Kuhusu madai kwamba Lowassa ni fisadi, na kuhusu suala la CHADEMA kumkaribisha, na UKAWA kumteua kuwa mgombea wao wa urais, msimamo wangu ni kama ifuatavyo. Na napenda kuweka wazi kuwa mimi si mwanachama wala msemaji wa chama chochote cha siasa. Ni kiumbe huru, ninayetumia akili yangu na kuchambua mambo nipendavyo.
Kuna kitu kiitwacho haki za binadamu, na kuna kitu kiitwacho utawala wa sheria. Kwa mujibu wa tangazo la kimataifa la haki za binadamu, mtu yeyote anayetuhumiwa au kushtakiwa kwa kosa lolote ana haki ya kuhesabiwa kuwa hana kosa hadi mahakama ithibitishe vinginevyo.
Na hata huko mahakamani, inatakiwa uthibitisho wa hatia ya huyu mshtakiwa uwe wazi bila shaka ("reasonable doubt"). Pakiwa na hiyo "reasonable doubt," ni manufaa kwa mshtakiwa, yaani mahakama inapaswa kumwachia huru, arudi zake uraiani.
Haki hii unayo wewe, ninayo mimi, anayo Lowassa. Lowassa hajapelekwa mahakamani na kuthibitishwa ana hatia kwa vigezo nilivyotaja hapa juu.
Kwa msingi huo, CHADEMA hawajakosea kumkaribisha katika chama chao. UKAWA wamefanya jambo sahihi kumweka kama mgombea wao wa urais.
Ni kweli kuwa CHADEMA hao walikuwa wanamtukana sana Lowassa, wakamwita fisadi mkubwa, wakamweka hata kwenye orodha yao, maarufu kama "List of Shame."
Lakini nahisi CHADEMA wametambua kuwa walikosea, kwa maana kwamba hakuna mahakama iliyothibitisha kuwa Lowassa ni fisadi. Ni sahihi kwa CHADEMA kuwa na msimamo walio nao sasa juu ya Lowassa.
Wenye matatizo, wasiofuata haki, wahujumu wa haki za binadamu, ndio wanaendelea kuimba huu wimbo kuwa Lowassa ni fisadi. Wenye matatizo ni hao akina Samuel Sitta na Harrison Mwakyembe, wanaotangaza kuwa wanamtaka Lowassa aje kwenye mdahalo juu ya ufisadi wake. Akina Sitta na Mwakyembe wanafanya usanii na ulaghai. Watuhumiwa hatuwaiti kwenye mdahalo. Tunawapeleka mahakamani.
Nawashauri watu hao wajifunze kutoka kwa CHADEMA, kujirekebisha na kuzingatia utawala wa sheria na haki za binadamu.