Wednesday, December 30, 2015

Nimekutana na Mdau wa Miaka Mingi

Leo nimekutana na mdau wangu wa miaka mingi, Dr. Barbara Poole Galyen, ambaye anaishi California. Kwa siku chache hizi za Krismasi na Mwaka Mpya, yuko hapa Minnesota kwa ndugu zake. Kwa kupitia facebook tuliwasiliana na leo nilikwenda mjini Lakeville alikofikia.

Dr. Galyen na mimi tulifahamiana mwaka 1995, wakati nilipokuwa natafiti masimulizi ya jadi na tamaduni mkoani Mwanza. Utafiti huo ambao nilifanya tangu mwaka 1993 hadi 1996 uligharamiwa na shirika la Earthwatch. Dr. Galyen alikuwa mmoja wa watu kutoka nchi mbali mbali waliokuwa wanakuja Tanzania kushiriki utafiti wangu. Yeye alikuja wakati wa utafiti kisiwani Ukerewe.

Kwa kauli yake mwenyewe, huu ulikuwa mwanzo na msingi wa yeye kuipenda Afrika, hadi akaenda kufanya kazi Kenya katika United States International University, ambapo nilimtembelea mwaka 1997. Hatimaye alianzisha kampuni ya ushauri kuhusu masuala tamaduni ulimwenguni. Shughuli hizi, ambazo zinafanana na zangu, zimempa fursa ya kuzunguka sehemu mbali mbali za dunia na kujenga mtandao wa kimataifa wa washiriki.

Leo imekuwa furaha kubwa kuonana tena baada ya miaka mingi, kubadilishana mawazo na kupiga michapo. Nilimchukulia nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambamo nimegusia mambo yaliyotokana na utafiti wangu wa Earthwatch.

Dr. Galyen mwenyewe katika ukurasa wake wa facebook, ameandika kuhusu kukutana kwetu leo:

I enjoyed a wonderful visit with Dr. Joseph Mbele who was the one who originally introduced me to Africa in 1995 on an "Earthwatch" adventure. I give him credit for changing my life completely after I moved to Kenya as a result of our fascinating studies on a remote island in Lake Victoria, TZ. Born in Tanzania, Dr. Mbele is currently a professor at St. Olaf College in MN where he continues to work on special projects around the world! He's inspiring me again to get more involved in heart-felt projects globally.

Monday, December 28, 2015

Kitabu Juu ya Charles Dickens

Siku chache zilizopita, niliingia katika gereji yangu ambayo imefurika vitabu. Katika kufukua fukua, nilikiona kitabu Dickens, kilichotungwa na Peter Ackroyd. Sikumbuki nilikinunua lini na wapi, ila niliamua kukichukua, kwa lengo la kukipitia angalau juu juu. Nina vitabu kadhaa vilivyotungwa na Dickens. Baadhi nimevisoma na baadhi sijavisoma.

Dickens ni kati ya waandishi ambao watu wa rika langu tuliwasoma miaka ya ujana wetu Tanzania, tukawapenda sana. Kutokana na mvuto huu, nimeandika juu ya Dickens mara kadhaa katika blogu hii. Mifano ni hapa, na hapa. Kwa hivyo, nilivyokigundua kitabu cha Dickens katika gereji,  nilifurahi, nikakichukua hima.

Nilikuwa nafahamu jina la mwandishi Peter Ackroyd, ingawa sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu chake chochote. Katika kupitia taarifa kwenye jalada la kitabu chake cha Dickens, nimeona orodha ya vitabu alivyoandika na umaarufu wake. Kwa mfano, amejijengea heshima kubwa kwa kuandika vitabu vya historia na wasifu wa waandishi kama William Shakespeare na William Blake .

Kitabu cha Dickens ni wasifu wa Dickens, maelezo kuhusu maisha yake na maandishi yake, pamoja na maelezo kuhusu jamii alimoishi na kuandika. Ni kitabu kilichosheheni uchambuzi wa maandishi ya Dickens, sambamba na uchambuzi wa uhusiano baina ya maandishi hayo na jamii. Ni matunda ya utafiti wa kina na mpana. Dickens ni hazina kubwa, kitabu chenye kurasa 1195.

Nimekuwa nikikipitia kwa mshangao juu ya juhudi na umakini uliotumika katika utafiti na uandishi wake. Ninafahamu kuwa wenzetu wa nchi kama za Ulaya na Marekani wana jadi ya kufanya utafiti wa kina na kuandika kwa umakini kuhusu waandishi wao maarufu. Kwa mfano, kuna vitabu vya aina hiyo juu ya William Shakespeare, Johann Wolfgang von Goethe, Henrik Ibsen, Leo Tolstoy, Mark Twain, Ernest Hemingway, na William Faulkner.

Tukijifananisha na hao wenzetu, sisi wa-Tanzania tumefanya utafiti gani na tumeandika nini juu ya waandishi wetu maarufu kama Mgeni bin Faqihi na Shaaban Robert? Hakuna chochote ambacho tumefanya kinachoweza kufananishwa na majuzuu makubwa aliyoandika Michael Reynolds juu ya Ernest Hemingway, achilia mbali majuzuu waliyoandika wengine juu ya huyu huyu Charles Dickens. Labda, kwa kutafakari hayo tutagundua na kukiri kuwa tuna njia ndefu mbele yetu.

Saturday, December 26, 2015

Jólabókaflóð: Mafuriko ya Vitabu Nchini Iceland

Nchi ya Iceland inaongoza ulimwenguni kwa usomaji wa vitabu, na pia kwa asilimia ya watu wanaochapisha vitabu. Hilo linatosha kuipambanua nchi ile. Lakini kuna pia jadi iitwayo Jólabókaflóð, yaani mafuriko ya vitabu, ambayo hutokea majira ya Krismasi.

Kila mwaka, kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba, pilika pilika zinazohusiana na vitabu zinapamba moto. Wachapishaji wa vitabu wanaongeza juhudi ya kutangaza vitabu, na jamii nzima huwa katika heka heka ya kununua vitabu. Mazungumzo na malumbano kuhusu vitabu hushamiri kila mahali.

Mwezi Novemba, katalogi kubwa ya vitabu iitwayo bókatíðindi inachapishwa na kugawiwa bure karibu kila nyumba. Katalogi hii huorodhesha vitabu karibu vyote vilivyochapishwa katika mwaka husika. Kadiri Krismasi inavyokaribia, shughuli ya kuzawadiana vitabu inapamba moto. Kilele huwa ni tarehe 24 Desemba, ambayo ni mkesha wa Krismasi. Watu hutumia mkesha wa Krismasi wakisoma vitabu.

Taarifa hizo sikuwa ninazifahamu, hadi leo. Sikujua kuwa utamaduni wa Iceland umefungamana na vitabu kiasi hicho. Nimejikuta ninawazia hali ilivyo nchini mwangu Tanzania. Nimekumbuka makala niliyoandika katika blogu hii nikiwazia ingekuwaje iwapo wa-Tanzania tungeanzisha utamaduni wa kupeana vitabu kama zawadi ya Idd el Fitr au Krismasi.

Je, sisi wa-Tanzania tunaweza kuthubutu kuwapelekea wa-Tanzania wenzetu vitabu kama zawadi ya sikukuu au ya sherehe kama arusi? Tafakari mwenyewe.

Wednesday, December 23, 2015

Ninajivunia Binti Huyu: Bukola Oriola

Nimefurahi kupata taarifa kuwa Rais Obama amemteua Bukola Oriola, kuwa mjumbe katika tume ya kumshauri kuhusu masuala ya usafirishwaji wa ghilba na utumikishwaji wa binadamu, kama ilivyotangazwa katika taarifa hii. Bukola ni binti kutoka Nigeria anayeishi hapa Minnesota, Marekani. Nimemfahamu tangu mwaka 2009, kwa kusoma taarifa zake katika magazeti ya wa-Afrika hapa Minnesota.

Niliguswa kwa namna ya pekee niliposoma kauli yake kuwa alikuwa ameandika mswada wa kitabu bali hakujua auchapishe vipi. Kwa kuwa nilikuwa na uzoefu wa kujichapishia vitabu, dhamiri yangu ilinisukuma niwasiliane naye ili nimsaidie. Nilielezea kisa hicho katika blogu hii.

Baada ya kitabu chake, Imprisoned: The Travails of a Trafficked Victim kuchapishwa, niliendelea kumhamasisha. Kwa mfano, nilimwalika kwenye tamasha la vitabu mjini Minneapolis tarehe 10 Oktoba, 2009, ambalo nilikuwa nashiriki. Nilitaka yeye kama mwandishi chipukizi aone na kujifunza kazi inayomngoja mwandishi baada ya kuchapisha kitabu. Alikuja, tukapiga picha inayoonekana hapa kushoto tukiwa kwenye meza yangu.

Kitabu kilimfungulia milango. Alikuwa anazunguka sehemu mbali mbali kutoa mihadhara kuhusu utumwa na mateso wanayopata wanawake wanaorubuniwa, kutoroshwa, kutekwa, na kisha kutumikishwa na kunyanyaswa. Alianzisha kipindi cha televisheni na pia taasisi aliyoiita The Enitan Story. Yote hayo ni kwa ajili ya kuwasaidia waathirika na kuielimisha jamii kuhusu tatizo hili ambalo limeota mizizi duniani.

Ninafurahi kwa mafanikio ya binti huyu. Naye, kwa kukumbuka nilivyomsaidia, aliandika ifuatavyo katika utangulizi wa kitabu chake:

     I would also like to thank those who worked with me to get this book published. My profound gratitude goes to Prof. Joseph Mbele of St. Olaf College, Northfield, Minnesota, who showed me how to get my book published, otherwise it would have been another Word Document on my computer. It would have not been able to give the message of hope to the hopeless. God bless you sir.

Kitendo cha Rais Obama kumteua Bukola kwenye tume hiyo ni heshima kubwa kwake. Hapa Minnesota na Marekani kwa ujumla watu wamezipokea taarifa hizi kwa furaha. Nchini kwake Nigeria taarifa hii imekuwa kishindo katika vyombo vya habari. Kwa upande wangu, naona fahari kuwa niliitikia wito wa dhamiri yangu nikamwelekeza namna ya kuchapisha kitabu ambacho kilichangia na bado kinachangia mafanikio yake. Mungu ni mkubwa.

Bukola mwenyewe anatambua kuwa kuna mkono wa Mungu katika mambo anayopitia na kuyashuhudia maishani. Anaamini kuwa ana wajibu mbele ya Mungu wa kuwasaidia wanyonge, na kuwa mtetezi wa wanaonyanyaswa na kudhulumiwa. Msikilize anavyojieleza:

Saturday, December 19, 2015

Kuchapisha Vitabu Mtandaoni

Kutokana na taarifa ninazoandika katika blogu hii, na sehemu zingine, watu wengi wanafahamu kuwa nimechapisha vitabu vyangu mtandaoni. Nimeshawasaidia waandishi kadhaa wa mataifa mbali mbali kuchapisha vitabu vyao kwa mtindo huo. Kwa upande wa Tanzania, niliwahi kuongea na wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu suala hilo, na nilinukuliwa katika gazeti la Mwananchi.

Mara kwa mara, watu huniulizia kuhusu kuchapisha vitabu vyao. Napenda kuongelea tena suala hili, hasa matokeo ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Kwanza, ni muhimu kufahamu kwamba kuna njia nyingi za kuchapisha vitabu mtandaoni. Ni juu ya mwandishi kuchagua. Binafsi, ninatumia njia ambayo ni rahisi kabisa, isiyo na gharama, au yenye gharama ndogo kiasi kwamba haiwi kizuizi kwangu.

Kuchapisha kwa namna hii ni rahisi sana. Mbali ya kutokuwa na gharama, haichukui muda, ili mradi mswada umeshaandaliwa kama faili la kielektroniki. Kinachobaki ni kuuingiza mswada kwenye tovuti ya kuchapishia, na haichukui dakika kumi kumaliza shughuli hii na kitabu kikawa tayari kununuliwa na watu popote ulimwenguni.

Jambo moja linalovutia sana katika kuchapisha vitabu mtandaoni kwa namna nifanyavyo ni kwamba vitabu hupatikana bila kikomo. Vinahifadhiwa kama mafaili ya kielektroniki, na huchapishwa kama kitabu halisi pale tu mdau anapoagiza nakala. Akiagiza nakala moja, inachapishwa hiyo hiyo. Akiagiza mia au elfu ni hivyo hivyo. Hakuna udhia wa kutunza shehena ya vitabu ghalani na kungojea wateja, huku vikiwa katika hatari ya kuharibiwa na unyevu, mende, au panya.

Hata hivi, nimeona kuna matatizo. Kwanza kwa upande wa mnunuzi. Ni lazima awe na namna ya kununua mtandaoni. Kwa kawaida hii inamaanisha awe na "credit card" kama vile VISA na Mastercard. Jambo la pili ni bei. Nikiangalia vitabu vyangu, naona wazi kuwa kama vingechapishwa mahali kama Tanzania kwa mtindo wa jadi, vingekuwa na bei nafuu kuliko ilivyo sasa.

Lakini, kwa upande mwingine, kama kitabu kinachapishwa kama kitabu pepe, yaani "e-book," kinaweza kuuzwa kwa bei ndogo sana, kuliko bei ya kuchapisha kwa mtindo wa jadi. Mdau anatakiwa awe na kifaa cha kuhifadhia na kusomea kitabu pepe, yaani "e-reader" au "e-book reader," kama vile Kindle au Nook.

Pamoja na kuwepo kwa vitabu pepe na vifaa vya kuhifadhia na kusomea vitabu hivyo, imethibitika tena na tena kwamba wadau wengi bado wanavitaka vitabu vya jadi, yaani vya karatasi na majalada. Mazoea haya na mapenzi ya vitabu vya jadi yamejengeka na hayaonekani kutoweka mioyoni mwa wengi.

Tekinolojia ya kuchapisha vitabu mtandaoni inawaathiri wachapishaji wa jadi kwa namna mbali mbali. Kadiri siku zinavyopita, wengi wao wanaona faida ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Tekinolojia hii mpya inawasukuma kwenda na wakati ili wasipoteze biashara katika mazingira ya ushindani na mabadiliko yasiyoisha.

Thursday, December 17, 2015

Mdau Kanishukuru kwa Kutafsiri "Kimbunga"

Ninavyoandika katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza huwa sina namna ya kujua ni nani atasoma nilichoandika. Siwezi hata kujua kama niandikacho kitasomwa na yeyote. Ni kubahatisha. Kwa kutambua hilo, nimediriki kusema kwamba ninapoandika katika blogu, ninajiandikia mwenyewe.

Hata hivi, ukweli unajitokeza kuwa kuna watu wanaosoma niandikayo. Katika blogu kuna sehemu ambapo ninafuatilia na kuona takwimu za utembeleaji wa blogu na orodha ya makala zinazosomwa au kupitiwa siku hadi siku.

Nimefurahi kusoma leo ujumbe wa mdau akinishukuru kwa tafsiri yangu ya "Kimbunga," shairi la Haji Gora Haji. Ameandika:

Thank you so much for translating this poem. I'd been searching to read poems originally written in Swahili. Immense gratitude Joseph.

Nimefurahi kuwa nimempa mdau huyu angalau tone la kutuliza kiu yake kuhusu mashairi ya ki-Swahili. Amenipa motisha ya kuendelea kutafsiri tungo za ki-Swahili, ili afaidike zaidi kwa kutambua utajiri wa jadi ya tungo za ki-Swahili ambayo imekuwepo na kustawi kwa karne kadhaa.

Ninamkumbuka pia mtunzi Haji Gora Haji. Nikiweza, kwa idhini yake, kutafsiri mashairi yake na kuyachapisha kama kitabu, kama alivyofanya Clement Ndulute kwa mashairi ya Shaaban Robert, itakuwa ni jambo la manufaa katika kumtangaza na kuuelimisha ulimwengu.

Wednesday, December 16, 2015

Nimeitafsiri Sala ya Papa Francis

Nilielezea katika blogu hii nia yangu ya kuitafsiri sala ya Papa Francis ambayo ni sehemu ya waraka wake wa kitume, "Laudato Si." Papo hapo, ninafahamu vizuri kuwa kutafsiri ni suala tata. Katika ujumbe wangu, niliandika kuwa

"napenda kusema kwamba sala hii ilivyo katika ki-Ingereza ikiwa imesheheni uchaji, busara, na maudhui, imeundwa kwa lugha iliyotukuka. Ninajiuliza iwapo tunaweza kuitafsiri kwa ki-Swahili, tukahifadhi utukufu wake kwa msingi wa uhalisia wa ki-Swahili. Ninajiuliza hivyo pamoja na kufahamu jinsi suala la tafsiri lilivyo gumu na tata. Ninatarajia kujaribu kuitafsiri sala hii siku zijazo."

Hata hivi, nimejaribu kutafsiri sala ya Papa Francis, ili kuwapa angalau fununu wale ambao hawajui ki-Ingereza. Ni bora kufanya hivyo, kuliko kuacha kabisa. Ye yote anayekijua ki-Ingereza vizuri, na pia anakijua ki-Swahili vizuri, ataona kuwa nimejipa mtihani mgumu. Ninamhimiza naye ajaribu kutafsiri.

A prayer for our earth

All-powerful God, you are present in the whole universe
and in the smallest of your creatures.
You embrace with your tenderness all that exists.
Pour out upon us the power of your love,
that we may protect life and beauty.
Fill us with peace, that we may live
as brothers and sisters, harming no one.
O God of the poor,
help us to rescue the abandoned and forgotten of this earth,
so precious in your eyes.
Bring healing to our lives,
that we may protect the world and not prey on it,
that we may sow beauty, not pollution and destruction.
Touch the hearts
of those who look only for gain
at the expense of the poor and the earth.
Teach us to discover the worth of each thing,
to be filled with awe and contemplation,
to recognize that we are profoundly united
with every creature
as we journey towards your infinite light.
We thank you for being with us each day.
Encourage us, we pray, in our struggle
for justice, love and peace.

Sala Kuiombea Dunia Yetu

Mungu mweza yote, upo kila mahali

na hata katika viumbe vyako vidogo kabisa.
Unakumbatia kwa upole wako kila kilichopo.
Tufurikie nguvu ya upendo wako
ili tuuhifadhi uhai na uzuri.
Tujaze amani, ili tuishi
kama kaka na dada, bila kumdhuru yeyote.
Ee Mungu wa maskini,
tusaidie kuwanusuru waliotelekezwa na kusahauliwa katika dunia hii,

ambao wana thamani isiyo kifani machoni mwako.
Tuletee uponyaji maishani mwetu,
ili tuihifadhi dunia badala ya kuwania kuipora,
ili tustawishe uzuri, si uchafuzi na uharibifu.
Gusa mioyo
ya wale wanaowania maslahi yao tu
yanayowagharimu maskini na dunia.
Tufundishe kuibaini thamani ya kila kitu,
kujawa na uchaji na tafakari,
kutambua
 kuwa tumefungamana
na kila kiumbe
tunavyoelekea kwenye nuru yako isiyo na mwisho.
Tunakushukuru kwa kuwa nasi kila siku.

Tuhimize, tunakuomba, katika juhudi zetu
za kutafuta haki, upendo na amani.

Wednesday, December 9, 2015

Mtunzi Haji Gora Haji

Leo nimeamua kuongelea kifupi utunzi wa Haji Gora Haji wa Zanzibar, mmoja wa waandishi maarufu wa ki-Swahili wa zama zetu hizi. Nafurahi kuwa niliwahi kuonana naye mjini Zanzibar na kuzungumza naye. Panapo majaliwa, nitaandika taarifa ya mazungumzo yetu, ambayo yalihusu maisha yake katika sanaa. Ni muhimu kuutangazia ulimwengu kazi murua inayofanywa na watu wetu wenye vipaji kama Haji Gora Haji.

Nina vitabu vyake vinne: Kimbunga (Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press, 1994), Utenzi wa Visa vya Nabii Suleiman Bi Daudi (A.S.) (Zanzibar: Al-Khayria Press Ltd, 1999), Kamusi ya Kitumbatu (Zanzibar: Express Printing Services, 2006), na Siri ya Ging'ingi (Dar es Salaam: Taasisi ya Taaluma za Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam, 2009).

Kadiri siku zinavyopita, wasomaji na wahakiki wanajitokeza na kuongelea uandishi wa Haji Gora Haji. Mifano ya kutambuliwa huko ni taarifa ya Amanda Leigh Lichtenstein, ya Ridder Samson, na ya Pascal Bacuez. Nami nimetafsiri mashairi yake mawili nikayachapisha hapa, hapa, na hapa.

Haji Gora Haji, kama walivyo watunzi wengi, wa zamani hadi leo, wamejengeka katika jadi ya fasihi simulizi. Wanaitumia jadi hii katika utunzi wao, iwe ni mashairi kama walivyofanya W.B. Yeats na Derek Walcott, au riwaya, kama walivyofanya Charles Dickens na Chinua Achebe, au tamthilia, kama walivyofanya William Shakespeare, Wole Soyinka na Ebrahim Hussein, au hadithi fupi, kama walivyofanya Lu Hsun na Ama Ata Aidoo.

Ni hivyo hivyo kwa Haji Gora Haji, kama nilivyowahi kutamka. Utumiaji wa mbinu, miundo, na hata dhamira zitokanazo na fasihi simulizi kunachangia uwezo wa tungo kugusa fikra na hisia za hadhira kwa namna ya pekee kutokana na kwamba fasihi simulizi ni urithi wa wanadamu wote. Maudhui yatokanayo na fasihi simulizi ni ya thamani kwa wanadamu wote.

Kuthibitisha zaidi namna Haji Gora Haji alivyojengeka katika fasihi simulizi, sikiliza anavyosimulia hadithi ya Paa na Pweza.


Monday, December 7, 2015

Nimesaini Vitabu Kwa Ajili ya Filamu ya "Papa's Shadow"

Wakati wa kampeni ya Ramble Pictures ya kuchangisha fedha kulipia gharama za filamu ya Papa's Shadow, nilichangia fedha kiasi na pia nakala za kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Walikuwa wameweka viwango mbali mbali vya michango ambavyo viliendana na vizawadi na vivutio kwa wachangiaji. Waliochangia dola 200 au zaidi waliahidiwa nakala ya kitabu changu kama zawadi.

Leo, Jimmy Gildea, mwanzilishi wa Ramble Pictures na mtengenezaji wa Papa's Shadow, ambaye alikuwa mwanafunzi katika kozi yangu ya Hemingway, alinifuata hapa chuoni St. Olaf, nikasaini nakala tano za kitabu changu, na kumkabidhi.

Tulipata fursa ya kuongelea habari za Ernest Hemingway, ziara yetu ya Montana, msisimko na mafanikio ya kampeni ya kuchangisha fedha, na kadhalika. Vile vile, Jimmy alinirekodi nikiwa nasoma kitabu cha Green Hills of Africa na pia nikiwa natembea katika sehemu iliyoonyesha vizuri mandhari ya chuo. Jimmy aliniuliza iwapo nina picha za ujana na utoto wangu. Anakusanya hayo ili kuyatafutia nafasi katika filamu ya Papa's Shadow, ingawa tayari ni nzuri sana, kwa jinsi nilivyoiona.

Papa's Shadow inategemewa kupatikana wiki chache kuanzia sasa, labda mwezi Februari. Si filamu ya kuigiza bali ni mazungumzo juu ya maisha, uandishi, na falsafa, ya Ernest Hemingway, hasa inavyohusiana na safari zake Afrika Mashariki, miaka ya 1933-34 na 1953-54. Sehemu kubwa ya filamu hii ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliye bado hai. Ni filamu inayoelimisha, si burudani.

Saturday, December 5, 2015

Kuwalea Watoto Kupenda Vitabu

Kati ya mambo yanayonivutia sana hapa Marekani ni namna wazazi wanavyowalea watoto katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu. Katika matamasha ya vitabu, maduka ya vitabu, na maktaba, ninawaona wazazi wakiwa na watoto. Nimewahi kuandika kuhusu suala hilo katika blogu hii. Lakini kwa kuwa hii ni mada ninayoitilia maanani sana, nimeamua kuiongelea tena.

Picha ya juu hapa kushoto ilipigwa mwaka 2008, niliposhiriki sherehe za kumbukumbu ya uhuru wa Nigeria hapa Minnesota. Nilikuwa na meza ya vitabu vyangu. Nakumbuka vizuri jinsi huyu mama m-Nigeria anayeonekana pichani alivyokuja mezani pangu na binti yake. Tulisalimiana, wakaangalia na kuvifurahia vitabu vyangu, kama inavyoonekana pichani.

Picha ya pili hapa kushoto nilipiga katika tamasha la vitabu la Deep Valley, mjini Mankato, Minnesota. Nilivutiwa na namna hao watoto walivyokuwa wanafuatana na mama yao kutoka meza hadi meza wakiangalia vitabu.

Picha ya tatu hapa kushoto nilipiga mwezi Agosti mwaka huu mjini Brooklyn Park, Minnesota, katika tamasha la Afrifest. Huyu bwana, m-Marekani Mweusi, alikuja na watoto wake kwenye meza yangu, kuangalia vitabu. Watoto hao ni wadogo sana, na sijui kama walikuwa wanajua kusoma, lakini, nilivutiwa na kitendo cha baba yao kuwaleta kuangalia vitabu.

Kwa wa-Marekani, umri wa mtoto si tatizo. Wanawasomea vitabu hata watoto wadogo sana, hasa kabla ya kulala. Watoto wanapenda kusomewa vitabu. Hapa naikumbuka video ya kusisimua inayomwonyesha mtoto mdogo akisomewa vitabu, halafu anavyoangua kilio kila anapoambiwa kuwa hadithi imeisha. Hebu iangalie.


Thursday, December 3, 2015

Kuhusu Kublogu

Nimekuwa mwanablogu tangu mwaka 2008. Ninaendesha blogu hii ya Hapa Kwetu na nyingine ya ki-Ingereza. Kublogu kuna mambo mengi. Kublogu kunanipa fursa ya kujieleza kwa uhuru. Hili ni jambo la msingi, kama alivyoelezea mwanablogu Christian Bwaya.

Lakini kublogu kuna matokeo yenye manufaa. Kumeniwezesha kuwafikia watu mbali mbali ambao wanatembelea blogu zangu. Siwezi kujua wanapata ujumbe gani katika maandishi yangu. Kama taaluma inayotufundisha, hili ni suala tata.

Ujumbe wa andiko ni zao la kazi anayofanya msomaji juu ya andiko. Na kwa kuwa wasomaji wana akili zinazotofautiana, na wana nidhamu na uzoefu tofauti wa kusoma, kila mmoja anaibuka na ujumbe tofauti, kwa kiwango kidogo au kikubwa.

Niliwahi kuelezea kwa nini ninablogu, lakini sidhani kama nilikuwa na majibu ya uhakika. Baadaye, katika kutafakari suala hili, nilifikia hatua ya kutamka kwamba ninablogu kwa ajili yangu mwenyewe. Labda huu ndio ukweli wa mambo.

Imani iliyojengeka katika jamii ni kuwa mwandishi anawaandikia wasomaji. Tumezoea kuona waandishi wakiulizwa wanamwandikia nani, nao wanaelezea walengwa wao. Jadi hii na imani hii imekosolewa kwa uhodari na Roland Barthes katika makala yake, "The Death of the Author."

Makala hii ya Barthes naona inaipa uzito hoja yangu kuwa ninapoblogu ninajiandikia mwenyewe. Sijui ni nani atasoma au anasoma ninachoandika. Kusema kwamba ninawaandikia wasomaji ni kama kuota ndoto. Ni kujiridhisha kwa jambo ambalo halina uhakika bali ni bahati nasibu. Nikisema ninajiandikia mwenyewe ninasema jambo la uhakika.

Tuesday, December 1, 2015

Nilitembelea Duka la Vitabu la Amkal

Tarehe 23 Mei, 2015, nilitembelea duka la vitabu la Amkal mjini Minneapolis, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Ni duka la wa-Somali ambalo linauza zaidi vitabu vinavyohusu dini ya ki-Islam. Siku hiyo nilinunua kitabu kiitwacho Jesus: Prophet of Islam. Ninapenda kuongelea, kwa kifupi na wepesi kabisa, mawazo yanayonijia ninapokumbuka ziara yangu katika duka lile.

Jambo la msingi kwamba katika kuishi kwangu hapa Marekani, nimeona jinsi wa-Afrika wa nchi mbali mbali wanavyovithamini vitabu. Kwa mfano, nimewahi kuwaongelea wa-Kenya.

Wa-Somali ni mfano mwingine. Nimekutana na wa-Somali wanaoishi hapa Minnesota ambao wanaandika vitabu. Nimejionea wanavyojitokeza kuwasikiliza waandishi wa vitabu wa ki-Somali. Mfano ni Nuruddin Farah, ambaye huonekana hapa Minnesota mara kwa mara, ingawa makao yake kwa miaka hii ni Afrika Kusini. Wanamheshimu kwa jinsi anavyowakilisha taifa lao katika ulimwengu wa uandishi.

Kwa ujumla, hao wa-Somali ni wakimbizi au wahamiaji. Lakini pamoja na kadhia hiyo, pamoja machungu waliyoyapitia, wameshikilia umuhimu wa vitabu na elimu. Katika vyuo vya hapa Minnesota, kama vile Chuo Kikuu cha Minnesota, Metropolitan State University. Mankato State University, South Central College, na Minneapolis Community and Technical College, wanafunzi wa ki-Somali ni wengi. Wanawekeza katika elimu. Wanajijengea mtaji ambao wataweza kuutumia kwa maendeleo ya nchi yao.

Suala la elimu wanalishughulika kwa namna nyingine pia, kama vile magazeti na vituo vya televisheni. Hali hii nimeiona pia miongoni mwa wa-Afrika wengine, kama vile wa-Kenya na wa-Ethiopia. Kwa kutumia njia hizo, wanazitangaza nchi zao na shughuli zao, kama vile biashara. Ninawaona ni mfano wa kuigwa.

Thursday, November 26, 2015

Utendi wa Mikidadi na Mayasa

Wiki hii, bila kutegemea, nimevutiwa na wazo la kusoma Utendi wa Mikidadi na Mayasa. Ninazo tendi kadhaa, kuanzia za zamani kama vile Mwana Kupona, Fumo Liongo, na Ras il Ghuli, hadi za enzi zetu hizi. Ninapenda kuzisoma na kuzitafakari, sambamba na tungo za aina hiyo za mataifa mengine, kama vile Gilgamesh, Iliad na Odyssey, Sundiata, na Kalevala.

Nimeusikia Utendi wa Mikidadi na Mayasa tangu zamani. Sijui lini nilinunua nakala yangu ya utendi huu, lakini sikupata wasaa wa kuusoma. Kwa kuupitia haraka haraka, nimeona kuwa una mambo yanayofanana na yale yaliyomo katika tendi zingine maarufu za ki-Swahili kama Ras il Ghuli. Kwa mfano, dhamira ya mapigano kama njia ya kuthibitisha ushujaa imejengeka katika Utendi wa Mikidadi na Mayasa, kama ilivyo katika Utendi wa Ras il Ghuli.

Mayasa ni shujaa mwanamke anayenikumbusha shujaa mwanamke aitwaye Dalgha katika Utendi wa Ras il Ghuli. Wote wawili ni wapiganaji hodari na hatari sana, ambao yeyote anayetaka kuwaoa sherti kwanza apigane nao na kuwashinda. Hata ungekuwa mwanamme hodari na jasiri kiasi gani, kupambana nao ni kama kujitakia aibu au kifo.

Baada ya kuonja mvuto wa  Utendi wa Mikidadi na Mayasa, ninajizatiti kuusoma kikamilifu. Nikiweka nidhamu nikamaliza kuusoma, nitafurahi kuandika juu yake katika blogu hii, angalau kifupi, kama nilivyoandika juu ya Tenzi Tatu za Kale.

Tuesday, November 24, 2015

Kitabu Changu Bado Kiko Maoneshoni

Nimepita tena katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf, kama ilivyo kawaida yangu, kuangalia vitabu vipya, na pia kuangalia vitabu ambavyo maprofesa wa masomo mbali mbali wanapangia kufundisha.

Katika kuzunguka humo dukani, nilipita tena sehemu ambapo vinawekwa vitabu vilivyoandikwa na maprofesa wa chuo hiki. Kabla sijafika kwenye sehemu hiyo, macho yangu yalivutiwa na kitabu change cha Matengo Folktales, ambacho kilikuwa bado kiko sehemu maalum vinakowekwa vitabu ambavyo uongozi wa duka huamua kuvipa fursa ya kuonekana vizuri zaidi kwa kipindi fulani, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii.

Kuna mambo yanayonigusa kila niingiapo katika duka hili la vitabu na maduka mengine ya vitabu popote hapa Marekani. Kubwa zaidi ni jinsi wahudumu wanavyokuwa ni watu makini katika masuala ya vitabu. Wanajua habari za vitabu, na wanaweza kukuelimisha kwa namna mbali mbali. Hawako katika kazi hii kwa kubahatisha au kwa kubabaisha. Wanajua wanachokifanya. Unaweza kuingia katika duka la vitabu hapa Marekani bila mpango wa kununua kitabu, lakini ukianza kuongea na wahudumu, unaweza kujikuta umeelimishwa kuhusu vitabu fulani ukaishia kununua.

Katika haya maduka ya vyuo, nimeona wana huu utaratibu wa kuwa na sehemu ya kuweka vitabu vilivyoandikwa na maprofesa wa vyuo hivyo, na pengine pia vitabu vya watu waliohitimu zamani, ambao huitwa "alumni" (wanaume) au "alumnae" (wanawake). Ni namna mojawapo ambayo taasisi hizo huwatambua na kuwaenzi waalimu na wahitimu. Nami najisikia vizuri kama profesa wa chuo hiki cha St. Olaf kuwa kazi zangu zinatambuliwa, vikiwemo vitabu.

Kwa upande wa biashara, naona kuwa haya maduka ya vitabu ya vyuo vya Marekani yanaonyesha ubunifu wa kibiashara kwa kuweka vitabu vyetu namna hiyo. Mbali  ya wanafunzi, tuna wageni wengi wanaopita hapa chuoni kila siku, wakiwemo wazazi wa wanafunzi, wahitimu wa zamani, na wale wanaokuja kuangalia ubora wa chuo ili wawalete vijana wao kusoma hapa. Duka la vitabu ni sehemu moja muhimu wanamoingia. Humo wanakuwa na fursa ya kununua vitabu vyetu hasa inapokuwa kwamba wamesikia habari zetu. Kwa mfano, duka la St. Olaf limeshauza nakala mia kadhaa za vitabu vyangu.

Hayo ni baadhi ya mambo niliyojifunza katika suala hili ambayo nimeona niyaweke katika blogu yangu, kwa lugha rahisi kabisa. Labda yanaweza kuwa na manufaa kwa vyuo nchini mwangu.

Monday, November 23, 2015

Kutafsiri Fasihi

Dhana ya tafsiri si rahisi kama inavyoaminika na jamii. Wataalam wanaijadili, kwa misimamo tofauti. Kuna vitabu na makala nyingi juu ya nadharia za tafsiri na shughuli ya kutafsiri. Kati ya vitabu vyangu, kuna ninachopenda kukipitia, kiitwacho Theories of Translation, ambacho ni mkusanyo wa insha za watu kama Johann Wolfgang von Goethe, Friedrich Nietzsche, Walter Benjamin, Roman Jakobson, Michael Riffaterre na Jacques Derrida.

Insha hizi zinafikirisha. Jose Ortega y Gasset, kwa mfano, anasema kuwa kutafsiri ni jambo lisilowezekana. Ni kama ndoto. Ni kujidanganya. Walter Benjamin anauliza masuali mengi magumu. Derrida, katika insha yake juu ya Mnara wa Babel, iliyotafsiriwa na Joseph F. Graham, anaandika:

          The "tower of Babel" does not merely figure the irreducible multiplicity of tongues; it exhibits an incompletion, the impossibility of finishing, of totalizing, of saturating, of completing something on the order of edification, architectural construction, system and architectonics. What the multiplicity of idioms limits is not only a "true" translation, a transparent and adequate inter-expression, it is also a structural order, a coherence of construct. There is often (let us translate) something like an internal limit to formalization, an incompleteness of constructure. It would be easy and up to a certain point justified to see there the translation of a system in deconstruction.
          One should never pass over in silence the question of the tongue in which the question of the tongue is raised and into which a discourse on translation is translated.

Kutokana na uzoefu wangu wa kutafsiri hadithi za jadi za ki-Matengo, nami nimeanza kuelezea suala la kutafsiri hadithi. Ninatafsiri pia mashairi ya ki-Ingereza kwa ki-Swahili na mashairi ya ki-Swahili kwa ki-Ingereza. Ninawazia kujijengea msingi wa kuandika zaidi kuhusu kazi ya kutafsiri, na ndoto yangu hatimaye ni kutafsiri Utenzi wa Ras il Ghuli. Ninaamini kwamba kuutafsiri utenzi huu utakuwa ni mtihani mkubwa kuliko yote ambayo nimejaribu kufanya, na kitakuwa ni kipimo thabiti cha uwezo wangu. Ninahamasika na namna mabingwa kama Richmond Lattimore na Robert Fagles walivyotafsiri tenzi za The Iliad na The Odyssey.

Sunday, November 15, 2015

Jana Nilikwenda Kusimulia Hadithi

Jana jioni nilikwenda Maple Grove, Minnesota, kwenye sherehe ya watu wa Liberia ya kumbukumbu ya kuzaliwa mtoto. Nilikuwa nimealikwa kusimulia hadithi, kama nilivyoandika katika blogu hii.

Nilifika saa moja jioni, kama nilivyotegemewa, nikakuta sherehe zimeshamiri. Watoto walikuwa katika michezo, na watu wazima walikuwa katika mazungumzo.  Baada ya kukaribishwa kuongea, nilijitambulisha kifupi, nikashukuru kwa mwaliko. Nilifurahi kumwona binti mdogo ambaye alikuwa amehudhuria niliposimulia hadithi katika tamsha la Afrifest. Yeye na mama yake, ambaye alikuwa mwenyeji wangu hiyo jana, ndio watu pekee nilowafahamu.

Nilijiandaa kusimulia hadithi kutoka Afrika Magharibi. Nilisimulia hadithi moja kuhusu urafiki baina ya Chura na Buibui ("Frog and Spider") na ya pili juu ya mhusika aitwaye Pesa ("Money").

Baada ya kusimulia hadithi ya Chura na Buibui, nilitumia muda kuwauliza watoto mawazo yao kuhusu hadithi hiyo. Hawakusita kujieleza. Sikushangaa, kwani katika uzoefu wangu wa kuwasimulia watoto hadithi hapa Marekani, nimeona kuwa wanapenda kuelezea maoni yao kuhusu tabia za wahusika, maudhui, na kadhalika.

Vile vile, kabla ya kusimulia hadithi ya pili, nilisema kuwa iwapo watoto wanapenda kuendelea na michezo yao wafanye hivyo, na wale ambao wanapenda kusikiliza hadithi nyingine, wabaki. Nilisema hivyo kwa kuona kuwa watoto wengine walikuwa wadogo mno, ambao hupenda kubadili shughuli mara kwa mara. Sio rahisi kuwakalisha wakakusikiliza kwa zaidi ya dakika 20.

Nilisimulia hadithi ya pili, ambayo ni ndefu zaidi kidogo kuliko ile ya kwanza. Ilifaa kabisa kwa watoto wenye umri mkubwa zaidi na kwa watu wazima.

Baada ya hapo, nilisema kuwa ninashughulika na kurekodi na kutafsiri hadithi za jadi, nikawaonyesha kitabu cha Matengo Folktales. Mtu mmoja aliuliza iwapo kinauzwa, nami nikamkubalia. Kwa bahati nzuri nilikuwa na nakala za ziada, na watu walizinunua. Sina shaka kwamba watazifurahia hadithi hizo pamoja na uchambuzi wangu.

Safari ya jana nitaikumbuka miaka ijayo. Unaweza kusoma taarifa nyingine niliyoandika katika blogu ya ki-Ingereza.

Thursday, November 12, 2015

Waumini Waikumbuka Hotuba Niliyotoa Lands Lutheran Church

Niliwahi kuandika katika blogu hii kuhusu hotuba niliyotoa tarehe 11 Aprili, 2015, katika mkutano wa waumini wa Sinodi ya Minnesota ya Kusini Mashariki ya Kanisa la ki-Luteri la Marekani. Nimeona ripoti fupi ya hotuba katika jarida la kanisa la First Lutheran la mjini Red Wing, Minnesota, The Spire (July/August 2015) uk. 4. Ninaiweka hapa kwa kumbukumbu yangu.

-------------------------------------------------------------------------------------

CANNON RIVER CONFERENCE REPORT

In April some representatives from First Lutheran, United Lutheran, and St. Paul’s Lutheran attended the women’s Cannon River Conference in Zumbrota. There was a very thorough explanation of the history of the beginnings of the Lutheran church in this area of the country, so there was less time for the main speaker, Joseph Mbele, a St. Olaf professor.

Besides teaching, Professor Mbele works with groups in the area to mediate cultural conflicts. He asked us to look at the positive and the potential in all people; do not rush to judgment. What is natural in one culture may not be correct in another, and what is an issue in one culture might not be an issue in another. 

For example, in Faribault the storekeepers were upset because the Somali men stood in front of the stores or nearby and talked. The storekeepers felt this was loitering and bad for business. In Africa this was the custom to talk together outside stores and it was considered impolite to make a quick purchase and leave. Americans are very concerned about being on time. In Africa it is considered rude to rush by people and not talk to them, and in small villages many are related. On the way to a meeting an African might stop and talk to a number of people, and probably will arrive late to a meeting.

Other examples: In Brooklyn Park other residents were complaining about loud music. In Africa everyone in the small town is invited to a wedding and no invitations are sent out. Child raising views are quite different too; Africans take the phrase, “It takes a village” quite literally. Everyone is supposed to help watch the kids while Americans believe they should only watch their own children and don’t want any help from other people. 

Professor Mbele wrote a book about some of these differences, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, which we purchased for the church library.

The next meeting of the Cannon River Conference will be held in April 2016 at St. Paul’s Lutheran Church in Red Wing with United and First assisting.

Respectfully submitted,
Nancy Thorson, FLCW President

Wednesday, November 11, 2015

Shairi la "The Layers" la Stanley Kunitz na Tafsiri Yangu

Tarehe 9 Machi, 2005, nilipata ujumbe kutoka kwa Dr. Arthur Dobrin, mwandishi na profesa katika Chuo Kikuu cha Hofstra, New York, akiniulizia iwapo ningekubali kulitafsiri kwa ki-Swahili shairi la Stanley Kunitz liitwalo "The Layers." Aliniambia kuwa inaandaliwa sherehe ya kumbukumbu ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Stanley Kunitz na kwamba tafsiri za shairi hili katika lugha mbali mbali zitawasilishwa kama sehemu ya kumbukumbu. Aliambatanisha shairi hilo katika ujumbe wake.

Sikuwa ninalifahamu shairi hilo. Jina la Stanley Kunitz huenda nilikuwa nalifahamu kwa mbali, lakini sidhani kama nilikuwa nimesoma mashairi yake. Katika mazingira hayo yaliyokuwa mithili ya giza akilini mwangu, nililisoma shairi la "The Layers" nikakubali kulitafsiri, ingawa niliona ingekuwa kazi ngumu.

Kazi ya kutafsiri haikuwa rahisi, kutokana na jinsi fikra na taswira zilivyosukwa katika shairi hili. Ingawaje kwa ujumla ni shairi linaloelezea mawazo ya mzee anayeangalia maisha aliyopitia pamoja na magumu yake na mabadiliko yake, nilivutiwa na msisitizo wake kuwa kuna kiini cha uwepo wake ambacho amekuwa akipambana kukihifadhi salama katika hali zote alizopitia, ambazo zimejengeka na kulaliana nafsini mwake kama matabaka. Hata hivi kuna dhana tata kadhaa katika shairi hili ambazo huenda hata mtunzi mwenyewe zilimwia vigumu kuzielezea.

Tangu nitafsiri shairi la "The Layers," mara moja moja nimekuwa nikilikumbuka. Stanley Kunitz mwenyewe alifariki mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 101. Ni mmoja wa washairi maarufu kabisa wa -Marekani. Jana jioni niliingia mtandaoni nikaona video yake akisoma "The Layers." Niliguswa na usomaji wake, nikaamua kuitafuta tafsiri niliyofanya mwaka 2005, pamoja na video, kama nilivyoweka hapa. Kama unakifahamu ki-Ingereza na ki-Swahili vizuri sana, utakubaliana nami kuwa kuthubutu kutafsiri kazi ya fasihi ni kama kujipalia mkaa au kucheza na moto.





 THE LAYERS

I have walked through many lives,
some of them my own,
and I am not who I was,
though some principle of being
abides, from which I struggle
not to stray.
When I look behind,
as I am compelled to look
before I can gather strength
to proceed on my journey,
I see the milestones dwindling
toward the horizon
and the slow fires trailing
from the abandoned camp-sites,
over which scavenger angels
wheel on heavy wings.
Oh, I have made myself a tribe
out of my true affections,
and my tribe is scattered!
How shall the heart be reconciled
to its feast of losses?
In a rising wind
the manic dust of my friends,
those who fell along the way,
bitterly stings my face.
Yet I turn, I turn,
exulting somewhat,
with my will intact to go
wherever I need to go,
and every stone on the road
precious to me.
In my darkest night,
when the moon was covered
and I roamed through wreckage,
a nimbus-clouded voice
directed me:
"Live in the layers,
not on the litter."
Though I lack the art
to deciper it,
no doubt the next chapter
in my book of transformations
is already written.
I am not done with my changes.


MATABAKA

Nimepitia maisha mengi,
baadhi yakiwa yangu,
na mimi si yule nilokuwa,
japo msingi fulani wa kuwa
ungali, ambao nakazana
kutouacha.
Niangaliapo nyuma,
kama niwajibikavyo kuangalia
kabla sijakusanya nguvu
za kuendelea na safari yangu,
naona nguzo za maili barabarani zikizidi kufupika
kuelekea mbali upeoni mwa macho
na mioto ikiwaka kidhaifu
katika makambi mahame,
ambayo juu yake malaika wasaka nyama
wanaruka kwa mabawa mazito.
Oh, nimejigeuza kabila
kutokana na mapenzi yangu ya dhati,
na kabila langu limetawanyika!
Moyo utaridhikaje
na shehena yake ya maafa?
Katika upepo uvumao
vumbi ovu ambalo ni marafiki zangu,
wale ambao waliachika njiani,
linaumiza uso wangu.
Hata hivyo, napinduka, napinduka,
nikifurahi kiasi,
na nia yangu thabiti ya kuelekea
kokote kunakolazimu,
na kila jiwe barabarani
ni la thamani kwangu.
Katika usiku wangu wa giza sana,
mwezi ukiwa umefunikwa
nami nikirandaranda katika yaliyoharibiwa,
sauti ya nyepesi kama wingu
iliniongoza:
"Uishi baina ya rusu
si juu ya takataka."
Japo sina ufundi
wa kuitafsiri,
hakuna shaka sura ifuatayo
katika kitabu changu cha mabadiliko
tayari imeshaandikwa.
Sijahitimisha mabadiliko yangu.

 translation by Joseph L. Mbele

Sunday, November 8, 2015

Nimealikwa Kusimulia Hadithi

Leo nimepata ujumbe kutoka kwa mama mmoja m-Liberia aishiye hapa Minnesota. Amejitambulisha kwamba tulikutana katika tamasha la Afrifest, akauliza iwapo nitaweza kwenda kusimulia hadithi mjini Maple Grove tarehe 14 mwezi huu, katika sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa mtoto.

Nilielezea katika blogu yangu ya ki-Ingereza nilivyosimulia hadithi katika tamasha la Afrifest, hapa na hapa. Nilisimulia hadithi mbili kutoka katika kitabu cha Matengo Folktales. Mama aliyeniletea mwaliko wa tarehe 14 amenikumbusha kwamba mtoto wake na wengine walioshuhudia hadithi zangu katika Afrifest walivutiwa na wanataka nikasimulie tena.

Hii itakuwa mara yangu ya kwanza kusimulia hadithi katika mkusanyiko wa wanafamilia na marafiki zao, katika sherehe ya kifamilia. Nimezoea kusimulia katika vyuo. Nitatumia sehemu ya muda nitakaokuwa nao kuelezea dhima ya hadithi katika jadi za wa-Afrika na wanadamu kwa ujumla, halafu nitasimulia hadithi, na kisha nitawahimiza wasikilizaji kusaidia kuichambua hadithi nitakayosimulia. Ninawazia kusimulia hadithi kutoka Afrika Magharibi, labda Liberia, Senegal, au Burkina Faso, zilizomo katika kitabu cha West African Folktales.

Hadithi za jadi ni hazina yenye mambo mengi, kama vile falsafa, mafundisho kuhusu saikolojia na tabia za wanadamu, kuhusu mema na mabaya. Ziko zinazosikitisha, zinazofurahisha na kuburudisha, na zinazochemsha bongo, kama zile ziitwazo kwa ki-Ingereza "dilemma tales." Zote ni muhimu katika maisha ya wanadamu, kama nilivyojaribu kuelezea katika kitabu cha Matengo Folktales.

Friday, November 6, 2015

Tafsiri ya "Nyang'au," Shairi la Haji Gora Haji

Kwa siku kadhaa sasa, nimekuwa nikisoma Kimbunga, kitabu cha mashairi ya Haji Gora Haji wa Zanzibar. Sambamba na kusoma, nimevutiwa na wazo la kujaribu kuyatafsiri baadhi. Nimeshatafsiri shairi la "Kimbunga." Leo nimeona nitafsiri "Nyang'au." Ni shairi linalohusiana na fasihi simulizi, kama yalivyo mashairi na maandishi mengine kadhaa ya Haji Gora Haji. Kwa kuwawezesha wasomaji wa ki-Ingereza kuonja utunzi wa Haji Gora Haji, ninategemea kuchangia kumtangaza ulimwenguni mshairi huyu mahiri. Anastahili kuenziwa kwa kila namna.

Yeyote anayekijua ki-Swahili vizuri, na pia ki-Ingereza, atajionea ugumu wa mtihani niliojipa wa kutafsiri shairi hili. Ingawa nimejitahidi sana, siwezi kusema ninaridhika na tafsiri yangu. Jaribu nawe kulitafsiri shairi hili, upate maumivu ya kichwa, na pia raha ukifanikiwa.

                              
                               Nyang'au

1.        Fisi alikichakani, mtu kapita haraka
          Kwa vile yuko mbiyoni, mkono unakwepuka
          Ndipo akatumaini, karibu ya kuanguka
          Mate yakimdondoka, kwa tamaa ya mkono

2.       Kayanowa yake meno, tayari na kujiweka
          Ukidondoka mkono, afike na kuudaka
          Ajipatie vinono, ale na kufaidika
          Mate yakimdondoka, kwa tamaa ya mkono

3.       Kafata huku na kule, hakuwa mwenye kuchoka
          Fisi nyuma mtu mbele, endako ajipeleka
          Kungoja mkono ule, apate kunufaika
          Mate yakimdondoka, kwa tamaa ya mkono

4.       Hakujuwa kama vile, mkono kupeperuka
          Ndiyo yake maumbile, si kwa kuwa wakwanyuka
          Kafatia vile vile, kwa tamaa kumshika
          Mate yakimdondoka, kwa tamaa ya mkono

5.        Yule anayemfata, anakokwenda kafika
          Ndoto aliyoiota, ikakosa uhakika
          Mkono hakuupata, bure alihangaika
          Majuto yakamfika, hakuupata mkono


                                The Hyena

1.        The hyena was in the bush, when a man hurried past
          Speeding as he was, his arm flagged about
          Raising the hyena's hopes that soon it would fall off
          He kept salivating, hungering for the arm

2.        He sharpened his teeth, positioning himself properly
          So that when the arm fell off, he should promptly catch it
          And enjoy a tasty treat, eating to satisfaction
          He kept salivating, hungering for the arm

3.        He followed hither and thither, not one to tire of striving
          Coming behind with the man ahead, the hyena trailed the man
          Waiting for that arm, hoping to feast on it
          He kept salivating, hungering for the arm

4.        Little did he know, that for the arm to flap about
          Was its natural wont, no harbinger of dismemberment
          He nevertheless kept following, choking with desire
          He kept salivating, hungering for the arm

5.        The one he was following, reached his destination
          The dream he had been dreaming, ended in uncertainty
          The arm he failed to get, in vain had he striven
          Deep regrets assailed him, for failing to get the arm.

Tuesday, November 3, 2015

"Equal Rights:" Wimbo wa Peter Tosh

Mimi ni shabiki mkubwa wa miziki ya aina mbali mbali, ikiwemo "reggae." Kati ya wana "reggae ninaowapenda sana ni Peter Tosh wa Jamaica, ambaye ni marehemu sasa. Wimbo wake mojawapo niupendao sana ni "Equal Rights." Nilianza kuusikia wimbo huu miaka zaidi ya 30 iliyopita. Ujumbe wake ni chemsha bongo ya aina fulani. Anasema "I don't want no peace; I need equal rights and justice," yaani "Sitaki amani; nahitaji usawa kwa wote na haki."




Monday, November 2, 2015

Hifadhi ya Majengo ya Kihistoria

Miezi kadhaa iliyopita, niliposikia kuwa jengo la CCM mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, limebomolewa ili kujengwa jengo la kisasa, nilifadhaika. Niliwazia utamaduni ninaouona hapa Marekani wa kuhifadhi majengo ya kihistoria. Nimeona katika miji wanahifadhi maeneo wanayoyaita "historic districts." Mfano ni picha zinazoonekana hapa, ambazo nilipiga mjini Faribault. Ninaona maeneo haya katika miji mingine pia.

Maeneo ya kihistoria, yenye majengo ya zamani, ni kumbukumbu ya historia ambayo inastahili kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo. Vile vile, ni kivutio kwa watalii. Kwa mtazamo huo, nililiwazia jengo la awali la CCM Lumumba. Lilikuwa na umuhimu wa pekee katika historia za harakati za kupigania Uhuru. Ni jengo ambamo TANU ilizaliwa. Ni urithi wetu sote wa-Tanzania.

Sijui ni nani walioamua kulibomoa na kwa nini. Sijui kwa nini hawakutafuta sehemu nyingine ya kujenga hilo jengo la kisasa. Ninafahamu kuwa majengo yanaweza kuzeeka mno yakawa si salama kwa watu kuingia. Papo hapo, ninafahamu kuna aina za ukarabati ("restoration") zinazowezekana na jengo likabaki salama. Sidai kwamba nina sababu zaidi ya hizo nilizotoa, na labda mtu ataweza kusema kuwa sababu zangu ni zile ambazo kwa ki-Ingereza huitwa "sentimental."

Thursday, October 29, 2015

Shairi la "Kimbunga" (Haji Gora Haji)

Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasihi. Tofauti na inavyoeleweka katika jamii, kutafsiri ni suala pana kuliko kuwasilisha ujumbe kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine, bali ni kutunga upya kazi ya fasihi inayotafsiriwa. Hili suala linajadiliwa sana na wataalam wa lugha, fasihi, na falsafa.

Pamoja na matatizo yote, ninapenda kuchemsha akili yangu kwa kutafsiri kazi za fasihi. Kwa mfano, nimetafsiri hadithi za ki-Matengo, na shairi la Mama Mkatoliki.

Hapa naleta shairi la Haji Gora Haji, mshairi maarufu wa Zanzibar, ambaye niliwahi kukutana naye. Shairi hilo ni "Kimbunga" ambalo limo katika kitabu chake kiitwacho Kimbunga. Jisomee shairi hilo na ujionee nilivyopambana na lugha katika kutafsiri. Ni mapambano, na kuna wakati unajikuta umepigwa butwaa au mwereka.
-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------

                               Kimbunga

1.     Kimbunga mji wa Siyu, kilichowahi kufika
       Si kwa yule wala huyu, ilikuwa patashika
       Kimeing'owa mibuyu, minazi kunusurika
       Nyoyo zilifadhaika.

2.     Yalizuka majabali, yakabirukabiruka
       Zikadidimia meli, ngarawa zikaokoka
       Kimbunga hicho kikali, mavumbi hayakuruka
       Nyoyo zilifadhaika.

3.     Nyumba kubwa za ghorofa, siku hiyo zimeruka
       Zikenenda kwa masafa, kufikia kwa kufika
       Vibanda vyao malofa, vyote vikasalimika
       Nyoyo zikafadhaika.

4.     Chura kakausha mto, maji yakamalizika
       Pwani kulikuwa moto, mawimbi yaliyowaka
       Usufi nusu kipeto, rikwama limevunjika
       Nyoyo zikafadhaika.

5.     Kuna kikongwe ajuza, viumbe kimewateka
       Hicho kinamiujiza, kila rangi hugeuka
       Wataokiendekeza, hilaki zitawafika
       Nyoyo zikafadhaika.


                                 A Hurricane

1.     A hurricane once arrived in Siyu town
       Sparing neither that one nor this one, it was sheer mayhem
       It uprooted babobab trees, the coconut trees surviving
       Hearts went panicking.

2.     Big rocks turned up, tumbling over and over
       Ships were sinking, while mere boats survived
       Fearsome as the hurricane was, it raised no dust
       Hearts went panicking

3.     Great storied houses were blown away that day
       They flew quite a distance, landing wherever they landed
       The huts of the lowly, all survived intact
       And hearts went panicking

4.     The frog drained the river, the water all dried up
       On the shore was conflagration, of the waves flaming
       Half a container of kapok, broke the coolie's cart
       And hearts went panicking

5.     A wizened hag there was, who held beings captive
       She is given to magical powers, changing hues at will
       Those who let her be, perdition will be their lot
       And hearts will go panicking.

Wednesday, October 28, 2015

Maprofesa na Wajibu wa Kuandika

Profesa ni mtu aliyefikia kiwango cha juu cha ufanisi katika ufundishaji, utafiti, uandishi, na kutoa ushauri kwa jamii katika masuala mbali mbali yanayohusiana na utaalam wake. Siwezi kuongelea hapa vipengele vyote vya suala hili, kama vile vigezo vinavyotumika katika kupima ufanisi wa mhusika hadi kumfikisha kwenye hadhi ya uprofesa. Ninakumbushia tu suala la wajibu wa profesa wa kuandika.

Baadhi yetu wa-Tanzania tumeliwazia na kuliongelea suala hili kwa miaka mingi, kwa manufaa ya jamii, tukiliunganisha na masuala kama sera ya elimu, matatizo ya uchapishaji, na kukosekana kwa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu.

Kilichonifanya nirejeshe mada hii leo ni kwamba nimejikumbusha tamko la Rais Kikwete, "Maprofesa Wananisikitisha," ambalo lilijadiliwa katika blogu yangu hii na blogu ya Profesa Matondo. Mambo yaliyosemwa katika majadiliano yale ni muhimu na yataendelea kuwa muhimu. Wajibu wa profesa wa kuandika, kama njia mojawapo ya kufundisha na kuchangia maendeleo ya taaluma ni jambo lililo wazi.

Hata hivi, kwa kuzingatia kuwa dunia inabadilika muda wote, kuna umuhimu wa kulitafakari suala hili kwa mtazamo unaozingatia mabadiliko haya. Fikra zilizokuwa sahihi miaka michache iliyopita, huenda zimepitwa na wakati. Wataalam katika nyanja mbali mbali, kama vile ujasiriamali, elimu, na biashara wanatufundisha kuwa mabadiliko yanatulazimisha kuwa wabunifu na wepesi wa kubadilisha fikra, mahusiano, mbinu na utendaji wetu. Ndio maana ni muhimu kusoma daima na kujielimisha kwa njia zingine.

Katika dunia ya utandawazi wa leo, ambamo tekinolojia mbali mbali zinastawi, zikiwemo tekinolojia za mawasiliano, tunawajibika kuwa na fikra mpya kuhusu usomaji, uchapishaji na uuzaji wa vitabu, na kadhalika. Shughuli nyingi sasa zinafanyika mtandaoni, ikiwemo ufundishaji, kama nilivyowahi kugusia katika blogu hii. Tunawajibika kufunguka akili na kuacha kujifungia katika hiki tunachokiita sera ya elimu ya Tanzania. Je, inawezekana kuandika kitabu chenye umuhimu kwa Tanzania lakini si kwa ulimwengu? Taaluma inaweza kufungiwa katika mipaka ya nchi? Kuna dhana katika ki-Ingereza tunayopaswa kuitafakari: "The local is global."

Naona ni jambo jema kuirejesha mada hii, tuendelee kuitafakari katika mazingira ya leo. Lakini, naona tusome kwanza mjadala uliofanyika katika blogu hii na blogu ya Profesa Matondo.

Monday, October 26, 2015

Shukrani kwa Wa-Tanzania Wadau wa Kitabu Changu

Blogu yangu ni mahali ninapojiandikia mambo yoyote kwa namna nipendayo. Siwajibiki kwa mtu yeyote, wala sina mgeni rasmi. Leo nimewazia mafanikio ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nimejikumbusha kuwa mtu hufanikiwi kwa juhudi zako pekee, hata ungekuwa hodari namna gani. Kuna watu unaopaswa kuwashukuru.

Nami napenda kufanya hivyo, kama ilivyo jadi yangu. Nimewahi kuwaongelea na kuwashukuru wanablogu wa-Tanzania, na nimewahi kuwaongelea na kuwashukuru wa-Kenya. Ninapenda kuendelea kuwakumbuka wa-Tanzania.


Mwanzoni kabisa, nilipokuwa nimeandika mswada wa awali kabisa wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, rafiki yangu Profesa Joe Lugalla, wa Chuo Kikuu cha New Hampshire, alipata kuusoma, akapendezwa nao.

Yeye, kwa jinsi alivyoupokea mswada ule, alikuwa kati ya watu wa mwanzo kabisa kunitia hamasa ya kuuboresha. Tangu wakati ule hadi leo amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha watu wakisome kitabu hiki. Kwangu hili ni jambo la kushukuru sana, nikizingatia kuwa Profesa Lugalla sio tu ni m-Tanzania mwenzangu anayefahamu ninachosema kitabuni, bali pia yeye ni mtaalam wa kimataifa wa soshiolojia na anthropolojia.


Mtu mwingine aliyenihamasisha tangu miaka ya mwanzo ya kuwepo kwa kitabu changu ni Mhashamu Askofu Owdenburg Mdegella wa dayasisi ya Iringa ya Kanisa la ki-Luteri Tanzania. Nakumbuka tulivyokutana katika eneo la shule ya Peace House, Arusha, na hapo hapo akaanza kuongelea kitabu changu, akisema kuwa ni muhimu wazungu wakisome ili watufahamu sisi wa-Afrika. Siwezi kusahau kauli yake hiyo na namna alivyoongea kwa msisimko. Nilimwelewa vizuri kwa nini aliongea hivyo, kwani yeye anahusika moja kwa moja na mipango ya ushirikiano baina ya wa-Marekani na wa-Tanzania, hasa wa Iringa.


Dada Subi, mwanablogu maarufu miongoni mwa wa-Tanzania, ni mtu mwingine ambaye namkumbuka kwa namna ya pekee, kwa yote aliyofanya katika kunihamasisha na kukipigia debe kitabu changu. Nakumbuka aliwahi kuwasiliana nami juu ya kitabu hiki, lakini cha zaidi ni kuwa alikipigia debe katika blogu yake.

Dada Subi alinisaidia sana katika shughuli zangu za kublogu. Ingawa hatujawahi kuonana, ninamfahamu ni mkarimu sana.




Napenda nichukue fursa hii kumtaja na kumshukuru Bwana Muhiddin Issa Michuzi, mwanablogu maarufu wetu wa-Tanzania. Ingawa tumewahi kukutana mara moja tu, Michuzi amekuwa mstari wa mbele kutangaza shughuli zangu katika blogu yake, ikiwemo kitabu changu. Kutokana na hayo tumekuwa kama watu tuliozoeana. Kwangu hilo ni jambo la kushukuru.

Sitachoka kuwashukuru wachangiaji wa mafanikio yangu. Kama nilivyosema, hakuna mtu anayefanikiwa kwa uwezo wake peke yake. Ule usemi wa ki-Ingereza, "No man is an island," yaani hakuna mtu ambaye ni kisiwa, una ukweli usiopingika.

Kwa wanaotaka, walioko Tanzania, Kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kinapatikana Burunge Visitor Centre, simu 0754 297 504.

Monday, October 19, 2015

Matamasha ya Vitabu: Tanzania na Marekani

Nimehudhuria matamasha ya vitabu Tanzania na Marekani. Kwa usahihi zaidi, niseme nimeshiriki matamasha hayo, kama mwandishi, nikiwa na meza ya vitabu vyangu. Nimeona tofauti baina ya Tanzania na Marekani katika uendeshaji wa matamasha haya. Hapa napenda kugusia kidogo suala hilo, nikizingatia kwamba ni suala linalowahusu waandishi, wasomaji, wachapishaji na wauza vitabu.

Tofauti moja ya wazi ni kuwa matamasha ya vitabu ni mengi zaidi, maradufu, Marekani kuliko Tanzania. Marekani kuna matamasha makubwa ya kitaifa na matamasha makubwa kiasi ya kiwango cha majimbo, na pia matamasha ya kiwango cha miji. Mtu ukitaka, unaweza kuzunguka nchini Marekani ukahudhuria matamasha ya vitabu kila wiki, kila mwezi, mwaka mzima. Angalia, kwa mfano, orodha hii hapa. na hii hapa.

Kwa upande wa Tanzania, hali ni tofauti. Matamasha ya vitabu hayafanyiki mara nyingi. Tunaweza kuwa na tamasha la vitabu la kitaifa mara moja kwa mwaka. Lakini hatuna utamaduni wa kuwa na matamasha ya sehemu mbali mbali za nchi, kwa mfano tamasha la vitabu mikoa ya Kusini, tamasha la vitabu mikoa ya Magharibi, mikoa ya Mashariki, na kadhalika.

Tofauti hizi zinatokana na tofauti za utamaduni wa kusoma vitabu. Utamaduni wa kusoma vitabu umejengeka miongoni mwa watu wa Marekani, tangu utotoni. Watoto, hata wanapokuwa wadogo sana, husomewa vitabu; vijana, watu wazima, na wazee husoma vitabu. Utawakuta katika matamasha ya vitabu, kama ninavyoeleza mara kwa mara katika blogu hii.

Katika matamasha ya vitabu ya Marekani, ni kawaida waandishi kuwepo. Wengine huja kuonesha na kuuza vitabu vyao. Wengine huwa wamealikwa kama wageni rasmi. Waandishi huongelea vitabu vyao. Nilivyoona Tanzania ni kwamba wachapishaji ndio huleta vitabu kwenye matamasha. Mtu ukihudhuria matamasha hayo, ukawa na hamu ya kujua kuhusu vitabu vya mwandishi fulani, utaongea na mchapishaji. Mwandishi humwoni.

Ninaona kuwa hii ni dosari. Ni jambo ambalo tunaloweza kujifunza kutoka kwa wa-Marekani. Kuwepo kwa waandishi ni kivutio kimojawapo katika matamasha ya vitabu. Hapa Marekani, ni kawaida kuona matangazo katika vyombo vya habari, au mabango kwenye meza za waandishi yameandikwa "MEET THE AUTHOR." Ni kivutio. Watu hupenda kuonana na waandishi, kuongea nao, kununua vitabu na kusainiwa, na pia kupiga nao picha.

Utaratibu huu ungeweza kufanyika Tanzania, ungesaidia. Ninafahamu, kwa mfano, kwamba wengi wanalijua jina la Ngoswe. Wamesikia, na wanatumia usemi "Ya Ngoswe mwachie mwenyewe Ngoswe." Lakini hawajui asili ya jina Ngoswe. Kumbe, hili ni jina la tamthilia ya Ngoswe: Penzi Kitovu cha Uzembe iliyotungwa na Edwin Semzaba.

Kutokana na umaarufu wa jina la Ngoswe, kama waandaaji wa tamasha la vitabu wangeweka tangazo kuwa mtunzi wa Ngoswe atakuwepo katika tamasha, naamini itakuwa ni kivutio kwa watu kuhudhuria tamasha. Ninaweza kutoa mifano mingine. Jina kama Kinjeketile ni maarufu. Ebrahim Hussein, mwandishi wa tamthilia ya Kinjeketile akijitokeza katika tamasha la vitabu, atakuwa kivutio. Kadhalika Euphrase Kezilahabi, mwandishi wa riwaya maarufu kama Rosa Mistika na Dunia Uwanja wa Fujo.

Waandishi, wachapishaji, na wadau wengine wa vitabu tunakubaliana kwamba kuna haja kubwa ya kujenga utamaduni wa kusoma vitabu katika nchi yetu ya Tanzania. Hilo wazo langu la kuboresha matamasha ya vitabu huenda likachangia mafanikio ya ndoto yetu.

Saturday, October 17, 2015

Kitabu Kinapouzwa Amazon

Nina jadi ya kuandika kuhusu vitabu katika blogu hii. Ninaandika kuhusu vitabu ninayonunua na ninavyosoma, uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu. Ninaandika ili kujiwekea kumbukumbu na pia kwa ajili ya wengine wanaotaka kujua mambo hayo, iwe ni wasomaji na wadau wa vitabu, waandishi, au wanaotarajia kuwa waandishi. Leo napenda kuongelea kidogo juu ya vitabu vinavyouzwa katika tovuti ya Amazon.

Nimewahi kuandika kuhusu mada hii. Lakini nimeona si vibaya kuirudia, ili kuelezea kama yale niliyoyasema mwanzo yamebaki vile vile au kama kuna lolote jipya. Ninaongea kutokana hali halisi ya vitabu vyangu Amazon.

Kwanza kabisa, mambo ya msingi niliyosema mwanzo yamebaki vile vile. Vitabu vyangu viliingia Amazon bila mimi kuvipeleka kule. Vinauzwa kule kuliko sehemu nilipovichapisha au kwenye duka langu la mtandaoni. Ninajionea mwenyewe kuwa Amazon ni mtawala wa himaya ya uuzaji wa  vitabu mtandaoni.

Kila niendako, kwenye matamasha ya vitabu au katika kukutana na watu popote, likijitokeza suala la upatikanaji wa vitabu vyangu, watu wanaovitaka wanaulizia kama vinapatikana Amazon. Imefikia mahali sasa sioni hata umuhimu wa kuwatajia sehemu nyingine. Amazon imejengeka vichwani mwa watu sawa na nyumba ya ibada ilivyojengeka kichwani mwa muumini wa dini: mu-Islamu na msikiti, au m-Kristu na kanisa.

Mimi mwenyewe sina tofauti na hao watu. Ninapotaka kununua kitabu mtandaoni, ninakwenda moja kwa moja Amazon. Ninavutiwa na urahisi wa kuviagiza na kuletewa, na uhuru wa kuchagua bei unayotaka kulipia, kwani kitabu hicho hicho kinauzwa kwa bei mbali mbali.

Hiyo ndio hali halisi ya ununuaji wangu wa vitabu mtandaoni. Tofauti ni pale ninapotaka kununua vitabu vyangu. Hapo siendi Amazon, bali kwenye duka langu. Ninavipata kwa bei pungufu. Punguzo la bei linaongezeka kufuatana na uwingi wa vitabu ninavyonunua. Ninapenda kununua vingi, kwa sababu ninapenda pia kutoa nakala za bure kwa taasisi, vikundi, au watu binafsi wanaojishughulisha kama mimi mwenyewe katika kujenga mahusiano mema baina ya jamii mbali mbali.

Kama nilivyosema katika ujumbe wangu wa mwanzo na kurudia hapa juu, Amazon inauza vitabu kwa bei pungufu. Kwa upande mmoja, hii ni hasara kwa mwandishi. Ni hali halisi ya mfumo wa biashara, na hakuna sheria inayokiukwa. Kwa upande mwingine, hii ni baraka kwa mteja. Kama methali isemavyo, Kuvuja kwa pakacha, nafuu ya mchukuzi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...