Sunday, March 29, 2015

Chama cha Kijamaa na Uzalendo Tanzania (C.K.U.T.)

Nimeona leo katika mtandao wa Facebook kuwa kuna chama kipya cha siasa ambacho kinawania usajili. Kinaitwa Chama cha Kijamaa na Uzalendo Tanzania (C.K.U.T.).

Kama ni chama cha Kijamaa, kitanifurahisha, tofauti na CCM, chama ambacho kinahujumu ujamaa na mapinduzi kwa ujumla, kama yalivyoelezwa katika "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na maandishi mengine.

Kuanzisha chama au kujumuika na wengine katika chama kwa misingi ya amani ni moja ya haki za binadamu. Na mimi nina haki ya kuwa nilivyo, raia ambaye si mwanachama wa chama cho chote cha siasa, haki ambayo inahujumiwa na katiba ya Tanzania iliyopo kwa kuwa inaniwekea vikwazo nikitaka kugombea uongozi katika siasa.

Pamoja na yote, ninapenda tu kusisitiza kuwa vyama vya siasa vijitegemee. Tutengue sheria ya kuvipa ruzuku, kama nilivyoandika katika blogu hii.

Saturday, March 28, 2015

Vyama vya Siasa Vijitegemee

Ninaandika ujumbe huu kwa wa-Tanzania wenzangu. Ninatoa hoja kuwa vyama vya siasa vijitegemee. Tuachane na utaratibu wa sasa wa serikali kuvipa ruzuku vyama vya siasa. Nimeweka picha yangu hapa kuthibitisha kuwa ninayeandika ujumbe huu ni mimi, si "anonymous."

Fedha inayotolewa na serikali kama ruzuku kwa vyama vya siasa ni kodi ya walipa kodi wote, na wengi wao si wanachama wa chama cho chote cha siasa. Ruzuku hii ni hujuma dhidi ya hao walipa kodi ambao si wanachama wa chama cho chote cha siasa. Ni hujuma, ingawa imehalalishwa kisheria. Sheria na haki si kitu kile kile. Ukaburu ulikuwa halali kisheria, lakini ulikuwa ni hujuma dhidi ya haki.

Fedha inayotolewa kwa vyama hivi ni nyingi sana, mamilioni mengi ya shilingi kila mwezi. Ni fedha ambazo zingeweza kununulia madawati na vitabu mashuleni, kulipia mishahara ya walimu au madaktari, kukarabati barabara, kuwanunulia baiskeli walemavu wanaotambaa chini, kujenga maghala ya kuhifadhia mahindi ambayo yanaoza katika mikoa kama vile Ruvuma, na kadhalika.

Kutoa ruzuku kwa chama kimoja tu, kama kingekuwepo kimoja tu, tayari ni hasara na hujuma. Sasa tunavyo vingi, na hasara ni kubwa mno. Utitiri wa vyama unavyoongezeka, hali itazidi kuwa mbaya. Huduma za jamii zitaendelea kuzorota, na hata kutoweka, kwa fedha kutumika kama ruzuku kwa vyama vya siasa.

Kama kweli vyama hivi vina maana kwa wanachama wao, wanaweza kuvichangia vikastawi bila tatizo. Vyama kama Simba, Yanga, Maji Maji, na Tukuyu Stars havitegemei ruzuku. Wanachama, kwa mapenzi waliyo nayo kwa vyama vyao, wanaviwezesha kuwepo na kustawi, na hawako tayari vitetereke. Wako tayari kuvichangia wakati wowote ikihitajika. Nini kitawazuia wanachama wa vyama vya siasa kufanya vile vile, kama kweli vyama hivi vina maana kwao?

Sisi raia ambao si wanachama wa vyama vya siasa tuna wajibu wa kuanza kampeni ya kushinikiza itungwe sheria ya kufuta ruzuku kwa vyama vya siasa, ili kuokoa fedha, ziweze kutumika kwa huduma muhimu kwa jamii yetu.

Kama umevutiwa na makala hii na ungependa kufuatilia zaidi mawazo yangu ya kichokozi na kichochezi, utayapata kwa wingi katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Wednesday, March 25, 2015

Picha Nilizopigwa Katika Studio ya Afric Tempo, Machi 21

Tarehe 21 Machi, nilifanyiwa mahojiano na Ndugu Petros Haile Beyene, mkurugenzi wa African Global Roots, katika studio ya Afric Tempo mjini Minneapolis. Aliomba tufanye mahojiano kuhusu kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ambacho alikuwa amekisoma na kukipenda. Niliandika taarifa ya mahojiano hayo katika blogu hii.

Hapa naleta picha mbili alizopiga Ndugu Malick, mmiliki wa studio, aliyerekodi kipindi kwa ajili ya televisheni. Amenitumia leo hii. Hapa kushoto anaonekana Ndugu Petros Haile akiwa nami, tayari kwa mahojiano, ambayo watakaoyaona katika televisheni watayafurahia. Kama wasemavyo mitaani, kaeni mkao wa kula.

Nimeona niweke picha hizi hapa, nikizingatia kuwa wako ambao wangependa kuona sura yangu ilivyo kwa sasa, baada ya muda mrefu wa kuumwa. Ninaendelea kupona vizuri, ingawa pole pole. Hata safari kama hizi za Minneapolis, umbali wa maili 45, ninaendesha gari mwenyewe. Na majukumu yangu niliyozoea, kama vile kutoa mihadhara na kufundisha, nayamudu bila shida. Namtegemea Mungu daima; alichonipangia ndicho kitakachojiri.

Monday, March 23, 2015

Mwandishi Grace Ogot Amefariki

Wikiendi hii, habari zimetapakaa kuwa mwandishi Grace Ogot wa Kenya amefariki. Habari hizi zimenishtua na zimenikumbusha mengi kuhusiana na mwandishi huyu.

Nilipokuwa kijana, miaka ya sitini na kitu, ndipo nilianza kusikia habari zake. Nilikuwa nasoma masomo ya sekondari katika seminari ya Likonde. Shule ilikuwa na maktaba nzuri sana, chini ya usimamizi wa Padri Lambert, OSB, ambaye alikuwa mwalimu wetu wa ki-Ingereza na historia.

Nilikuwa msomaji makini wa vitabu, na nilikuwa nafuatilia kwa karibu uandishi katika Afrika Mashariki, Afrika, na sehemu zingine za dunia. Ndipo nilipoanza kuyafahamu maandishi ya Grace Ogot.

Riwaya yake, The Promised Land, ilikuwa na maana sana katika ujana wangu, kwani ilichangia kunifanya niipende zaidi fasihi. Hadithi fupi ya "The Rain Came" ilinigusa kwa namna ya pekee. Miaka ya mwishoni mwa sabini na kitu, wakati nafundisha katika Idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nakumbuka nilifundisha kitabu cha Gikuyu Folktales cha Grace Gecau. Humo niliona hadithi ambayo ilinikumbusha "The Rain Came," nikapata kuelewa vizuri jinsi Grace Ogot alivyotumia urithi wa hadithi za jadi katika uandishi wake.

Miaka ile nilikuwa navutiwa na waandishi wengine wa Afrika Mashariki, kama vile Okot p'Bitek, Taban lo Liyong, James Ngugi (ambaye baadaye alibadili jina lake na kujiita Ngugi wa Thiong'o), Austin Bukenya, Laban Erapu, Barbara Kimenye, na wengine kadha wa kadha.

Ile ilikuwa ni miaka ya kukumbukwa, kwani ni wakati ule ndio nami nilihamasika kuandika hadithi kwa ki-Ingereza. Nilifurahi kwa namna isiyoelezeka hadithi yangu ya "A Girl in the Bus" ilipochapishwa katika jarida maarifu la Busara, mwaka 1972, nilipokuwa mwanafunzi Mkwawa High School.

Kumbukumbu zote hizi, na nyingine kem kem zimenijia na zinazunguka kichwani mwangu tangu niliposikia kuwa Grace Ogot amefariki. Ametoa mchango uliotukuka katika fasihi. Astarehe kwa amani.

Sunday, March 22, 2015

Siendi Mahali Kuuza Vitabu

Mimi ni mwalimu, mwelimishaji, darasani na katika jamii. Ili kufanikisha majukumu yangu, ni mtafutaji wa elimu bila kuchoka. Ni mwanafunzi muda wote ili kujiimarisha katika ualimu na uelimishaji.

Nafundisha na kujufunza kwa kuongea na watu ana kwa ana, iwe ni darasani au nje ya darasa. Nafundisha na kujifunza kwa mawasiliano ya masafa marefu, iwe kwa barua pepe au kwa simu. Hivi karibuni, nimeanza pia kutumia Skpe. Hizi zote ni njia za kuelimisha sambamba na kujielimisha.

Lakini vile vile, mimi ni mwandishi wa makala na vitabu. Kwa kawaida uandishi wa nakala huchukua muda mwingi, na vitabu ndio zaidi, kwani kitabu kinaweza kuchukua miaka kukiandaa na kukiandika. Kwa ujumla unaandika katika upweke. Nakubaliana na kauli ya Ernest Hemingway, "Writing, at its best, is a lonely life."

Kwangu mimi kama mwalimu naona uandishi wa aina ya vitabu ninavyoandika kuwa ni mwendelezo wa ufundishaji. Ninapokwenda na vitabu vyangu kwenye tamasha au maonesho, ninakwenda kama mwalimu. Siendi kufanya biashara.

Ni tofauti na mvuvi anapoenda na tenga lake la samaki sokoni, au mkulima anapoenda na mkungu wake wa ndizi. Hao wanaenda kuuza samaki au ndizi. Ikifika mwisho wa siku hawajauza hizo samaki au ndizi, wanaona wameshindwa biashara siku hiyo, au wanaona wamepata hasara.

Mimi, pamoja na kuwa ninaenda maoneshoni na vitabu vyangu, nisipouza hata kimoja sioni kama nimeshindwa kwani ninakuwa nimeshaongea na watu wengi, kuwaelimisha na kuelimishwa nao. Wengine huulizia kuhusu uandishi au uchapishaji wa vitabu. Wengine huulizia kuhusu masomo ninayofundisha au kuhusu utafiti wangu. Niligusia masuala haya katika blogu hii.

Hutokea, mara kwa mara, kuwa katika kuongelea mambo hayo, watu hao hupenda wenyewe kununua vitabu vyangu. Labda wanataka kufahamu zaidi fikra na mitazamo yangu. Labda wanataka kumbukumbu ya kukutana kwetu na maongezi yetu. Na hapo ndipo linapoingia suala la watu kutaka kusainiwa kitabu. Ni kumbukumbu.

Nikirejea tena kwa mvuvi muuza samaki au mkulima na mkungu wa ndizi, sijui kama kuna watu wanapokuwa sokoni wanaenda kumwuliza mvuvi habari za uvuvi au wanaenda kwa muuza ndizi kupata elimu kuhusu kilimo cha ndizi. Na sijui kama muuza samaki mwenyewe au muuza ndizi mwenyewe anategemea hivyo.

Zaidi ya yote, mimi kama mwalimu sina masaa ya kazi. Najiona niko kazini muda wote, tangu asuhuhi mpaka usiku, labda tu ninapokuwa katika majukumu mengine ya binafsi, familia, au jamii. Kama siko darasani, niko ofisini, maktabani, au nyumbani, ninasoma. Niko mahali ninatayarisha masomo au ninasahihisha kazi za wanafunzi. Hakuna jamii hapa duniani ambayo inamlipa mwalimu kwa masaa yote hayo anayokuwa kazini.

Kwa kurudia, ninapokuwa maoneshoni na vitabu vyangu, niko pale kama mwalimu. Si mfanyabiashara, ambaye anahesabu mafanikio yake kwa kigezo cha fedha anachopata siku hiyo.

Saturday, March 21, 2015

Leo Nimehojiwa na "African Global Roots"

Nimerejea mchana huu kutoka Minneapolis, kwenye mahojiano na African Global Roots (AGR). Wiki mbili hivi zilizopita, Ndugu Petros Haile, mkurugenzi wa AGR alikuwa ameniomba tufanye mahojiano hayo.

Ndugu Haile nami tumefahamiana kwa miaka kadhaa. Nimewahi kushiriki katika program zake kwa kupeleka vitabu vyangu. Vile vile, alivyovyofahamu kuwa nimepeleka wanafunzi Tanzania kwenye kozi ya Hemingway, aliniomba niandike makala, ambayo aliichapisha.

Kwa mahojiano ya leo, Ndugu Haile alitaka tuongelee kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho alishakisoma miaka iliyopita. Alitamani, kwa kutumia mawasiliano ya AGR kusambaza ujumbe katika jamii ya wa-Afrika hapa Marekani na ulimwenguni na kwa watu wengine, kuhusu umuhimu wa kuyaelewa masuala ninayoongelea katika kitabu changu.

Kwa kuwa nilijua kuwa Ndugu Haile alitaka kunihoji kuhusu dhughuli zangu za kuelimisha umma, nilichukua pia nakala ya kitabu changu cha Matengo Folktales, ambacho ni ushahidi wa namna ninavyojitahidi kujifunza kutokana na masimulizi ya jadi ya mababu na mabibi zetu wa Afrika, na namna ninavyotumia hazina hii kuuelimisha ulimwengu kuhusu mchango wa wahenga wetu katika dunia.

Mahojiano yalikuwa mazuri. Ndugu Haile alitunga masuali muhimu kutokana na yaliyomo katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na pia aliniuliza masuali kuhusu utafiti wangu ulioniwezesha kuandika kitabu cha Matengo Folktales.

 Mahojiano haya tumefanyia katika kituo cha Afric Tempo, kinachomilikiwa na Ndugu Malick wa Senegal. Leo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufika mahali hapo, ambapo pana mgahawa, stoo, na studio ya kurekodia programu za televisheni.

Sitaandika zaidi kwa leo. Nangojea hadi mahojiano yatakapopatikana mtandaoni, ndipo niwaeleze walimwengu. Inafurahisha sana kuweza kukutana na kushirikiana na watu kama Malick na Petros, wenye kupenda kujitolea kwa hali na mali ili kujenga maelewano katika jamii. Jambo moja tuliloongelea leo na kukubaliana ni kuwa tunaamini kuwa Mungu ametuweka duniani kwa madhumuni kama hayo.


Wednesday, March 18, 2015

Neema Komba Ashinda Tuzo ya Uandishi

Neema Komba ni mwandishi chipukizi wa ki-Tanzania. Kama wewe ni mfuatiliaji wa uandishi wa Tanzania wa siku hizi, huenda tayari unafahamu habari zake. Mbali na uandishi, Neema ni mhamasishaji wa uandishi na sanaa husika kupitia jukwaa liitwalo la Poetista.

Mwaka 2011 Neema alichapisha kitabu cha mashairi yake, See Through the Complicated. Nilikisoma muda si mrefu baada ya kuchapishwa. Mwishoni mwa mwezi Julai, 2012, nilipokuwa Tanzania, tulikutana Lion Hotel, Dar es Salaam, tukaongelea uandishi wake.

Pamoja na mashairi, Neema ni mwandishi wa insha. Hivi karibuni nilianza kufahamu kuwa anaandika pia hadithi, niliposoma kuwa hadithi yake "Setting Babu on Fire" imeteuliwa kuwemo kati ya hadithi tatu zilizoteuliwa kushindania tuzo ya "Flash Fiction" ya Etisalat. Hayo yalikuwa mashindano makubwa ya uandishi barani Afrika. Hatimaye, "Setting Babu on Fire" imeshinda tuzo ya kwanza.




Ushindi huu ni sifa kubwa kwa Neema mwenyewe na kwa Tanzania. Nikizingatia kuwa huyu ni mwandishi chipukizi, lakini mwenye ubunifu wa hali ya juu na mwenye kukimudu vizuri ki-Ingereza, sina shaka kuwa nyota yake itazidi kutukuka na kung'ara miaka ya usoni. Nampa hongera sana na kumtakia kila la heri.

Sunday, March 15, 2015

Darasa la "Hemingway in East Africa 2013" Kando ya Ziwa Babati

Mwezi Januari, 2013, nilikuwa Tanzania na wanafunzi kutoka Chuo cha St. Olaf katika kozi ya "Hemingway in East Africa."

Niliitunga kozi hii mwaka 2006, kwa ajili ya Chuo cha Colorado. Kwa miaka kadhaa, kabla ya kutunga kozi hiyo, nilisoma maandishi ya Ernest Hemingway aliyoandika kufuatia safari zake mbili Afrika Mashariki, miaka ya 1933-34 na 1953-54.

Lengo la kozi lilikuwa kuwafundisha wanafanuzi kwa kusafiri nao katika baadhi ya maeneo alimopita Hemingway, huku tukisoma maandishi yake kuhusu safari zake katika maeneo haya. Maandishi hayo ni pamoja na kitabu cha Green Hills of Africa na Under Kilimanjaro, hadithi ya "The Short Happy Life of Francis Macomber," barua, na insha kadhaa katika magazeti.

Pichani wanaonekana wanafunzi na madereva wetu pembeni mwa Ziwa Babati. Katika Green Hills of Africa, Hemingway aliandika kuhusu Babati na Ziwa Babati:

     We left, soon after midnight, ahead of the outfit, who were to strike camp and follow in the two lorries. We stopped in Babati at the little hotel overlooking the lake and bought some more Pan-Yam pickles and had some cold beer (uk. 143).

Thursday, March 12, 2015

Vitabu Nilivyonunua Jana na Leo

Kila mtu ana mambo anayoyapenda sana, na yuko tayari kuyapata au kuyafanya kwa gharama yoyote. Vitabu ni kati ya vitu ninavyovipenda sana, na niko tayari kutumia gharama yoyote kuvipata. Imekuwa hivyo tangu nilipokuwa shule ya msingi.

Mara kwa mara, katika blogu hii, nimeandika taarifa ya vitabu nilivyonunua. Siandiki taarifa ya kila kitabu, kwani wakati mwingine nasahau. Lakini leo nimekumbuka. Naandika kuhusu vitabu nilivyonunua jana na leo.

Nilitoka zangu ofisini, nikaelekea kwenye duka la vitabu. Nje ya duka kulikuwa na "seli" ya vitabu. Kulikuwa na vitabu vingi sana vikiuzwa kwa bei nafuu. Hapo hapo nilijiunga na wengine waliokuwa wanavichambua vitabu hivyo na kuvinunua.

Jungu kuu halikosi ukoko. Niliviona vitabu vinne vilivyonivutia kwa namna ya pekee, nikavinunua.

Kimojawapo ni Wine to Water: How One Man Saved Himself While Trying to Save the World. Hilo jina tu lilinivutia, nikakumbuka hadithi ya muujiza wa Yesu wa kugeuza maji kuwa divai. Katika kukiangalia, niliona kuwa mtungaji wake, Doc Hendley, ameandika kitabu hiki kuelezea harakati zake za kuwasaidia watu wa Darfur kuchimba visima vya maji, akipambana na hatari zote zilizoko Darfur. Niliona kitabu hiki kitanifundisha mengi, na nilitaka kiwemo kati ya vitabu vya nyumbani mwangu.

Kitabu cha pili ni Walk in Their Shoes: Can One Person Change the World? kilichoandikwa na Jim Ziolkowski. Hicho nacho kilinivutia. Jina lake lilinikumbusha kitabu ambacho nilikinunua miaka michache iliyopita, kiitwacho Leaving Microsoft to Change the World: An Enterpreneur's Odyssey to Educate the World's Children, kilichoandikwa na John Wood. Mtu unaposoma vitabu vya aina hii, unajikuta ukijifunza sio tu uwezekano bali umuhimu wa kujitoa katika ubinafsi na badala yake kutumia vipaji na uwezo wako kuwanufaisha walimwengu.

Nilikiona kitabu kingine, And Then Life Happens: A Memoir, chenye jina la Auma Obama kama mwandishi, na picha yake. Hilo jina peke yake lilinifanya nikiangalie, nikaona kuwa huyu dada ni binti wa Barack Hussein Obama, baba mzazi wa Rais Obama wa Marekani. Binti huyu alizaliwa Kenya, akaishi miaka mingi na kusoma Ujerumani. Kitabu chake hiki, ambacho ni juu ya maisha yake, alikiandika kwa ki-Jerumani, kikatafsiriwa na Ross Benjamin. Nilivutiwa na taarifa hizo, nikakichukua bila kusita.

Kitabu cha nne nilichokinunua hiyo jana ni Indigenizing The Academy: Transforming Scholarship and Empowering Communities. Wahariri wake ni Devon Abbot Mihesuah na Angela Cavender Wilson. Mimi kama mwanataaluma, nilivutiwa moja kwa moja na kitabu hiki. Nilivutiwa zaidi nilipogundua kuwa kinahusu utafiti na uandishi juu ya wenyeji asili wa Marekani, ambao tunawaita Wahindi Wekundu. Niliona kuwa ni kitabu kinachohoji jadi ya utafiti, taaluma, na uandishi kuwahusu hao Wahindi Wekundu, na, inavyoonekana, kinaleta fikra za kimapinduzi, kama yale ambayo kwetu Afrika yalianzishwa na wataalam kama Cheikh Anta Diop na Walter Rodney.

Katika maisha yangu, kununua vitabu na kuvisoma ni kama ugonjwa usiotibika. Leo nilipita tena pale kwenye duka la vitabu, nikaona "seli" bado inaendelea. Nilijitosa tena katika kuchambua vitabu, nikaibuka na kitabu kikubwa sana kiitwacho Beyond Human Nature: How Culture and Experience Shape the Human Mind, kilichotungwa na Jesse J. Prinz. Nilikiangalia, nikafahamu kuwa, kwa kutumia utafiti wa "neuroscience," "psychology," na "anthropology," mwandishi analeta fikra mpya juu ya mambo yanayomjenga binadamu kitabia. Bila kusita, nilikikwapua kitabu hiki. Kitabu chochote kinacholeta fikra mpya ni dhahabu.

Wednesday, March 11, 2015

Video ya Kumbukumbu ya Miaka Kumi ya Kitabu

Jana, binti yangu Zawadi na mimi tulirecodi video ya kumbukumbu ya miaka kumi tangu nilipochapisha kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Hatukuwazia tungefanya shughuli hiyo jana. Tulijishitukiza bila maandalizi. Tulitayarisha kompyuta nami nikaanza kuongea. Zawadi alifanya shughuli yote ya kiufundi hadi kuiweka video katika
mtandao wa You Tube.

Katika kumbukumbu hii ya miaka kumi ya kitabu changu, napenda kuwashukuru wasomaji wangu, familia, na marafiki na wengine wote walionihamasisha kwa namna moja au nyingine.

Kwa mwezi huu wote, yeyote anayetaka kitabu hiki, popote duniani, ataweza kukipata kutoka kwangu kwa bei nafuu ya dola 12. Awasiliane nami kwa barua pepe, africonexion@gmail.com au simu (507) 403 9756. Mwisho wa fursa hii ni tarehe 31.

Tuesday, March 10, 2015

Mdau Anauliza Kama Ufisadi Utaisha Nchini

Mdau anonymous ameomba tusome makala ifuatayo na ameuliza iwapo ufisadi utaisha Tanzania.

Makala aliyoleta inamhusu Dr. Fulgence Mosha, anayeonekana pichani, daktari bingwa mstaafu wa hospitali ya KCMC, ambaye amekuwa akihangaikia mafao yake ya ustaafu kwa miaka kumi bila mafanikio. Makala aliyoileta mdau ni hii hapa.

Sunday, March 8, 2015

Natamani Kuwatukana Akina "Anonymous"

Katika blogu kuna maudhi ya aina aina. Wanaoleta maudhi hayo ni hao wanaojiita "anonymous." Kwa kujificha namna hii, wanajisikia huru kusema cho chote, wakijua kuwa hakuna atakayewawajibisha.

Siku chache zilizopita, niliandika ujumbe katika blogu ya Michuzi, nikiulizia kuhusu taratibu za ibada ya mazishi ya ki-Katoliki. Sikujificha. Kama ilivyo kawaida yangu, nilijitambulisha kikamilifu.

Walitokea akina "anonymous" wakaongelea mambo ambayo hayakuonyesha nia ya kujibu suali nililouliza. Nilivyokuwa nasoma waliyoandika, niliona kuwa wananipotezea muda. Walikuwa wanakera. Kwa silika za kibinadamu, nilitamani kuwatukana, lakini niliamua kuachana nao, nikahamishia mada yangu katika blogu yangu.

Kwanza, sidhani kama ni uungwana kuingia katika blogu ya mtu na kuigeuza kuwa uwanja wa malumbano yasiyo na tija au ya kuwakera watu. Ni kama kukaribishwa nyumbani mwa mtu halafu uanze kufanya utovu wa heshima.

Miaka kadhaa iliyopita, Michuzi alilalamika kuhusu watu waliokuwa wanafanya utovu wa nidhamu katika blogu yake. Hadi leo, ameweka angalizo kuwa mchangiaji aangalie asichafue hali ya hewa wala kujeruhi hisia za mtu au watu.

Mimi mwenyewe nimekumbana tena na tena na akina "anonymous" wasio na uungwana. Kwa mfano, "anonymous" mmoja aliwahi kuniambia kwa kiburi kuwa ana uhuru wa kusema katika blogu yangu.

Napingana na "anonymous" huyu. Ingawa binafsi nimejiamulia kuifanya blogu yangu iwe huru kwa yeyote kutoa maoni yake, lakini sikubali kwamba yeyote ana haki ya kuandika katika blogu yangu.

Mtu anapokuja katika blogu yangu ninamwona kama mtu ninayemkaribisha nyumbani mwangu. Hawezi kudai kuwa ana uhuru kusema lolote atakalo katika nyumba yangu. Lazima atumie busara.

Mwenye nyumba ana haki ya kumtolea nje yeyote asiyeheshimu nyumba. Hivyo hivyo, nina haki ya kumzuia mtu yeyote kuweka maoni yake katika blogu yangu. Ninaweza kutumia njia iliyopo katika muundo wa blogu ya kuzuia maoni au kuondoa maoni.

Kwa hiari yangu, nimeamua kutotumia utaratibu huu wa kuzuia au kuondoa maoni. Lakini mtu asiniambie kwamba ana haki ya kutoa maoni katika blogu yangu.

Hii si mara yangu ya kwanza kuwaongelea akina anonymous wanaokera. Mara ya kwanza, niliandika makala hii hapa. Baadaye niliandika makala hii hapa.

Sijui wanablogu wenzangu wana maoni gani. Sijui wanaoandika au wanaowazia kuandika katika blogu wana maoni gani. Sijui wasomaji wa blogu wanasemaje.

Thursday, March 5, 2015

Kofia Katika Mazishi ya Ki-Katoliki

Niliona taarifa za msiba na mazishi ya Kapteni John Komba mitandaoni. Ni jambo la kushukuru kwamba waandishi na wapiga picha walituwezesha tulio mbali kuelewa mambo yalivyokuwa.

Nilivyoona picha inayoonekana hapa kushoto, ya jeneza likiteremshwa kaburini, niliamua kuandika ujumbe katika blogu ya Michuzi nikisema kuwa nimekerwa na kitendo cha wahusika kuwa wamevaa kofia wakati wa shughuli hiyo. Niliuliza iwapo jambo hili linaruhusiwa kwa mujibu wa ibada za mazishi ya ki-Katoliki.

Akina "anonymous" kadhaa wamejitokeza na kuandika hili au lile, katika sehemu ya maoni. Nami katika sehemu ile ya maoni, nimejaribu kuelezea zaidi suala langu, nikisema, kwa mfano, kuwa kwa askofu kuvaa kofia ya kiaskofu wakati wa kuendesha ibada ni sehemu ya mavazi yake rasmi ya ibada.

Sikuona kama duku duku yangu imejibiwa. Badala yake, niliona watu wanazua mambo ambayo hayahusiani na ulizo langu, ulizo ambalo lilitokana na nia njema, yaani kujiridhisha kuwa tunaheshimu ibada na tunamheshimu marehemu.

Nimeamua kuhamishia suali langu hapa kwenye blogu yangu. Ningependa kusikia maoni ya wa-Katoliki wenzangu, ambao wana ufahamu zaidi yangu kuhusu uvaaji wa kofia wakati wa ibada ya mazishi ya ki-Katoliki.

Tuesday, March 3, 2015

Utamaduni wa Kuwasomea Watoto Vitabu

Nimeandika mara kwa mara kuhusu suala la elimu, sio tu katika blogu hii, bali pia katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, kitabu ambacho nilitegemea kitasomwa na wa-Tanzania wenzangu, lakini mambo yamekuwa kinyume.

Kati ya mambo ambayo nimekuwa nikiyaongelea ni umuhimu wa kuwasomea watoto vitabu, jambo ambalo limejengeka katika utamaduni wa wa-Marekani. Nimekumbuka yote hayo leo baada ya kusoma makala hii hapa
kama uthibitisho na changamoto.

Hili ni kati ya mambo ambayo wa-Tanzania tunapaswa kujifunza. Nimethibitisha mwenyewe kuwa watoto wa Tanzania wanapenda vitabu, bali, kadiri wanavyokua, mapenzi hayo huzimishwa na watu wazima na jamii kwa ujumla.

Kama wahenga walivyosema, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Baada ya muda, watoto wa ki-Tanzania hufuata utamaduni wa jamii wa kutothamini vitabu, na Taifa linaendelea kuzorota kielimu., wakati wenzetu wa-Marekani wanawalea watoto wao katika kupenda vitabu.

Mwalimu Nyerere alikuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha watu wawe na tabia ya kutafuta elimu. Alikuwa mwandishi na msomaji makini. Alionyesha mfano kwa vitendo. Aliongoza njia.

Leo tuna watu ambao tunawaita viongozi ambao sielewi kwa nini wanaitwa viongozi. Wangekuwa ni viongozi, wangetambua kuwa elimu ni msingi wa maisha na maendeleo. Wangekuwa wanaihamasisha jamii kwa kauli na vitendo katika kutafuta elimu. Lakini, badala yake, hawaonekani kujali kabisa kwamba wanachangia katika kuliangamiza Taifa badala ya kuliongoza, yaani kulipeleka mbele.

Monday, March 2, 2015

Nimeulizwa Inakuwaje Siuzi Vitabu Vyangu Tanzania

Leo katika mtandao wa Facebook kuna mdau kaniuliza inakuwaje siuzi vitabu vyangu Tanzania. Nimemshukuru kwa ulizo lake, nikajaribu kulijibu. Napenda kuandika machache kuhusu suali hili.

Napenda kuanza kwa kusema kuwa vitabu hivyo vinapatikana mtandaoni, kama vile kwenye tovuti ya lulu na tovuti ya Amazon. Yeyote mwenye kadi ya "credit" kama vile VISA au MasterCard, anaweza kuvinunua. Haijalishi kama yuko Chake Chake, Dar es Salaam au Tukuyu. Ataletewa. Kama ana kifaa kama "kindle," ananunua bila tatizo.

Ninafahamu kuwa ni wa-Tanzania wachache walioko Tanzania wanaoweza kununua vitu mtandaoni. Lakini kuna maelfu ya wa-Tanzania katika nchi kama Marekani wenye hizo kadi. Kama kuna nia ya dhati ya kununua kitabu, haikosekani njia.

Mimi mwenyewe nimekuwa tayari kufanya mipango na wa-Tanzania wenye nia ya kuuza vitabu vyangu, kwa kuwapelekea. Nimewahi kufanya hivyo na Cultural Tourism Program (Longido), Bougainvillea Lodge (Karatu), na Cultural Tourism Program (Mto wa Mbu).

Kila inapowezekana, nafanya mpango wa kuvifikisha vitabu vyangu kwenye matamasha nchini Tanzania, kama ilivyoelezwa hapa.

Kwa kuwa mimi si mfanyabiashara, ningependa kuona wafanyabiashara wanajipatia faida kutokana vitabu vyangu. Duka la vitabu chuoni St. Olaf linauza vitabu vyangu kwa bei kubwa kuliko mtandaoni. Vile vile, nilipotembelea chuo cha South Central, katika duka la vitabu walikuwa wanauza kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kwa dola 17.95.

Hata hivi, huwa najiuliza ni wa-Tanzania wepi wanaotaka kusoma vitabu vyangu. Sijaona kama kuna utamaduni wa kununua na kusoma vitabu. Wa-Marekani ndio wasomaji wangu wakuu, kama ninavyobainisha mara kwa mara katika blogu hii. Kwa vyovyote, kuepusha lawama, na kuwatendea haki wa-Tanzania wanaoamini nina jambo la kuwaambia, najitahidi kuhakikisha vitabu vyangu vinapatikana Tanzania.

Sunday, March 1, 2015

Imekuwa Wiki ya Mafanikio

Wiki hii inayoisha imekuwa ya mafanikio makubwa kwangu. Napenda kwanza nifafanue kuwa dhana yangu ya mafanikio ni tofauti na ya wale wanaowazia fedha. Mimi ni mwelimishaji, darasani na katika jamii. Ni mtoa ushauri katika masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake, hasa katika dunia ya tandawazi wa leo. Ushauri huo natoa kwa njia mbali mbali, hasa maandishi na mazungumzo na watu binafsi au vikundi. Dhana yangu ya mafanikio imejengeka katika shughuli hizo.

Kwanza, nilijiandaa kwa ziara ya chuo cha South Central, mjini Mankato, ambako nilifanya mazungumzo na darasa la wanafunzi wanaojiandaa kwenda Afrika Kusini kimasomo, na halafu nikatoa mhadhara kwa wanajumuia hapo chuoni, ambao mada yake ilikuwa "Writing About Americans."

Maandalizi ya mazungumzo hayo yote yalikhusu kukusanya fikra zilizokuwa akilini mwangu na kuziweka pamoja ili kukidhi mahitaji ya mazungumzo yale. Ilikuwa rahisi kujitayarisha kwa maongezi na wanafunzi waendao Afrika Kusini. Nmaongezi ya aina hiyo na wa-Marekani wengi katika maandalizi ya kwenda Afrika.

Katika kuandaa mhadhara wa "Writing About Americans," nilijikuta ninatafakari namna ya kuwasilisha mada yangu. Hatimaye, niliamua kuzingatia uzoefu wangu wa kuandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Niliamua nielezee chimbuko la wazo na azma ya kuandika kitabu hicho, mchakato wa kuandika, na mambo niliyojifunza katika kuandika huko. Baada ya kuamua hivyo, nilikaa chini nikatmia dakika chache tu kuandika dondoo ambazo ningetumia katika mhadhara.

Nilipoziangalia dondoo hizo, nilijua kwa hakika kwamba nitatoa mhadhara mzuri. Na ndivyo ilivyokuwa, kama alivyoeleza Mwalimu Becky Fjelland Davis katika blogu yake. Baada ya ziara yangu, niliandika katika blogu yangu kwamba nilitegemea kuwa tathmini ya ziara yangu ingeendelea miongoni mwa wale waliohidhuria.

Ukweli wa dhana yangu umeendelea kujitokeza, na hapa napenda kuleta ujumbe ulioandikwa na mtu aliyehudhuria mhadhara wangu:

Dr. Mbele,

I attended the talk you gave at South Central and found it to be very interesting and insightful. You showed how valuable writing is in itself, by giving us a mirror of ourselves as authors.

Thank you for your willingness to share you observations of Africans and Americans as well as your own self-assessments.

I thoroughly enjoyed your talk and only wish that I could have remained loner to hear the questions from the audience.

Thank you for sharing your life and writing experiences with us at South Central College
.

Baada ya ziara ya Mankato, nilijikuta nikiongea kwa njia ya Skype na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Montana, ambao walikuwa wanasoma kitabu changu cha Matengo Folktales. Niliandika kuhusu mazungumzo hayo katika blogu hii. Mazungumzo yale yalikwenda vizuri sana. Wanafunzi na mwalimu wao walifurahi, na mimi pia.

Wameendelea kuelezea furaha yao. Mwanafunzi mmoja ameniandikia hivi:

Hello Dr. Mbele!

I was a student from Professor Olsen's Skype class earlier today, my name is Sara Saxton. I'm I just wanted to say thank you so much for your time and expressing your mind to our class! I really enjoyed hearing about your definition of a classroom. I agree with the aspect of having a classroom be a "safe place" for learning. I feel as though I have experienced many things outside of the classroom, but there is nothing that compares to being able to ask questions you've always wanted to ask in a classroom. Anyway, I just wanted to let you know I really enjoyed hearing about your tales and watching you preform them. It was great!

Thank you again
!!

Mwanafunzi mwingine kaniandikia hivi:

Shikamoo Dr. Mbele,

I hope I have used the greeting properly. I wanted to say thank you taking the time to speak with, and preform for our class today over Skype. Growing up in Montana there are not many oppertunities to experience the vastness of culture the world has to offer and your time and knowledge was greatly appreciated. I hope to have the chance to speak with you again someday.

Asante sana
!

Kama ninavyosema mara kwa mara, blogu yangu hii ni mahali ambapo nahifadhi mambo yangu, kama vile mawazo, hisia na kumbukumbu. Nafurahi nimeandika hayo niliyoandika, muhtasari wa mafanikio niliyoyapa wiki hii inayoisha. Ni mafanikio yanayougusa moyo wangu na yenye maana kwangu kuliko fedha.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...