
Kati ya hao alikuwepo mama mmoja ambaye si rahisi kumsahau. Alifika mezani petu, na wakati tunasalimiana alinyanyua nakala ya Matengo Folktales, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, Notes on Achebe's Things Fall Apart, na Africans in the World, akasema anavinunua.
Wakati wote alikuwa anatuelezea kuwa alikuwa na binti yake ambaye aliishi China kwa miaka nane kisha akaenda Namibia, na kwamba ameipenda Namibia tangu mwanzo. Alituambia tumwekee vitabu vyake, na kwamba binti yake angefika baadaye.
Yapata nusu saa kabla ya tamasha kwisha, huyu binti alikuja. Tuliongea naye, akatuambia jinsi alivyoipenda Namibia akifananisha na China. Mama yake naye akaja. Akaulizia vile vitabu tulivyomwekea, tukavichukua chini ya meza tulipovihifadhi, tukampa. Aliziangalia "t-shirt," akainyanyua moja na kuilipia. Kwa kuwa alinunua vitu vyote hivi: vitabu vinne na "t-shirt," tulimpunguzia bei, ingawa hakutegemea. Tulisahau kupiga picha pamoja naye na binti yake, kwa kumbukumbu.

Huyu mwenzake alijitambulisha kwangu na binti yangu hiyo jana, akasema kwamba alihudhuria mhadhara wangu Chuoni South Central, "Writing About Americans." Huku akiusifia mhadhara ule, alinunua kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Paul kwenda Afrika, lakini Afrika iliuteka moyo wake kiasi kwamba anataka kwenda tena. Nimekutana au kuwasiliana na wa-Marekani wengi ambao wakishafika Afrika wanatekwa mioyo hivi hivi. Mwandishi Ernest Hemingway alikumbwa na hali hiyo wakati alipokuwa akizunguka Tanganyika mwaka 1933-34, kama alivyoandika katika Green Hills of Africa. Yeye na mke wake Pauline walijawa na hisia za kuipenda sana Tanganyika, kiasi kwamba hawakupenda kuondoka. Kwa maneno yake mwenyewe: "We had not left it, yet, but when I would wake in the night I would lie, listening, homesick for it already.”