Thursday, May 26, 2016

"The Snows of Kilimanjaro" Yatimiza Miaka 80

Mwaka huu 2016, The Snows of Kilimanjaro, hadithi maarufu ya Ernest Hemingway, inatimiza miaka 80 tangu ichapishwe kwa mara ya kwanza. Ilichapishwa katika jarida la Esquire, toleo la Agosti, 1936. Sidhani kama kuna hadithi fupi katika fasihi ya ki-Ingereza inayofahamika na ni maarufu kuzidi The Snows of Kilimanjaro.

Hemingway aliandika utangulizi mfupi wa hadithi yake, ambao unaamsha hisia zinazoendelezwa katika hadithi nzima, ikiwemo hisia ya masuali yasiyojibika:

"Kilimanjaro is a snow covered mountain 19,710 feet high, and it is said to be the biggest mountain in Africa. Its western summit is called the Masai "Ngáje Ngái," the House of God. Close to the western summit there is the dried and frozen carcass of a leopard. No one has explained what the leopard was seeking at that altitude." 

The Snows of Kilimanjaro inamhusu mtu aitwaye Harry, mzungu. Tunamwona akiwa mgonjwa kutokana na kidonda alichopata baada ya kuchomwa na mwiba porini. Kilichosababisha kidonda kufikia hali ya kutishia uhai wake ni kucheleweshwa kwa matibabu. Harry tunamwona amelala kwenye machela huku akihudumiwa na mkewe Helen, mzungu pia. Kuna pia watumishi wa-Afrika.

Mazingira inapotokea hadithi hii ni chini ya mlima Kilimanjaro. Lakini sehemu kubwa ya hadidhi ni kumbukumbu za Harry za mambo aliyofanya au kushuhudia sehemu mbali mbali za Ulaya, kama vile Paris, ikiwemo ushiriki wake katika vita. Juu ya yote, hadithi hii ni mtiririko wa fikra za Harry kuhusu uandishi. Tunamshuhudia akiwazia mengi ambayo alitaka aandike miaka iliyopita, au angependa kuwa ameandika, lakini hakuandika kwa sababu mbali mbali. Anajisikitikia kuwa sasa hataweza kuandika, kwani kifo kinamwelemea. Helen anafanya kila awezalo kumtuliza na kumpa matumaini kuwa atapona. Anamtunza na kujaribu kumzuia kujidhuru kwa ulevi. Anamweleza kuwa ndege itakuja kumwokoa.

Kwa kuwa huu ni mwaka wa kumbukumbu ya miaka 80 ya The Snows of Kilimanjaro, na kwa kuzingatia umaarufu wa Ernest Hemingway ulimwenguni, na umaarufu wa The Snows of Kilimanjaro, na kwa kuwa Mlima Kilimanjaro uko nchini mwetu, hii ilikuwa ni fursa ya kuitangaza nchi yetu. Niliwahi kuandika kidogo kuhusu jambo hili katika blogu hii. Ingekuwa wa-Tanzania tuna utamaduni wa kusoma na kuthamini vitabu, tungeichangamkia fursa ninayoelezea hapa.

Kuna mambo ambayo tungeweza kufanya. Wizara, taasisi na makampuni yanayohusika na utalii yangefurika matangazo na makala juu ya Hemingway na The Snows of Kilimanjaro. Wasomaji wa Hemingway, wanafasihi, na wengine tungekuwa tunafanya mijadala na makongamano. Vyombo vya habari, kama vile magazeti na televisheni, vingekuwa vinarusha matangazo na taarifa na mijadala hiyo. Huu ungekuwa mwaka wa kuitangaza nchi yetu na kuwavutia watalii nchini kwetu kwa namna ya pekee kabisa.

Kuna wenzetu ambao wanatumia jina na maandishi ya Hemingway kujitangaza na kuvutia watalii. Mifano ya wazi ni Cuba na mji wa Pamplona ulioko Hispania. Dunia ya leo ya ushindani mkubwa inahitaji ubunifu wa kwenda na wakati.  Dunia si ya kuichezea. Muyaka alitahadharisha hayo aliposema, "dunia mti mkavu, kiumbe siulemele" na tusijidanganye kuwa twaweza "kuudhibiti kwa ndole."

Tuesday, May 24, 2016

Uandishi wa ki-Ingereza Bora

Ninafundisha katika idara ya ki-Ingereza katika Chuo cha St. Olaf, hapa Marekani. Moja ya masomo ninayofundisha ni uandishi bora wa ki-Ingereza, yaani ki-Ingereza sanifu. Ninawajengea wanafunzi nidhamu ya kuboresha uandishi wao wa insha. Wakishaandika insha, ninawashinikiza waiboreshe, kwa kuangalia na kutafakari kila neno, na kila sentensi, mara nyingi iwezekanavyo. Hii ni kazi ngumu kwa yeyote, wakiwemo wanafunzi wangu, pamoja na kwamba ki-Ingereza ni lugha mama yao.

Moja ya kazi ninazowapa ni kuiboresha insha yangu iitwayo "Do You Have an Accent?" ambayo niliandika miaka iliyopita, ikachapishwa hapa Minnesota. Nilikuwa nimeandika mswada wake, nikaurekebisha tena na tena, hadi kufikia kiwango cha kuweza kuchapishwa.

Lakini, hata baada ya kuchapishwa, niliendelea kuiangalia makala hii kwa jicho kali, tena na tena. Katika jitihada hii, niligundua vipengele visivyopungua nane ambavyo vinaweza kurekebishwa na insha ikawa bora zaidi. Ninapowapa wanafunzi wangu zoezi hili, ninakuwa na lengo la kuwathibitishia kuwa uandishi bora ni kazi inayohitaji umakini mkubwa.

Ninaileta hapa insha hiyo iliyochapishwa, ili wasomaji wa blogu hii wanaoamini wanakijua ki-Ingereza waone kama wanaweza kugundua vipengele hivyo vinavyohitaji marekebisho. Mtu akitaka kuleta rekebisho la sentensi yoyote, ili kuiboresha, anakaribishwa kufanya hivyo. Niliwahi kuleta zoezi hili kabla katika blogu hii. Fundisho ninaloleta ni kuwa hata kama mtu umesoma kiasi gani, usidhani umefikia mwisho wa safari.

DO YOU HAVE AN ACCENT?

(Joseph L. Mbele)

If you are like me, with deep roots in Africa, you probably have heard Americans say you have an accent. You might feel that having an accent is not a good thing. Many new immigrants in America are embarrassed about their foreign accents and struggle to learn to speak like Americans. I met a Somali youth in Faribault, Minnesota, who felt that way. I think all this is rather unfortunate. I teach English at college level in America. With apologies to no one, I speak English with my distinctive Tanzanian accent.

An accent is an intrinsic aspect of spoken language. Nobody can say a word, let alone speak a language, without an accent. Basically, an accent is one’s distinctive way of speaking. Though an accent is an individual characteristic, it is also a collective one. Despite their individual differences, people from a given country or region tend to speak with a recognizable accent. I can tell a South African from a Nigerian, or an American from an Indian, based on the way they speak English. Those who know Americans say that Texans, for example, have their own accent, so do Californians, and Americans from other regions.

The accent we grew up with sounds normal to us. We might not even notice it. That we notice the accents of foreigners doesn’t mean that they alone have accents. American English sounds normal to Americans, but it is not a universal norm. English is an international language, with different varieties. With the world getting increasingly interconnected, people who ignore those varieties do so at their own peril, just as those who think they don’t need other languages. Our best option is to learn to hear and understand as many varieties and accents as possible.

Unfortunately, most people have not thought about the issue in this way. Immigrants who struggle to change their accents in order to “fit in” should think about this, so should those who complain about immigrants who speak with foreign accents. Why should someone with a proper Nigerian or Ugandan accent be pressured to speak like an American? Why should someone with a proper Jamaican or British accent be pressured to speak like an American? In Africa, no one asks foreigners to speak English like Africans: the British speak with their own accent; so do the Indians, the Australians and others. That, I think, is the way to go.

Monday, May 23, 2016

Hatimaye, Ninatafsiri Shairi la "Kibwangai"

Hivi karibuni, nililalamika katika blogu hii kuwa nilikuwa nikijaribu kutafsiri shairi la "Kibwangai" la Haji Gora Haji, lakini nilikwama. Shairi hili lililoandikwa kwa ki-Swahili linaeleweka vizuri kabisa kwangu. Lugha niliyotaka kulitafsiri shairi, yaani ki-Ingereza, ninaifahamu vizuri sana.

Sasa tatizo lilikuwa nini? Hili ni suala moja la msingi katika shughuli na taaluma ya tafsiri. Tafsiri sio suala la ufahamu wa lugha tu, bali ufahamu wa mambo mengine pia, ikiwemo lugha ya kifasihi. Unaweza kuwa unakijua ki-Ingereza, kwa mfano, lakini hujui ki-ingereza cha fasihi. Ukitafsiri shairi kama Kibwangai, utaishia kuleta kitu ambacho hakina ladha ya sanaa.

Hiyo dhana yenyewe ya ladha ya sanaa inahitaji ufafanuzi. Lugha, iwe ni ki-Swahili, ki-Ingereza, au lugha nyingine, ina matumizi ya kawaida na matumizi ya kisanaa. Kiswahili cha kishairi kinatofautiana na ki-Swahili cha kawaida. Vivyo hivyo ki-Ingereza.

Kwa hivi, mtu unapotafsiri shairi kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine, unapaswa kufahamu matumizi ya kisanaa ya lugha zote mbili. Hapo ndipo mtu unapojikuta umekwama kama nilivyokwama siku kadhaa zilizopita.

Kukwama huku hakuwafiki wale wanaotafsiri tu, bali waandishi pia. Katika nadharia ya uandishi kuna kitu ambacho kwa ki-Ingereza huitwa "writer's block," yaani mkwamo wa kiuandishi. Hii ni hali ya mwandishi kujikuta amekwama asiweze kuandika. Akili haikubali kufanya kile anachotamani mwandishi. Ernest Hemingway aliwahi kuelezea hali hiyo:

There is no rule on how to write. Sometimes it comes easily and perfectly; sometimes it's like drilling rock and then blasting it out with charges.

Kwa ki-Swahili, anasema:

Hakuna sheria za namna ya kuandika. Wakati mwingine huwa ni rahisi na kwa ukamilifu; wakati mwingine huwa ni kama kutoboa mwamba na kisha kuupasua kwa milipuko.

Nimeandika utangulizi huu mrefu kwa kuwa tangu jana jioni nimejikuta katika hali ya kuweza kulitafsiri shairi la "Kibwangai." Jana nimetafsiri beti sita. Nimebakiza tano. Hata hivi, nikishamaliza, kitakachofuata ni kuipita tafsiri nzima kwa uangalifu, neno kwa neno. Hii nayo inaweza ikawa kazi ngumu ya kuumiza, sawa na kupasua mwamba.

KIBWANGAI

1.    Kuna hadithi ya kale, kwa babu nimepokeya
       Kwa manyani zama zile, mkasa ulotokeya
       Nilikuwa mwanakele, hayo nikazingatiya
       Leo nawadokezeya, kwa nilivyoyafahamu

2.    Nyani bada kugundua, watu wanawaviziya
       Sababu yake kwa kuwa, huila yao mimeya
       Na ndipo wakaamuwa, mwenzao kumtumiya
       Ende akawalimiye, mazao yalo muhimu

3.    Kwenye uamuzi huo, baada ya kukusudiya
       Kibwangai jama yao, wakamkata mkiya
       Unyani kwa mbinu zao, kwake ukajitokeya
       Akawa yeye si nyani, bali ni binaadamu

4.    Yalisudi watakayo, nyani wakafurahiya
       Yaliposadifu hayo, wote wakachekeleya
       Walidhani watakayo, atawakamilishiya
       Nyoyo zikategemeya, na nyuso kutabasamu

5.    Pana mmoja kasema, Kibwangai kumwambiya
       Kama tutalokutuma, weza kututimiziya
       Isiwe kurudi nyuma, ewe mwenzetu sikiya
       Wewe tumekuchaguwa, utumikiye kaumu

6.    Kibwangai akasema, hayo nimezingatiya
       Kidete nitasimama, jitijada kutumiya
       Kwa kusia na kulima, mpate jifaidiya
       Sitobadili mawazo, ilipwe yangu kaumu

7.    Kibwangai lipoona, ni mtu kakamiliya
       Akaanza kujivuna, na dharau kuzidiya
       Wala hakujali tena, wenzake walomwambiya
       Akahisi hawi nyani, umbo lile litadumu

8.    Kawa na tabia moja, nyani walipomwendeya
       Akajifunga mkaja, mijiwe kuwarushiya
       Hakujali zao haja, wala kuwahurumiya
       Kapiga na kukemeya, pia na kuwashutumu

9.    Nyani likawakasiri,  ghadhabu wakaingiya
       Wakafanyiza shauri, Kibwangai kumwendeya
       Kwa nguvu au hiyari, kumpa wake mkiya
       Ili awe nyani tena, asiwe binaadamu

10.  Mkia bada kumpa, mambo yakawa mabaya
       Nguo zake kazitupa, unyani kumrudiya
       Kaanza kuchupa chupa, mitini akarukiya
       Akawafata wenzake, akiwa nyani katimu

11. Wenzake wakamcheka, wote na kumzomeya
       Akakosa la kushika, kwa haya kujioneya
       Majuto yakamfika, akabakia kuliya
       Akarudia porini, iliko yake kaumu.

Sunday, May 22, 2016

Leo Nimemwandikia Mzee Patrick Hemingway

Leo nimemwandikia barua pepe Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliye hai wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Nilipiga naye picha inayoonekana hapa kushoto tarehe 27 Aprili, 2013, nyumbani pake mjini Craig, katika jimbo la Montana.

Nilifahamu habari zake kwa miaka mingi kabla ya kufahamiana naye na halafu tukakutana. Ni mzee mwenye maongezi ya kusisimua kuhusu baba yake Ernest Hemingway na waandishi wengine wa wakati wake. Pia ana kumbukumbu nyingi za Tanganyika, na kisha Tanzania, ambako aliishi kwa miaka yapata 25 kabla ya uhuru na baada ya uhuru, akiendesha kampuni ya utalii, na hatimaye akiwa mkufunzi katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Mwika.

Tangu tulipoanza kufahamiana, ameguswa na ari yangu ya kutafiti maandishi, falsafa, na maisha ya Ernest Hemingway, na amevutiwa na msimamo wangu kuwa Ernest Hemingway ni mwandishi aliyetuenzi sana sisi watu wa Afrika Mashariki, na tunapaswa kujielimisha kuhusu mchango wake, na kisha kuutumia katika kujitangaza kama alivyotutangaza.

Hayo yamemfanya Mzee Patrick Hemingway awe tayari kunisaidia kwa dhati katika juhudi zangu za kujielimisha na kuuelimisha ulimwengu juu ya Ernest Hemingway. Miezi kadhaa iliyopita, nilivyomweleza kuwa napangia kutembelea hifadhi ya Ernest Hemingway katika John F. Kennedy Library, aliniambia kuwa nitakapokuwa tayari nimfahamishe ili anitambulishe kwa wahusika.

Nilipoongea naye tarehe 19 mwezi huu na kumtajia tarehe nilizopangia kwenda kwa shughuli hiyo, aliniagiza nimpelekee maelezo yangu kwa barua pepe, ili aweze kuandaa utambulisho huo. Aliniambia kuwa ninakwenda wakati mzuri, kwani kuna maonesho maalum juu ya Hemingway, ambayo yameanza siku chache zilizopita na yatadumu kwa miezi kadhaa.

Basi, leo nimemwandikia. Kilichobaki sasa ni kuandaa safari, nikajionee hiyo hifadhi kubwa kuliko zote duniani juu ya Ernest Hemingway. Hii itakuwa ni mara yangu ya kwanza kuitembelea hifadhi hiyo, lakini sitegemei kuwa itakuwa ni mara ya mwisho.

Thursday, May 19, 2016

Nimenunua "Good Prose," Kitabu Kuhusu Uandishi

Siku chache zilizopita, katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf, nilikiona kitabu kiitwacho Good Prose: The Art of Nonfiction. Jina hilo lilinivutia, nikapata duku duku ya kukiangalia. Nilivyoona kuwa mwandishi mojawapo, Tracy Kidder alikuwa amepata tuzo ya Pulitzer, nilivutiwa kabisa. Hii ni tuzo ya uandishi yenye hadhi kuliko zote zinazotolewa hapa Marekani.

Nilivyochungulia kurasa zake, niliona kina mawaidha mazuri kuhusu uandishi bora. Si uandishi wa kazi za fasihi, bali uandishi kama wa insha. Huu ndio uandishi wangu, na ndio uandishi ninaofundisha. Nilivutiwa pia nilipoona waandishi maarufu wamenukuliwa katika kitabu hiki, kama vile Norman Mailer,  Ernest Hemingway, Vladimir Nabokov, na William Strunk, Jr.

Kwa bahati mbaya sikuwa na hela, nikaondoka bila kukinunua, kwa shingo upande. Leo nilikwenda tena dukani, nikakuta kitabu bado kipo. Nilikinunua hapo hapo.

Pamoja na kwamba nina uzoefu wa miaka mingi wa kufundisha uandishi bora wa ki-Ingereza, na pamoja kwamba ninawafundisha watu ambao ki-Ingereza ni lugha mama yao, siridhiki na ufahamu wangu. Ninajifananisha na waandishi wa ki-ingereza ambao ni maarufu duniani, na hiki ndicho kigezo sahihi, kwani katika kujipima huko, ninatambua kuwa sijawafikia. Kwa hivyo, ninatambua umuhimu wa kujielimisha muda wote. Ni ujinga kuridhika na elimu uliyo nayo.

Mtu ukitaka kujipima katika fani yako, jifananishe na wale walifanikiwa kwa kiwango cha juu kabisa. Kwa mwandishi, naona ni wajibu kujipima dhidi ya waandishi waliotwaa tuzo maarufu kama Nobel, Booker, na Pulitzer. Hapo mtu utatambua kuwa bado una njia ndefu ya kusafiri.

Good Prose: The Art of Nonfiction ni kitabu nitakachokisoma kwa makini. Kimeelezwa kwenye jalada kama "Stories and advice from a lifetime of writing and editing," na kwamba ni "an inspiring book about writing--about the creation of good prose." Bila shaka kitabu hiki kitanihamasisha kutafakari zaidi suala la uandishi bora, suala ambalo nimekuwa nikilizungumzia katika blogu hii.


Wednesday, May 18, 2016

Muhula Unaisha; Umebaki Utafiti

Jana tumemaliza muhula wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Nilikuwa ninafundisha "Folklore," Muslim Women Writers, na "First Year Writing." Kwa utaratibu wa chuo hiki, masomo matatu kwa muhula ndio kiwango cha juu kabisa. Hatufundishi zaidi ya masomo matatu. Kwa hivi, nilitegemea ningekuwa nimechoka, lakini sisikii uchovu. Alhamdulillah.

Kwa wiki nzima inayokuja, tutakuwa na mitihani. Baada ya hapo tutaanza likizo ndefu ya miezi mitatu na kidogo. Inaitwa likizo, lakini maprofesa tunaona ni wakati muafaka wa kufanya shughuli za kitaaluma kama utafiti na uandishi.

Nami nimeamua kwenda Boston kwa siku chache kufanya utafiti juu ya Ernest Hemingway katika maktaba ya John F. Kennedy. Humo kuna hifadhi kubwa kuliko zote duniani ya vitabu, miswada, picha na  kumbukumbu zingine zinazomhusu Hemingway. Ingawa nimefika Boston mara kadhaa, sijawahi kwenda katika maktaba hiyo maarufu.

Nina bahati kuwa ninafahamiana na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway ambaye bado yuko hai. Yeye ndiye mmiliki wa haki zote za urithi wa Hemingway. Nilipomwambia kwa mara ya kwanza kwamba napangia kwenda kufanya utafiti katika maktaba ya John F. Kennedy,  aliniambia nimfahamishe ni lini ili anitambulishe kwa wahusika. Wiki chache zilizopita, katika maongezi yetu, nilimwambia tena kuwa napangia kwenda kwenye maktaba ile, alikumbushia kuwa nimweleze ni muda upi nitakwenda ili awafahamishe.

Ninashukuru sana kwa hilo, kwani katika kusoma taarifa za maktaba ile, nimefahamu kuwa kuna masherti yanayohusu kuitumia hifadhi ya Ernest Hemingway. Mtu hukurupuki tu ukafika pale na kufanya utafiti. Kuna baadhi ya kumbukumbu ambazo zimefungiwa. Mtafiti unahitaji kibali maalum kuweza kuzifanyia utafiti. Sherti nichukue hatua hima.

Sunday, May 15, 2016

Dini ya Kweli

Leo ni Jumapili, nami nimerejea kutoka kanisani kusali. Nilipokuwa njiani, nilijikuta nikiwazia suala la dini, nikajiuliza kuhusu dhana ya dini ya kweli. Nini maana ya dini ya kweli? Kuna dini ya kweli? Kama ipo, ni ipi? Hili ni suala tata, nami napenda kuthibitisha angalau kidogo utata huo. Ninategemea kuwa wasomaji wangu watachangia mawazo.

Kwa mtazamo mmoja, tunaweza kusema kuwa kila dini ni dini ya kweli, kwa maana kwamba iko. Ni sawa na kitu chochote kinginecho kilichopo. Kila kilichopo ni kitu cha kweli, iwe ni chakula, bangi, au kifo. Vyote hivyo ni vitu vya kweli, kwa maana kwamba vipo. Na dini ni hivyo hivyo. Dini ziko. Kila dini ni dini ya kweli.

Kwa mtazamo mwingine, watu wanapoongelea dini ya kweli, wanamaanisha dini inayokubalika kwa Mungu. Wanamaanisha dini itakayomfikisha binadamu kwenye uokovu. Hapo pana utata mkubwa, kwani waumini wa dini mbali mbali wana tabia ya mwamba ngoma, ambaye huvutia ngozi upande wake. Matokeo yake katika historia ya binadamu yamekuwa mabaya. Uhasama, magomvi, mauaji, na ushetani wa kila namna.

Kwa watu hao, misahafu imekuwa silaha yao kuu. Wanalumbana kwa msingi wa misahafu. Wanatambiana kuhusu misahafu, kila mtu akiunadi msahafu wa dini yake kuwa ndio neno la Mungu.

Msimamo wangu ni tofauti. Msahafu si dini. Msahafu ukitumiwa vizuri unaweza kuwa mwongozo. Dini inatokea na inadhihirika pale mtu anapofuata huo muongozo katika maisha yake, kwa mawazo na vitendo. Uthibitisho wa dini unaonekana katika maisha ya waumini, si katika maneno au porojo.

Ni kama elimu. Mtu huwezi kusema una elimu kwa kuwa tu una vitabu. Kinachotakiwa ni kuvisoma vitabu ukiwa na akili timamu, kuvichambua, kuchota yale yanayofaa, na kisha kujijengea fikra, ufahamu, mtazamo, mwelekeo na maisha yako kwa mujibu wa yale uliyoyapata vitabuni. Uwe mtu unayefikiri, kuongea, kuishi, kama mtu mwenye elimu.

Kuna jambo moja ambalo naliona kuwa la kipuuzi, nalo ni jadi ya waumini kudai kwamba msahafu wao ndio pekee neno la Mungu. Dhana hii inatokana na ujinga. Kila jamii duniani tangu miaka maelfu yaliyopita, ilitambua kuwepo kwa Mungu. Watafiti wa masomo kama "Folklore" tunajua hilo vizuri, kwani tunayafahamu masimulizi ya mataifa mbali mbali yaliyotokana na jadi za kabla ya kuwepo maandishi, kabla ya kuandikwa kwa misahafu.

Mambo ya msingi ya imani za dini yalikuwemo katika haya masimulizi ya jadi. Wanadamu wote walitambua kuwepo kwa Mungu na walikuwa na ufahamu mzuri wa mema na mabaya. Walijua Mungu anataka nini na anakataza nini, na walijifunza na kufundishana hayo kwa masimulizi ya mdomo. Misahafu imekuja baadaye na imechota mengi kutoka kwenye hayo masimulizi ya jadi.

Kwa msingi huo, sioni kama ni sahihi kudai kuwa kitabu cha dini fulani ndio pekee neno la Mungu. Mimi kama muumini ninayefuatilia taaluma ya "Folklore," ambayo inatuingiza katika masimulizi yaliyotokana na kila taifa au kabila hapa duniani, nakiri kuwa Mungu alijitambulisha kwa mataifa yote. Kitabu si msingi. Mataifa na makabila mengi duniani hayakuwa na vitabu na mengi hayana vitabu. Lugha zao hazijaandikwa, na wanajifunza na kufundishana kwa masimulizi ya mdomo. Kwa mtindo huo, neno la Mungu daima limekuwepo miongoni mwao.

Kuna jambo jingine napenda niliseme, kuhitimisha ujumbe wangu. Ninapowazia dhana ya dini, na hasa ninapowazia dhana ya dini ya kweli, ninaihusisha na amani, upendo, na haki kwa wanadamu wote bila ubaguzi. Kwangu mimi, hivi ndivyo vigezo na ushahidi wa kuwepo kwa dini kwa maana ya dini ya kweli. Bila vigezo hivyo, sioni dini ya kweli bali ulaghai. Niliwahi kufafanua wazo hilo katika blogu hii, na kwenye sehemu ya maoni, mwishoni mwa Makala yangu, Christian Bwaya alifafanua vizuri kwamba dini kama tunavyoziona ni chimbuko la matatizo. Ninaona kuwa anachomaanisha, ndicho hiki ninachomaanisha ninapoongelea dini ya kweli, yaani kutambua umuhimu wa kuwatendea wanadamu wote kama tunavyopenda kutendewa, bila ubaguzi, tukizingatia kuwa Mungu hana ubaguzi. Hayo ndiyo mawazo yangu ya leo Jumapili.

Saturday, May 14, 2016

Nimepita Tena Katika Duka la Half Price Books

Leo alasiri nilikwenda eneo la Minneapolis, mwendo wa maili 40, kwa shughuli binafsi. Ilikuwa siku nzuri, ya jua la wastani na hali ya hewa ya kupendeza. Wakati wa kurudi, nilipita mjini Apple Valley, nikaamua kupitia katika duka la Half Price Books. Nilitaka hasa kuangalia kama kuna chochote juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Kufuatilia vitabu juu ya Hemingway imeshakuwa mazoea kwangu, wala siwezi kujizuia.

Ninajua kuwa sitakikuta kitabu kipya kilichoandikwa na Hemingway. Inafahamika kwamba miswada yote ya vitabu vya Ernest Hemingway imeshachapishwa. Kinachotokea ni kuwa yanachapishwa matoleo mapya ya vitabu vyake, kama vile matoleo yanayohaririwa na mjukuu wake, Sean Hemingway, ambavyo Mzee Patrick Hemingway, mtoto wa Ernest Hemingway, anaviandikia utangulizi.

Maandishi mapya kabisa ya Ernest Hemingway yanayochapishwa ni barua zake. Kuna mradi wa kukusanya barua zote za Ernest Hemingway tangu utotoni mwake. Wahariri wa mradi huu ni maprofesa Sandra Spanier na Robert W. Trogdon, ambao wamebobea katika utafiti juu ya Ernest Hemingway. Hadi sasa majuzuu matatu yamechapishwa, na kila juzuu ni mkusanyo wa barua za miaka michache. Inatarajiwa kuwa mradi huu ambao utachukua miaka mingi, utatoa majuzuu yatachapishwa 17.

Vitabu vingine vipya ambavyo vinaendelea kuchapishwa ni matokeo ya utafiti juu ya maisha na maandishi ya Ernest Hemingway. Tangu zamani, kumekuwa na watafiti wengi wanaojishughulisha na utafiti huu, na vitabu ambavyo wamechapisha na wanaendelea kuchapisha ni vingi. Si rahisi kwa mtu yeyote kufuatilia suala hili kikamilifu, lakini ninakuwa na duku duku ya kuona kuna vitabu gani vipya juu ya Hemingway katika duka la vitabu.

Nimefurahi leo kukikuta kitabu juu ya Hemingway ambacho sikuwa hata nimekisikia, The True Gen: An Intimate Portrait of Hemingway by Those Who Knew Him kilichoandikwa na Denis Brian. Katika kukipitia, niliona kuwa kitabu hiki ni taswira ya Hemingway inayotokana na kumbukumbu za watu waliomfahamu. Niliamua hapo hapo kukinunua. Baada ya kufika nyumbani, nimeanza kukisoma.  Kuna maelezo ya watu wengi, kuanzia wale waliokuwa watoto wakienda shule na mtoto Ernest Hemingway hadi waandishi, wake zake, na watu wengine.

Kama ilivyo kawaida, nilipokuwa hapo dukani Half Price Books niliwaona watu wengi humo wakizunguka zunguka kuangalia vitabu na kuvinunua. Wazazi wengi walikuwa na watoto wao. Kama kawaida, inavutia kuwaona watoto wa ki-Marekani wanavyolelewa katika utamaduni wa kupenda vitabu.

Sikukaa sana humo. Baada ya kununua kitabu changu, niliona niwahi nyumbani nikaanze kukisoma.


Thursday, May 5, 2016

Nimepata Qur'an Mpya

Nimekuwa na kawaida ya kuandika katika blogu hii taarifa za vitabu ninavyonunua, au vitabu ninavyosoma, ingawa siandiki juu ya vyote. Kwa siku nyingi sijafanya hivyo, lakini leo nimeamua kuandika kuhusu Qur'an mpya niliyoipata hivi karibuni, ambayo ni tafsiri ya ki-Ingereza ya Maulana Wahiduddin Khan na Farida Khanam ambaye ni binti yake.

Ninayo nakala nyingine ya Qur'an tangu mwaka 1982, ambayo ni tafsiri ya Abdullah Yusuf Ali. Hii ni kubwa kwa kuwa ina maelezo mengi. Hii mpya niliipata tarehe 28 Aprili, mwaka huu, kutoka kwa Dr. Nadia Mohamed, mzaliwa wa Misri.


Anaonekana amesimama kulia pichani. Nimefahamiana naye zaidi ya mwaka, tangu tuliposafiri kwenda kwenye semina chuoni Leech Lake, ambapo tulipiga hii picha, pamoja na profesa mwingine wa chuo kile.

Dr. Nadia Mohamed ni profesa mwenye shahada ya uzamili katika sheria za ki-Islam na shahada ya uzamifu katika elimu. Nilikuwa nimemwalika kuja kutoa mhadhara katika darasa langu la Muslim Women Writers, na baada ya kipindi ndipo alinipa Qur'an hiyo.

Tafsiri ni mtihani mkubwa, nami nimesema hivyo tena na tena katika blogu hii. Kwa kuwa hii Qur'an niliyopata karibuni ni tafsiri tofauti na ile ya Abdullah Yusuf Ali, ninategemea kufananisha hizi tafsiri mbili kutanisaidia kupata mwanga zaidi kuhusu yasemwayo katika Qur'an.

Ninasoma Qur'an sawa na ninavyosoma misahafu ya dini zingine kwa lengo la kujielimisha. Ninaamini kuwa ni muhimu kwa wanadamu kufahamiana ili tuweze kujenga maelewano miongoni mwetu. Kuzifahamu dini za wengine, tamaduni zao, na lugha zao ni njia ya kulifikia lengo hilo.

Ninapenda kusisitiza hilo, kwani nimeshakumbana na watu wanaodhani au kutegemea kwamba kwa kuwa ninasoma Qur'an, hatimaye nitasilimu. Sioni mantiki ya dhana hiyo. Je, ninaposoma msahafu wa dini ya Hindu, inamaanisha nitaacha u-Kristu niwe m-Hindu? Ninaposoma maandishi ya watu wanaozikana dini, kama vile akina Karl Marx, inamaanisha kuwa hatimaye nitaikana dini? Nimesoma fikra za Karl Marx na wapinzani wengine wa dini kwa zaidi ya miaka 40, na bado mimi ni m-Katoliki.

Wednesday, May 4, 2016

Tamasha la Kimataifa, Rochester, Aprili 30

Tarehe 30 April, nilihudhuria tamasha la kimataifa mjini Rochester ambalo nililizungumzia katika blogu hii. Nilipeleka vitabu vyangu, kwani ninashiriki matamasha kama mwalimu na mwandishi. Nilichukua pia bendera ya Tanzania. Meza yangu ilikuwa inavyoonekana pichani hapa kushoto, picha ambayo ilipigwa na mama mmoja kutoka China, mmoja wa watu walioniambia kuwa walipendezwa na mwonekano wa meza yangu, wakapiga picha.

Kwa kuiona bendera yangu, watu kadhaa wa Kenya na Uganda walikuja kuongea nami. Kwa utani na moyo wa ujirani, Wa-Kenya walitumia jina la Bongo muda wote.

Pichani hapa kushoto ni jamaa wawili kutoka Guatemala. Niliwapa makala yangu fupi, "Chickens in the Bus," tukaongea kuhusu tamaduni zetu, tukaona jinsi zinavyofanana. Ni kawaida kuwaona watu  Guatemala wakisafiri ndani ya basi wakiwa wamebeba kuku au hata nguruwe. Kwa mujibu wa mama mmoja Mmarekani aliyefika mezani pangu na kuiona makala hiyo, Mexico nako unaweza kuwaona watu ndani ya basi wakiwa na kuku au nguruwe.

Kwa kufahamu kwamba wa-Marekani wanashangaa mambo hayo, nimekumbushia katika makala yangu kuwa hapa Marekani ninawaona watu wakisafiri na mbwa katika magari yao.

Kama picha zangu zinavyoonyesha, tamasha lilihudhuriwa na watu wa tamaduni mbali mbali. Mji wa Rochester una watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kutoka Afrika, kwa mfano, kuna wa-Somali wengi katika mji huu.

Kulikuwa na maonesho ya bidhaa, mavazi, kazi za sanaa, kama vile michoro na vinyago, na ala za muziki. Kulikuwa na burudani ya nyimbo na ngoma, na hata mchezo wa karate.


























Jumuia na taasisi mbali mbali za huduma za jamii ziliwakilishwa pia.





Pichani hapa kushoto ni meza iliyowakilisha Trinidad. Nilisogea hapo, nikaongea na huyu mama. Nilimwambia kuwa ninafahamu kiasi fasihi na utamaduni wa Trinidad, tukazungumza juu ya waandishi maarufu kama V.S. Naipaul, Sam Selvon, Shiva Naipaul, na Earl Lovelace.

Tulipomwongelea mwandishi Selvon, huyu mama aliniuliza kama nimesoma riwaya yake ya The Lonely Londoners, nami nikamweleza kuwa ni riwaya mojawapo ambayo naipenda sana, nimeifundisha mara nyingi.



Lengo la tamasha, kuwaleta watu wa mataifa na tamaduni za ulimwengu pamoja kwa ajili ya kufahamiana, kuelimishana, na kufurahia maonesho mbali mbali lilifanikiwa sana. Nimeandika taarifa ya tamasha hili katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Waandaji wa tamasha, Rochester International Association, wanastahili sifa na pongezi kwa kazi yao nzuri.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...