Monday, February 27, 2017

Mahojiano: Beca Lewis na Joseph Mbele

Miezi michache iliyopita, jirani yangu mmoja, mama Mmarekani, aitwaye Merrilyn, ambaye ni mpiga debe wa maandishi na shughuli zangu za uelimishaji, alimwelezea habari zangu rafiki yake aishiye Ohio. Halafu alimpelekea kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Wakati huo huo, alituunganisha kupitia mtandao wa Facebook.

Beca Lewis, nilikuja kufahamu, ni mwandishi, mwelimishaji, na mmiliki na mwendeshaji wa kituo cha mawasiliano kiitwacho The Shift. Kutokana na alivyomsikia rafiki yake Merrilyn na kutokana na kusoma kitabu changu, Beca Lewis aliniuliza kama ningekubali kufanya mahojiano naye. Nilivyokubali, tulipanga siku, tukafanya mahojiano tarehe 14 Februari, saa tano asubuhi.

Leo, Beca Lewis ameyaweka mahojiano yetu hewani, nami nayaleta hapa katika blogu yangu:
http://theshift.com/podcast/every-culture-is-weird-and-wonderful/

Sunday, February 26, 2017

Mpiga Debe Wangu Kutoka Liberia

Nina jadi ya kuwatambulisha wasomaji na wapiga debe maarufu wa vitabu vyangu katika blogu hii. Ninafanya hivyo ili kuwashukuru, nikizingatia kuwa wanachangia mafanikio yangu kwa jinsi wanavyoupokea mchango wangu.

Leo ninapenda kumtambulisha Charles Chanda Dennis, raia wa Liberia ambaye anaishi hapa Marekani, jimbo la Minnesota. Huyu ni mtu maarufu, hasa katika jamii ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi. Ni mtangazaji na mwendeshaji wa kipindi kiitwacho African Roots Connection katika KMOJ Radio.

Sikumbuki ni lini nilifahamiana na Charles, lakini nadhani ni miaka karibu kumi iliyopita. Aliwahi kunialika kama mgeni katika kipindi chake tukahojiana juu ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Wiki chache zilizopita, alinialika tena, tukafanya mahojiano marefu na ya kina ambayo unaweza kuyasikiliza hapa:

https://www.dropbox.com/home?preview=Story+Telling.mp3

Miaka yapata mitano iliyopita, Charles alialikwa na wanafunzi hapa chuoni St. Olaf kutoa mhadhara juu ya historia ya mahusiano na harakati za watu wa asili ya Afrika. Nilihudhuria mhadhara ule. Charles alithibitisha kuwa ni msomi wa uhakika, mwenye uwezo mkubwa wa kuchambua mambo. Anafahamu vizuri njia waliyopitia watu weusi barani Afrika na nje ya Afrika, hasa Marekani.

Alivyonialika kwenye mahojiano safari hii, hatukuongelea angenihoji kuhusu nini hasa, bali nilihisi kuwa alitaka kufuatilia masuala ambayo ninashughulika nayo katika jamii, kama mwalimu na mtoa ushauri kuhusu tamaduni. Niliguswa na masuali yake, kama inavyosikika katika ukanda wa mahojiano niliyoweka hapa juu.

Niliguswa kwa namna ya pekee jinsi Charles alivyonitambulisha kwa wasikilizaji, akinipigia debe kwa bidii na kuwahamasisha watu wasome Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Ninamshukuru kwa hilo, nikizingatia umaarufu wa kipindi chake cha African Roots Connection na KMOJ Radio kwa ujumla.

Saturday, February 25, 2017

Tafsiri Yangu ya "A Time to Talk" (Robert Frost)

Leo nimetafsiri shairi fupi la Robert Frost, "A Time to Talk." Hili ni shairi nililolisoma kwa mara ya kwanza miaka mitatu iliyopita, baada ya binti yangu Zawadi kuninunulia kitabu cha mashairi ya Frost, Robert Frost: Selected Poems. Kama nilivyoelezea katika blogu hii, nilikuwa nimelazwa hospitalini mjini Minneapolis, na binti yangu, kwa kujua ninavyopenda vitabu, alininunulia hiki kitabu kinisaidie kukabili hali niliyokuwemo.

Shairi hili la "A Time to Talk" lina mawaidha mazito kuhusu maisha. Linatukumbusha umuhimu wa uungwana na ukarimu katika mahusiano yetu binadamu. Tuache fikra ya kwamba hatuna muda wa kujumuika na wenzetu, kujuliana hali, na kadhalika. Robert Frost anavyoelezea mambo katika shairi hili ananikumbusha maisha ya vijijini, ambayo niliishi tangu utotoni. Kusalimiana ni wajibu, na watu hutumia muda kujuliana hali.

Bila shaka, Frost anaukosoa utamaduni wa ubinafsi, na utamaduni wa kila mtu na maisha yake. Anaikosoa hali ambayo wanafalsafa kama Karl Marx na wafuasi wake wameiongelea vizuri kwa kutumia dhana ya "alienation." Anavyoongelea kuhusu kuwa na muda wa kuongea na wenzetu, ninaona kuwa Frost anaikejeli jamii ambayo imejiaminisha kuwa muda ni hela ("time is money"). Ninavyosema hayo mambo yanayohusu utamaduni, kama yalivyoelezwa katika shairi hili, ninakumbuka nilivyoyaelezea katika kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Kwa kumalizia, napenda nirudie jambo ambalo ninalitamka daima. Kutafsiri kazi ya fasihi ni shughuli ngumu yenye mitego na vipingamizi vingi. Nilivyojaribu kulitafsiri shairi la Frost, simaanishi kuwa tafsiri yangu ndio kilele cha ufanisi. Msomaji makini anayezifahamu vizuri sana lugha za ki-Ingereza na ki-Swahili, na sio lugha tu, bali lugha ya kifasihi, bila shaka ataona vipengele ambayo vingeweza kuboreshwa. Kwa mfano, katika mstari wa pili, utatafsirije "a meaning walk," ili uziwasilishe kwa ki-Swahili dhana zilizomo katika huo usemi wa ki-Ingereza?
------------------------------------------------------------------------------------------------------------

A TIME TO TALK (Robert Frost, 1874-1963)

When a friend calls to me from the road
And slows his horse to a meaning walk,
I don't stand still and look around
On all the hills I haven't hoed,
And shout from where I am, What is it?
No, not as there is a time to talk.
I thrust my hoe in the mellow ground,
Blade-end up and five feet tall,
And plod: I go up to the stone wall
For a friendly visit.

MUDA WA MAONGEZI

Rafiki anaponiita kutoka barabarani
Huku akipunguza kwa makusudi mwendo wa farasi wake,
Sisimami tu na kuangalia huko na huko
Kubaini idadi ya vilima ambavyo bado sijalima
Na kisha kupaaza sauti pale nilipo, Vipi?
Hapana, hapana kwani kuna muda wa kuongea.
Nasimika jembe langu katika ardhi tepetepe,
Ubapa wa jembe ukiwa juu futi tano toka ardhini,
Na ninatembea taratibu: ninaelekea kwenye ukuta wa mawe
Kukutana na rafiki.

Friday, February 24, 2017

Ninafurahia Kusoma "Eugene Onegin"

Siku chache zilizopita, niliandika kuwa utungo wa Pushkin, Eugene Onegin, ni mtihani. Madhumuni ya kuandika taarifa ile ilikuwa ni kujiwekea kumbukumbu ya usomaji wangu, sio kufanya uchambuzi au tathmini ya utungo. Nilivyotaja dhana ya mtihani, nilimaanisha kuwa utungo huo unahitaji tafakari ya dhati kuelewa vizuri. Wazo hilo lilijengeka akili mwangu wakati nasoma sura ya kwanza ya Eugene Onegin.

Lakini lazima nikiri pia kuwa kuna beti ambazo hazihitaji juhudi kubwa kuzielewa. Kwa kuwa ninasoma tafsiri, siwezi kujua kama ugumu unatokana na utungo wa asili au tafsiri. Kwa pamoja, ingawa ni tafsiri, hizi beti zote zinavutia kwa ukwasi wa sanaa. Mfano ni beti mbili za mwanzo wa sura ya pili ya Eugene Onegin:

They bored Onegin past all measure
These woodlands, though a charming spot.
A friend of innocent, sweet pleasure
Might well thank Heaven for this plot.
The lonely manor found protection
From wind in hills, and in reflection
It danced upon the brook below.
The distant meadows' blurry glow
Was gold from untold blooms collected.
Far hamlets glistened through the air,
And flocks sought pasture here and there.
A garden, grand but long neglected,
Was choked with weeds grown thick and tight:
Fine shelter for a dreamy sprite.

The stately manse had been erected
As manses ought to be: to last.
'Twas solid, tranquil, well-protected:
A tasteful tribute to the past.
The rooms were high and overawing,
And in the drawing-room, some drawing --
Tsarina, tsar -- graced every tall
And plushly damask-covered wall.
The ovens featured flow'ry tiles.
Although this sounds passe today,
The reason why, I can't quite say.
At any rate, to all such styles
The squire was equally undrawn:
At old rooms, new rooms, he'd just yawn.

Katika beti hizi, tunaona kuwa Onegin, ambaye ndiye mhusika mkuu, ni mtu wa ajabu. Mazingira ambayo yangemvutia binadamu mwingine, yeye hayamshitui, wala haoni mvuto wake. Mazingira haya yanaelezwa kwa mtindo unaonikumbusha mkondo wa fasihi uitwao "Romanticism," kama inavyodhihirika, kwa mfano, katika shairi la William Wordsworth, "Lines Composed a Few Miles Above Tintern Abbey," ambalo linaanza hivi :

Five years have past; five summers, with the length
Of five long winters! and again I hear
These waters, rolling from their mountain-springs
With a soft inland murmur.--Once again
Do I behold these steep and lofty cliffs,
That on a wide secluded scene impress
Thoughts of more deep seclusion; and connect
The landscape with the quiet of the sky.

Pushkin alifahamu fasihi za mataifa mbali mbali, kama nilivyogusia katika blogu hii.
Hata hao waandishi wa mkondo wa "Romanticism" aliwafahamu. Kwa mfano, katika sura ya pili ya Eugene Onegin, kwa mfano, Pushkin anawataja Goethe na Schiller, waandishi maarufu wa Ujerumani.

Tuesday, February 21, 2017

Kitabu Nilichonunua Leo: "The Fundamentals of Tawheed"

Leo nilikuwa mjini Minneapolis. Baada ya shughuli zangu, niliamua kwenda kwenye duka la vitabu vya dini ya Uislam liitwalo Akmal Bookstore. Niliwahi kulitembelea duka hilo, kama nilivyoandika katika blogu hii.

Kama nilivyoona mara ya kwanza, duka hili lina vitabu vingi vya Uislam. Leo nilitumia muda kuvipitia. Hatimaye niliamua kununua The Fundamentals of Tawheed: Islamic Monotheism, cha Dr. Abu Ameenah Bilal Philips. Huyu nilifahamu habari zake tangu miaka kadhaa iliyopita. Alizaliwa Jamaica, lakini alikulia Canada, ambako alisilimu mwaka 1972. Nimesikiliza hotuba zake mtandaoni. Ni mmoja wa watu wanaosifika kwa ufahamu wao wa dini ya Uislam.

Kama nilivyowahi kuandika tena na tena katika blogu hii, ninasoma vitabu vya Uislam na dini zingine kwa ajili ya kujielimisha, sio kwa ajili ya kubadili dini. Nina dini yangu, na nitabaki hivyo. Ninaiheshimu dini yangu, na ninaziheshimu dini za wengine. Ninategemea wengine nao wafanye hivyo, vinginevyo sisiti kuwakabili kwa hoja.

Vile vile, kwa kuwa ninafundisha kozi niliyoitunga iitwayo Muslim Women Writers, na mara kwa mara katika kozi zingine za fasihi ninafundisha maandishi ya wa-Islam, ni muhimu nijielimishe juu ya Uislam. Mwalimu wa somo lolote ana wajibu wa kujielimisha daima. Katika kufundisha tunachambua mambo, hatufundishi kama wafanyavyo katika nyumba za ibada, kwa lengo la kuimarisha imani ya dini au kuwavuta watu wawe waumini wa dini. Darasa langu si kanisa au msikiti. Hoja zozote zinakaribishwa na kutafakariwa kwa uhuru kamili, hata zile zinazokosoa au kupinga dini.

Kwa mtazamo wangu, kila mtu ana wajibu wa kujielimisha kuhusu dini za wengine. Kujielimisha kuhusu dini mbali mbali ni sawa na kujielimisha juu ya tamaduni mbali mbali. Ni hatua muhimu katika kujenga maelewano duniani, kama ninavyoelezea katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Sunday, February 19, 2017

Utungo wa Pushkin, "Eugene Onegin," Ni Mtihani

Siku chache zilizopita, niliandika katika blogu hii kuwa nilikuwa ninajiandaa kusoma Eugene Onegin, utungo maarufu wa Alexander Pushkin. Nilianza hima, na sasa ninaendelea.

Nilifahamu tangu zamani kuwa Pushkin alikuwa ameandika tungo zingine pia. Nilifahamu kuwa Eugene Onegin ndio utungo wake maarufu kuliko zingine. Nilifahamu kuwa utungo huo ni riwaya iliyoandikwa kwa mtindo wa kishairi.

Nilidhani kuwa ningesoma Eugene Onegin bila matatizo, kama ninavyosoma kazi za waandishi wengi. Baada ya kuanza kuusoma, na ninavyoendelea kusoma, ninajikuta kama vile niko katika mtihani. Eugene Onegin si rahisi kama nilivyodhani.

Pushkin ameusuka utungo wake kwa umahiri mkubwa, akitumia mbinu mbali mbali za kisanii, na pia taarifa za wasanii wa mataifa mbali mbali, kuanzia zama za kale, hadi zama zake. Humo kuna majina ya watunzi wa mataifa mbali mbali, kama vile Theocritus, Juvenal, Ovid, Racine, Chateaubriand, Lord Byron, pamoja na waandishi na waigizaji kadha wa kadha wa u-Rusi, wa wakati wa Pushkin na kabla yake, ambao hata mimi sikuwa ninawafahamu.

Kwa kufuatilia dondoo, dokezo, na maelezo yaliyomo, ninajifunza mambo mengi mapya. Mtindo huu wa Pushkin unanikumbusha ushairi wa Derek Walcott. Kusoma mashairi yake ni chemsha bongo. Unajikuta ukipelekwa sehemu nyingi katika historia, ikiwemo historia ya fasihi, sanaa, na falsafa.

Tafsiri ya Eugene Onegin ninayosoma ni ya Hofstadter. Katika kupambana na tafsiri yake, nimefikia uamuzi kuwa nikimaliza kusoma tafsiri, nisome tafsiri nyingine angalau moja ya mtu tofauti. Lakini ukweli utabaki kuwa ingekuwa bora zaidi kama ningekuwa ninakifahamu ki-Rusi, nikajisomea mwenyewe alichoandika Pushkin. Kama taaluma inavyotufundisha, hakuna tafsiri ambayo inaweza kuwa sawa na utungo unaotafsiriwa.

Mtu unaweza kujiuliza: Kwa nini ninajipitisha katika mtihani huu wa kusoma Eugene Onegin, badala ya kusoma vitabu rahisi? Jibu langu ni kuwa chemsha bongo ni muhimu kwa afya ya ubongo, kama vile mazoezi ya viungo yalivyo muhimu kwa afya ya binadamu. Utungo kama Eugene Onegin, kwa jinsi ulivyosheheni utajiri wa fikra na kumbukumbu za aina mbali mbali, ni njia bora ya kutajirisha akili. Nitajisikia mwenye furaha nitakapoweza kusema nimeusoma na kuutafakari kwa makini utungo huu mashuhuri wa Pushkin.

Saturday, February 18, 2017

Mahojiano Radio KMOJ: Charles Dennis na Joseph L. Mbele

Tarehe 4 Februari, 2017, nilikuwa mgeni katika programu ya African Roots Connection ya Radio KMOJ, Minnesota. Mwendesha kipindi Charles Dennis alifanya mahojiano nami juu ya masuala mbali mbali yanayohusu historia na utamaduni wa watu wenye asili ya Afrika. Unaweza kuyasikiliza mahojiano hayo hapa:
https://www.dropbox.com/home?preview=Story+Telling.mp3

(mpiga picha Zawadi Mbele)


Friday, February 17, 2017

Umuhimu wa Kuzifahamu Tamaduni za Wengine

Mada ya tofauti za tamaduni na athari zake duniani ninaishughulikia sana. Kwa mfano, nimeandika kitabu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nimeongelea suala hilo pia katika kitabu changu kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Vile vile ninaliongelea mara kwa mara katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza.

Umuhimu wa kuzifahamu tofauti za tamaduni unaonekana wazi wazi wakati tunapokumbana na matatizo katika mahusiano yetu na watu wa tamaduni ambazo si zetu. Tusijidanganye kwamba jambo hilo ni la kinadharia tu na kwamba halituhusu. Miaka michache iliyopita, wafanya biashara wa Tanzania walikwenda Oman kushiriki maonesho ya biashara. Walipata shida kutokana na kutojua utamaduni wa watu wa Oman. Taarifa hiyo iliandikwa katika blogu ya Michuzi.

Suala hili haliwahusu wafanya bashara tu, bali wengine pia, kama vile wanafunzi wanaokwenda nchi za nje, wanadiplomasia, watu wanaokwenda mikutanoni, na kadhalika. Kwa kuzingatia hayo, na kwa kuwa nimekuwa nikifanya utafiti katika masuala hayo, nimekuwa nikipata mialiko ya kutoa ushauri kwa jumuia na taasisi mbali mbali hapa Marekani. Vyuo vya Marekani, kwa mfano, vinapopeleka wanafunzi nchi za nje, kama vile nchi za Afrika, vinazingatia suala la kuwaandaa wanafunzi kwa kuwaelimisha kuhusu utamaduni wa huko waendako. Mwaka hadi mwaka nimealikwa kutoa elimu hiyo.

Nimewahi pia kuendesha semina Tanzania, kwenye miji ya Arusha, Tanga, na Dar es Salaam. Vile vile, kwa kuombwa na ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, niliwahi kutoa mihadhara Zanzibar na Pemba, juu ya utamaduni wa Marekani, kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Kwa jinsi ninayofahamu umuhimu wa suala hili, nimekuwa nikikumbushia mara kwa mara kila ninapoweza. Kwa mfano, uhusiano ulipoanza kuimarika baina ya Tanzania na u-Turuki, nilikumbushia suala hilo katika blogu hii. Ningependa kuona suala hili la athari za tofauti za tamaduni linapewa kipaumbele katika maisha yetu kwani kulipuuzia ni kujitakia matatizo yasiyo ya lazima. Hii ndio sababu iliyonifanya nianzishe kampuni ya kutoa elimu na ushauri iitwayo Africonexion: Cultural Consultants.

Sunday, February 12, 2017

Nimemaliza Kusoma The Highly Paid Expert

Leo nimemaliza kusoma The Highly Paid Expert, kitabu kilichotungwa na Debbie Allen, ambacho nilikitaja katika blogu hii. Nimekifurahia kitabu hiki, kwa jinsi kilivyoelezea misingi na mbinu za kumwezesha mtu kuwa mtoa ushauri mwenye mafanikio kwake na kwa wateja.

Mambo anayoelezea mwandishi Debbie Allen yananihusu moja kwa moja katika ya kampuni yangu ya Africonexion: Cultural Consultants. Kwa hivi, kitabu hiki kimekuwa na mvuto wa pekee kwangu. Nimevutiwa na namna mwandishi anavyoelezea mbinu za mtu kujijenga katika uwanja wake hadi kufikia kileleni. Anaelezea mategemeo ya wateja na namna ya kushughulika nao. Anaelezea umuhimu wa kujifunza kutoka kwa wataalam wengine, matumizi ya tekinolojia katika kuwasiliana na wateja, kuendesha mikutano, na kujitangaza. Vile vile anasisitiza uaminifu na uwajibikaji.

Ameelezea vizuri namna wengi wetu tunavyoshindwa kujitangaza na tunavyoshindwa au kusita kutambua umaarufu na umuhimu wetu na thamani ya ujuzi wetu, jambo ambalo linatufanya tusitegemee malipo yanayoendana na ubingwa wetu. Tunaridhika na malipo hafifu, wakati tulistahili malipo makubwa.

Sura ya 24 ya The Highly Paid Expert inaelezea uandishi wa kitabu. Mwandishi anasema kuwa kitabu ni nyenzo muhimu ya mtaalam katika fani yake. Kitabu kinamjengea sifa na kuonekana. Kinamfanya mtaalam aaminike. Mwandishi anaeleza wazi kuwa kitabu hakileti utajiri, bali kinafungua milango ya fursa.

Hayo nimejionea mwenyewe. Kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kimenifungulia fursa nyingi. Nimepata mialiko ya kwenda kutoa mihadhara au ushauri katika taasisi na jumuia mbali mbali, kama vile makanisa, vyuo, na makampuni.

Nimevutiwa na mambo anayoelezea mwandishi wa The Highly Paid Expert kuhusu uandishi na uuzaji wa kitabu. Yanafanana na yale ambayo nami nimekuwa nikieleza katika blogu hii. Kwa mfano, anasema kuwa jukumu kubwa la kutangaza na kuuza kitabu ni la mwandishi.

The Highly Paid Expert ni kati ya vitabu ambavyo nimevifurahia kwa dhati. Mawaidha yake mengi ni ya kukumbukwa daima. Mfano ni msisitizo wake juu ya kushirikiana na wengine. Mtu hufanikiwi kwa uwezo wako mwenyewe tu na kutojihusisha na wengine wenye utaalam, hata kama ni washindani wako.

Saturday, February 11, 2017

Ninamwazia Mwandishi Alexander Pushkin

Kwa wiki yapata mbili, nimekuwa nikimwazia sana Alexander Pushkin, mwandishi maarufu wa u-Rusi. Nimefahamu tangu ujana wangu kuwa wa-Rusi wanamwenzi kama baba wa fasihi ya u-Rusi. Miaka ya baadaye, nilikuja kufahamu kuwa Pushkin alikuwa na asili ya Afrika, na kwamba hata katika baadhi ya maandishi yake aliongelea suala hilo.

Nilisoma makala za profesa moja wa Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, nikafahamu zaidi suala hilo. Katika kufuatilia zaidi, niliguswa na mengi, hasa maelezo juu ya kipaji cha Pushkin cha ajabu katika matumizi ya lugha ya ki-Rusi na ubunifu wake, na pia jinsi alivyokufa. Aliuawa katika ugomvi akiwa na umri wa miaka 37 tu.


Siku kadhaa zilizopita, nilitoa mhadhara katika darasa la Nu Skool, kuhusu umuhimu wa Afrika na wa-Afrika katika historia ya ulimwengu. Kati ya watu maarufu wenye asili ya Afrika ambao niliwataja kwa mchango wao ni Antar bin Shaddad wa Saudi Arabia na Pushkin. Antar bin Shaddad ni mshairi aliyeishi kabla ya Mtume Muhammad, na ambaye tungo zake zinakumbukwa kama hazina isiyo kifani katika lugha ya ki-Arabu. Pushkin ni hivyo hivyo; wa-Rusi wanakiri kuwa umahiri wake katika kuimudu lugha yao hauna mfano.

Kutokana na hayo nimekuwa na hamu ya kumsoma Pushkin, nikakumbuka kuwa nilishanunua kitabu chake maarufu, Eugene Onegin, ambayo ni hadithi iliyoandikwa kishairi. Ninajiandaa kuisoma.

Friday, February 3, 2017

Miaka 50 ya Azimio la Arusha

Tarehe 5 Februari, mwaka huu, itakuwa ni siku ya maadhimisho ya miaka 50 tangu "Azimio la Arusha" litangazwe, tarehe 5 Februari, 1967. Watu wa rika langu na wale wa umri mkubwa zaidi wanakumbuka jinsi "Azimio la Arusha" lilivyotangazwa na kupokelewa nchini. Wanakumbuka msisimko wa furaha na matumaini ulioigubika nchi kutokana na Azimio hilo.

Azma ya kuondoa unyonyaji, kuweka njia kuu za uchumi katika mikono ya wakulima na wafanyakazi, kujenga usawa, kuhakikisha kila mtu mwenye uwezo anafanya kazi na anapata malipo halali ya kazi yake, na kujenga nchi yenye kujitegemea, yote hayo yaliisisimua nchi nzima.

"Azimio la Arusha" lilielezea kuwa tumekosea kwa imani yetu kuwa pesa ndio msingi wa maendeleo. Lilitufundisha kuwa msingi wa maendeleo ni watu wenyewe, sio pesa. Na huo ni ukweli hata katika mazingira ya leo. Msingi wa maendeleo ni watu kutumia nguvu yao, akili, maarifa, ubunifu, na uthubutu, bila kutetereka. Maendeleo yanatokana na watu, ni maamuzi ya watu wenyewe, kujipangia malengo, wala hayaletwi kutoka nje.

Leo wa-Tanzania wamepotea njia. Wanaamini kuwa serikali itawaletea maendeleo, au rais atawaletea maendeleo. Wanaamini kuwa pesa ndio msingi wa maendeleo. Wakati wa serikali ya awamu ya nne, palikuwa na mpango ulioitwa "mabilioni ya Kikwete" ambao ulikuwa ni mpango wa kuwagawia watu pesa za miradi. Vile vile, katika kampeni za urais za mwaka 2015, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, John Pombe Magufuli, aliahidi kupeleka shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Imani imejengeka kuwa pesa ndio msingi wa maendeleo.

Lakini, kwa kuzingatia kuwa watu ndio msingi wa maendeleo, "Azimio la Arusha" lilituelekeza katika kutambua umuhimu wa kuwekeza katika watu, kwa njia ya elimu, maarifa, uhuru wa kutoa mawazo, na demokrasia. Huu ulihesabiwa kama msingi muhimu wa maendeleo. Maendeleo yanategemea watu walioelimika, wenye kufikiri, kuhoji mambo, na kutoa mawazo. Kwa ajili hiyo, "Azimio la Arusha" lilifuatiwa na matamko mengine, yaliyofafanua dhana hizi, kama vile "Elimu ya Kujitegemea."

Kwa maneno mengine "Azimio la Arusha" liliona mbali likaweka msingi ambao leo unawafanya watu makini ulimwenguni waongelee kile kinachoitwa "knowledge economy" kwa ki-Ingereza. Wa-Tanzania hatuna habari hiyo; tunasubiri mabilioni ya Kikwete au milioni 50 za Magufuli.

Mwalimu Julius Nyerere, muasisi wa "Azimio la Arusha," hakuchoka kuendelea kufafanua maana na malengo ya "Azimio la Arusha." Kwa mfano, dhana ya kuwa msingi na lengo la maendeleo ni watu aliifafanua katika kitabu cha "Binadamu na Maendeleo." Dhana ya demokrasia iliendelea kufafanuliwa katika "Mwongozo wa TANU," ambao ulisisitiza kuwa uongozi si unyapara. Kiongozi alitakiwa awe sambamba na watu katika kujadili masuala na kutoa maamuzi.

Hayo yote ni ishara ya namna Mwalimu Nyerere alivyojali dhana ya kwamba watu ndio msingi wa maendeleo. Ninaposema hivi, ninakumbuka jinsi dhana hii inavyofanana na ile ya Mao Tse-tung, ambayo kwa ki-Ingereza ilitafsiriwa kama "mass line," na pia ninakumbuka dhana ya Kim il Sung iliyoitwa "the juche idea."

Kuna mengi ya kutafakari juu ya "Azimio la Arusha." Kwa mtazamo wangu, ukiachilia mbali kupatikana kwa Uhuru na Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, hakuna jambo jingine la muhimu lililowahi kutokea katika miaka yetu hii kama "Azimio la Arusha." Uhuru, Muungano, na "Azimio la Arusha" ndio mambo muhimu kuliko yote.

Kwa hivyo, haipendezi kushuhudia namna siku hizi za kuelekea siku ya kumbukumbu ya miaka 50 ya "Azimio la Arusha" zinavyopita kama vile ni siku za kawaida tu. Ilitakiwa kuwe na msisimko mkubwa nchi nzima kwa mikutano, warsha, na hotuba za kutathmini nafasi na maana ya "Azimio la Arusha" katika Taifa letu na ulimwenguni.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...