Thursday, December 17, 2015

Mdau Kanishukuru kwa Kutafsiri "Kimbunga"

Ninavyoandika katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza huwa sina namna ya kujua ni nani atasoma nilichoandika. Siwezi hata kujua kama niandikacho kitasomwa na yeyote. Ni kubahatisha. Kwa kutambua hilo, nimediriki kusema kwamba ninapoandika katika blogu, ninajiandikia mwenyewe.

Hata hivi, ukweli unajitokeza kuwa kuna watu wanaosoma niandikayo. Katika blogu kuna sehemu ambapo ninafuatilia na kuona takwimu za utembeleaji wa blogu na orodha ya makala zinazosomwa au kupitiwa siku hadi siku.

Nimefurahi kusoma leo ujumbe wa mdau akinishukuru kwa tafsiri yangu ya "Kimbunga," shairi la Haji Gora Haji. Ameandika:

Thank you so much for translating this poem. I'd been searching to read poems originally written in Swahili. Immense gratitude Joseph.

Nimefurahi kuwa nimempa mdau huyu angalau tone la kutuliza kiu yake kuhusu mashairi ya ki-Swahili. Amenipa motisha ya kuendelea kutafsiri tungo za ki-Swahili, ili afaidike zaidi kwa kutambua utajiri wa jadi ya tungo za ki-Swahili ambayo imekuwepo na kustawi kwa karne kadhaa.

Ninamkumbuka pia mtunzi Haji Gora Haji. Nikiweza, kwa idhini yake, kutafsiri mashairi yake na kuyachapisha kama kitabu, kama alivyofanya Clement Ndulute kwa mashairi ya Shaaban Robert, itakuwa ni jambo la manufaa katika kumtangaza na kuuelimisha ulimwengu.

Wednesday, December 16, 2015

Nimeitafsiri Sala ya Papa Francis

Nilielezea katika blogu hii nia yangu ya kuitafsiri sala ya Papa Francis ambayo ni sehemu ya waraka wake wa kitume, "Laudato Si." Papo hapo, ninafahamu vizuri kuwa kutafsiri ni suala tata. Katika ujumbe wangu, niliandika kuwa

"napenda kusema kwamba sala hii ilivyo katika ki-Ingereza ikiwa imesheheni uchaji, busara, na maudhui, imeundwa kwa lugha iliyotukuka. Ninajiuliza iwapo tunaweza kuitafsiri kwa ki-Swahili, tukahifadhi utukufu wake kwa msingi wa uhalisia wa ki-Swahili. Ninajiuliza hivyo pamoja na kufahamu jinsi suala la tafsiri lilivyo gumu na tata. Ninatarajia kujaribu kuitafsiri sala hii siku zijazo."

Hata hivi, nimejaribu kutafsiri sala ya Papa Francis, ili kuwapa angalau fununu wale ambao hawajui ki-Ingereza. Ni bora kufanya hivyo, kuliko kuacha kabisa. Ye yote anayekijua ki-Ingereza vizuri, na pia anakijua ki-Swahili vizuri, ataona kuwa nimejipa mtihani mgumu. Ninamhimiza naye ajaribu kutafsiri.

A prayer for our earth

All-powerful God, you are present in the whole universe
and in the smallest of your creatures.
You embrace with your tenderness all that exists.
Pour out upon us the power of your love,
that we may protect life and beauty.
Fill us with peace, that we may live
as brothers and sisters, harming no one.
O God of the poor,
help us to rescue the abandoned and forgotten of this earth,
so precious in your eyes.
Bring healing to our lives,
that we may protect the world and not prey on it,
that we may sow beauty, not pollution and destruction.
Touch the hearts
of those who look only for gain
at the expense of the poor and the earth.
Teach us to discover the worth of each thing,
to be filled with awe and contemplation,
to recognize that we are profoundly united
with every creature
as we journey towards your infinite light.
We thank you for being with us each day.
Encourage us, we pray, in our struggle
for justice, love and peace.

Sala Kuiombea Dunia Yetu

Mungu mweza yote, upo kila mahali

na hata katika viumbe vyako vidogo kabisa.
Unakumbatia kwa upole wako kila kilichopo.
Tufurikie nguvu ya upendo wako
ili tuuhifadhi uhai na uzuri.
Tujaze amani, ili tuishi
kama kaka na dada, bila kumdhuru yeyote.
Ee Mungu wa maskini,
tusaidie kuwanusuru waliotelekezwa na kusahauliwa katika dunia hii,

ambao wana thamani isiyo kifani machoni mwako.
Tuletee uponyaji maishani mwetu,
ili tuihifadhi dunia badala ya kuwania kuipora,
ili tustawishe uzuri, si uchafuzi na uharibifu.
Gusa mioyo
ya wale wanaowania maslahi yao tu
yanayowagharimu maskini na dunia.
Tufundishe kuibaini thamani ya kila kitu,
kujawa na uchaji na tafakari,
kutambua
 kuwa tumefungamana
na kila kiumbe
tunavyoelekea kwenye nuru yako isiyo na mwisho.
Tunakushukuru kwa kuwa nasi kila siku.

Tuhimize, tunakuomba, katika juhudi zetu
za kutafuta haki, upendo na amani.

Wednesday, December 9, 2015

Mtunzi Haji Gora Haji

Leo nimeamua kuongelea kifupi utunzi wa Haji Gora Haji wa Zanzibar, mmoja wa waandishi maarufu wa ki-Swahili wa zama zetu hizi. Nafurahi kuwa niliwahi kuonana naye mjini Zanzibar na kuzungumza naye. Panapo majaliwa, nitaandika taarifa ya mazungumzo yetu, ambayo yalihusu maisha yake katika sanaa. Ni muhimu kuutangazia ulimwengu kazi murua inayofanywa na watu wetu wenye vipaji kama Haji Gora Haji.

Nina vitabu vyake vinne: Kimbunga (Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press, 1994), Utenzi wa Visa vya Nabii Suleiman Bi Daudi (A.S.) (Zanzibar: Al-Khayria Press Ltd, 1999), Kamusi ya Kitumbatu (Zanzibar: Express Printing Services, 2006), na Siri ya Ging'ingi (Dar es Salaam: Taasisi ya Taaluma za Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam, 2009).

Kadiri siku zinavyopita, wasomaji na wahakiki wanajitokeza na kuongelea uandishi wa Haji Gora Haji. Mifano ya kutambuliwa huko ni taarifa ya Amanda Leigh Lichtenstein, ya Ridder Samson, na ya Pascal Bacuez. Nami nimetafsiri mashairi yake mawili nikayachapisha hapa, hapa, na hapa.

Haji Gora Haji, kama walivyo watunzi wengi, wa zamani hadi leo, wamejengeka katika jadi ya fasihi simulizi. Wanaitumia jadi hii katika utunzi wao, iwe ni mashairi kama walivyofanya W.B. Yeats na Derek Walcott, au riwaya, kama walivyofanya Charles Dickens na Chinua Achebe, au tamthilia, kama walivyofanya William Shakespeare, Wole Soyinka na Ebrahim Hussein, au hadithi fupi, kama walivyofanya Lu Hsun na Ama Ata Aidoo.

Ni hivyo hivyo kwa Haji Gora Haji, kama nilivyowahi kutamka. Utumiaji wa mbinu, miundo, na hata dhamira zitokanazo na fasihi simulizi kunachangia uwezo wa tungo kugusa fikra na hisia za hadhira kwa namna ya pekee kutokana na kwamba fasihi simulizi ni urithi wa wanadamu wote. Maudhui yatokanayo na fasihi simulizi ni ya thamani kwa wanadamu wote.

Kuthibitisha zaidi namna Haji Gora Haji alivyojengeka katika fasihi simulizi, sikiliza anavyosimulia hadithi ya Paa na Pweza.


Monday, December 7, 2015

Nimesaini Vitabu Kwa Ajili ya Filamu ya "Papa's Shadow"

Wakati wa kampeni ya Ramble Pictures ya kuchangisha fedha kulipia gharama za filamu ya Papa's Shadow, nilichangia fedha kiasi na pia nakala za kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Walikuwa wameweka viwango mbali mbali vya michango ambavyo viliendana na vizawadi na vivutio kwa wachangiaji. Waliochangia dola 200 au zaidi waliahidiwa nakala ya kitabu changu kama zawadi.

Leo, Jimmy Gildea, mwanzilishi wa Ramble Pictures na mtengenezaji wa Papa's Shadow, ambaye alikuwa mwanafunzi katika kozi yangu ya Hemingway, alinifuata hapa chuoni St. Olaf, nikasaini nakala tano za kitabu changu, na kumkabidhi.

Tulipata fursa ya kuongelea habari za Ernest Hemingway, ziara yetu ya Montana, msisimko na mafanikio ya kampeni ya kuchangisha fedha, na kadhalika. Vile vile, Jimmy alinirekodi nikiwa nasoma kitabu cha Green Hills of Africa na pia nikiwa natembea katika sehemu iliyoonyesha vizuri mandhari ya chuo. Jimmy aliniuliza iwapo nina picha za ujana na utoto wangu. Anakusanya hayo ili kuyatafutia nafasi katika filamu ya Papa's Shadow, ingawa tayari ni nzuri sana, kwa jinsi nilivyoiona.

Papa's Shadow inategemewa kupatikana wiki chache kuanzia sasa, labda mwezi Februari. Si filamu ya kuigiza bali ni mazungumzo juu ya maisha, uandishi, na falsafa, ya Ernest Hemingway, hasa inavyohusiana na safari zake Afrika Mashariki, miaka ya 1933-34 na 1953-54. Sehemu kubwa ya filamu hii ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliye bado hai. Ni filamu inayoelimisha, si burudani.

Saturday, December 5, 2015

Kuwalea Watoto Kupenda Vitabu

Kati ya mambo yanayonivutia sana hapa Marekani ni namna wazazi wanavyowalea watoto katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu. Katika matamasha ya vitabu, maduka ya vitabu, na maktaba, ninawaona wazazi wakiwa na watoto. Nimewahi kuandika kuhusu suala hilo katika blogu hii. Lakini kwa kuwa hii ni mada ninayoitilia maanani sana, nimeamua kuiongelea tena.

Picha ya juu hapa kushoto ilipigwa mwaka 2008, niliposhiriki sherehe za kumbukumbu ya uhuru wa Nigeria hapa Minnesota. Nilikuwa na meza ya vitabu vyangu. Nakumbuka vizuri jinsi huyu mama m-Nigeria anayeonekana pichani alivyokuja mezani pangu na binti yake. Tulisalimiana, wakaangalia na kuvifurahia vitabu vyangu, kama inavyoonekana pichani.

Picha ya pili hapa kushoto nilipiga katika tamasha la vitabu la Deep Valley, mjini Mankato, Minnesota. Nilivutiwa na namna hao watoto walivyokuwa wanafuatana na mama yao kutoka meza hadi meza wakiangalia vitabu.

Picha ya tatu hapa kushoto nilipiga mwezi Agosti mwaka huu mjini Brooklyn Park, Minnesota, katika tamasha la Afrifest. Huyu bwana, m-Marekani Mweusi, alikuja na watoto wake kwenye meza yangu, kuangalia vitabu. Watoto hao ni wadogo sana, na sijui kama walikuwa wanajua kusoma, lakini, nilivutiwa na kitendo cha baba yao kuwaleta kuangalia vitabu.

Kwa wa-Marekani, umri wa mtoto si tatizo. Wanawasomea vitabu hata watoto wadogo sana, hasa kabla ya kulala. Watoto wanapenda kusomewa vitabu. Hapa naikumbuka video ya kusisimua inayomwonyesha mtoto mdogo akisomewa vitabu, halafu anavyoangua kilio kila anapoambiwa kuwa hadithi imeisha. Hebu iangalie.


Thursday, December 3, 2015

Kuhusu Kublogu

Nimekuwa mwanablogu tangu mwaka 2008. Ninaendesha blogu hii ya Hapa Kwetu na nyingine ya ki-Ingereza. Kublogu kuna mambo mengi. Kublogu kunanipa fursa ya kujieleza kwa uhuru. Hili ni jambo la msingi, kama alivyoelezea mwanablogu Christian Bwaya.

Lakini kublogu kuna matokeo yenye manufaa. Kumeniwezesha kuwafikia watu mbali mbali ambao wanatembelea blogu zangu. Siwezi kujua wanapata ujumbe gani katika maandishi yangu. Kama taaluma inayotufundisha, hili ni suala tata.

Ujumbe wa andiko ni zao la kazi anayofanya msomaji juu ya andiko. Na kwa kuwa wasomaji wana akili zinazotofautiana, na wana nidhamu na uzoefu tofauti wa kusoma, kila mmoja anaibuka na ujumbe tofauti, kwa kiwango kidogo au kikubwa.

Niliwahi kuelezea kwa nini ninablogu, lakini sidhani kama nilikuwa na majibu ya uhakika. Baadaye, katika kutafakari suala hili, nilifikia hatua ya kutamka kwamba ninablogu kwa ajili yangu mwenyewe. Labda huu ndio ukweli wa mambo.

Imani iliyojengeka katika jamii ni kuwa mwandishi anawaandikia wasomaji. Tumezoea kuona waandishi wakiulizwa wanamwandikia nani, nao wanaelezea walengwa wao. Jadi hii na imani hii imekosolewa kwa uhodari na Roland Barthes katika makala yake, "The Death of the Author."

Makala hii ya Barthes naona inaipa uzito hoja yangu kuwa ninapoblogu ninajiandikia mwenyewe. Sijui ni nani atasoma au anasoma ninachoandika. Kusema kwamba ninawaandikia wasomaji ni kama kuota ndoto. Ni kujiridhisha kwa jambo ambalo halina uhakika bali ni bahati nasibu. Nikisema ninajiandikia mwenyewe ninasema jambo la uhakika.

Tuesday, December 1, 2015

Nilitembelea Duka la Vitabu la Amkal

Tarehe 23 Mei, 2015, nilitembelea duka la vitabu la Amkal mjini Minneapolis, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Ni duka la wa-Somali ambalo linauza zaidi vitabu vinavyohusu dini ya ki-Islam. Siku hiyo nilinunua kitabu kiitwacho Jesus: Prophet of Islam. Ninapenda kuongelea, kwa kifupi na wepesi kabisa, mawazo yanayonijia ninapokumbuka ziara yangu katika duka lile.

Jambo la msingi kwamba katika kuishi kwangu hapa Marekani, nimeona jinsi wa-Afrika wa nchi mbali mbali wanavyovithamini vitabu. Kwa mfano, nimewahi kuwaongelea wa-Kenya.

Wa-Somali ni mfano mwingine. Nimekutana na wa-Somali wanaoishi hapa Minnesota ambao wanaandika vitabu. Nimejionea wanavyojitokeza kuwasikiliza waandishi wa vitabu wa ki-Somali. Mfano ni Nuruddin Farah, ambaye huonekana hapa Minnesota mara kwa mara, ingawa makao yake kwa miaka hii ni Afrika Kusini. Wanamheshimu kwa jinsi anavyowakilisha taifa lao katika ulimwengu wa uandishi.

Kwa ujumla, hao wa-Somali ni wakimbizi au wahamiaji. Lakini pamoja na kadhia hiyo, pamoja machungu waliyoyapitia, wameshikilia umuhimu wa vitabu na elimu. Katika vyuo vya hapa Minnesota, kama vile Chuo Kikuu cha Minnesota, Metropolitan State University. Mankato State University, South Central College, na Minneapolis Community and Technical College, wanafunzi wa ki-Somali ni wengi. Wanawekeza katika elimu. Wanajijengea mtaji ambao wataweza kuutumia kwa maendeleo ya nchi yao.

Suala la elimu wanalishughulika kwa namna nyingine pia, kama vile magazeti na vituo vya televisheni. Hali hii nimeiona pia miongoni mwa wa-Afrika wengine, kama vile wa-Kenya na wa-Ethiopia. Kwa kutumia njia hizo, wanazitangaza nchi zao na shughuli zao, kama vile biashara. Ninawaona ni mfano wa kuigwa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...