Ualimu unahitaji moyo. Anayedhani ni mchezo, aiangalie na kuitafakari katuni hii.Bahati mbaya jina la mchoraji sijalipata, ningemshukuru.
Nilimpigia simu Mzee Patrick Hemingway tarehe 22 mwezi huu, tukaongea kwa saa moja na robo. Tuliongelea mambo mengi, kama nilivyogusia katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Mzee Patrick Hemingway ni mtoto pekee aliyebaki wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway.
Leo nilikwenda Minneapolis kwenye mkutano mdogo wa watu wanne ambao tulifanyia katika jengo la maduka na biashara mbali mbali liitwalo Somali Mall. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuingia katika jingo hili. Nilipata fursa ya kuingia katika duka la vitabu liitwalo Akmal Bookstore, ambalo limejaa vitabu vya ki-Islam katika ki-Arabu na ki-Somali.
Naandika makala hii kuwapa moyo wengine, hasa vijana, wanaojituma kujiendeleza katika fani yoyote na kimaisha kwa ujumla. Kwa ujumla, mawaidha haya yanapatikana vitabuni.
Mungu huyo huyo amenipa fursa ya kutembea katika nchi nyingi na kuonana na watu wa aina mbali mbali. Mwaka 1991, kwa mfano, nilikwenda India, nikaishi na watu wa dini tofauti na yangu. Nilipata bahati ya kutembezwa katika nyumba za ibada za dini ya Hindu, kama inavyoonekana pichani. Picha moja inanionyesha nikiwa nje ya nyumba ya ibada. Kuna sanamu nyingi, ambazo ni za miungu wa dini ya u-Hindu.
Napenda kujiwekea hapa kumbukumbu za vitabu nilivyonunua katika siku chache zilizopita. Ni faraja kuweza kupita tena katika maduka ya vitabu, baada ya miezi ya kuwa katika hali ngumu kiafya.
Kimoja ni Without a Name and Under the Tongue. Hizi ni riwaya mbili ambazo zimechapishwa katika hiki kitabu kimoja. Mtunzi ni Yvonne Vera wa Zimbabwe, ambaye ni kati ya waandishi wa kizazi kipya wa Zimbabwe. Nilishafundisha riwaya yake Butterfly Burning, na nilivyokiona kitabu chake hiyo juzi, nilifikiwa na hamu ya kusoma zaidi uandishi wake, nisikie tena sauti ya mwandishi anayeandika kuhusu nchi ya karibu na nyumbani Tanzania.
Leo nimeagiza mtandaoni kitabu cha hadithi za Luis Bernardo Honwana wa Msumbiji kiitwacho We Killed Mangy Dog and Other Stories. Kwa wiki kadhaa, nimemwazia sana mwandishi huyu, ambaye kitabu chake hiki nilikipenda sana nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1973. Nilivutiwa na jinsi alivyoielezea maisha nchini Msumbiji, ambayo ilikuwa daima mawazoni mwetu kutokana na vita vya ukombozi vilivyoongozwa na FRELIMO.
Mimi ni mwandishi wa vitabu. Ninaandika vitabu vya tahakiki ya fasihi, juu ya masuala ya jamii, fasihi simulizi, na masuala ya athari za tofauti za tamaduni, hali halisi ya uandishi wa vitabu, mbinu za kujichapishia vitabu. Naandika kuhusu utangazaji na uuzaji wa vitabu, na kuhusu hali halisi ya usomaji wa vitabu Tanzania na ughaibuni.
Siku chache zilizopita niliandika taarifa kuhusu vitabu nilivyonunua hivi karibuni. Kati ya vitabu kilikuwepo kimoja cha Moyez Vassanji, The Gunny Sack. Wakati huo, nilikuwa navingojea vitabu vingine viwili vya Moyez Vassanji, ambavyo nilikuwa nimeshavilipia. Vimefika.
Moyez Vassanji ni mwandishi maarufu, nasi wa-Tanzania tuna haki ya kusema ni mtu wetu, kwani mnali ya kukulia Tanzania, amekuwa akiipeperusha vizuri sana bendera ya nchi yetu katika ulimwengu wa fasihi. Ninaamini tunawajibika kuwa naye bega kwa bega kwa kusoma vitabu vyake.
Leo napenda kukiongelea kitabu kiitwacho Going Visual: Using Images to Enhance Productivity, Decision-Making and Profits, kilichoandikwa na Alexis Gerard na Bob Goldstein. Nilikinunua kitabu hiki miaka michache iliyopita. Kama ilivyo kawaid yangu ninaponunua kitabu, sikiweki katika maktaba yangu bila kukipitia angalau juu juu, ili nijue kinahusu nini.
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...