama nilivyogusia, yananikumbusha Green Hills of Africa, ambamo kuna mengi kuhusu uandishi na waandishi. Katika Green Hills of Africa, tunamsikia Hemingway akiongelea uandishi hasa katika mazungumzo yake na mhusika aitwaye Koritchner. Vitabu kama A Moveable Feast vinatajirisha akili ya msomaji. Si vitabu vya msimu, bali ni urithi wa kudumu kwa wanadamu tangu zamani vilipoandikwa hadi miaka ya usoni.

Toleo la A Moveable Feast ninalosoma ni jipya ambalo limeandaliwa na Sean Hemingway. Toleo la mwanzo liliandaliwa na Mary Welsh Hemingway, mke wa nne wa Hemingway. Kutokana na taarifa mbali mbali, ninafahamu kuwa kuna tofauti fulani baina ya matoleo haya mawili, hasa kuhusu Pauline, mke wa pili wa Hemingway. Sean Hemingway amerejesha maandishi ya Hemingway juu ya Pauline ambayo Mary hakuyaweka katika toleo lake. Bahati nzuri ni kuwa miswada ya kitabu chochote cha Hemingway imehifadhiwa, kama nilivyojionea katika maktaba ya JF Kennedy.

Jambo moja linalonivutia katika maandishi ya Hemingway ni jinsi anavyorudia baadhi ya mambo kutoka andiko moja hadi jingine, iwe ni kitabu au hadithi, insha au barua. Kwa namna hiyo, tunapata mwanga fulani juu ya mambo yaliyokuwa muhimu mawazoni mwa Hemingway. Mfano moja ni namna Hemingway anavyoelezea athari mbaya za fedha katika uandishi. Mwandishi anaposukumwa au kuvutwa na fedha au mategemeo ya fedha anaporomoka kiuandishi. Dhana hiyo ya Hemingway inanikumbusha waliyosema Karl Marx na Friedrich Engels katika The Communist Manifesto, yakaongelewa pia na wengine waliofuata mwelekeo wa ki-Marxisti, kama vile Vladimir Ilyich Lenin.


Wednesday, June 22, 2016

Mhadhiri wa Algeria Akifurahia Kitabu

Jana, katika ukurasa wangu wa Facebook, mhadhiri wa fasihi ya ki-Afrika katika chuo kikuu kimoja cha Algeria ameandika ujumbe kuhusu mchango wangu katika fasihi na elimu, akataja kijitabu changu, Notes on Achebe's Things Fall Apart. Hatufahamiani, isipokuwa katika Facebook.

Yeye ni mfuatiliaji wa kazi zangu za kitaaluma, na niliwahi kumpelekea nakala ya Notes on Achebe's Things Fall Apart. Ameandika:

Dear professor Joseph you're one of God's gifts to the world of literature and education. I always keep praying for you when I read you book Notes On Achebe's TFA. I love you so much dear. Greetings from Algeria.

Kwangu ujumbe huu ni faraja, hasa kwa kuwa unatoka kwa mhadhiri wa somo ambalo ndilo nililoandikia mwongozo. Ninafurahi kuwa mawazo yangu yanawanufaisha watu Algeria. Kijitabu hiki niliwahi kukiongelea katika blogu hii, nikataja kilivyoteuliwa kama mwongozo kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Cornell.

Taarifa za aina hii hazinifanyi nitulie na kujipongeza, bali napata motisha ya kuendelea kusoma, kutafakari, na kuandika. Kuandika miongozo ya kazi ya fasihi ni jukumu ambalo nimeendelea kulitekeleza, kama nilivyoandika katika blogu hii.

Saturday, June 18, 2016

Nimepitia Tena Duka la Half Price Books

Leo nilimpeleka profesa mwenzangu Mall of America na halafu St. Paul ambako atakaa siku kadhaa. Wakati wa kurudi, niliamua kupita mjini Apple Valley kwa lengo la kuingia katika duka la vitabu la Half Price Books ambalo nimekuwa nikilitaja katika blogu hii. Ingawa lengo langu lilikuwa kuona vitabu vya aina mbali mbali, hamu yangu zaidi ilikuwa kuona kama kuna vitabu juu ya Ernest Hemingway ambavyo sijaviona kabla.

Niliangalia sehemu vinapowekwa, nikaviona vitabu ambavyo ninavifahamu. Lakini, kuna kimoja ambacho sikuwa ninakifahamu, Paris Without End: The True Story of Hemingway's First Wife. kilichotungwa na Gioia Diliberto. Ninafahamu kiasi habari za huyu mke, ambaye jina lake ni Hadley, na nilimtaja siku chache zilizopita katika blogu hii. Niliwazia kukinunua, lakini badala yake niliamua kununua kitabu cha By-Line cha Ernest Hemingway, ingawa nilishanunua nakala miaka kadhaa iliyopita, bali niliiacha Dar es Salaam mwaka 2013.

By-Line ni mkusanyo wa makala alizochapisha Hemingway katika magazeti na majarida miaka ya 1920-1956. Baadhi ya makala zilizomo zilinigusa kwa namna ya pekee nilipozisoma kwa mara ya kwanza, miaka kadhaa iliyopita. Mifano ni insha iitwayo "The Christmas Gift" na barua ziitwazo "Three Tanganyika Letters." Sikuwa na hela za kutosha, nikanunua hiki kimoja.

Mtu mwingine anaweza kuhoji mantiki ya kununua nakala ya kitabu ambacho tayari ninacho, lakini kwangu hii si ajabu. Nakala iliyoko Dar es Salaam ina jalada jepesi, niliyonunua leo ina jalada gumu. Hiyo kwangu ni sababu tosha. Jambo la zaidi ni kuwa kuna vitabu ambavyo napenda niwe navyo mwenyewe nilipo, hata kama ningeweza kuviazima maktabani. Hii si ajabu, kwani kila binadamu ana mambo yake anayoyapenda na yuko tayari kuyagharamia.

Friday, June 17, 2016

Maktaba ya John F. Kennedy

Wanasema tembea uone. Siku chache zilizopita, nilikwenda Boston kwenye maktaba ya John F. Kennedy kuendelea na utafiti wangu juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Maktaba hii ina hifadhi kubwa kuliko zote duniani za maandishi na kumbukumbu zingine zinazohusiana na mwandishi huyu.

Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kuitembelea maktaba hii, ingawa taarifa zake nilikuwa ninazifahamu na picha za jengo hili nilikuwa nimeziona mtandaoni. Nilijisikia vizuri nilipolikaribia jengo hili na kuingia ndani, nikafanya utafiti kama nilivyogusia katika blogu hii.

Katika kutafakari ziara hii, nimekuwa nikiwazia tofauti iliyopo baina yetu wa-Tanzania na wenzetu wa-Marekani katika kuwaenzi waandishi wetu maarufu. Je, sisi tumefanya nini kuhifadhi, kwa mfano, kumbukumbu za Shaaban Robert? Tuna mkakati gani wa kutafuta na kukusanya miswada yake. Huenda iko, sehemu mbali mbali. Mfano ni barua zake ambazo zilizohifadhiwa na mdogo wake Yusuf Ulenge, kisha zikachapishwa.

Lakini je, tumefanya juhudi gani za kutafuta barua zingine za Shaaban Robert, labda na marafiki na washirika wake, kwa wachapishaji wake, kama vile Witwatersrand University Press. Tumefanya juhudi gani kutafuta miswada ya mashairi yake na ya vitabu vyake, huko kwa wachapishaji wake, kama hao Watersrand University Press, Macmillan, Thomas Nelson, na kadhalika?

Tumefanya juhudi gani kuvitafuta vitu vingine vyovyote vya Shaaban Robert, kama walivyofanya na wanavyoendelea kufanya wa-Marekani juu ya waandishi wao, kama huyu Ernest Hemingway? Ninasema hivi kwa sababu ninafahamu kuwa hifadhi kama hii ya Ernest Hemingway bado inaendelea kutafuta na kupokea kumbukumbu zaidi, kama vile barua. Sijui, labda iko siku tutaamka usingizini.

Thursday, June 16, 2016

Nimemshukuru Mzee Patrick Hemingway

Leo baada ya kurejea kutoka Boston, nimempigia simu Mzee Patrick Hemingway kumweleza angalau kifupi kwamba ziara yangu kwenye maktaba ya John F. Kennedy imefanikiwa sana. Nimejionea menyewe utajiri wa kumbukumbu zilizomo katika Ernest Hemingway Collection, kuanzia maandishi hadi picha. Nimemwambia kuwa wahusika walinikaribisha vizuri sana na kunisaidia kwa ukarimu mkubwa.

Nimemwambia kuwa nimejifunza mengi na nimemshukuru kwa kunitambulisha kwao. Amefurahi kusikia hayo. Ameniuliza iwapo niliwaachia nakala ya kitabu changu, yaani Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilijisikia vibaya kuwa sikuwa nimefanya hivyo, nikamwahidi kuwa nitawapelekea. Ni furaha kwangu kuona jinsi mzee huyu anavyokipenda kitabu changu, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii.

Jambo mojawapo nililomweleza ni namna nilivyoshtuka kuona jinsi Hemingway alivyokuwa mwandishi makini, aliyeandika sana, kama hifadhi inavyodhihirisha. Mzee Patrick Hemingway alikumbushia habari ambayo nilikuwa ninaifahamu, ya namna Mary Hemingway alivyofanikiwa kuleta shehena ya nyaraka kutoka nyumbani mwa Hemingway nchini Cuba na kuziweka katika maktaba ya John F. Kennedy. Akaongezea kuwa hali ya hewa katika sehemu za dunia kama Cuba si salama kwa nyaraka.

Nimefarijika kupata wasaa wa kumweleza Mzee Patrick Hemingway angalau kifupi juu ya mafanikio ya ziara yangu, naye amefurahi kusikia nilivyonufaika na ziara hiyo.


Wednesday, June 15, 2016

Vitabu Nilivyochukua Safarini

Ninaposafiri kwa basi au ndege, ninapenda kuchukua kitabu au vitabu. Kwa kuwa si mimi ninayeendesha hilo basi au ndege, ninakuwa na muda mwingi wa kujisomea. Siku tatu zilizopita, tarehe 12 Juni, nilisafiri kwenda Boston, nikiwa na kitabu cha A Moveable Feast cha Ernest Hemingway, na Kusadikika cha Shaaban Robert.

Nilichukua A Moveable Feast kwa sababu safari yangu ilikuwa ya kwenda kufanya utafiti juu ya Hemingway na pia kwa kuwa kitabu hiki, ambacho nilifahamu habari zake, nilikuwa nimeanza kukisoma miaka michache iliyopita, hata nikanukuu sehemu yake moja katika blogu hii. Niliona kuwa ingekuwa jambo jema kuendelea kukisoma katika safari yangu ya Boston.
Nilichukua kitabu cha Kusadikika, kwa kujiweka tayari endapo ningependa kusoma pia kitabu tofauti. Sioni kama ni lazima nimalize kusoma kitabu nikiwa safarini. Inatosha kusoma kiasi fulani.

Jana, nikiwa bado mjini Boston, nilitembelea sehemu iitwayo Harvard Square, ambayo niliifahamu zamani kuwa ni sehemu yenye maduka ya vitabu. Niliingia katika duka moja la vitabu. Niliangalia vitabu vingi, nikanunua kimoja kiitwacho Rethinking Architecture: A Reader in Cultural Theory, kilichohaririwa na Neil Leach.

Nilivutiwa nilipoona kuwa ni mkusanyo wa makala za wataalam wengi, wakiwemo Theodor Adorno, Gaston Bachelard, Roland Barthes, Georges Bataille, Jean Baudrillard, Walter Benjamin, Ernst Bloch, Helene Cixous, Gilles Deleuze, Jacques Derrida, Umberto Eco, Michel Foucault, Jurgen Habermas, Martin Heidegger, Hans-Georg Gadamer, na Fredrick Jameson,



Majina ya wataalam hao niliowataja tulikuwa tunayasikia na maandishi yao tukiyasoma, nilipokuwa masomoni Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, miaka ya 1980-86. Nilivutiwa kuona maandishi kama ya Walter Benjamin, "On Some Motifs in Baudelaire;" Gaston Bachelard, "Poetics of Space;" Martin Heidegger, "Building, Dwelling, Thinking;" Roland Barthes, "Semiology and the Urban;" Umberto Eco, "Function and Sign: The Semiotics of Architecture;" Fredrick Jameson, "Is Space Political?" Michel Foucault, "Space, Knowledge and Power (interview conducted with Paul Rabinow).

Kama nilivyogusia, nimevutiwa na juhudi ya mhariri wa Rethinking Architecture: A Reader in Cultural Theory kuzitafuta makala zinazohusu mada moja lakini kwa mitazamo mbali mbali kutoka uwanja mpana wa falsafa. Kwa jinsi ninavyowaheshimu wataalam ambao maandishi yao yamo katika kitabu hiki, nina imani kuwa hiki ni kitabu bora sana.

Monday, June 13, 2016

Ziarani Maktaba ya John F. Kennedy

Jana nimefika hapa Boston kwa lengo la kutembelea maktaba ya John F. Kennedy na kuangalia kumbukumbu za mwandishi Ernest Hemingway. Nilijua kwa muda mrefu kuwa maktaba hii inahifadhi idadi kubwa ya kumbukumbu, kama vile miswada, picha, na vitu vingine, kuliko maktaba nyingine yoyote duniani.

Leo nimeshinda katika kuangalia hifadhi hii.  Nilianzia na maonesho maalum "Hemingway Between Two Wars," yaliyomo katika maktaba kwa wakati huu, na yatadumu kwa miezi kadhaa. Nimefurahi kuona picha na dondoo muhimu kutoka katika maandishi ya Hemingway baina ya vita kuu ya kwanza na vita kuu ya pili.

Uchaguzi wa picha hizi na dondoo umefanywa kwa umakini. Zimewekwa kumbukumbu hizo kutoka kwenye vitabu kama A Moveable Feast, The Sun Also Rises, Death in the Afternoon,  A Farewell to Arms, Green Hills of Africa, na picha za Hemingway akiwa mwanafunzi, akiwa majeruhi wa vita, akiwa katika mchezo wa "bull fighting" nchini Hispania, akiwa na watoto wake wavulana watatu pande za Bimini, na kadhalika.

Kuna picha ambazo sijawahi kuziona kabla. Kwa mfano picha inayomwonyesha kijana Hemingway akiwa na msichana Hadley walipokuwa wachumba. Hadley alikuja kuwa mke wa kwanza wa Hemingway. Mfano mwingine ni picha ya Hemingway akiwa amelazwa katika hospitali mjini Milano, baada ya kujeruhiwa vibaya na mlipuko wakati wa vita.

Maktaba ya JF Kennedy kwanza kabisa inahifadhi kumbukumbu juu ya Rais John Kennedy na enzi zake. Mtu ukitaka kutafiti mambo kama "Cuban missile crisis" au historia ya "Peace Corps" maktaba hii ni mahali muhimu pa kufanyia utafiti. Maktaba ya JFKennedy ni moja ya maktaba nyingi za kumbukumbu za marais wa Marekani tangu zamani hadi sasa. Ni jadi yao. Ni jadi nzuri kwani wastaafu hao wanachangia elimu kwa watu wao na kwa ulimwengu, na wanaweka urithi wa thamani kwa vizazi vijavyo.

Hii ni mara yangu ya kwanza kuitembelea maktaba ya JF Kennedy. Sitegemei itakuwa mara ya mwisho. Nimejisajili kama mtafiti na nimepata kitambulisho cha mwaka mzima, kufuatana na utaratibu wao. Ninamshukuru Mzee Patrick Hemingway, msimamizi mkuu wa urithi wa Hemingway, kwa jinsi alivyowaandikia na kuwapigia simu wahusika wa hifadhi ya Hemingway akiwaeleza juu yangu. Nilifurahi kuwasikia, nilipofika leo, kuwa walishapata habari zangu kutoka kwake.

Thursday, June 9, 2016

Kitabu Andika Kwa Ajili Yako

Mara kwa mara ninapata ujumbe kutoka kwa watu wanaohitaji ushauri kuhusu uandishi wa vitabu. Baadhi wanakuwa wameshaandika miswada na wanatafuta ushauri kuhusu kuchapisha vitabu.

Wengine, baada ya kupata ushauri wangu ambao kwa kawaida unahusu uchapishaji wa mtandaoni, wanaulizia utaratibu wa malipo. Yaani wanataka kujua watalipwaje kutokana na mauzo ya vitabu vyao.

Ninakaribisha maulizo kuhusu masuala haya ya uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu, kama ninavyothibitisha katika blogu hii. Hapa ninapenda kusema neno la jumla kwa watu hao, hasa wanaowazia mauzo na malipo: kitabu andika kwa ajili yako.

Nimeona kuwa watu wana kiherehere cha kuchapisha vitabu na kuviuza, wajipatie fedha. Wanaamini kuwa wakishachapisha kitabu, kuna utitiri wa watu watakaonunua, na wao waandishi watajipatia fedha, na labda fedha nyingi.

Kwa ujumla, hii ni ndoto. Kwanza, ni waandishi wachache sana duniani wanaopata fedha kutokana na vitabu vyao za kutosha hata kumudu gharama za kawaida za maisha. Pili, tutafakari hali halisi ya mwamko wa jamii katika suala la kununua na kusoma vitabu. Je, tuna utamaduni wa kununua na kusoma vitabu? Wewe mwenyewe unanunua na kusoma vitabu? Kama sivyo, una sababu gani au una haki gani ya kudhani kuwa wengine watanunua kitabu chako?

Pamoja na yote hayo, ni kweli kuwa kama unaandika vitabu vinavyoitwa vya udaku, au vya mambo ya kusisimua hisia, kama vile mapenzi, kuna uwezekano kuwa vitanunuliwa. Lakini hivi ni vitabu vya msimu, au vitabu vya chap chap, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii. Havina thamani ya kuvifanya vidumu kama vinavyodumu vitabu vya akina William Shakespeare, Charles Dickens, Leo Tolstoy, au Shaaban Robert. Waandishi wa vitabu vya msimu wanaweza kujipatia fedha kiasi.

Kuna aina nyingine ya waandishi ambao nao wanaweza kujipatia fedha. Hao ni waandishi wanaofuata jadi mbaya ambayo imekuwepo Tanzania, ya watu kuandika vitabu na kuvisukumia mashuleni. Mashule yamekuwa kama majalala ya kupokea vitabu kiholela. Wahusika wanatafuta fedha na wanafunzi wanaathirika, kwa kuwa vitabu hivi havikidhi viwango vya hali ya juu kabisa vya taaluma na uandishi sahihi.

Tukiachilia mbali aina hizi za uandishi, tutafakari uandishi wa vitabu vya kuelimisha jamii, ambavyo havisukumwi na mahitaji ya shule. Tutafakari vitabu ambavyo mwandishi makini mwenye ujuzi fulani anaandika ili kuelezea yale anayoyajua kwa umahiri wote awezao. Ni aina ya uandishi unaotokana na msukumo wa ndani ya nafsi ya mwandishi, kiasi kwamba hawezi kutulia bila kuhitimisha kazi ya kujikomboa kutokana na msukumo huo.

Uandishi huo huwa ni kwa manufaa ya mwandishi mwenyewe. Ninaamini kuwa huo ndio uandishi wa dhati. Ndio uandishi wa kweli. Kitabu cha namna hiyo kikishachapishwa, haijalishi kama kinanunuliwa na kusomwa na yeyote. Mwandishi unakuwa umetua mzigo. Umejikomboa, na uko tayari kuanza shughuli nyingine, kama vile kuandika kitabu kingine.

Binafsi, nina ajenda yangu ya vitabu ninavyotaka kuandika. Siangalii kama vitasomwa au kama vitatumika mashuleni. Kuna vitabu vya fasihi ambavyo nimevisoma, ambavyo ninaviandikia tahakiki, kwa kupenda mimi mwenyewe, wala si kwa kusukumwa na mahitaji ya wengine.

Kwa mfano, kwa miaka mingi nilikuwa ninatafakari utungo wa Okot p'Bitek, uitwao Song of Lawino, na kuandika mawazo yangu, hadi hivi karibuni nikachapisha mwongozo, Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino. Vile vile, nilishawahi kuandika katika blogu hii kuwa ninataka kuandika mwongozo kuhusu kitabu cha Camara Laye kiitwacho The African Child. Ninaridhika kabisa na mtazamo wangu kwamba kitabu andika kwa ajili yako mwenyewe, na dhana hii nimeigusia kabla katika blogu hii.


Wednesday, June 8, 2016

Nimempigia Simu Mzee Patrick Hemingway

Leo, saa 12.52 jioni, nimempigia simu Mzee Patrick Hemingway, kumwarifu kuwa nimeshawasiliana na wahusika wa maktaba ya J.F. Kennedy kuhusu safari yangu ya kwenda kufanya utafiti. Nimemwambia kuwa nimepata majibu kutoka kwa wahusika sehemu zote mbili za hifadhi ya Hemingway.  Wote wameniletea maelezo ya taratibu za kufuata nitakapofika katika maktaba ile.

Nimemwambia kuwa nimefurahishwa na ukaribisho wao, na nimemshukuru kwa kunitia moyo katika azma yangu ya kwenda kwenye maktaba ile. Nimemwambia kuwa nimesoma taarifa ya yaliyomo katika maktaba ile, nikizingatia yanayohusiana na utafiti wangu, ambao ni juu ya Hemingway na Afrika.

Nimemkumbusha alivyoniambia kuhusu simba aliyehifadhiwa katika maktaba ya J.F. Kennedy, na kuwa ninangojea kwa hamu kumwona simba huyu ambaye amesimuliwa na Hemingway katika Under Kilimanjaro kama "Mary's lion." Mzee Patrick ameniambia kuwa simba huyu aliye maoneshoni si yule wa Mary, bali aliuawa na Clara Spiegel, na kwamba Sara Spiegel anaonekana katika picha mojawapo iliyomo katika kitabu cha Mary Hemingway, How It Was, picha ambamo naye yumo. Nimemwambia kuwa ninacho kitabu hiki, ila nimejifunza jambo jipya, kwani nilidhani ni simba wa Mary.

Nilivyomwambia kuwa ninapangia kuangalia zaidi miswada na nyaraka zinazohusiana na maandishi ya Ernest Hemingway kama Green Hills of Africa, Under Kilimanjaro, "Snows of Kilimanjaro," na "The Short Happy Life of Francis Macomber," Mzee Patrick alikumbushia chimbuko la hadithi hiyo, akamtaja John Patterson, na kisha akaongelea simba wa Tsavo ambao wamehifadhiwa Chicago katika Field Museum of Natural History.

Aliendelea kunielezea kuwa kuna mtaa mjini Tel Aviv ambao unaitwa Patterson, kwa heshima yake, kwani alikuwa ameshiriki vita kwenye eneo la mashariki mwa Mediteranean na kujipatia heshima katika nchi ya Israel. Mzee Patrick ameniambia pia kuwa Patterson alikuja kuishi California. Hayo ni mambo ambayo sikuwa ninayajua, lakini sasa ninayafuatilia. Inashangaza jinsi Mzee Patrick Hemingway alivyo na kumbukumbu, ingawa umri wake sasa ni miaka 88.

Tuligusia pia namna Ernest Hemingway alivyoanza kuvutiwa na Afrika. Mzee Patrick alianza kwa kusema kuwa Hemingway alisoma riwaya juu ya Afrika wakati alipokuwa kijana Paris. Hapo nilitaja jina la kitabu na mwandishi, yaani Batouala na mwandishi, yaani Rene Maran, tukaongelea mapitio ya Hemingway ya kitabu hiki, yaliyochapishwa mwaka 1922, na jinsi mtindo wa uandishi wa Maran ulivyochangia uandishi wa Ernest Hemingway mwenyewe.

Tulimaliza mazungumzo akinitakia safari njema, akaahidi kuwapigia simu wahusika wa maktaba ya J.F. Kennedy kuhusu ujio wangu, akasema pia niwasiliane naye kumweleza kuhusu ziara yangu. Mazungumzo yetu yalikuwa ya dakika kumi na mbili tu. Kama ilivyo kawaida yangu, nimeona niandike kumbukumbu hizi.

Thursday, June 2, 2016

Tafsiri ya Ubeti wa Kwanza wa "Kibwangai"

Niliandika katika blogu hii kwamba ninatafsiri kwa ki-Ingereza shairi la Haji Gora Haji liitwalo "Kibwangai." Baada ya kukabiliana na matatizo katika kila ubeti, nimeshatafsiri beti zote kumi na moja, na leo nimeona nioneshe nilivyojaribu kutafsiri ubeti wa kwanza. Ubeti huo unasema hivi:

Kuna hadithi ya kale, kwa babu nimepokeya
Kwa manyani zama zile, mkasa ulotokeya
Nilikuwa mwanakele, hayo nikazingatiya
Leo nawadokezeya, kwa nilivyoyafahamu

Mstari wa kwanza una sehemu mbili, kama ilivyo mistari mingine yote katika ubeti huu. Niliutafsiri mstari wa kwanza namna hii: "There is an age-old story, I got from grandfather." Katika hizo sehemu mbili, sehemu ya kwanza haikunipa tatizo. Tatizo lilikuwa katika sehemu ya pili,  "kwa babu nimepokeya."

Mtu ukitaka kuhifadhi mpangilio wa sentensi kama ulivyo, unaweza, na tafsiri inaweza kuwa "from grandfather I received," au "from grandfather I got," au "from my grandfather I received," au "from my grandfather I got." Mtihani hapo ni kuchagua tafsiri ambayo unaona ina ladha nzuri masikioni, na ni fupi iwezekanavyo, kulingana kwa kadiri iwezekanavyo na ufupi wa "kwa babu nimepokeya." Shairi limeandikwa kwa namna ya kubana matumizi ya maneno. Kwa kuzingatia hayo, nikaona tafsiri yangu ya mstari wa kwanza iwe "There is an age-old story, I got from grandfather."

Mstari wa pili ulikuwa ni mtihani pia. Kwanza niliutafsiri hivi, "To the monkeys that time, a calamity came down." Lakini baada ya siku kadhaa, nimebadili tafsiri hiyo na kuifanya iwe, "Among the monkeys that time, a calamity came down." Ningefurahi zaidi iwapo ningesema "Among the monkeys long ago," kwani "long ago" ni usemi uliozoeleka katika hadithi. Lakini nimeona nizingatie usemi wa "zama zile" kama ulivyo.

Hata hivi, tafsiri ya hiyo sehemu ya pili hainiridhishi, kwani kiuhalisi, tafsiri ya "mkasa ulotokeya" kwa kuzingatia ubeti ulivyoanza, ni "a calamity that occured." Sasa, kama ningetafsiri hivi, ningeharibu mantiki ya sentensi ya ki-Ingereza. Hapo tunaona jinsi muundo wa sentensi katika lugha moja unavyohitaji kuwa tofauti katika lugha nyingine ili tafsiri iwe ipasavyo.

Jambo jingine linalonifanya nisiridhike na tafsiri ya huu mstari wa pili ni pana zaidi, kwani maana kamili ya mistari miwili ya kwanza ya shairi hili ni "There is an age-old story I got from my grandfather, about a calamity that occured among the monkeys long ago."

Baada ya juhudi yote hii, leo nimepata wazo kuwa badala ya kutumia neno "story," nitumie "tale." Kwa hivi, baada ya kuandika makala hii, nitabadili tafsiri. Badala ya "There is an age-old story," itakuwa "There is an age-old tale."

Mstari wa tatu ulikuwa mgumu. Mwanzoni niliutafsiri hivi, "Mere child that I was, I kept this in mind." Lakini leo asubuhi nimeamua kubadilisha na kuwa "Though I was still a child, I kept it all in mind." Naona tafsiri hii ya leo ina mtiririko mzuri zaidi. Hiyo ni hisia yangu, na wengine wanaweza wakawa na hisia tofauti.

Mstari wa mwisho nao umekuwa mgumu sana kuutafsiri. Kwanza niliutafsiri hivi, "And today I am imparting to you, the things I understood." Lakini tafsiri hii haikuniridhisha. Sikuona namna ya kutafsiri "nawadokezeya" ambayo ingependeza masikioni. Ningeweza kutumia neno "hinting," lakini maana halisi ya neno hili katika mustakabali wa shairi hili si kudokeza tu, kwani inasimuliwa hadithi nzima.

Kwa hivi, matumizi ya neno "nawadokezeya" yanaleta utata, kwani shairi lenyewe si dokezo tu bali ni hadithi nzima. Narejea kwenye dhana ya Cleanth Brooks kwamba lugha ya ushairi ni "language of paradox." Na kwa kweli, mtiririko wa shairi la Kibwangai limejengeka katika misingi ya "paradox." Hilo suala nategemea kulifafanua siku za usoni.

Baada ya kuutafakari huu mstari wa mwisho wa "Kibwangai," leo nimefikia uamuzi wa kuutafsiri hivi "Today I share with you, of what I understood." Tafsiri hii inaweza kuwa inapwaya kidogo, kwa namna mbili. Kwanza, maana halisi ya "Leo nawadokezeya," ikiwa nje ya shairi hili, ni "Today I am hinting to you." Lakini, kama nilivyosema, shairi halidokezi tu, bali linasimulia hadithi nzima. Pili, kwa kuwa mshairi katumia dhana ya kudokeza, na mimi sikutaka kuififisha kabisa dhana hiyo, nimeamua kutumia "of what I understood." Kwa kufanya hivyo, huenda nimeleta mkanganyiko juu ya mkanganyiko.

Nategemea kuwa maelezo yangu haya, ingawa mafupi, na yanahusu ubeti moja tu, yanathibitisha kuwa kutafsiri shairi au kazi za fasihi kwa ujumla ni mtihani ambao unaweza kuumiza kichwa na bado usiwe na ufumbuzi wa kuridhisha. Pamoja na hayo yote, hadi hii leo, tafsiri yangu ya ubeti wa kwanza wa "Kibwangai" ni hii:

There is an age-old tale, I got from grandfather
Among the monkeys that time, a calamity came down
Though I was still a child, I kept it all in mind
Today I share with you, of what I understood.



Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...